Waziri Kivuli Ester Thomas: Maji ni Mtego wa Umasikini

ACT Wazalendo

JF-Expert Member
May 5, 2014
605
1,536
HOTUBA YA MSEMAJI WA SEKTA YA MAJI NA MZINGIRA NDUGU ESTER A. THOMAS KUHUSU BAJETI YA WIZARA YA MAJI KWA MWAKA WA FEDHA 2022-2023.

UTANGULIZI:

Jana jumatano tarehe 12 Mei 2022, Waziri wa Maji, Mhe. Jumaa Hamidu Aweso aliwasilisha katika Bunge la Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania makadirio ya mapato na matumizi ya fedha ya Wizara ya Maji kwa mwaka wa fedha 2022/23.

Katika mwaka huu wa fedha Serikali, aliomba Bunge liidhinishe jumla ya shilingi bilioni 709. 361 kwa Wizara ya Maji. Kati ya fedha hizo, kwa ajili ya maendeleo zimetengwa shilingi bilioni 657.889 na fedha za matumizi ya kawaida ni shilingi bilioni 57.462.

Pamoja na makadirio ya mapato na matumizi, Hotuba ya wizara ya maji hutazama maeneo ya hali ya sekta ya maji (upatikanaji wa maji safi na salama mijini na vijijini, ubora wa maji na hali ya rasilimali ya maji), Utekelezaji wa bajeti kwa mwaka wa fedha uliopita na vipaumbele na mpango wa utekelezaji kwa mwaka huu.

Sisi ACT Wazalendo kupitia Msemaji wa Sekta ya Maji na Mazingira tumeifuatilia hotuba ya wizara na kuisoma ili kuweza kuitazama kwa kiasi gani imeweza kubeba matarajio au kutatua changamoto katika sekta hii nyeti kwa maisha ya wananchi. Pia, huu ni mwendelezo wetu wa kuzichambua hotuba za bajeti za wizara zote na kutoa mtazamo mbadala wa bajeti na vipaumbele.
Katika uchambua wetu wa hotuba ya bajeti, tumeona tuangazie maeneo nane (8) kutoka kwenye hotuba ya baj ya wizara kwa mwaka wa fedha 2022/23.

1. Maji ni Mtego wa Umasikini wa Watanzania:

Asilimia 80% ya watanzania wanaokadiriwa wanaishi vijijini, licha ya idadi kubwa ya watu kuonekana wanaishi vijijini na mchango wao katika pato la taifa kupitia shughuli za kilimo, uvuvi, madini na mazao ya misitu. Hali ya upatikanaji wa huduma za maji safi na salama ni asilimia 74.5. Ijapokuwa asilimia hizo zinatajwa kwa matumaini, uhalisia unaonyesha kuwa kutokana na kutofanyika kwa ukarabati na uwekezaji mdogo kati ya miradi ya maji iliyowekezwa vijijini takribani asilimia 30, haifanyi kazi kwa ufanisi au imekoma kabisa kutoa huduma ya maji. Mwenendo wa upatikanaji wa maji vijijini upo nyuma ya maelengo ya muda wa kati ambayo yanasema kufikia asilimia 80 ya wananchi vijijini watapata huduma ya maji ifikapo 2020 na sasa tupo 2022 huku bado tukiwa kwenye asilimia 74.5 tu.

Changamoto ya upatikanaji wa Maji inachangia sana kuwashikilia watu wa vijijini kwenye dimbwi la umasikini. Gharama za maji wanazotumiwa wananchi ili waweze kuishi ni kubwa mno maeneo ya vijijini kiasi kwamba zinazidi wastani wa pato la mtu mmoja (per capital income) kwa siku nchini Tanzania.
Kwa mujibu wa ripoti ya Hali ya Uchumi ya Taifa ya Juni 2021, “Pato la Taifa mwaka 2020 lilikuwa shilingi trilioni 148.5, huku idadi ya watu Tanzania Bara ilikadiriwa kuwa watu milioni 55.9 mwaka 2016. Hivyo, Pato la wastani la kila mtu lilikuwa shilingi 2,653,790 mwaka 2020.”

Kwa kipato hicho, nitatoa mfano wa Kijiji cha Gehandu huko Hanang, mkoani Manyara ambako mwananchi ananunua maji pipa moja la lita 200 kwa shilingi 7000 na familia moja inahitaji angalau pipa moja kwa siku kwa matumizi ya kujibana kabisa ya maji. Kwa hiyo mwananchi huyu atahitaji takribani shilingi milioni 2.5 kwa mwaka kwa ajili ya Maji tu ya kutumia yeye na familia yake. Kwa familia ya Watu 6, huu ni wastani wa 16% ya kipato cha kila mwanafamilia hata mtoto mdogo wa siku 1 kutumika kununua Maji.

Hivyo familia moja inatumia wastani wa kipato cha mtu mmoja kwa mwaka kwa ajili ya Maji tu. Lazima familia hii iendelee kushikwa kwenye mtego wa umasikini. Zaidi muda unaotumika kutafuta haya maji ni mkubwa sana, na hupatikana kwa mateso ya kubeba maji haya kwa kutumia Wanyama kama punda, lakini maji yenyewe yakiwa ni chanzo cha maradhi kwa kuwa si safi na salama.

ACT Wazalendo tunaamini Tanzania tunao uwezo wa kuondoa kabisa hali hii ikiwa Wizara hii yam aji itapewa Bajeti ya kutosha kutekeleza miradi ya maji, itaongeza umakini na ufanisi kwenye usimamizi wa miradi hiyo na kuhakikisha inazalisha kiwango cha juu cha maji kama ilivyokusudiwa, Pamoja na kuondoa upotevu wa mapato kwenye usimamizi wa miradi husika Pamoja na uendeshaji wa mamlaka za maji nchini.

2. Wizara Imeshindwa Kusimamia Miradi:

Kwa miaka mitatu sasa, tangu mwaka wa fedha 2018/19 mahitaji ya maji kwa umma yanaongezeka kwa 7% kila mwaka, lakini uzalishaji wetu wa maji unaongezeka kwa 2% kwa mwaka. Sababu kubwa ya uzalishaji kuwa chini sana tofauti na uhitaji, ni uwezo mdogo wa Wizara ya Maji kusimamia miradi mbalimbali ya maji, jambo linalochangia miradi mimgi ya maji kutotoa maji kabisa ama kuzalisha kiwango kidogo cha maji.

Kwa mwaka wa fedha wa 2020/21 uzalishaji wa maji nchini ni 56% tu ya uhitaji wa maji wa wananchi, hivyo kupelekea wananchi kutumia muda mwingi na gharama kubwa kutafuta maji.

Rai ya ACT Wazalendo ni kuitaka Wizara ya Maji kuongeza umakini na ufanisi kwenye usimamizi wa miradi ya maji nchini, jambo ambalo kwa sasa halipo, ili kuhakikisha miradi ya maji inazalisha maji kwa kiwango kikubwa Zaidi kuliko ilivyo sasa.

3. Bajeti ya Maji ya finyu, mahitaji yetu ni makubwa sana:

Kuna msemo usemao kuwa‚“maji ni uhai hii inamaanisha kuwa hupatikanaji wa maji safi na salama ni huduma muhimu kwa binadammu na maendeleo ya jamii kwa ujumla.
Kutokana na Tamko namba 64 la umoja wa mataifa la mwaka 2010 maji na usafi wa mazingira imekua ni moja za ya haki za msingi za binadamu na ni Lengo namba sita la malengo endelevu ya umoja waa mataifa ya mwaka 2015-2030.

Katika mwaka huu wa fedha Serikali imeliomba Bunge liidhinishe jumla ya shilingi bilioni 709. 361 kwa ajili ya wizara ya maji. Kati ya fedha hizo, kwa ajili ya miradi ya maendeleo zimetengwa shilingi bilioni 657.889 na fedha za matumizi ya kawaida ni shilingi bilioni 57.462. Kwanza, kwa kuilingalisha na bajeti ya mwaka huu na mwaka uliopita 2021/22 bajeti hii ni pungufu kiasi cha shilingi bilioni 110.381 sawa na asilimia 13.46 ya kuporomoka. Pili, bajeti hii ya maji haiendani na mahitaji halisi ya maji nchini kwetu.

Takwimu zinaonyesha wastani wa uwezo wetu wa kuwekeza kwenye miradi ya maji ili kukabiliana na mahitaji ya maji kwa kila mwaka wa fedha ni wastani wa asilimia 2.2 huku mahitaji ya maji yanaongezeka kwa wastani wa asilimia 7 kila mwaka. Mwenendo huu wa bajeti, utachukua miaka mingi zaidi ili kukabiliana na changamoto za sasa za upatikanaji na usambazaji wa maji mijini na vijijini. Mathalani miradi minne ya mkakati ya ujenzi wa mabwawa ya maji ya Kidunda, Farkwa, Lugoda na Songwe ili iweze kukamilika inahitaji kutengewa bajeti.

Ili kuendana na kasi hiyo ACT Wazalendo katika Ilani ya Uchaguzi, tulisema tutawekeza shilingi trilioni 2 kila mwaka, kwa miaka mitano mfululizo (kwa jumla ya shilingi trilioni 10) ili kumaliza kabisa matatizo ya maji nchini.

4. Ubadhirifu mkubwa katika miradi ya Maji, unalitafuna taifa:

Kumekua na wimbi kubwa sana la ubadhillifu wa feddha ya miradi ya maji inayopelekea uucheleweshwaji wa upatikanaji wa maji katika maeneo husika hili linadhibitiswa na ripoti ya mkaguzi wa hesabu za serikali CAG za mwaka 2021 inaeleyz kuwa kumekuwa na ucheleweshwaji wa utekelezaji wa miradi ya maji safi na usafi wa mazingira wa kiasi wa shilingi bilioni 37.1 na dola za kimarekani 6.05 ambao ulikua na malengo mbalimbali ya kuwezesha maji yanapatikana sehemu husika.
ACT Wazalendo inaitaka serikali kuwawajibisha wakandarasi, watendaji na watumishi wote waliohusika na uzembe huu.

5. Ucheleweshwaji wa Miradi ya Maji Vijijini:

Katika hotuba za waziri wa maji za kila mwaka zinaishia kutaja orodha ndefu ya miradi iliyotekelezwa lakini kila mwaka inatajwa miradi ambayo ukamilishwaji wake unachukua wastani miaka mitatu hadi kumi. Ucheleweshaji wa Miradi uligharimu taifa kifedha na upotevu wa nguvu kazi (kijamii).

Hali ya ucheleweshwaji wa miradhi unathibitishwa na Mkaguzi na mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa hesbau za Serikali. CAG anabainisha kuwza kuchelewa kukamilika kwa mradi wa maji wenye thamani ya shilingi bilioni 7.49 kutokana na vurugu za wanancchi mfanonkijiji cha Bacho wilayani Babbati chini ya mradi wa mamlaka ya maji na usafi wa mazingira Dareda (Dareda WSSA) ambayo illivunjwa na kuundwa BAWASA mnamo mwaka 2019.

Miradi iliyocheleweshwa sana kama inavyotajwa na CAG ni Mradi wa ujenzi wa mtambo wa kusafisha maji Jijini Dar es Salaam kando ya Bonde la Msimbazi. Pili, Mradi wa mtandao wa majitaka katika Manispaa ya Musoma wenye thamani ya shilingi bilioni 27.6 kwa muda wa miezi 18 uliopaswa kukamilika mwezi Juni 2021 chini ya ufadhili wa Wizara ya Maji. Vilvile, Mradi wa upanuzi wa mtandao wa majitaka wenye thamani ya shilingi bilioni 2 kwa kipindi cha miezi 12 uliopangwa kukamilika tarehe 11 Agosti 2021; lakini hadi wakati wa ukaguzi Oktoba 2021 ni asilimia 65 tu ya mradi ilikuwa imetekelezwa na muda uliongezwa hadi mwezi Desemba 2021. Pia, Kuna mradi wa kuboresha huduma ya maji katika vitongoji vya Dareda, Singu, Dagailoy, Sigino, na Bagara wenye thamani ya shilingi bilioni 7.5, ambapo kufikia tarehe 30 Juni 2021 kiasi cha shilingi milioni 105 kilikuwa kimelipwa.

Mfano mwingine mzuri ni ucheleswaji wa ukamilifu wa mradi wa maji wa Same—Mwanga—Korogwe ambao umechelewa takribani kwa miaka nane sasa toka uanze kutekelezwa
Kumekuwa na ahadi zaa kisiasa kila mmwaka wa uchaguzi toka kipindi cha Kikwete mpaka sasa mama Samiaa mradi huu badou na sitofahamu ya kumalizika na watu kupata maji. Kumekua na ukamilifu wa miradi baadhi pia ila hakuna usambazaji wa maji hili limekua ttatizo kwenye baadhi ya maeneo, unakuta kil akitu kimekamilika lakini maji hayatoki. Au watu kukosa maji kwa muda mrefu bila sababu zozotee za msingi.

6. Upotevu wa maji katika miji mikuu ya mikoa, wilaya, miji midogo na miradi ya kitaifa- wenye thamani ya Shilingi bilioni 332.59 :

Pamoja kuwa na uwezo mdogo wa ujenzi na usambazaji wa huduma za maji kwa wananchi, bado uendeshaji wa huduma za maji unakabiliwa na changamoto ya upotevu wa maji. Kwa mujibu wa takwimu za wizara ya maji, kiasi cha maji yanayopotea yamefikia asilimia 36 kwa ngazi ya kitaifa, huku Dar es Salaam kiwango cha upotevu ni wastani wa asilimia 47 kwa mwaka.

Kwa sehemu kubwa upotevu wa maji, kunasababishwa na ubovu wa miundombinu ya usambazaji wa maji miji.

Thamani ya upotevu huu kwa baadhi ya miradi iliyokaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa hesabu za Serikali inafikia bilioni 157 kwa mwaka wa fedha 2019/20 na shilingi bilioni 175 kwa mwaka wa fedha 2020/21. CAG anasema kuwa ‘Kama upotevu wa maji hautadhibitiwa, mamlaka za maji safi na usafi wa mazingira zitaendelea kupata hasara na hivyo kupunguza tija na ufanisi katika utoaji wa huduma za maji“
ACT Wazalendo tunaitaka serikali kufanya ukaguzi na ukarabati wa miundombinu ya maji kama vile, mita, mabomba, matanki,kuzuia upotevu wa maji na pia kuhakikisha upatikanaji wa maji kwa wananchi unafika kwa wakati. Pia, Bajeti ya ukarabati na ujenzi wa miundombinu bora zaidi inapaswa kutengwa ili kuzuia gharama tunazozipata kutokana na upotevu wa maji.

7. Udhibiti mdogo wa uchafuzi wa vyanzo vya Maji

Serikali kupitia wizara ya maji kama msimamizi mkuu wa uzingatiaji na utekelezaji wa Sheria ya Usimamizi wa maji limeonyesha udhaifu mkubwa sana kushughulikia changamoto za uchafuzi unaofanywa kwenye miradi ya viwanda, migodi, mabomba ya mafuta, mitambo ya gesi na mafuta, mitambo ya nishati za umeme, maghala ya kemikali na vyombo vya usafiri katika kuteririsha majitaka kwenye vyanzo vya maji. Tunakumbuka kwa siku za hivi karibu uchafuzi uliofanyika kwenye vyanzo vya maji katika Mto Mara hadi leo serikali haijachukua hatua Madhubuti kuwawajibisha wahusika wa uchafuzi mto badala yake imekuja na taarifa za mkanganyiko kwa wananchi.

Bado matukio ya utiririshwaji wa kemikali kwenye vyanzo vya maji, uharibifu wa ardhi uoevu na uchafuzi wa maji ya ardhi ni kubwa sana. Kupitia hotuba ya bajeti ya mwaka huu serikali haijaja na hatua za kuchukuliwa kukabiliana na changamoto hizi.

8. Mifumo mibovu ya Uondoaji Majitaka ni kero kubwa katika miji yetu:

Huduma ya usafi na mazingira ni muhimu katika kuhakikisha wananchi wanaishi katika mazingira bora na kuepusha maradhi yanayoweza kusababishwa na uwepo wa majitaka katika mazingira yetu. Ili kuweza kuondokana na milipuko ya magonjwa kama vile magonjwa ya matumbo na kipindupindu Mamlaka za maji safi na usafi wa mazingira zinalazimika kutoa huduma za usafi wa mazingira pamoja na kuhakikisha matibabu salama na utupaji wa majitaka katika maeneo yao ya huduma angalau kufika asilimia 40.
Hali ya sasa kwenye miji yetu, inatia shaka sana, kuna miundombinu mibovu ya kuweza kuondosha majitaka. Ni jambo la kawaida kukuta majitaka yanatiririshwa mitaani, mitaro kutofunikwa, uvujaji wa mitaro na matenki ya majitaka. Kwa takwimu zilizopo uwezo wa uondoshaji wa majitaka ni kwa sasa ni asilimia 13.5 kwa mwaka 2022, wakati mwaka jana ilikuwa asilimia 13 tu, ikishuka kutoka 2020 kutoka asilimia 15. Kiwango kinachokubalika na kilichopangwa kufikiwa ni asilimia 40 ya undoshaji wa maji taka.

Mfumo wa sasa wa uondoaji wa maji taka kwa kubeba na magari ya bowser sio mfumo salama kabisa. Hakuna miundombinu imara iliyojengwa kwajili ya kuondokana na changamoto ya majitaka kusambaa mitaani na kusababisha milipuko ya magonjwa.

Kwa namna hali ilivyokuwa mbaya, ipo haja ya kuwa na udhibiti na usimamizi mzuri wa mifumo yetu ya taka lakini Serikali haijafanya juhudi za kutosha kuwekeza kwenye kujenga miundombinu ya kuondoa majitaka majumbani, sehemu za taasisi za serikali.
Tafiti zinaonyesha ili kupata ufanisi katika usimamizi wa mifumo ya ukusanyaji wa taka kunahitaji bajeti ya kutosha, bajeti ya Serikali ya mwaka huu iliyotengwa kwa ajili ya usimamizi wa mifumo ya taka ni finyu sana.

ACT Wazalendo tunaendelea kusisitiza kuwa wizara ifanye jitihada kusimamia mamlaka za maji safi na usafi wa mazingira nchini ziweze kukamilisha na kuanza ujenzi wa miundombinu.

HITIMISHO:
Mwisho kabisa, hali ya upatikanaji wa huduma za maji safi na usafi wa mazingira unachora mstari mkubwa wa usawa wa kimaendeleo uliopo kati ya miji na vijiji, Hali ya namna hii inaendelea kubebwa na Hotuba ya bajeti kwa mwaka wa fedha 2022/23. Kwa takribani miaka 61 ya uhuru wa nchi yetu wanakijiji zaidi ya asilimia thelathini hawajawahi kuona maji ya bomba na kuyatumia, ni jambo linaloonyesha hawajanufaika na matundu ya uhuru wa nchi yao. Ili kuweza kuwaondoa wananchi kwenye unyonge na manungúniko haya hatuhitaji kuwa nambwembwe nyingi bali vitendo. Vitendo ni kutenga fedha za kutosha.

Ndg. Esther Akoth Thomas
Msemaji wa Sekta ya Maji - ACT Wazalendo
13 Mei 2022
 
Hata Zitto alishasema, water is a povert trap! kwanini unarudia? waambieni serikali si niwashirika wao.
 
Back
Top Bottom