Wasomi Kenya wanamfananisha Nyerere na malaika

BAK

JF-Expert Member
Feb 11, 2007
124,952
287,542
Wasomi Kenya wanamfananisha Nyerere na malaika
Thursday, 13 October 2011 21:04

Na Florence Majani
Mwananchi

TUNAPOFANYA kumbukumbu ya miaka 12 tangu Mwalimu Julius Kambarage Nyerere atutoke, hapana shaka wengi wanamkumbuka kwa yale aliyoyafanya kwa nchi yake.
Yumkini, wengine wanatafakari ya kuwa labda,angekuwepo - pengine hekima zake zingeweza kuliokoa taifa hili ambalo linaonekana kutumbukia zaidi katika umaskini.

Wanaharakati wengi wa wakati ule, wanamzungumzia Baba wa Taifa kwa namna mbalimbali.
Mmoja wao, Mwandawiro Mghanga, mbunge wa zamani wa jimbo la Wundanyi nchini Kenya na mwanafalsafa wa Ujamaa ana mengi ya kusema kuhusu Nyerere.

Mghanga anasema, kwa juhudi alizozifanya Mwalimu, alistahiki tuzo ya heshima (Nobel Prize), lakini mpaka mauti yanamfika, hakuwahi kupata tuzo hiyo. Na badala yake, wanapewa viongozi wengine ambao hata hawajafanya kazi nzito kama ya kiongozi huyo.

“Nyerere alitetea haki za wana Afrika. Hakutetea hata siku moja siasa za ubeberu, na kwa sababu hao mabeberu ndiyo hutoa tuzo hizo, kwa makusudi walimnyima,” anasema Mghanga na kuongeza: “hakupewa tuzo ya heshima kwa sababu aliupinga ubepari.”

Mghanga, anauzungumzia mustakabali wa Tanzania tangu Mwalimu Nyerere atutoke na anasema, Tanzania inaonekana kama imeelemewa mzigo wa matatizo ambayo haiwezi kuyatatua. Na hiyo ni kwa sababu imetetea siasa za ubepari.
Anazitaja siasa za ubepari kuwa ni siasa za matumbo na ndiyo maana, viongozi wachache wanafaidi huku wananchi wakiteseka.

“Tangu waingie hawa viongozi baada ya Nyerere(anawataja Ali Hassan Mwinyi, Benjamin Mkapa na sasa Jakaya Kikwete) wameileta sera ya ubinafsishaji. Na matokeo yake, viwanda, mashirika ya umma vyote vimebinafsishwa,”Anasema.

Mghanga, ambaye mpaka saa bado yungali katika harakati za kulijenga bara la Afrika anasema, hata yeye mwenyewe amekula matunda ya nguvu za Nyerere. Watoto wake anasema walipata elimu bure katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na hali kadhalika yeye.
Anaongeza: “Nilipofukuzwa na Jomo Kenyata hapa Kenya, nilikwenda kuishi kule (Tanzania) na niliishi kwa amani. Tulikuwa tukipewa ruzuku ya vyakula kila mara,”

Anasema wakati wa Nyerere Tanzania haikuwa kama ilivyo sasa. Hivi sasa anaziona chembechembe za ukabila na udini.
“Kama kuna vitu ambavyo Tanzania inabidi ivishike kwelikweli, basi ni vita vya ukabila na udini. Hivyo ndivyo baba wa taifa alivyofanikiwa kuviondoa katika taifa hilo,” Anasema.

Mghanga ambaye anadai alikuwa rafiki wa karibu wa Nyerere anasema, wakati wake (Nyerere) hakukuwa na chembe ya ufisadi. Anasema anashangazwa na jinsi viongozi wa sasa wanavyojilimbikizia mali wakati Baba wa Taifa hakufanya hivyo hata kidogo.

Pia, anazungumzia Jumuia ya Afrika Mashariki iliyovunjika mwaka 1977 wakati ule ikiwa chini ya Milton Obote wa Uganda, Jomo Kenyata wa Kenya na Nyerere kwa Tanzania.
“Kenyata ndiye aliyechangia kuvunjika kwa jumuia ile kwa kuwa alipendelea siasa za kibepari. Obote na Mwalimu walisimamia katika ujamaa. Basi, mpishano ule ndiyo uliangusha EAC,” anasema Mghanga

Anaitaja jumuia ya sasa na kusema, inakwamishwa na Watanzania ambao bado wanaweka vikwazo kadhaa vya kiuchumi na kisiasa.

