Baada ya kusambaa kwa taarifa za watu 7 kupata upofu kutokana na ugonjwa wa macho mekundu (Red Eyes), Wizara ya Afya nchini, imekanusha taarifa hiyo, huku ikisisitiza kuwa taarifa hiyo haijatolewa na Wizara hiyo kama ambavyo imeripotiwa.
Kupitia Taarifa ya kanusho iliyolewa na Wizara hiyo leo Februari 19, 2024, imebainisha kuwa mnamo Februari 6, 2024, Mkurugenzi wa Huduma za Tiba wa Wizara ya Afya, Prof. Paschal Ruggajo, alisema kuwa Wizara hiyo imepokea taarifa za watu ambao wamefika kwenye vituo vya kutolea huduma za Afya wakiwa na vidonda kwenye kioo cha mbele cha jicho, baada ya kutumia tiba zisizo rasmi kutibu Red Eyes, lakini hakutaja idadi ya watu waliopata upofu kutokana na ugonjwa huo.
Kutokana na sintofahamu hiyo, Wizara hiyo imevitaka vyombo vya Habari kuzingatia weledi wa taaluma ya habari kwa kutoa habari za ukweli kutoka kwenye vyanzo vilivyothibitishwa kwani kusambaa kwa taarifa hiyo inaweza kuleta taharuki zaidi ndani ya jamii juu ya ugonjwa wa macho mekundu (Red Eyes).
Chanzo: ITV