Ngoja niwape hii. Miaka hiyo nasoma Mtendeni kwa Ally Futo, tunaishi posta mtaa wa Libia dada yangu anaishi Ubungo zile kota ndogo jirani na RUBADA. Akawa amekuja kututembelea jumapili. Ilipofika jioni tukamsindikiza na mdogo wangu ili akapande basi Mnazi mmoja. Wakati huo kuna njia katikati ya bustani. Kabla hajapanda Ikarus akatupa dala ili tugawane kila mtu shilingi mbili na senti hamsini. Wakati tunarudi tukiwa kwenye zile njia za bustani nikamwambia mdogo wangu hela imeanguka. Nikajifanya naitafuta wakati hela iko mfukoni. Na yeye akainama, mara akatokea mtu akauliza mnatafuta nini mwenzangu akamjibu tumeangusha shilingi tano. Yule mtu akaanza kutafuta wakaanza kuongezeka watu wengi. Sasa jinsi ya kusema kwamba nilikuwa natania nikawa naogopa kwa sababu kulikuwa na watu wazima.
Jinsi ya kumwambia mwenzangu tuondoke nashindwa. Nikasogea pembeni nikatoa hela mfukoni huku nikiwa natetemeka, nimeinama nikasema hii hapa. Wakati huo watu kibao na wamechafuka mikono kwa vumbi.