PreGE2025 Waziri mkuu kwa kauli hii kuelekea taifa salama zaidi: Sasa ni muda tuwaamini viongozi wenye maarifa na weledi wa kiutendaji siyo umaarufu pekee

PreGE2025 Waziri mkuu kwa kauli hii kuelekea taifa salama zaidi: Sasa ni muda tuwaamini viongozi wenye maarifa na weledi wa kiutendaji siyo umaarufu pekee

Mijadala ya Uchaguzi Mkuu wa Tanzania 2025 (Kabla)

Rijali jandoni

JF-Expert Member
Joined
Apr 5, 2018
Posts
2,165
Reaction score
2,251
Katika kusikiliza hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ujumbe wake umebeba uzito mkubwa unaweza kugusa hali halisi ya sasa na maono ya nchi yetu kwa miaka ijayo. Kauli hiyo, yenye kina cha uongozi na uchambuzi wa mwenendo wa taifa, inapaswa kutazamwa kama mwanga unaoongoza katika vipindi tofauti vya kila kiongozi atakaepata dhamana ya kuongoza taifa hili, kwenye chama chochote, taasisi ama shirikisho ndani ya nchi yetu.

Kwa muktadha wa hali ya sasa duniani, tunashuhudia migogoro mingi inayoanzia kwenye ushawishi wa makundi yenye ajenda binafsi, pamoja na upungufu wa elimu ya usalama na amani miongoni mwa wananchi wa kawiada. Ujumbe huo nadhani unadokeza umuhimu wa kuwa na wananchi walioelimika na kutambua wajibu wao wa kulinda amani, kuongeza ushirikiano na serikali ilio pewa dhamana, maana hakuna kitendo kibaya kama kiongozi kuongoza wananchi wasio fuatilia au kuonesha ushirikiano na kauli, ajenda au malengo yanayo wasilishwa kwa wananchi hao.

Kwa mantiki hiyo, ni muhimu kila chama cha siasa nchini kijitahidi kuwa sehemu ya suluhisho, na sio chanzo cha matatizo. Tunapaswa kuhakikisha kuwa viongozi wanaoletwa mbele ya wananchi ni watu wenye weledi, uadilifu, na maono ya kweli yenye maendeleo juu ya nchi yetu. Ni viongozi wa aina hii tuu wanaweza kujenga uhusiano wa imani kati ya serikali na wananchi wake.

Tukiruhusu chaguzi ziongozwe na umaarufu badala ya uwezo, basi tutakuwa tunahatarisha msingi wa amani ya taifa letu. Ni wakati wa kuachana na siasa za majina na badala yake tuangalie uwezo wa mtu, falsafa yake ya uongozi, na mchango wake katika jamii kutokana na uwezo wake wa kufikiri na kutatua mambo tofauti.

Maumivu ya wananchi wengi mara nyingi hutokana na kujisikia wamesahaulika na wale waliowahi kuwaahidi matumaini. Kukosekana kwa mshikamano baina ya viongozi na raia kunazua upweke wa kihisia unaoweza kuwa chanzo cha machafuko kimyakimya. Ni wajibu wa kila kiongozi kurudi kwa wananchi na kushiriki nao katika kujenga taifa.

Naamini Tanzania ina hazina kubwa ya viongozi vijana, kwa wazee wenye weledi na maadili. Tukiwapa nafasi, watakuwa nguzo ya maendeleo ya kweli.

Watanzania ni watu wanaoipenda nchi yao kwa dhati. Tusijaribu kuwapa hali ya upweke au kutothamini mchango wao. Mwananchi mnyonge, asiye na sauti, ni rahisi sana kushawishika na mtu mwenye nia mbaya juu ya nchi yetu. Tukumbuke kwamba utulivu wa kweli hujengwa kwa ushirikishwaji wa wazi kwa wananchi.

Naomba katika kipindi hiki, kila chama cha siasa na taasisi ya kijamii irudishe imani kwa wananchi kwa kusimamisha watu waadilifu, wenye weledi, na wenye moyo wa kweli wa kulinda na kuendeleza taifa letu.

Mungu Ibariki Tanzania.
 
Back
Top Bottom