Wavuvi haramu wabuni mbinu za kijasusi | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Wavuvi haramu wabuni mbinu za kijasusi

Discussion in 'Habari na Hoja mchanganyiko' started by Pdidy, May 24, 2009.

 1. Pdidy

  Pdidy JF-Expert Member

  #1
  May 24, 2009
  Joined: Nov 22, 2007
  Messages: 33,389
  Likes Received: 5,670
  Trophy Points: 280
  Na Lulu George

  24th May 2009  [​IMG]

  Wavuvi wakishusha samaki ufukweni baada ya kurejea kutoka katika shughuli za uvuvi.

  Baadhi ya wavuvi wanaojihusisha na vitendo vya uvuvi haramu kwenye ukanda wa Bahari ya Hindi, wilayani hapa, wamebuni mbinu mpya ya kupingana na serikali katika jitihada zake za udhibiti wa vitendo hivyo kwa kuajiri wapelelezi na kujenga vibanda vya simu karibu na ofisi za doria kwa lengo la kupashana habari mara wanapobaini kuwepo kwa doria baharini.

  Hayo yalibainishwa na Ofisa Uvuvi wa Halmashauri ya Jiji la Tanga, Alen Nyirenda, wakati wa ziara ya Mbunge wa Jimbo la Tanga, Harith Bakari Mwapachu, alipotembelea kwenye masoko ya samaki pamoja na kuzungumza na wavuvi wa jijini hapa juzi.

  Nyirenda, alisema kuwa mara kwa mara jitihada za kufanya doria zimekuwa zikigonga mwamba kutokana na watu wanaofanya vitendo hivyo vya uvuvi haramu kuweka vibanda vya simu karibu na ofisi za doria ili kupashana habari mara wanapoona zoezi linataka kuanza.

  Kufuatia hali hiyo, Ofisa huyo alisema baada ya kubaini kuwepo kwa uvujaji wa taarifa walifanya upelelezi na kufanikiwa kumkamata kijana mmoja aliyefahamika kwa jina la Ramadhan Madagaa, ambaye alikiri kutumwa na baadhi ya wavuvi wanaojihusisha na vitendo vya uvuvi haramu.

  “Tulikuwa tukijiuliza siku tukipanga kwenda baharini kufanya doria hatukuti mtu kumbe wameweka vibanda vya simu jirani na ofisi sasa mawasiliano yote yanayofanyika wanayajua mapema.....wana maajenti kule polisi ambao huwapa taarifa tunapochukua silaha na kule Yatch tunapofuata boti, kote huko wanavibanda vyao vya kupashana habari na haya yote aliyakiri huyo kijana baada ya kumkamata” alisema .

  Hata hivyo, Nyirenda alisema ufutwaji wa kesi dhidi ya watuhumiwa wa uvuvi haramu pamoja na kulipishwa faini ndogo mara wanapofikishwa mahakamani, kunachangia kwa kiasi kikubwa kuendelea kuwepo kwa vitendo vya uvuvi haramu kwenye wilaya ya Tanga.

  Nyirenda alisema tangu mwaka 2007 mpaka sasa kesi zilizo Mahakamani ni 156 ambapo hukumu kubwa kuliko zote iliyowahi kutolewa dhidi ya watuhumiwa ni mbili tu, mtuhumiwa mmoja alifungwa kifungo cha nje na mwingine alitakiwa kulipa faini ya Shilingi 150,000.

  Naye Katibu Msaidizi wa vikundi vya uvuvi katika Soko la Kasera, Kata ya Mazingani, Jijini Tanga, John Biblia, akisoma risala kwa niaba ya wavuvi wenzake, alisema soko hilo limekuwa likikabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo kukosekana kwa vyoo, maji pamoja na umeme.

  Biblia alitaja changamoto nyingine kuwa ni pamoja na kuvuja kwa banda wanalolitumia kuuzia samaki kunakotokana na uchakavu uliokithiri, kukosekana kwa chombo cha uhakika cha kuokolea wavuvi mara wanapopatwa na majanga wakiwa baharini, sambamba na kulazimishwa kuuza mali zao na watoza ushuru.

  Mwapachu alisisitiza umuhimu wa wavuvi kutumia zana za kisasa zinazokubalika kisheria na kutoa ushirikiano kwa vyombo vya dola katika kuwadhibiti wanaoendeleza vitendo vya uvuvi haramu kwenye Jiji hilo.

  Halamashauri ya Jiji la Tanga ina wavuvi wanaokadiriwa kufikia 3000 na vyombo vya uvuvi 600 ambapo maeneo yaliyokithiri kwa uvuvi haramu na aina ya uvuvi ni pamoja na Mundura, Tongoni, Mwarongo ya Digo, Mchukuuni, Sahare, Chumvini na Mvuuni
   
Loading...