neema shamuhenya
JF-Expert Member
- May 24, 2018
- 312
- 216
WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amewataka madiwani wa Halmashauri ya Manispaa ya Tabora wajiondoe katika kufanya biashara na halmashauri hiyo kwa kuwa wanakiuka maadili ya utumishi wa umma.
Ametoa agizo hilo wakati anazungumza na watumishi wa ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Manispaa ya Tabora na Hospitali ya Rufaa ya Kitete katika ukumbi wa Isike Mwanakiyungi.
“Madiwani mjiondoe kuwa wasimamizi wa kampuni zinazozofanyakazi na halmashauri yenu na wakuu wa idara nanyi muwe makini mfanye kazi na kampuni huru ili muweze kuchukua hatua pale linapotokea tatizo,” amesema.
“Nyie madiwani ndio mnaopaswa kuisimamia halmashauri, sasa kama watu mliopewa dhamana mkiingia katika kufanya shughuli nyingine mnawakwaza wakuu wa idara na kuharibu mambo. Fanyeni kazi yenu ya kuisimamia halmashauri kwa mujibu wa dhamana mliyopewa.” amesema Waziri Mkuu.
Ametoa mfano wa mradi wa ununuzi malori mawili na makontena 20 ya kukusanyia taka mitaani ya Manispaa hiyo na kampuni inayomilikiwa na diwani ilipewa zabuni ya kununua vifaa hivyo, ambapo ilikabidhi lori moja likiwa bovu na kukataliwa.
“Yeye akaenda kulipaka rangi na kuwaletea, walilikataa tena,” alieleza.
Aidha, Waziri Mkuu amemuagiza Katibu Tawala wa Mkoa, Msalika Makungu aifanyie uchunguzi ofisi ya Mweka Hazina wa Halmashauri ya Manispaa ya Tabora baada ya kuwepo kwa utafunaji wa fedha za umma kwa visingizio mbalimbali.
Amesema zaidi ya Sh milioni 12.4 zimelipwa na Mweka Hazina wa halmashauri ya manispaa hiyo, Abbas Mwanzori kwa ajili ya malipo ya wahasibu waliofanya kazi muda wa ziada na watumishi, huku kukiwa hakuna fomu zilizojazwa na watumishi hao.
“Hatuwezi kwenda mbele tukiwa na watu wa namna hii. Halmashauri haiwezi kuendelea mtu anatumia vibaya ofisi kwa manufaa yake binafsi. Na kati ya fedha hizo sh. milioni 8.4 mlizitoa kwa kutumia ‘password’ ya Halima (Mhasibu) bila ya kumjulisha na alipogundua akahoji mkamuhamishia sokoni, Naagiza arudishwe mara moja,” alisema.