Wazazi hospitali kubwa walala ‘mzungu wa nne’ wodini

asakuta same

JF-Expert Member
Mar 1, 2011
14,835
0
wodini.jpg

Wakimama wakiwa wamelala zaidi ya mmoja kwenye kitanda katika hospitali ya Amana jijini Dar es Salaam.Picha na Maktaba

HALI si shwari kwenye wodi za wazazi katika hospitali karibu zote kubwa nchini baada ya kubainika kuwa wagonjwa wanalala kati ya wawili na watatu (maarufu kama mzungu wa nne), kwenye kitanda kimoja na wengine sakafuni wakisubiri kujifungua.

Uchunguzi uliofanywa na Mwananchi katika baadhi ya hospitali za rufaa na baadhi ya hospitali za mikoa, umebaini kuwa kama hali hiyo haitashughulikiwa haraka, kuna hatari ya wazazi hao na vichanga vyao, kuambukizana magonjwa.
Hospitali hizo ni Muhimbili, KCMC (Moshi), Bombo (Tanga), Hospitali za Mikoa ya Morogoro, Dodoma, Mwananyamala, Temeke na Amana za Dar es Salaam.

Hospitali zilizopo Dar es Salaam
Mgonjwa Zawadi Salehe aliyelazwa Wodi namba 38 Muhimbili, alisema siku ya kwanza alilazwa kwenye kitanda kilichokuwa na mgonjwa mwingine na baada ya kujifungua kwa upasuaji, alitakiwa kulala sakafuni ili kupisha kitanda kitumiwe na wagonjwa wengine.“Ukifika (wodini) unapelekwa kwenye kitanda ambacho tayari kina mgonjwa. Inapofika siku ya Jumanne na Jumapili wanaletwa wagonjwa wengi zaidi ambao wamepewa rufaa ya kuja hapa. Wakishaingia, sisi ambao tulikuwapo tunaambiwa na wauguzi tulale chini ambako godoro moja wanalala watu watatu na wanaokosa nafasi kwenye godoro wanatandika kanga zao na kulala sakafuni.”Ofisa Habari wa Hospitali hiyo, Aminieli Aligaesha alikiri kuwapo kwa tatizo hilo na kueleza kuwa inatokana na uhaba wa nafasi wodini na siyo vitanda. Alisema Muhimbili inapokea zaidi ya wagonjwa 70 kila wodi.“Kila wodi ina vitanda 26. Wagonjwa wanapozidi huwezi kuwarudisha nyumbani. Kutokana na ukosefu wa vitanda hulazimika kuwalaza chini kwenye magodoro huku tiba ikiendelea.”

Kwa upande wake, Mganga Mkuu wa Amana, Dk Meshack Shimwela alisema kwamba wodi ya wazazi katika hospitali hiyo inapokea wagonjwa wengi, lakini wengi wao hawana matatizo makubwa na walipaswa kwenda katika vituo vya afya.

“Hii ni Hospitali ya Rufaa, tunapokea wagonjwa wenye matatizo makubwa tu hivyo wagonjwa wanaojifungua kwa njia ya kawaida wanatakiwa waende katika vituo vya afya vilivyopo katika maeneo yao, lakini utakuta kila mgonjwa anakimbilia hapa ndiyo maana kuna huu msongamano wa mkubwa,” alisema Dk Shimwela.

Katika Hospitali ya Mwananyamala, mgonjwa Elizabeth Mgimwa alisema: “Kwenye wodi hii ya wazazi kinachoangaliwa ni hela, kama hauna huyo mzazi atatukanwa na nesi na hata huduma muhimu hatapatiwa kwa wakati.”Katibu wa Afya katika Hospitali hiyo, Edwin Bisakala alikiri kupata taarifa za baadhi ya wagonjwa kutoa fedha kwa wauguzi lakini akaeleza kuwa malipo hayo hutolewa kama asante. Hata hivyo alisema: “Tunataka mama ambaye ameombwa fedha atoe ushirikiano kwenye uongozi wa hospitali kwa kuwa haitakiwi mgonjwa kutoa asante. Hawa wauguzi wameajiriwa kwa kazi hiyo.”

Hospitali ya Mkoa Dodoma
Wajawazito katika Hospitali ya Mkoa wa Dodoma wanalalamikia kile wanachokiita manyanyaso kutoka kwa wauguzi wa wodi ya wazazi, huku baadhi wakielezea kitendo cha kulazwa sakafuni kuwa ni kero.Akizungumzia malalamiko hayo, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dk Ezekiel Mpuya alisema uongozi una tabia ya kuwaita wauguzi wanaolalamikiwa na wagonjwa kisha kuwaonya. “Kwa sasa malalamiko ya kunyanyaswa wajawazito kwa kiasi kikubwa yamepungua baada ya uongozi kuanza kumshughulikia mtu mmoja baada ya mwingine,” alisema. Mmoja wa wazazi ambaye aliomba jina lake lihifadhiwe, alisema japokuwa huduma ni nzuri, baadhi ya wauguzi wamekuwa na kauli chafu kwa wagonjwa.

Zanzibar
Tatizo lililopo katika Hospitali ya Rufaa ya Mnazi Mmoja ni ufinyu wa nafasi katika wodi za wajawazito na wazazi kiasi cha kufanya baadhi ya wagonjwa kulala wawili hadi watatu kitandani.Katibu Msaidizi wa Hospitali hiyo, Mohammed Nadi alikiri kuwapo kwa tatizo hilo na kueleza kuwa wagonjwa hupunguzwa kwa kupelekwa vituo vya Afya Makunduchi, Fuoni, Kivunge na Mwemberadu.“Nakala za barua tulizoandikia Mamlaka ya Mji MKongwe zipo na ramani ya jengo lililosudiwa kujengwa, ili kukabiliana na ufinyu wa nafasi hospitalini vipo. Lakini tumekwama kwa kuwa sheria hairuhusu kujengwa chochote kwenye mji,” alisema Nadi.

Bombo, Tanga
Mbali na wajawazito kulala kati ya wawili hadi watatu, wengine wanalazimika kujifungulia sakafuni kutokana na idadi ya vitanda kwenye chumba cha kujifungulia katika hospitali hiyo kuwa sita pekee.
“Ni jambo la kuhuzunisha. Mjamzito mwenye uchungu unahangaika kwa sababu ya uchungu katika kitanda tena si kikubwa mmelala wawili, si mateso mengine haya?” alisema Mkazi wa Kilulu, Mwamvua Hassan muda mfupi baada ya kujifungua.

Morogoro
Kina mama waliojifungua katika Hospitali ya Mkoa wa Morogoro walisema wamekuwa wakilazwa wawili kwenye kitanda kimoja na baadhi yao sakafuni.Mmoja wao, Rebecca Michael alisema kunahitajika jitihada za makusudi kuwanusuru wazazi wanaohangaika na uchungu kwenye Zahanati ya Mafiga kabla ya kufikishwa katika hospitali hiyo ambako pia wanakumbana na adha nyingine.Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa, Dk Ritha Lyamuya alikiri kuwapo kwa tatizo hilo na kusema kina mama wanaopata uchungu wanapaswa kwenda Zahanati ya Mafiga kujifungua akisema mpango huo umelanga kupunguza msongamano wa wagonjwa kwenye hospitali hiyo.‘’Zahanati ya Mafiga ina wataalamu wa kutosha na vifaa vyote vya kujifungulia. Kama mjamzito atapata tatizo zaidi anaweza kupewa rufaa ya kuja hospitali ya mkoa,” alisema Dk Lyamuya.

Bugando, Mwanza
Mkurugenzi wa Hospitali ya Bugando, Dk Charles Majinge alikiri kuwapo kwa msongamano wa wagonjwa katika hospitali hiyo akitaja baadhi ya sababu kuwa ni ubovu wa huduma katika hospitali za mikoa na wilaya nchini.

Alipoulizwa kuhusu madai hayo, Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Hussein Mwinyi alisema jana: “Kwa sababu ninyi mlifanya uchunguzi, ngoja nami nifuatilie tutafutane siku ya kazi.”
source; mwananchi

my take; hivi kumbe hata baada ya mgomo mambo ni yale yale ,watanzania amkeni mjipiganie.
 

Toa taarifa ya maudhui yasiyofaa!

Kuna taarifa umeiona humu JamiiForums na haifai kubaki mtandaoni?
Fanya hivi...

Umesahau Password au akaunti yako?

Unapata ugumu kuikumbuka akaunti yako? Unakwama kuanzisha akaunti?
Contact us

Top Bottom