Wengine Wetu Mafisi

Filipo Lubua

JF-Expert Member
Nov 18, 2011
339
578
Ubinadamu si sisi, kwa tafsiri sisisi
Wengine wetu mafisi, wa mawazo mufilisi
Wajitia majasusi, wajifanya mamilisi
Nasema hao si sisi, wana chembe za ufisi

Wana wingi wa matusi, zina sumu zao hisi
Wamejawa uyabisi, machoni utusitusi
Wafurikwa na ubinafsi, wajiona ni wakwasi
Nasema hao si sisi, wana chembe za ufisi

Wajifanya mambingusi, ila wao ni mangisi
Wamebeba nyingi ndusi, zizojaa unajisi
Tusiwafanye wambasi, watatuletyea mikosi
Nasema hao si sisi, wana chembe za ufisi

Mwonekano wa shemasi, ndani wana unuhusi
Kamwe siwape nafasi, wakimbie kwa upesi
Wachunge kwa udadisi, wasikutie utasi
Nasema hao mafisi, tusiwafanye mamisi

© Filipo Lubua, 10 Novemba 2013
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom