wa stendi
JF-Expert Member
- Jul 7, 2016
- 26,013
- 28,347
```Kariakoo ni jina linaloitambulisha Kata Mojawapo ya Wilaya ya Ilala, Mkoa wa Dar es Salaam, Tanzania yenye postikodi namba 11106. Kata hii inakadiriwa kuwa na zaidi ya watu 13,780 waishio humo hii ni kwa mujibu wa sensa iliyofanyika mwaka 2012.
Jina la Kariakoo lina historia ndefu sana, jina lililotokana na neno la Kingereza “Carrier Corps” yaani kikosi cha wapagazi waliobeba mizigo ya jeshi wakati wa Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia. Hii ilikuwa ni Vita iliyopigwa mwaka 1914 hadi 1918. Carrier Corps kwa Kiswahili lilitamkwa Karia-Koo na liliendelea kutumika hadi leo.
Kariakoo ni Soko Kuu Jijini Dar es Salaam na Tanzania ambapo kunafanyika biashara za aina zote za mahitaji muhimu ya kila siku ya binadamu. Biashara zinafanyika kwa jumla na rejareja. Historia ya jina la Kariakoo na soko la Kariakoo inaanzia tangu enzi za ukoloni wa Mjerumani wakati Tanzania Bara ikiitwa Tanganyika. Mahala lilipo soko hilo palijengwa jengo la Utawala wa Wajerumani ambalo lilikusudiwa litumike kama ukumbi wa kuadhimisha sherehe za kutawazwa kwa Mfalme Kaiser Wilheim wa Ujerumani kwa wakati huo.
Hata hivyo lengo langu la leo siyo kujikita kwenye maana na asili ya Kariakoo. Natamani kuona wenye mamlaka wanaiangazia upya Kariakoo na jinsi ambavyo wanaweza kuienzi historia yake ambayo inaonekana kufifishwa kwa kiasi kikubwa. Biashara na Wafanyabiashara wa eneo hilo la Kariakoo wamepitia kipindi kigumu sana miaka ya hivi karibuni. Kariakoo ile iliyokuwa inajulikana Afrika nzima na duniani kwa ujumla imelala usingizi wa pono.
Wafanyabiashara wa Kariakoo walioonekana kuwa ni wezi na wakwepa kodi, hali ilisababisha kila mamlaka kuja kuangazia eneo hili huku wakiwa na mtazamo hasi. Hali hii imesababisha biashara nyingi sana za eneo hili kufa huku zikiinuka biashara kama hizo nchi za jirani yaani DRC, Mozambique, Malawi, Zambia, Zimbabwe, Burundi, Rwanda, Sudani Kusini, Kenya na Uganda. Mamlaka ikaziangalie upya tozo mbalimbali zinazotozwa kwa mfanyabiashara wa Kariakoo, kwani ni nyingi sana kuliko kinachoingizwa na mfanyabiashara huyo.
Natamani kuona ile Kariakoo ya kipindi cha Awamu ya Tatu na Nne inarudi tena. Natamani kuona zile pilikapilika za watu kutoka Mataifa jirani wanakuja tena Tanzania hasa Kariakoo kuuza na kununua bidhaa mbalimbali. Natamani kuona wanunuzi wanaokuja madukani kuulizia au kununua bidhaa wanaongea lugha yenye lahaja za watu kutoka mataifa mbalimbali kama DRC, Mozambique, Malawi, Zambia, Zimbabwe, Burundi, Rwanda, Sudani Kusini, Kenya na Uganda.
Wenye mamlaka waambieni hawa jamaa zetu kuwa ile kamatakamata ya stakabadhi za Kielekroniki (EFD) haipo tena. Waambieni kuwa wale wote waliokamatwa na mizigo kutokana na kupoteza kwa stakabadhi ya malipo, hawatakamatwa tena. Waambieni kuwa ile Kariakoo iliyofananishwa na Dubai imerudi tena. Wafanyabiashara waliopoteza mitaji yao kutokana na changamoto mbalimbali, watarudi tena kwa nguvu mpya.
Ingawa nipo huku Masyamba Bulongwa, Makete Njombe huku nikipambana na Manyani kutoka bonde la Kyela na Tukuyu baada ya shamba langu la miti ya mbao kuungua lote. Bado natamani sana kurudi tena Kariakoo kufanya vibarua vya kuuza maduka ya Waha, Wachaga, Wabena, Wanyakyusa, Wawanji, Wakinga nk. Nawasihi viongozi wangu wote wenye mamlaka juu ya mustakabli wa maisha yetu, muyaangazie mambo yafuatayo kuhusu Kariakoo Mpya.
