Wiki ya unyonyeshaji duniani, tupambanie Hifadhi ya Jamii kwa wote

ACT Wazalendo

JF-Expert Member
May 5, 2014
610
1,540
Utangulizi
Juzi tarehe 07 Agosti 2023 ilikuwa kilele cha maadhimisho ya wiki ya unyonyeshaji wa maziwa ya mama duniani (World breastfeeding week), ambayo kila mwaka uadhimishwa katika wiki ya kwanza ya mwezi Agosti (Kuanzia tarehe 1-7 Agosti) katika nchi mbalimbali. Kwa Tanzania siku hii haijachukua nafasi kubwa sana kutumiwa na jamii na makundi mbalimbali kuhakikisha haki za msingi, tafakuri na kutazama changamoto zinazowakumba wazazi katika mchakato mzima wa unyonyeshaji pamoja na athari zake.

Katika kutafakari siku hii ACT Wazalendo tunaona unyonyeshaji ni haki za msingi za mtoto, haki ambayo inapaswa kuheshimiwa, kulindwa na kutekelezwa kikamilifu. Hali halisi katika nchi yetu kutokana na shughuli za uchumi na uzalishaji na sheria za kazi zilizopo, zinapelekea kuwepo kwa changamoto ya kutopatikana kwa muda wa kutosha kunyonyesha, mazingira salama ya unyonyeshaji na kutokuwepo kwa uangalizi (mafao ya uzazi).

Changamoto hizi zinatofautiana kutokana na uwezo wa uchumi wetu kuzalishi ajira na idadi ya Wanawake waliopo katika sekta ya ajira kwa maana ya kwenye ajira rasmi au ajira zisizo rasmi (waliojiajiri). Kwa mujibu wa takwimu za sensa ya mwaka 2022 taifa lina watu wenye uwezo wa kufanya kazi milioni 31.9 lakini ni watu milioni 1.8 pekee ndio walio kwenye Hifadhi ya Jamii wanaoweza kupatiwa fao la uzazi na likizo yenye malipo.

Hivyo basi, changamoto zinazorudisha nyuma kutekelezwa kwa haki ya unyonyeshaji nchi ni kama zifuatazo kutoka na makundi hayo mawili;

a. Kwa Wanawake walio wengi ambao wapo kwenye sekta isiyo rasmi- wakulima, wavuvi, wachimbaji wadogo, wafanyabiashara wadogo (hawako kwenye mfumo wa hifadhi ya jamii) hawana fao la uzazi; likizo ya uzazi; kutokuwa na muda wa kutosha wa matazamio (wengi wao wanafanya kazi ngumu hadi karibu na kujifungua au mapema tu baada ya kujifungua.

b. Kuwepo kwa muda mfupi wa likizo ya uzazi ambao kwa mujibu wa sheria ya kazi ya mwaka 2004 ni siku 84 kwa mzazi Mwanamke na siku 3 pekee kwa mzazi mwanaume.

c. Kukosa muda wa kutosha kunyonyesha mtoto pindi wanapoendelea na kazi baada ya likizo ya uzazi. Mazingira ya kazi kutokuwa rafiki kumfikia mtoto kwa saa mbili zinazotolewa sasa.

d. Kupunjwa au kutopatiwa kwa wakati fao la uzazi

Nchini Tanzania Tafiti zianaonyesha kwamba asilimia 30 ya watoto chini ya miaka mitano wamedumaa hii ni kutokana na kukosa lishe stahiki ikiwemo muda wa kutosha wa kunyonya maziwa ya mama. Kwani maziwa ya mama yana virutubisho vyote vinavyohitajika kwa mtoto. Wastani wa mtoto kunyonya kwa siku ni angalau Mara 8-12 kwa siku kwa wastani wa kila baada ya masaa mawili, hii ni kutokana na kuwa kiafya mtoto hatakiwi kula chakula chochote, wala maji kwa muda wa miezi 6 ya kwanza zaidi ya maziwa ya mama.

Kwa mujibu wa Mkataba wa 183 wa Ulinzi wa Uzazi (Maternity Protection Convention, 2000. Article 4) wa Shirika la Kazi la Kimataifa ambao Tanzania imesaini unaeleza Mama anapojifungua apewe likizo ya si chini ya wiki 14 ya uzazi baada ya kujifungua.

Aidha, mbali na hoja ya muda wa kunyonyesha na mazingira ya kazi suala la malezi ya mtoto si jukumu la mama peke yake. Sheria inamlazimisha baba wa mtoto kurejea kazini siku tatu tu baada ya mke kujifungua hali inayopunguza wajibu wa baba kwa familia na mtoto, jambo hili ndio linasababisha kuwakandamiza wanawake kwa kuwapa mzigo mkubwa wa malezi wakiwa peke yao.

Katika maadhimisho ya wiki ya unyonyeshaji Duniani ACT Wazalendo tunapendekeza;

i. Muda wa likizo ya uzazi kwa waajiriwa wanawake uongezwe mpaka miezi sita, hii kutokana na Ukweli kwamba mtoto anahitaji ukaribu wa mama na kunyonya mara kwa mara hivyo Kifungu cha Sheria ya ajira na mahusiano kazini ya mwaka 2004 Ibara ya 33 kifungu cha 6 (a) na (b) kibadilishwe kutoka siku 84 au 100 ikiwa ni mtoto Zaidi ya mmoja za sasa na kuwa siku 185.

ii. Mabadiliko haya yaende sambamba kifungu cha 34 Ibara ya 1 (a) na (b) na kumuongezea Baba wa mtoto baada ya mke kujifungua apewe ikizo ya angalau wiki tatu (Siku 21) ili ashiriki malezi ya mtoto.

iii. Tunapendekeza mwajiri atoe Lishe kama motisha kwa wazazi wa kike na wakiume pindi anapopata mtoto na fao la uzazi lisiwe na masharti magumu na lisicheleweshwe kama ilivyo sasa.

iv. Tunarudi wito wa kupanuliwa kwa mfumo wa Hifadhi ya Jamii kwa wote ili hata wanawake walio katika sekta isiyo rasmi wapate fao la uzazi, likizo ya malipo na bima ya afya.

Ndg. Janeth Joel Rithe
Twitter: @JaneRithe
Msemaji wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalamu.
ACT Wazalendo
07 Agosti, 2023
 
Back
Top Bottom