Urithi Mkuu wa Utamaduni Wetu Kisiasa-MWAKATOBE

Paparazi Muwazi

JF-Expert Member
Dec 23, 2007
310
79
Urithi Mkuu wa Utamaduni Wetu Kisiasa ni Nini?
(What is the Major Heritage of Our Political Culture?)

Na: Gwandumi G.A. Mwakatobe
(Mfuatiliaji na Mchambuzi wa Masuala ya Kitaifa na Kimataifa)
Simu: 0714 – 511622, Barua pepe: gwandumi@hotmail.com
Januari, 2008

1. Utangulizi

Pengine nitangulie kwa kuainisha kuwa kuna njia kuu tatu za kufikia malengo ya kisiasa, hususan katika harakati za kutwaa madaraka/utawala au kutwaa nguvu za dola katika nchi au taifa. Njia hizi ni kama zifuatazo:

i. Njia ya amani ambayo huambatana na mijadala, midahalo, maandamano ya amani, usuluhishi, maridhiano na maelewano kwa pande mbili zinazotofautiana kiitikadi na kiutawala.
ii. Njia ya kuchochea vurugu, chuki na uhasama kwa wananchi dhidi ya Chama na Serikali iliyoko madarakani kwa lengo la kuleta maasi ya umma.
iii. Njia ya mapinduzi ya kijeshi au maasi ya kijeshi.

Ni njia ya kwanza pekee ambayo inazaa amani na utengamano wa kudumu katika jamii na miongoni mwa wananchi. Njia ya pili na ya tatu zimesababisha na zinaendelea kusababisha maafa makubwa sana katika jamii. Madhara hayo ni pamoja na:

• Kuleta vita ya wenyewe kwa wenyewe,
• Mauaji ya kutisha miongoni mwa wananchi huku waasisi wa vurugu hizo wakiwa mafichoni ama uhamishoni nje,
• Uharibifu mkubwa wa mali, miundombinu na rasilimali za umma,
• Lundo la wakimbizi wakihangaika huku na kule na kuleta mateso makubwa hususan kwa watoto na wanawake,
• Uchungu wa kupotelewa na ndugu huendelea kuwaumiza wananchi miaka nenda rudi, hata kama vita itaisha,
• Chuki na uhasama miongoni mwa kabila na kabila, eneo na eneo na wananchi na serikali, huku nchi ikigawanyika vipande vipande, hata kama vita itaisha,
• Kukosekana kwa utaifa na umoja madhubuti miongoni mwa wananchi, hata kama vita itaisha.

2. Njia Ipi Sahihi Katika Kudai Haki za Kisiasa?

Kwa kuwa nchi yetu haijawahi kukumbwa na mapinduzi ya kijeshi, ukiondoa maasi ya muda mfupi ya mwaka 1964, katika makala hii tutajadili njia ya kwanza na ya pili tu, ili tuwekane sawa, mmoja mmoja na kama Taifa moja.

Njia ya amani ya kudai haki na mabadiliko ya kisiasa kwa kutumia mijadala, midahalo, maandamano ya amani, usuluhishi, maridhiano, maelewano na kusameheana, katika meza moja, imekuwa ndiyo Urithi Mkuu wa Utamaduni Wetu Kisiasa. Na pia ndiyo njia pekee na muafaka ya kusuluhisha migogoro, migongano na uhasama wa kisiasa. Naam, ndiyo njia pekee ya kudumisha utamaduni wa kupenda amani na utengamano wetu ambao kihistoria tumebahatika kuwa nao. Nasisitiza tumebahatika!

Kwanini nasema tumebahatika? Awali ya yote, ni hekima kutambua kuwa Mwenyezi Mungu ametujalia mengi hapa Tanzania. Mojawapo ya majaliwa makubwa ni sisi sote kama Taifa kujikuta tumezaliwa eneo la kijiografia katika Afrika Mashariki ambalo watu waishio eneo hili ni watulivu, wapole, waungwana na wapenda amani.

Nasema hivyo kwa kuwa hatukuchagua na wala hatukupenda kuzaliwa Tanzania, bali ni kwa kudra za Mwenyezi Mungu tukajikuta sisi na wazazi wetu tumezaliwa Tanzania - mahali ambapo watu wake wanapenda njia ya amani kusuluhisha na kuboresha mahusiano yao ya kila siku. Ama kwa hakika, tunawiwa na kuwajibika kumshukuru Mwenyezi Mungu na kulinda, kwa uwezo wetu wote, amani na utengamano tuliojaliwa na kuurithi. Natamani sana tuwe na siku maalum kila mwaka ya kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuzaliwa Tanzania na kuwa Watanzania!

Yamkini ndiyo maana hata mababu zetu mashujaa, hususan Babu yetu Kinjekitile Ngwale na Mtwa Muyigumba Mkwawa waliwiwa vigumu mno kuwashawishi wananchi wao kuingia vitani dhidi ya Wajerumani. Tunajua na kutambua nia yao njema waliyokuwa nayo, ya kupinga uvamizi na kutawaliwa na wageni. Lakini pia wananchi wao walikuwa wanasita sana kutumia njia ya vita kupinga uvamizi.

Tunakumbuka jinsi Kinjekitile alivyolazimika kuwadanganya kwamba risasi za Wajerumani zingegeuka maji. Katika vita hiyo ya Maji Maji, kuanzia mwaka 1905-1907, nchi yetu ilipoteza idadi ya watu wapatao 120,000, kiwango cha mauaji ambacho hakijawahi kutokea katika historia ya nchi yetu! Na mbaya zaidi, hata shujaa wetu Kinjekitile akanyongwa kinyama eneo la Mohoro, Kilwa.

• Tumerithi nchi ambayo watu wake hawapendi vurugu.
• Tumerithi nchi ambayo watu wake hawapendi uchochezi wa chuki.
• Tumerithi nchi ambayo watu wake hawana hulka ya kujengeana uhasama.
• Tumerihti nchi ambayo watu wake hawapendi vita.
• Naam, tumerithi nchi ambayo inatukuza na kuenzi amani na utengamano.
• Hakika ni muhimu sana kulifahamu hili, kabla ya kufumua hasira na jazba za kisiasa - Eh Mola wetu pishia mbali!

Aidha, pamoja na kwamba Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alikuwa mkakamavu mno mithili ya askari jeshi na mwenye ushawishi mkubwa, hakuthubutu hata kidogo kutumia njia za kivita au kuleta uhasama au vurugu zozote katika kudai uhuru. Alijua fika jinsi ambavyo Watanganyika hawakupenda vita.

Kuna wakati Mwalimu Nyerere aliwahi kusema watu walikuwa bado wana hofu na woga wa mauaji ya vita vya Maji Maji na kuanza kuogopa harakati zake za kudai uhuru wakihisi kujirudia kwa yaliyomkuta Kinjekitile Ngwale.

Mwalimu alisema kuna watu wengi walikuwa bado wana kumbukumbu za vita ya Maji Maji. Mwalimu akatumia njia ya amani na maelewano (Non-Violence Method) kwa hoja madhubuti, na zenye nguvu katika kudai uhuru, pasipo vurugu ama uhasama, na pasipo chembe ya tone la damu. Baada ya uhuru Mwalimu alizidi kudumisha na kuimarisha amani, kiasi ambacho Tanzania tumejikuta tuko katika nchi yenye misingi thabiti ya amani iliyotukuka. Nchi jirani zote zimetikisika na zingine zinaendelea kutikisika huku kimbilio lao pekee la usalama imebaki kuwa Tanzania.

Ingawa baadhi ya nchi za Afrika na kwingineko zilitumia njia za kijeshi kudai uhuru, pia kwa nia njema, bado madhara yake ni makubwa hadi leo. Haki zozote zinazodaiwa kwa njia zisizo za amani, madhara yake huendelea hata kama vita itaisha. Imethibitika sasa kuwa, ni heri kuchelewa kupata haki kwa njia ya amani na maridhiano kuliko kupata haki kwa njia dhalimu na dhalili, hasa kuchochea vurugu, chuki na uhasama wa kisasa. Kama haki huzaa amani, kamwe vurugu, chuki na uhasama haviwezi kuwa mbadala wa kuzaa amani - haviwezi kudumisha msingi wa umoja. Ni machafuko tu!

Hivyo basi, si ajabu kuona kwamba Rais wetu Jakaya Mrisho Kikwete alipokuwa akilihutubia Bunge kwa mara ya kwanza Desemba 30, 2005 alitaja vipaumbele 10 kama vigezo na shabaha za serikali ya awamu ya nne (SAN). Kipaumbele cha kwanza kabisa ni “Kuhakikisha kuwa Amani, Utulivu na Umoja wa nchi yetu na watu wake vinadumishwa.” Tukidumisha amani ndipo dira kuu ya CCM na SAN ya “Maisha Bora kwa Kila Mtanzania,” itafikiwa na kuonekana kwa dhahiri.

Nasikitika kwamba vurugu, chuki na uhasama unaanzishwa na wanasiasa, huku Wapinzani wakianzisha, kuchochea na kushabikia vurugu, chuki na uhasama huo, kwa matusi, lugha chafu na kejeli za kizushi. Siasa za vurugu, chuki na uhasama (political violence) si kasumba ya Watanzania. Si hulka yetu. Ndiyo, si utamaduni wetu. Tumesema mababu walishindwa kutumia njia hii. Tumesema Mwalimu akijua hilo, kamwe hakuthubutu kutumia njia ya kuchochea vurugu. Alikuwa mpatanishi, na aliendelea kuthaminiwa na kuheshimiwa na hata maadui wake wakoloni.

Sambamba na hili, lazima tutambue pia hata usemi wa Watanzania: maongezi yao, mahusiano yao na mawasiliano yao huashiria amani, upole na uungwana. Ni Watanzania pekee duniani kote ambao wakiingia dukani husema: “naomba sukari”, “naomba chumvi,” “naomba kiberiti,” “naomba kipande cha sabuni” – utadhani anapewa bure. Kumbe analipia! Kuomba kitu unachotaka dukani ni lugha ya upole, uungwana na unyenyekivu. Ni ishara ya upendo - hata kama unalipia. Nchi zingine hutumia maneno makali kama: “leta hapa sukari!” “toa kiberiti!” “nipe haraka chumvi kilo moja!” Lugha ya ukali na amri si hulka ya Mtanzania.

Tunashuhudia kwenye misiba na wakati wa kuuguza wagonjwa, utakuta mara nyingi watu ambao si ndugu zako wa damu au wa kabila moja wanakuwa wengi kuliko hata ndugu wa damu au kabila moja kuja kukufariji na kukusaidia, kudhihirisha kuwa Watanzania tuna umoja ambao umetufanya sote tujione ndugu. Aidha nimekuwa nikishuhudia misikitini na makanisani watu wakibubujika machozi kuombea amani nchi yetu na viongozi wetu. Jambo hili ni nadra sana kuliona nchi zingine isipokuwa Tanzania.

Mimi mwenyewe nakumbuka niliwahi kuasisi chama mwaka 2001 kilichoitwa HArakati za MAbadiliko SAhihi, kwa kifupi HAMASA. Katika harakati zetu za kujinadi tulijaribu kutumia maneno makali, lakini mwitikio wa wananchi ulituona ni wenye siasa kali na kuanza kutuogopa kila tupitapo na kutuona hatufai kabisa kuwa viongozi na watetezi wa utamaduni wa amani na utengamano. Kwanini?

Nikajifunza kwamba Watanzania hawapendi maneno makali na ya jazba. Kumbe unaweza kupeleka ujumbe ule ule, lakini kwa maneno yenye busara na upole, ukaeleweka na kukubalika. Tunakumbuka jinsi CUF walivyokuja na maneno makali ya “jino kwa jino” na “ngangari”, mwishowe tunajua wananchi waliwanyima kura na kuwapa CCM ushindi mkubwa, huku CUF wakihusishwa na watu wa siasa kali na za shari. Mpaka leo wengi huamini hivyo!

Wapinzani wanapodiriki kusema tumuenzi Nyerere, tujiulize wao wanamuenzi kwa lipi? Yeye aliienzi sana amani na kutoa fikra na mitazamo yake huru katika vikao mbalimbali pasipo kuchochea vurugu ama kujenga uhasama. Baada ya kumaliza mijadala yake alisisitiza kwa kusema “kiongozi bora atatoka CCM.” Ni wazi kwamba alijua ni CCM pekee ndiyo waliodumisha na ndiyo watakaodumisha amani ya nchi hii. Na hapa tunatambua sasa kwanini Rais Jakaya Kikwete kachagua shabaha ya Chama na Serikali yake kuwa ni “Amani.” Na kwa hakika, ndiye anayeonesha kumuenzi Mwalimu Nyerere na fikra zake. Wapinzani kuleta vurugu, matusi, chuki na uhasama kamwe si kumuenzi Mwalimu. Ni nini basi, kama si maneno ya mkosaji tu!?

3. Dosari Kuu za Vyama vya Upinzani Kuchochea na Kushabikia Njia za Vurugu, Chuki na Uhasama wa Kisiasa

• Kutaka wananchi wakichukie Chama Cha Mapinduzi na Serikali yake.
• Kutaka waonewe huruma na umma (public sympathy) pale wanapovunja ama kukiuka sheria kwa makusudi na kuchukuliwa hatua. Mfano ni kuendesha mihadhara hata baada ya muda unaoruhusiwa kiusalama kupita; kufanya maandamano pasipo taarifa ili wazuiwe na kulalamika kuwa wanaonewa na dola, huku wakijua wamefanya makusudi; kusema uongo wowote Bungeni au hata nje ya Bunge ili wachukuliwe hatua na kuanza kulalama kwamba wanakandamizwa na CCM. Bahati mbaya sana kwamba baadhi ya wananchi hawafanyi utafiti na kisha kuamini kuwa Wapinzani wanaonewa na kuanza kuwahurumia bila kujua kwamba ni ghiliba. Hapo ndipo Wapinzani hujisikia wametimiza malengo ya fitina na uongo wao. Hata hivyo, punde ukweli hujulikana na kuwaacha wakiumbuka na kudharaulika.
• Kujifanya wao ni dawa ya matatizo yetu bila kuonesha kinagaubaga ni namna gani ama jinsi gani watayaondoa. Tunakumbuka jinsi Watanzania walivyowahi kuahidiwa kwa mbwembwe ahadi hewa ya umeme wa bei rahisi na matrekta. Ni ajabu kwamba leo bado wanathubutu kuikosoa Serikali bila soni!
• Kupenda umaarufu wa kusikika kwenye vyombo vya habari. Wapinzani wengi hujisikia raha sana kuonekana magazetini na kwenye runinga. Wandishi wa habari ni mashahidi wanavyobughudhiwa na kufokewa ikiwa hawajawaandika ama kuwaonesha kwenye runinga.
• Kutaka kukubalika kwa wananchi sehemu ambayo hawakubaliki. Hutunga uchonganishi na kutaja kila tatizo kuwa linatokana na CCM na Serikali yake. Nakumbuka siku moja Ibrahim Lipumba alipotea kwenye barabara inayounganisha wilaya za Kiteto na Kondoa. Hakuona kuwa ni kutokuwa makini kwa dereva wake, au Chama chake, kutoijua vizuri jiografia ya Kondoa na Kiteto. Bali akakurupuka na kusema ni matatizo ya CCM na Serikali yake hawajaweka kibao! Ndiyo maana hawajifunzi, maana wanajua wa kumsingizia.
• Tamaa ya kupenda madaraka na kupata utawala kwa njia za haraka kwa mgongo wa matatizo ya wananchi - bila kujihoji uwezo wao.
• Wapinzani wengi wana wivu mkubwa wa kuona CCM kinaendelea kutawala. Kero yao kubwa si matatizo ya wananchi, bali kuona CCM ikizidi kuimarika na kukubalika. Wengi wanatamani angalau hata siku moja tu waje kuingia ikulu kama marais - basi! Hawana kabisa mikakati ya kuwa karibu na wananchi na kujua shida zao. Si ajabu basi kuona kuwa huwatembelea wananchi wakati wa kampeni za uchaguzi tu. Wivu na uroho wa madaraka ndiyo ambao huwafanya wapandwe na hasira na jazba pindi wanaposhindwa kidemokrasia.

4. Chanzo cha Vyama vya Upinzani Kutumia Njia za Vurugu, Chuki na Uhasama wa Kisiasa

• Upofu wao wa kutotaka kwanza kuwatambua na kuwaelewa wananchi wanachotaka. Hupenda kusikilizwa wao pasipo kuwasikiliza wananchi.
• Tamaa, uroho na ubinafsi wa kupindukia wa kupenda madaraka na utukufu. Kuna kiongozi mmoja wa Upinzani aliniambia msukumo wake mkubwa wa kutaka awe Rais kwa gharama yoyote ni mbwembwe za misafara ya Rais. Akasema anahusudu sana Rais anavyopitishwa barabarani huku magari na watu wakimpisha njia nzima! Nikastaajabu na kubaki mdomo wazi! Ubinafsi ulioje!!
• Kukosa dira (vision) inayowalenga wananchi, kama ambavyo dira ya wazi ya CCM na SAN chini ya Rais Jakaya Kikwete ni “Maisha Bora kwa Kila Mtanzania.” Wapinzani wote dira na lengo lao ni kuiong’oa CCM - si kung’oa kero za wananchi. Huko hawaoni - wamekosa dira!
• Kutumia ajenda za matakwa ya mataifa ya nje. Wapinzani hujinasibisha sana na wafadhili wa nje na kueneza masuala ambayo asilani hayalengi chanzo cha kero zetu na namna ya kutatua. Kama ni demokrasia, hakuna chama chenye demokrasia kama CCM. Kama ni misingi ya kidemokrasia, hakuna nchi yenye demokrasia pana kama Tanzania. Tunakumbuka jinsi ambavyo Mwalimu Nyerere alivyopiga marufuku Machifu na watemi, na kisha kuwapa wananchi mamlaka ya kuamua mambo yao na kuchaguana bila ubaguzi. Kutaka kujipendekeza kwa Wafadhili ndiko kulikowaponza CHADEMA mwaka 2005 na kujikuta wakiwaacha wagombea Ubunge na Udiwani wakikosa hata nauli ya daladala. Wagombea hao walijikuta wakikwama kabisa huku Mwenyekiti wao akiambaa ambaa angani na Helikopta kwa gharama kubwa sana kwa siku moja.

Kama pesa wanazopewa Wapinzani na Wafadhili wangezitumia kuchangia ujenzi wa madarasi, kutengeneza madawati na kununua vitabu vya kiada, tungesema kweli wana uzalendo.
Kama wangechangia fedha hizo wapatazo kurekebisha miundombinu. Mathalani kuchonga barabara, tungesema wanajua shida za wananchi.

Kama wangetoa fedha wanazopewa na wafadhili kwa kuwapa mikopo midogo midogo vijana, tungesema kweli wanawajali na kuwa na uchungu nao.

Kama wangejenga zahanati kwa fedha wanazopewa na Wafadhili wao wa nje, tungesema kweli wana huruma na wagonjwa.

Kama wangewasadia wakulima kupata zana za kisasa na pembejeo za kilimo, tungesema kweli hawa wanajua sekta muhimu katika nchi hii.

Kama wangechimba visima vya maji kwa fedha wanazopewa na Wafadhili wao wa nje, tungesema kweli wanajua jinsi wanawake wanavyohangaika kutafuta maji kila siku.

Je, wananchi watakosea wakifikia hatua ya kuwaita walafi? Haingii akilini kushinda kulumbana tu na kuilalamikia CCM hata shida ambazo wanaweza kuzitatua. Kwa kuwa hawana uchungu na wananchi na nchi yetu wanaamua kuambaa ambaa angani kama tai kwa gharama kubwa. Wanang’ang’ania CCM ifanye hiki na kile kama vile nchi hii si yao! Kama wanaweza kuwa angani kwa masaa machache kwa milioni 10 kwa siku, kwanini hawaoni busara ya kutumia pesa hizo kusaidia yatima? Pamoja na hayo, bado wanataka kuleta vurugu, chuki na uhasama. Nawashauri wananchi kwa ujumla, tusiwachukie, bali tuwapuuze - na ikibidi tuwaelimishe na kuwakumbusha wajibu wao kwa nchi na Taifa lao kwa amani.

5. Hitimisho

Hivi karibuni Rais wetu Jakaya Mrisho Kikwete alipokuwa akihutubia wanafunzi wanaosoma Kampala, Uganda, baada ya kuhudhuria mkutano wa Wakuu wa Jumuiya ya Madola (CHOGM) alisema: “Tusizifikishe tofauti zetu za kisiasa kiasi cha kukosa usalama.”

Kabla ya kuuawa mnamo Januari 30, 1948, Mohandis Karamchand Ghandi, almaarufu kama Mahatma Ghandi, aliwahi kusema: “My business in life has been for the past 33 years to enlist the friendship of the whole of humanity by befriending mankind, irrespective of race, colour or creed." Kwa tafsiri rahisi alimaanisha: “Kazi yangu katika maisha kwa miaka 33 iliyopita, imekuwa ni kuandaa orodha ya urafiki na binadamu wote, kwa kuwafanya wawe marafiki bila kujali asili ya mtu, rangi au imani.”

Nawaasa wanasiasa wote na hususan kutoka Vyama vya Upinzani, tuache kabisa kupandikiza lugha za ukatili, vitendo vya ukatili na tabia za ukatili kwa watoto wetu, kwa vijana wetu na kwa wananchi wetu wote kwa ujumla. Sio utamaduni wetu!

“Urithi Mkuu wa Utamaduni Wetu Kisiasa ni Amani na Utengamano.” Tuuenzi!
 
Labda jamaa angemalizia kwa kutukumbushia CCM inamwenzi vipi Mwalimu Nyerere siku hizi. Kwa wizi na ufisadi?
 
. Mimi mwenyewe nakumbuka niliwahi kuasisi chama mwaka 2001 kilichoitwa HArakati za MAbadiliko SAhihi, kwa kifupi HAMASA. Katika harakati zetu za kujinadi tulijaribu kutumia maneno makali, lakini mwitikio wa wananchi ulituona ni wenye siasa kali na kuanza kutuogopa kila tupitapo na kutuona hatufai kabisa kuwa viongozi na watetezi wa utamaduni wa amani na utengamano. Kwanini?"


Nothing but a sour looser, huyu anahitaji ku-get a life maana CCM sasa hivi baada ya kina Mwakyembe haichukui mtu tena huko Mlimani,

Kitila mwambie huyu mkuu kuwa he is nothing but a looser tena big time, na it is sad kwamba anawaona baadhi ya waliowamwagia wengine tindikali kuwa wanamuenzi Mwalimu kwa amani, kuliko kina Zitto na Dr. slaa, wanaojaribu kumsaidia rais wa Jamhuri yetu rais Jakaya Mrisho Kikwete, kuwafichua mafisadi wa madini yetu mpaka kumfanya aunde kamati ya kuchunguza mikataba ya madini kwamba wanaharibu amani,

CCM huwa haitoi vyeo kutokana na low-IQ article kama yake, maana hata mimi CCM damu ninamuona ni mnafiki, na rais wetu amezungukwa na watu kama huyu kazi yao ni kumwambia kuwa kila kitu kiko sawa, sasa kama huyu naye ni Mwalimu huko Mlimani, sasa tutegemee nini kwenye GPA za watoto wetu huko?

Yaaani mweeee taifa hili, kila tunapofikiri tunapiga hatua 10 mbele, then wanatokea hawa kina Mwakatobe kutukumbusha kuwa bado kina Zitto na Dr. slaaa, wana kazi nzito sana ya kuendelea kutuamsha sisi wananchi!

Mungu Aubariki Upinzani Bongo, Can you Imagine Tusingekuwa Nao?
 
Sambamba na hili, lazima tutambue pia hata usemi wa Watanzania: maongezi yao, mahusiano yao na mawasiliano yao huashiria amani, upole na uungwana. Ni Watanzania pekee duniani kote ambao wakiingia dukani husema: "naomba sukari", "naomba chumvi," "naomba kiberiti," "naomba kipande cha sabuni" – utadhani anapewa bure. Kumbe analipia! Kuomba kitu unachotaka dukani ni lugha ya upole, uungwana na unyenyekivu. Ni ishara ya upendo - hata kama unalipia. Nchi zingine hutumia maneno makali kama: "leta hapa sukari!" "toa kiberiti!" "nipe haraka chumvi kilo moja!" Lugha ya ukali na amri si hulka ya Mtanzania

Huu mfano sidhani kama unajitosheleza , hata jambazi likishamlima mtu risasi na kumnyang'anya mtu pesa likienda kwenye baa bado litasema Naomba bia, sasa kwa mtu asiyelijua anaweza kufikiri ni liungwana kwa sababu ya lugha yake kumbe siyo

wahenga walisema uzuri wa mkakasi ndani kipande cha mti, hivi lugha tu yatosha kuonyesha uungwana wa mtu?
 
Huu mfano sidhani kama unajitosheleza , hata jambazi likishamlima mtu risasi na kumnyang'anya mtu pesa likienda kwenye baa bado litasema Naomba bia, sasa kwa mtu asiyelijua anaweza kufikiri ni liungwana kwa sababu ya lugha yake kumbe siyo

wahenga walisema uzuri wa mkakasi ndani kipande cha mti, hivi lugha tu yatosha kuonyesha uungwana wa mtu?


mimi nnaukumbuka msemo huu hivi

uzuri wa mkakasi ukiingia maji basi
 
Nothing but a sour loser, huyu anahitaji ku-get a life maana CCM sasa hivi baada ya kina Mwakyembe haichukui mtu tena huko Mlimani,

Kitila mwambie huyu mkuu kuwa he is nothing but a loser tena big time, na it is sad kwamba anawaona baadhi ya waliowamwagia wengine tindikali kuwa wanamuenzi Mwalimu kwa amani, kuliko kina Zitto na Dr. slaa, wanaojaribu kumsaidia rais wa Jamhuri yetu rais Jakaya Mrisho Kikwete, kuwafichua mafisadi wa madini yetu mpaka kumfanya aunde kamati ya kuchunguza mikataba ya madini kwamba wanaharibu amani,

CCM huwa haitoi vyeo kutokana na low-IQ article kama yake, maana hata mimi CCM damu ninamuona ni mnafiki, na rais wetu amezungukwa na watu kama huyu kazi yao ni kumwambia kuwa kila kitu kiko sawa, sasa kama huyu naye ni Mwalimu huko Mlimani, sasa tutegemee nini kwenye GPA za watoto wetu huko?

Yaaani mweeee taifa hili, kila tunapofikiri tunapiga hatua 10 mbele, then wanatokea hawa kina Mwakatobe kutukumbusha kuwa bado kina Zitto na Dr. slaaa, wana kazi nzito sana ya kuendelea kutuamsha sisi wananchi!

Mungu Aubariki Upinzani Bongo, Can you Imagine Tusingekuwa Nao?


Mkuu nakuhakikishia huyu sio mwalimu wa mlimani. Tena ni mbabaishaji kweli hadi anajiita "mchambuzi na mfuatiliaji wa siasa za kitaifa na kimataifa", sasa hicho cheo amejipa mwenyewe na hilo ni tatizo lake la kwanza. Huyu alikuwa mpinzani zamani na akaona wapinzania wote hawafai isipokuwa yeye, hivyo akaanzisha chama chake-alishindwa hata kupata wanachama 200 hadi chama chake kikashindwa kupata usajili wa kudumu na hivyo akaamua kujisogeza CCM. Kwa kweli kama ulivyosema ni looser hasa maana hata kuishi anaishi kwa kutegemea NGO fulani fake ambayo nasikia nayo imekatiwa ufadhili na wazungu baada ya kugundua utapeli wake. Wananchi sasa hivi wameshajua nani ni mpinzani na nani ni mbambaishaji, kwa hiyo pumba kama hizi alizoandika huyu ndugu kila mtu anaona ni yaleyale ya akina Tambwe ya kujiuza kwa CCM. Utaona siku chache CCM watamsogeza kwenye kitengo chao cha propaganda ili akakae na akina Tambwe na Akwilombe. Wameshagundua kwamba kuandika makala kwenye gazeti za kukandia upinzani ni mtaji wa kikubalika kwa CCM. No serious citizen in our country can take this crap seriously. Sasa nafikiri CCM na wenyewe ifike mahala waone kwamba kuwakubali watu kama huyu ni liability kwao.
 
"Basi, mtu akiwaambieni siku hizo: Kristo yuko hapa au Yuko pale, msimsadiki. Maana watatokea kina Kristo wa uongo na manabii wa uongo. Watafanya ishara kubwa na maajabu ya kuweza kuwapotosha ikiwezekana hata wateule wa Mungu. Sikilizeni, nimekwisha kuwaonya kabla ya wakati. Basi, wakiwaambieni, Tazameni, yuko jangwani, msiende huko; au, Tazameni, amejificha ndani, msisadiki; maana, kama vile umeme uangazavyo toka mashariki hadi magharibi, ndivyo kutakavyokuwa kuja kwake Mwana wa Mtu. Pale ulipo mzoga, ndipo watakapokusanyika tai." (Mathayo 24 mstari wa 23-28.)
 
Mkuu nakuhakikishia huyu sio mwalimu wa mlimani. Tena ni mbabaishaji kweli hadi anajiita "mchambuzi na mfuatiliaji wa siasa za kitaifa na kimataifa", sasa hicho cheo amejipa mwenyewe na hilo ni tatizo lake la kwanza. Huyu alikuwa mpinzani zamani na akaona wapinzania wote hawafai isipokuwa yeye, hivyo akaanzisha chama chake-alishindwa hata kupata wanachama 200 hadi chama chake kikashindwa kupata usajili wa kudumu na hivyo akaamua kujisogeza CCM. Kwa kweli kama ulivyosema ni looser hasa maana hata kuishi anaishi kwa kutegemea NGO fulani fake ambayo nasikia nayo imekatiwa ufadhili na wazungu baada ya kugundua utapeli wake. Wananchi sasa hivi wameshajua nani ni mpinzani na nani ni mbambaishaji, kwa hiyo pumba kama hizi alizoandika huyu ndugu kila mtu anaona ni yaleyale ya akina Tambwe ya kujiuza kwa CCM. Utaona siku chache CCM watamsogeza kwenye kitengo chao cha propaganda ili akakae na akina Tambwe na Akwilombe. Wameshagundua kwamba kuandika makala kwenye gazeti za kukandia upinzani ni mtaji wa kikubalika kwa CCM. No serious citizen in our country can take this crap seriously. Sasa nafikiri CCM na wenyewe ifike mahala waone kwamba kuwakubali watu kama huyu ni liability kwao.

