WanaJF!
Nimekuwa nikiwaza mahusiano ya Tanzania na nchi jirani za Afrika ya mashariki baada ya ujio wa Obama yatakuwaje?
Kwani inasemekana kitendo cha Obama kuja Tanzania na kuiruka Kenya, kimeleta gumzo, sio tu ndani ya Kenya, bali hata mataifa mengine yameshangazwa na kitendo hicho. Kwani ukizingatia asili ya rais Obama na ahadi yake kwa Kenya, ni wazi kwamba alipaswa atembelee na Kenya kama sehemu ya ziara yake hapa Afrika mashariki.
Sitakuwa na mengi ya binafsi juu ya hili la Ruto na dhihaka yake kwa ujio wa Obama Afrika, bali nime ambatanisha maelezo yake mwenyewe kama ifuatavyo;
NAIBU wa Rais Bw William Ruto, jana alivunja kimya chake kuhusu hatua ya rais wa Marekani Barack Obama kutozuru nchini Kenya kwa kusema hatua hiyo haina madhara yoyote kwa Kenya.
Huku akiongea katika kanisa la Katoliki la St Gabriel Bahati, kaunti ya Nakuru, Bw Ruto alisema "nchi hii ina 'marafiki' wengine wengi duniani ambao inaweza kushirikiana nao huku akiongezea kuwa hatua ya rais Obama kukwepa kutembelea Kenya haiwezi kutatiza kwa vyovyote vile uhusiano mwema uliopo wa kibiashara baina ya Marekani na Kenya."
Bwana Ruto akasema, "Tunaiheshimu nchi ya Marekani nayo inafaa kuwaheshimu Wakenya,"
Alisema serikali ya Kenya tayari imeanzisha mikakati ya kuimarisha ushirikiano wa kibiashara na mataifa mengine huku akikariri kuwa safari ya Rais Uhuru Kenyatta nchini Uganda ambapo alikutana na rais wa nchi hiyo Yoweri Museveni na mwenzao wa Rwanda rais Paul Kagame kujadili jinsi nchi hizo tatu zinaweza kushirikiana kibiashara, ni miongoni mwa mikakati hiyo.
Pia akaongezea, "Nchi yetu inamcha Mungu na kamwe hatutaruhusu mataifa ya kigeni kutuletea tamaduni ambazo zinakinzana na desturi zetu," akasema Bw Ruto huku akirejea hotuba ya Rais Obama nchini Senegal ambapo aliitaka nchi hiyo kuheshimu haki za Mashoga."