Wenye kulewa madaraka, hulewa njwii! | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Wenye kulewa madaraka, hulewa njwii!

Discussion in 'Habari na Hoja mchanganyiko' started by Mzee Mwanakijiji, Jun 3, 2010.

 1. Mzee Mwanakijiji

  Mzee Mwanakijiji Platinum Member

  #1
  Jun 3, 2010
  Joined: Mar 10, 2006
  Messages: 31,364
  Likes Received: 6,396
  Trophy Points: 280
  Mwananchi Jumapili

  WAPO walevi na wapo walevi wanaolewa njwii. Walevi wa madaraka ni walevi njwii. Mara nyingi tumesikia msemo huo na kukubali kwa sauti moja tukisema watu wasilewe madaraka au tunasema "wamelewa madaraka" lakini bila kuangalia tunasema kitu gani hasa.

  Tunapozungumzia walevi wa madaraka hatuwazungumzii watu wanaokunywa madaraka na kulewa kidogo hata tusijue wamelewa kwani wanatenda kana kwamba hawajalewa kabisa; la hasha tunapozungumzia walevi wa madaraka tunawazungumzia watumishi na watendaji ambao wamekunywa madaraka na kulewa chakari. Hawa ndiyo walevi hasa wa madaraka kwani hawawezi hata kutudanganya kuwa hawajalewa.


  Unaweza kukutana na mtu njiani na ukajua kuwa "huyu kanywa" lakini hajalewa chakari kwani bado ana dalili zote za utimamu ila utamuona tu "amechangamka" kwa namna fulani au harufu ya ulabu wake itakufikia. Lakini amevaa nguo zake vizuri, hayumbi yumbi na hata kauli zake hazibabaiki au kuvuta vuta. Unaweza ukakutana na mtu ambaye toka mbali unajua kabisa kuwa ‘kalewa'. Anakwenda mwendo wa kuyumbayumba ukisindikizwa na nyimbo za "pombe si chai, amelewa mgandini." Mtu huyo utamuona hana haya ya kucheza ndombolo lake peke yake na hatosita kuwaamkia hata watoto kwa furaha.


  Wapo walioonja madaraka lakini hawakukubali kulewa. Wameuona utamu wake na wamechangamka lakini wanajilinda kila kukicha wasilewe, wasipitilize. Katika watumishi leo hii, wapo watu ambao wameonja madaraka na wakajua utamu wake na kama watu wanaojua madhara ya kileo hujilinda wasije wakalewa. Hawa huitwa watumishi waadilifu. Si kwamba hawana majaribu ya kulewa madaraka, si kwamba hawajui utamu wa madaraka, wanajua; lakini wanajua hatari ya kulewa madaraka.


  Madaraka kama kilivyo kileo huja na athari moja kubwa ambayo ni kuondoa soni yaani aibu. Sifa mojawapo ya kikemia ya kileo ni kuwa kinamfanya mtu aondoe vizuizi vyote vya kimaadili ni kutokana na hili, kimekuwa kikitumika katika shughuli mbalimbali ambazo watu wangependa kuondoa aibu. Sasa madaraka nayo yakishamlewesha mtu vizuri basi humfanya mtu asiwe na aibu ya anayoyafanya. Ndiyo maana narudia kusema kuwa anayelewa madaraka hulewa njwii.


  Aliyelewa kileo cha madaraka na akaondoka na aibu zote huwa na sifa mbili kubwa. Sifa hizi utaziona kwa kiongozi yeyote yule ambaye amelewa madaraka. Yaani, haijalishi cheo chake, jina lake, hadhi yake au watu wanavyomchukulia kwa kadri ya kwamba amelewa madaraka atazionyesha sifa hizi mbili.


  Kwanza, atajiona kuwa yeye ‘ndiyo yeye' na hakuna mwingine na hujichukulia katika umuhimu mkubwa mbele ya watu wengine. Hajali sheria zinasemaje, hajali maadili yanataka nini, hujiamini tu kuwa yeye ndiyo sheria na yeye ndiyo maadili. Sifa hii ya kwanza ukiikuta kwa mwanasiasa au mtumishi aliyelewa madaraka basi utaona mtu huyo hujiona kama mungu miongoni mwa wanadamu na hufikia mahali hujidhania kuwa yeye ni zawazi ya Mungu kwa binadamu.


  Sifa ya pili ya aliyelewa njwii madaraka hutokana na hiyo ya kwanza; mtu aliyelewa huamini kabisa ndani ya moyo wa moyo wake kuwa anaweza kufanya lolote bila kujali matokeo yake (with impunity). Mtu aliyelewa madaraka huweza kuagiza lolote, kuamuru lolote, kutaka lolote, kukataza lolote au kutenda lolote alimradi anajua kuwa watu hawatampinga au hawatamhoji na wakimhoji sana anaweza kuamuru watu hao wachukuliwa hatua (hata kama hana uwezo huo).


  Bila ya shaka unajiuliza kwa nini nazungumzia waliolewa madaraka njwii katika makala yangu ya kwanza katika gazeti hili. Wiki iliyopita tulishuhudia mmoja wa watendaji wa serikali yetu aliyelewa madaraka akionyesha sifa hizo mbili na inasikitisha kwamba walevi wengine wa madaraka wamekubaliana naye. Unajua walevi hujuana wenyewe na hulindana wenyewe. Usiulize ukweli wa mlevi kwa mlevi mwenzake. Namzungumzia Msajili wa Vyama vya Siasa, John Tendwa.


  Tendwa alifanya mambo mawili ambayo naamini kabisa asingeweza kufanya kama angejua kuwa cheo alichonacho ni dhamana na ni utumishi kwa taifa lake. Angejua nafasi aliyonayo katika utumishi umma na mbele ya jamii angepima maneno yake kabla hayajamtoka mdomoni.


  Kwanza, alijaribu (bila ya uwezo huo kuwa nao) kuwaambia wahubiri wa dini wahubiri nini kuhusu sheria mbaya na mbovu ya gharama za uchaguzi. Nasikitika hakuna kiongozi wa dini aliyekuwa na ujasiri wa kumwambia Tendwa kuwa hana uwezo, nafasi, wala haki ya kumshauri kiongozi yeyote wa dini kuhubiri nini kwa waumini zake.


  Kama vile wasivyotaka viongozi wa dini kuchanganya siasa kwenye dini, naamini tusiwaruhusu viongozi wa siasa kuchanganya dini kwenye siasa. Ni mlevi tu anaweza kusimama na kuwaambia viongozi wa dini "wagonge" na sheria ya uchaguzi kwenye mimbari.


  La pili, ni kuwa linatokana na ile sifa ya pili ya walevi wa madaraka. Tendwa ambaye cheo chake ni Msajili wa Vyama vya Siasa aliutangazia umma wa Watanzania kuwa hana bajeti ya kusajili vyama vya siasa linapokuja suala la CCJ!

  Yaani, pasipo haya wala soni alisimama na kutuambia kuwa hana fedha za kufanya kazi aliyoapa kwanza kuifanya kwa sababu ana kazi nyingine. Hiyo nyingine ni kutoa mafunzo na elimu juu ya sheria mbovu ya gharama za uchaguzi! Yaani, "msajili" ameamua kugeuza ofisi yake kuwa ya kutoa semina badala ya kusajili vyama vya siasa ambavyo vimetimiza masharti. Ati tangu aletewe fomu za kuomba usajili wa kudumu zimepita karibu siku 10 na yeye hajapata kuona hizo fomu ndani ya ofisi yake! Halafu watu wanashangaa kwa nini bodi ya mikopo wanasema hawana fedha za mikopo ya wanafunzi wakati wizara inasema fedha zipo!


  Ndugu zangu, tunavyoendelea tutakutana na watu waliolewa madaraka kama Tendwa. Tutakuwa na uamuzi wa kukubali na kukumbatia au kuwakatalia. Naamini changamoto kubwa ya uchaguzi huu mkuu ni uwezo wa Watanzania kuamua kama wanataka baadhi ya walevi wa madaraka warudi tena au kuwakataa.


  Tayari viongozi wa serikali wameanza kupita mitaani kutuambia uzuri na mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Nne. Wananchi wasikilize kwa makini na wawe na ujasiri wa kuchambua kama wanaosema hayo wameonja, wamekunywa au wamelewa madaraka.


  lulawanzela@yahoo.co.uk
   
 2. Annina

  Annina JF-Expert Member

  #2
  Jun 3, 2010
  Joined: Nov 15, 2009
  Messages: 437
  Likes Received: 2
  Trophy Points: 35
  Asante MMJ kwa kushare makala ya Lula. Tatizo hili ni kama kansa katika nchi yetu, na lipo katika ngazi zote hadi ya familia! Tuanze kusema hapana kuanzia ngazi ya familia ndio tutaweza kusema hapana kwa viongozi wa kitaifa. Ikumbukwe viongozi hawa ni sehemu ya familia zetu hawatoki hewani, kama hatuwezi kudhibiti kansa hii ya ulevi wa madaraka katika ngazi ya kaya - tusahau kuhusu ulevi wa madaraka yakatika ngazi ya kitaifa.

  Annina
   
 3. M

  Magezi JF-Expert Member

  #3
  Jun 3, 2010
  Joined: Oct 26, 2008
  Messages: 2,827
  Likes Received: 87
  Trophy Points: 145
  Mimi binafsi nilimshangaa tena alivyokuwa anongea kwa jeuri utadhani hataingia kaburini.....kweli ulevi wa madaraka ni ule wa mtu kulewa njwii.
   
 4. Ngambo Ngali

  Ngambo Ngali JF-Expert Member

  #4
  Jun 4, 2010
  Joined: Apr 17, 2009
  Messages: 3,197
  Likes Received: 135
  Trophy Points: 160
  "Power corrupts and absolute power corrupts absolutely" Abraham Lincolin
   
Loading...