Mbona hujajibu makala yake umebaki kumshambulia tu Mwalimu wako?

PM
 
Sio Mwalimu wao wa darasani pale mlimani bali ndiye Mwalimu wao wa Harakati. Aliwafundisha wakati wakiwa pamoja kwenye shirika moja lisilo la kiserikali.

PM

Kwi kwi kwi, Shirika moja lisilo la kiserikali...mambo ya per diem kumbe wengi ni wataalam.
 
Ndugu mheshimiwa Gwandumi Mwakatobe,

Hadithi ya mirathi ya tamaduni zetu kisiasa ni hadithi ndefu na inaweza tafsirika tofauti na jinsi unavyofikiria wewe. Binafsi kwanza sikubaliani na hoja yako unaposema:-
Awali ya yote, ni hekima kutambua kuwa Mwenyezi Mungu ametujalia mengi hapa Tanzania. Mojawapo ya majaliwa makubwa ni sisi sote kama Taifa kujikuta tumezaliwa eneo la kijiografia katika Afrika Mashariki ambalo watu waishio eneo hili ni watulivu, wapole, waungwana na wapenda amani

Yawezekan kabisa kuwa huo Utulivu, upole Uungwana na upenda amani ni ktk mfululuzo wa tafrisi ya UJINGA. Nasema Ujinga kwa sababu hizi ni dalili tosha kabisa za mtu mjinga ambaye elimu ya dunia ina mapana ya kuta nne zilizomzunguka na hawezi kuona nje ya hapo. Tumerithi mengi ambayo leo hii tunatakiwa sisi kukaa kitako na kupitia tena huu utamaduni tumerithi kwa faida ama ndio kubakia ktk ujuza na upotofu kifikra.

Kumbuka ni Tanzania hii wakati wa Mkoloni ndio pekee ilikuwa makao makuu ya UTUMWA. Waafrika tulibebwa kwa maelfu na kutumikishwa utumwa na hata kuenzi utumwa huo tusiweze inua mikono yetu kuukana hadi pale Umoja wa Mataifa ulipopiga marufuku. Tazama ramani ya utumwa Afrika mashariki utaona kweli nayoizungumzia.
Ni sababu hizo hizo zilizotufanya sisi tusiweze inua mokono yetu kupinga tawala za Kireno, Kijerumani hadi Utawala wa Muingereza alipopewa dhamana baada ya kumshinda Mjarumani vita kuu ya pili. Ajabu kubwa ni kwamba kati yetu sisi tulishika migobole kupigana tukiuunga mkono utawala dhalimu wa Hitler Mtawala wetu... Sidhani kama hiyo ilikuwa neema tukafananisha neema ya Uhuru wetu na nchi kama Kenya ambao walitawaliwa kwa mabavu. Labda niseme kuwa Uhuru wetu ndio ulipatikana kwa neema zake Mungu kwani baadaya ya Mjarumani kushindwa vita, Muingereza alikabidhiwa nchi hii kutawala hadi pale tutakapo kuwa tayari kudai UHURU huo tofauti na nchi nyinginezo laa sivyo nadhani hadi leo hii tungekuwa tukitawaliwa...
Hivyo basi neema hiyo imetuongezea ujinga wa kutofahamu ni wakati gani mtu hatakiwi kuendelea kukubali kutumikishwa kama mtumwa ktk nchi yake mwenyewe hata kama umetawaliwa.
Ni mirathi hii pekee ndiyo tunayoiendeleza ktk karne hii ya 21 ambapo watu wachache wanaweza kabisa kutumikisha taifa zima na tukashindwa kuyaona mabaya kutokana na udhaifu wetu kifikra. Kwa hiyo, Kutawaliwa kwetu toka Utumwa hadi leo na viongozi weusi sio neema ila ni UJINGA ulokomaa vichwani mwetu tukashindwa kufikiria nje ya kuta nne za kabati hili la Ujinga.
 
Mwakatobe,

Ni mpaka lini tutaendeleda kuwa wavumilivu wa kudhulumiwa haki zetu, mali zetu na urithi wetu?

Katiba yetu imetekwa na kikundi ambacho kinahakikisha kuwa kinakandamiza haki zetu kikatiba kwa kufanya maamuzi ya kitaifa na kikatiba kwa matakwa yao na si ya Taifa. Yanahujumu haki yetu kwa kukataa kuruhusu marekebisho ya katiba ambayo yatampa Mtanzania uhuru wa kujichagulia serikali bila woga, uhuru wa kuihakiki na kuiwajibisha Serikali na wawakilishi bila kutengwa na kubaguliwa kwa kunyimwa haki za msingi katika kuleta maendeleo yao ya kijamii.

Kikundi hiki kinatuhubiria tuwe wavumilivu kudumisha Amani, Mshikamano na Utulivu katika umasikini wa hali na mali, huku kikundi hiki kikijineemesha na kutajirika marudufu kwa kujitwalia hazina na mali asili kupitia mfumo huru wa Kibepari huku ukikandamiza kwa makusudi na ulafi wa matumbo na roho zao nguvu za wazawa kujumuika katika kujenga taifa na kuvuna mali asili.

Ni mpaka lini tuendelee kukubali na kuhalalisha kudhulumiwa ikiwa waliopewa dhamana kulinda katiba na mali yetu wameanza kutukandamiza na kutuburuza huku wao wakineemeka na kupindisha ukweli wa mambo kwa faida na manufaa yao?

Kila udhalimu na uhujumu una tamati. Tumejaribu kutumia njia za kiamani kama unavyoshauri na njia hizi hazifanyi kazi kutokana na ugumu wa mioyo ya hawa unaowatukuza na kutuasa tuwaachie waendelee kutuongoza katika umasikini, ujinga na unyonge wa kudumu.