Pamoja na mambo mengine, niwakumbushe tu kuwa kile kiburi tulichodhani Kariakoo ni yetu, tukiache kabisa. Karikaoo ilijengwa na Wafanyabiashara na wanunuzi kutoka nchi za DRC, Mozambique, Malawi, Zambia, Zimbabwe, Burundi, Rwanda, Sudani Kusini, Kenya na Uganda. Bila hawa hakuna Kariakoo wala hiyo KODI hamtaikusanya kwa kiwango mnachokitarajia.
Tuzitumie mamlaka zetu kuwajengea mazigira mazuri Wafanyabiashara kutoka nchi za jirani ili tuzidi kuitangaza nchi yetu. Wenye mamlaka jengeni mahusiano mazuri na majirani hasa wanunuzi wa bidhaa zetu maana bila wao hakuna Soko la Kariakoo. Hakuna uagizaji wa bidhaa kutoka China kama hakuna wateja. Wateja wa ndani ya nchi peke yao hawawezi kuzimaliza bidhaa zetu zote. Kuwajengea mazingira magumu wageni ni kuziua biashara za Watanzania wetu, kupunguza mapato ya kodi na kupunguza ajira kwa Watanzania wenzetu.
Mbali na kujenga mahusiano mazuri na wageni, pia wageni hao wanatutangaza vyema huko makwao. Hakuna faraja iliyo kuu kama kuona jina Tanzania linatajwa kwa mema kila penye mkusanyiko ya wafanyabiashara. Nilibahatika kupita Miji kadhaa ya nchi jirani. Nilifarijika sana kuona bidhaaa nyingi walikuwa wanazinunua kutoka Kariakoo Tanzania. Lakini sasa baada ya kuwabana na kuwajengea mazingira magumu, wameanza kununua moja kwa moja kutoka China. Bahati mbaya sana hizo bidhaa sasa zinapita Mombasa, Dar es Salaam na Maputo.
Bandari yetu ya Salama ilikuwa kiungo muhimu sana kutuunganisha na majirani kupitia biashara ya kuagiza mizigo kutoka nje ya Bara la Afrika. Biashara ya hoteli na nyumba za kulala wageni za Dar es Salaam zilikuwa zinajaa wageni kutoka nchi jirani. Wasafirishaji wa mizigo nao walipata fedha za kutosha kutokana na kusafirisha mizigo kwenda huko nchi jirani. Lakini sasa kila mtu analia kivyake.
Wenye mamlaka ifufueni tena Kariakoo ambayo ipo toka enzi za Vita Kuu ya kwanza ya Dunia. Tusaidieni kuboresha ulinzi na usalama kwa wageni wetu, boresheni miundombinu ya taka ngumu na taka laini, miundombinu ya maji safi na maji taka, umeme na simu ili wageni waje waione tena ile Kariakoo ya Awamu ya Tatu na Nne.
Wamachinga tunawapenda sana, lakini naomba niwambie wazi kabisa wenye mamlaka. Katika mahali mlipokosea pakubwa ni kumtetea anaelipa Sh. 20,000.00 (Shilingi Elfu Ishirini Tu) kwa mwaka na kumwangamiza Mfanyabiashara anaelipa mamilioni ya Kodi kwa mwaka. Hakuna nchi duniani iliyofanikiwa kuwainua masikini kwa kuwaangamiza matajiri. Matajiri ndio wanaotoa ajira kwa hao masikini. Hali ilivyo sasa Kariakoo njia zote zimefungwa na Wamachinga.
Wamachinga wanauza zaidi ya Wafanyabiashara, wameziba milango ya Wafanyabiashara na baadhi yao wananunua mizigo kutoka kwenye maduka ya wafanyabiashara kwa njia za kuwarubuni vijana wa madukani. Wamachinga wasipowekewa utaratibu mzuri, litakuja kuwa bomu kubwa sana hapo baadae.
Sasa hivi wameziba njia zote za kuingia na kutoka Kariakoo. Ole wako ukanyage mzigo wake au ujichanganye ugombane nao; watakachokufanya ni Mungu tu anajua. Sina nia mbaya na hawa Wamachinga, kilio changu ni kuwajengea utaratibu mwingine maana huu wa sasa unawaua wafanyabiashara ambao ndio walipa kodi wakubwa.
Mwisho kabisa nimpongeze sana Rais wangu Samia Suluhu Hassani kwa mwanzo mzuri na mwalimu wangu Dkt. Philipo I. Mpango kwa kuteuliwa kuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Naomba mtu yeyote atakaebahatika kuonana nae, amwambie kuwa yule mwanafunzi wako wa Uchumi uliemfundisha pale UDSM, ameikimbia Kariakoo baada ya kufukuzwa kazi ya kuuza duka. Sasa hivi yupo Kijijini kwake Masyamba Bulongwa, Makete Njombe anapambana na manyani yaliyovamia mashamba yote ya Wilaya ya Makete.
Ukizingua tunazinguana.