nngu007
JF-Expert Member
- Aug 2, 2010
- 15,862
- 5,797
Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk. Azavery Lwaitama, alisema kuwa hakuna safu mpya ndani ya CCM kwani Kinana ni yule yule aliyekuwa akisimamia chaguzi zote zilizowaleta washindi kwa mizengwe.
Alisema hata Migiro licha ya kuwa mwadilifu lakini hana ushawishi mkubwa ndani ya CCM kama alivyo Prof. Anne Tibaijuka, kwani kutokana na utendaji wake angeingia kwenye safu hiyo angeweza kuwasaidia.
Nguvu ya Migiro wakati huo ilikuwa UWT, kwa sasa si mbunge, hivyo bado ni vigumu kwa CCM kusema imepanga safu mpya ya kuwavusha. Kwa muda mfupi watafanikiwa kuweka ghiriba kwa watu lakini baadaye watarejea kulekule, alisema.
Dk. Lwaitama aliweka bayana kuwa kilichofanyika ni kwa rais kutaka kuendelea kulifurahisha kundi la rafiki yake wa zamani, Edward Lowassa, baada ya kubaini kuwa ndiye nguvu ya CCM ili kuendeleza utamaduni wa viongozi kulindana.
Alifafanua kuwa Mukama ndiye alikuwa adui mkubwa wa Lowassa na kundi lake, hivyo asingeweza kuachwa aendelee na wadhifa wa ukatibu mkuu wakati hawafurahishi maswahiba wa Kikwete.
Mhadhiri huyo alibainisha kuwa Kikwete amebaini kuwa Lowassa ndiye nguvu ya CCM, hivyo amemua kumjengea mazingira ya kuwasambaratisha wanaompinga ili kuwe na utulivu ndani ya chama.
Kwa hiki walichokifanya CCM ni dhahiri kuwa walioko ndani ya chama wataendelea kubaki wa walioko nje hawana sababu ya kuwashawishi kuingia huko, alisema.
Naye mhadhiri mwingine wa UDSM, Bashir Ally, alisema kuwa hana hakika kama CCM wanaweza kufanikiwa kujibadilisha kwani wameacha kuhangaika na masuala ya msingi ili kuvuka hapa walipo.
Ili uweze kusonga mbele kama taasisi ni lazima uwe na vitu vitatu, kwanza historia ya taasisi husika, pili ni dira au lengo la nini unataka kufanya na tatu ni nguvu ya rasilimali watu na vitu, alisema.
Kwa mujibu wa mhadhiri huyo, CCM inayo nguvu kazi na vitu, yaani viongozi wengi wazuri na mali kama viwanja, majengo, magari na vinginevyo ila inakosa dira na historia yake.
Alisema kuwa wakati huu ulikuwa wa CCM kuhangaika na dira na historia ya nchi na chama chao, kujitambua kuwa wao ni chama cha wanyonge na si matajiri kama sasa.
Huu si wakati wa wao kubadili sura za viongozi maana hilo wamefanya mara nyingi lakini hawajafanikiwa, hivyo lazima wajitafakari wametoka Dodoma na ajenda gani ya kuwatumikia wanyonge, watu wana njaa, wanaporwa viwanja, fedha zao zinatoroshewa nje, je, wamekuja na majibu hayo? alihoji.
Bashir alipingana na kauli ya Rais Kikwete ya kuwalaumu wapinzani kuwa hawaoni mafanikio yaliyofanywa na CCM, akisema ni dhahiri kuwa hayo yanayofanyika si sehemu ya mahitaji yao ya msingi.
CCM si chama cha matumaini ya watu wanyonge, tena kama zamani, hiki labda kinafaa kutawala Marekani kwa matajiri. Wamekuja na maazimio kwenye mkutano wao ambayo yalisemwa na CHADEMA kwenye ilani yao wakayapinga kuwa hayawezekani, alisema.