Kama amani na majadiliano kuhusu vitu vya msingi vinaendelea kupuuziwa na majigambo kusema hatima ya maisha ya Mtanzania na haki zake za msingi ni hiari ya kikundi hiki na si haki na hiari ya Taifa, je unatarajia ni lini mnyonge atakubali kuendelea kuonewa na mbabe au mtemi wa mtaani?

Je unategemea mpaka lini tuendelee kumtii Kristo aliposema kuwa tumsamehe adui saba mara sabini au tumgeuzie shavu la kushoto baada ya kuzabwa kibao shavu la kulia?

Ni upotofu gani ulionao wewe na hiki kikundi unachokitukuza(Chama Cha Mapinduzi na uongozi wake), kuwa mkitumia vitisho vya yaliyotokea kwa majirani na awali katika kutafuta uhuru wetu kuwa tutaangamia huku tayari mnatuangamiza kwa kutunyanganya haki zetu za kuwa na maendeleo ya fikira, hali na mali?

Hivi kweli unataka kutuambia kuwa wewe na CCM mna nia nzuri kwa Taifa letu?

Sisi kama Taifa, tumechoka kudanganywa na kudhalilishwa. Kwa miaka 46 tumewapa yamini na dhamana CCM na waasisi wake kuwa watatuongoza kutoka unyonge wa kuwa tegemezi, unyonge wa fikira, umasikini wa hali na mali na kutuleta katika uwanja wa haki ambapo jitihada binafsi na za jumla zitatupa haki sawa hivyo kukamilisha imani yetu kuwa binadamu wote ni sawa.

Hivo basi, miaka 46 ya mazungumzo na kusubiri miujiza inafikia ukingoni, kitakachotokea iwe ni kumwaga damu, kupoteza maisha au kuingia katika ukimbizi na mahangaiko kutetea haki zetu za msingi ndio suluhisho kwa ajili ya watoto na wajukuu wetu, basi tutaachana na siasa za mezani na kuanza vurugu. Maana katika Amani tumeendelea kuwa masikini wa kutisha na kuendelea kudhulumiwa na watawala wetu tuliowachagua, basi kwa nini tuogope kumwagika damu au kuwa na mapinduzi kudai haki zetu? Kama umasikini, tunao, unyonge tunaishi nao.

Mwamuzi wa kuepusha "vurugu" si wale unaowalaumu na kuwaogopesha Wananchi, bali ni wale unaowatetea "CCM"!
 
Mh. Gwandumi Mwakatobe,

Nashukuru sana kwa waraka wako mrefu. Nimeusoma kwa makini na nikaona nami nichangie kidogo kwani jambo hili linanitatiza sana kama Mtanzania. Ningependa pia kukueleza wewe na wasomaji wengine kuwa mimi si mwanachama wa chama chochote cha siasa (iwe tawala au upinzani). Hivyo naamini mawazo yangu ni huru.

Umeanza waraka wako kwa kutoa ufafanuzi wa namna ya kufikia malengo ya kisiasa, hususan, utawala. Pia ulitoa mifano ya viongozi wetu wa jadi waliopigana na wakoloni. Mifano mizuri sana kwani ni ya ukweli. Lakini pia, mfano huu unakuchimbia kaburi wewe na hoja yako. Kina Mkwawa, Kinjikitile, Mirambo, Meli, Sina, etc waliingia katika vita hivi si kwa sababu waliwachukia tu wakoloni. Ilikuwa ni kwa sababu walichoshwa na unyonyaji na uonevu wa wakoloni na wakaona ni vema kujitetea wenyewe, hata kama ikiwa ni kwa vita. Ufanani wake na CCM na maovu yake ni mkubwa mno na wananchi kwa kweli tumechoshwa. Vita yetu tunaipigania ndani na nje ya Bunge kwa kutumia upinzani, na kwa wengine wasiopenda kujihusisha moja kwa moja na chama fulani cha siasa, wanapigana vita hii kwa kutumia kumbi kama JF. Wengine wanapigana vita kwa kukaidi maagizo ya serikali kama vile Wamachinga, wanafunzi na wafanyakazi wanaogoma n.k.

Umezungumzia non-violence method, iliyoasisiwa na mtu uliyemnukuu, Mahatma Ghandi. Nasi tunatumia non-violence method. Ni serikali, kwa kutumia vibaya vyombo vya dola, ndio inavunja hii method. Kumbuka mauaji ya Zanzibar, Mwembe Chai? Je ilikuwa ni wananchi au ni CCM kupitia serikali yake na dola kama FFU ambao walikuwa na silaha za moto na kisha kuua raia?

Naafikiana nawe kuwa chuki na uhasama vinaanzishwa na wanasiasa na vibaraka wao. Lakini si wanasiasa wote. Zaidi ni makosa ya wachache wenye madaraka huko CCM. Hata kama ukisema upinzani unashabikia, kumbuka, “it takes two to start a fight”. Wewe kama mfuatiliaji (nasikitika kukuambia kuwa uchambuzi wako ni extremely shallow and biased) utasema ni wapinzani. Lakini ujiulize, kwanini wapinzani wanasema haya yote? Unafikiri kama kusingekuwa na ufisadi Dr. Slaa angejitoa mhanga na kuyasema aliyoyasema hadharani? Je ni watanzania wangapi wangejua uozo wa BoT na mabilioni yetu yaliyohamishiwa kwenye mifuko ya wachache wanaochoma nyama na viongozi wa serikali ya CCM? Bw. Gwakisa, mbona hukemei haya maovu ya CCM ambayo yanawafanya watu wapate uchungu wa nchi yao na kutaka kutetea maslahi yao? Shindwa na ulegee!

Ningependa nijibu tuhuma zako ulizosema kuwa ni "Dosari Kuu za Vyama vya Upinzani Kuchochea na Kushabikia Njia za Vurugu, Chuki na Uhasama wa Kisiasa".
• Siamini kuwa wapinzani wanataka wananchi wakichukie Chama tawala. Mimi kama mwananchi naona unanitusi kwa kunifanya mjinga. Wanachokifanya wapinzani ni kuanika uozo wa CCM na kueleza ni namna gani wanatofautiana kiitikadi. Si chuki.
• Sisi watanzania sio wajinga kusema kuwa tutakula ndoano ya chama fulani ili tuwape public sympathy. Tanzania ni nchi huru, sioni kwanini serikali itawale muda na mahali ambapo watu wanataka kukusanyika kwa sababu yoyote ile. Hizo rasilimali zingetumika pengine katika kujenga taifa na sio kushadadia wapinzani wanasema nini. CCM ndio waongo wakubwa na wanafiki ndani na nje ya Bunge. Wanatumia hoja za nguvu na ubabe usio na msingi.
• Ni mangapi serikali ya CCM imekuwa ikiahidi tangu nchi ipate uhuru? Sahau ya nyuma saana, hivi haya mambo ya umeme unayoyazungumzia, neno moja tu kwako: RICHMOND
• Wapinzani wanataka kuwiana na serikali tawala katika kuwapa taarifa wananchi na sio kutafuta umaarufu. CCM iko kila mahali na wapambe wake kila kona. Hivi utajitetea vipi nikikumbusha mazungumzo baada ya habari? Wakati Mrema alipoondoka CCM, RTD (chombo cha umma) ilimtumia Paul Sozigwa (wakati huo hakuwa mwajiriwa wa RTD) kumpaka matope Mrema. Sasa nani anayependa umaarufu hapo?

Umeshutumu wapinzani kwa kutotumia ruzuku na fedha wanazopata kutoka kwa wafadhili kudumisha miradi na huduma kwa wananchi. Mbona CCM haifanyi hivi? Mbaya zaidi, CCM imeweka vibaraka wake kwenye serikali kuu ambao wananyadhifa zinazowaruhusu kuwa na access na fedha za umma na wanazitumbua kama ni zao vile na bila woga. Serikali, iwe ni ya CCM au ya chama kingine, ina wajibu wa kuwapatia wananchi miundombinu. Ndio maana tunalipa kodi. Hii miundombinu ni hizo barabara, umeme, simu, maji safi, shule, hospitali (achana na zahanati). CCM imekuwa madarakani tangu tumepata uhuru na mpaka sasa hakuna njia ya reli (ukiachilia ya Dodoma-Singida) ambayo ilijenga. Barabara ni mpaka kulamba kucha za wafadhili (na kutumia vibaya misaada), watu bado hawana maji safi wala umeme, tenda za kutengeneza barabara zinapewa wakandarasi wenye kuchangia vigogo wa CCM wakati hawana ujuzi au uwezo wa kutengeneza barabara za kudumu.

Hitimisho:
Sisemi kuwa wapinzani wote ni watakatifu au wote wana nia ya dhati ya kufanya mabadiliko, nitakuwa mwongo. Lakini, wengi wao wana kila sababu ya kuisimamia CCM rohoni. Hoja zao ni za msingi na wanatetea ambayo wananchi wengi wanataka. Mimi kama mwananchi, nimechoka na uongo, uozo, ubabe usio na msingi na ufisadi wa CCM. Japo wapinzani wanaweza wasiwe na kila jibu au suluhisho la matatizo yetu, lakini wanaonyesha kuwa na mabadiliko. Na hicho ndicho watanzania wengi kama mimi, tunachotaka. Kwa miaka karibu hamsini, tumekuwa tunasikia hekaya hizo hizo kila siku bila kuleta mabadiliko ya kunufaisha umma. Hekaya na maazimio bila vitendo ni sawa na kutwanga maji.

Ningependa tuendelee kutunza na kudumisha tamaduni zetu nzuri ulizozitaja kwani ndizo zimetufanya tuwe ni kisiwa cha amani. Hapo nakubaliana nawe. Lakini, kuna tamaduni mbaya kama vile kuwa watu tunaofanywa wajinga na itikadi za CCM zenye kutumia reverse psychology, ya kudai kuwa wapinzani ndio wabaya wenye kueneza ubaya wakati hayo yote ni ya CCM na yalianza kabla ya kuwa na vyama vingi.
 
"• Tumerithi nchi ambayo watu wake hawapendi vurugu.
• Tumerithi nchi ambayo watu wake hawapendi uchochezi wa chuki.
• Tumerithi nchi ambayo watu wake hawana hulka ya kujengeana uhasama.
• Tumerihti nchi ambayo watu wake hawapendi vita.
• Naam, tumerithi nchi ambayo inatukuza na kuenzi amani na utengamano."

Kuna Ukweli na Uongo-Tumerithi kudumaa.



"Sambamba na hili, lazima tutambue pia hata usemi wa Watanzania: maongezi yao, mahusiano yao na mawasiliano yao huashiria amani, upole na uungwana. Ni Watanzania pekee duniani kote ambao wakiingia dukani husema: “naomba sukari”, “naomba chumvi,” “naomba kiberiti,” “naomba kipande cha sabuni” – utadhani anapewa bure. Kumbe analipia! Kuomba kitu unachotaka dukani ni lugha ya upole, uungwana na unyenyekivu. Ni ishara ya upendo - hata kama unalipia. Nchi zingine hutumia maneno makali kama: “leta hapa sukari!” “toa kiberiti!” “nipe haraka chumvi kilo moja!” Lugha ya ukali na amri si hulka ya Mtanzania"

Hivi hayo hapo juu sio kwasabau za ukoloni? Yes Bwana, Naomba Bwana,Ndio Bwana!
 
Nakubaliana na wewe Kitila,huyu bwana ana matatizo na bahati nzuri sisi wajanja wa huku kyela tumeanza kumchukulia tahadhari.Hiyo makala tayari imeonyesha ni mtu wa aina gani haina haja ya kumjibu.
 
Tukubaliane kuwa ktk msafara wa mamba hata kenge huwepo ila ktk msafara wa kenge mamba ni rahisi kugundulika.....
 
Nakubaliana na wewe Kitila,huyu bwana ana matatizo na bahati nzuri sisi wajanja wa huku kyela tumeanza kumchukulia tahadhari.Hiyo makala tayari imeonyesha ni mtu wa aina gani haina haja ya kumjibu.

Thank you sir, na ubarikiwe!
 
Back
Top Bottom