Naye Waziri wa Huduma za Matibabu Kenya, Profesa Anyang’ Nyong’o anamtaja Nyerere kuwa alikuwa ni binadamu lakini ni mfano wa malaika.

Anasema, wakati huu taifa linapokumbuka kifo cha Mwalimu, basi wakumbuke kitu kimoja cha muhimu kuliko vyote alichokifanya … nacho ni ‘ukabila’

“Kama kuna kitu cha muhimu alichokifanya Mwalimu, basi ni kutembea Tanzania nzima akihimiza Watanzania wawe kitu kimoja na kuutokomeza ukabila.
Kwa hilo Watanzania hamna budi kumuombea kila siku,” anasema Prof. Nyong’o.

Waziri huyo anasema, nchi nyingine za Afrika Mashariki, zinaionea wivu Tanzania kwa kuwa hakuna ukabila, hivyo anawasihi watanzania, pamoja na mengine, wadumishe hilo zaidi.

Anatolea mfano mapigano ya kisiasa yaliyotokea nchini Kenya mwaka 2007 na kusema, yalikuwa ni ya kisiasa lakini yalichochewa zaidi na ukabila.

Nyong,o amfananisha Nyerere na malaika
Anasema, akiwa mwanafunzi katika Chuo Kikuu cha Makerere, Uganda, anakumbuka kusikia hotuba ya Nyerere iliyokuwa ikitaka Afrika Mashariki iwe taifa moja.

“Alikuwa tayari kuiacha Tanganyika ichelewe kupata uhuru wake , ili Kenya na Uganda nazo zipate na baadaye nchi za Afrika Mashariki ziwe taifa moja. Alijitoa mhanga kweli kweli,” anasema Prof Nyong’o

Anasema, kilichokwamisha hayo ni wimbi zito la ubwanyeye lililokuwepo nchini Kenya na mzimu huo ndiyo ulioitafuna hata Jumuiya ya Afrika Mashariki baadaye.

Prof Nyong’o anahitimisha mazungumzo yake na kusema, roho ya Nyerere inalitazama taifa la Tanzania linapokwenda na hapana shaka kuwa, analia kwa huzuni kwani yale aliyoyahimiza kiongozi huyo yanaonekana kwenda mrama.

Anaeleza kuwa Nyerere alipenda kusisitiza, kuhusu kupigana na maadui watatu: ujinga, umaskini na maradhi. Mambo ambayo kwa kiasi kikubwa bado yamevijaza vyumba na korido za taifa hili.
Mawazo ya mwanahabari, mhariri wa zamani na mwanachama wa toleo la Kenya (Kenya Year Book), Philip Ochieng, hayakutofautina kwa kina na Wakenya wengine wa wakati ule. Ochieng naye anamsifu Nyerere kwa kuutokomeza ukabila.

Anasema, Mwalimu Nyerere aliua kabisa ukabila, jambo ambalo Kenya imeshindwa na tayari limekwishaigharimu nchi hiyo.
“Nimefanya kazi Tanzania katika gazeti la serikali wakati huo, nikiwa pamoja na rais wa zamani, Benjamin William Mkapa. Sikuwahi kusikia Watanzania wakizungumzia ukabila hata mara moja,” anasema Ochieng.

Anasema jambo la msingi ambalo Mwalimu alishindwa ni siasa za Ujamaa. Anasema, endapo Nyerere angetazama mbele na kuona kuwa kuna kitu kinaitwa ‘utandawazi’ kinakuja, basi angetambua kuwa ujamaa ni kazi ngumu.

Anasema utandawazi na ujamaa ni kama mafuta na maji na kamwe haviingiliani.

“Waliokuwa wakitetea ujamaa wakati ule ni wachache, Kingunge Ngombale Mwiru, Rashid Kawawa na Nyerere, hivyo wazo hilo lilikosa hamasa na uongozi makini. Hilo ndilo lililofanya Tanzania ikawa nyuma kimaendeleo ikilinganishwa na Kenya au hata Uganda,” anasema Ochieng.

“Tanzania ilikuwa ni nchi yenye makabila zaidi ya 100 ambayo yalipoteza uhuru wake, lakini taifa moja likauleta uhuru huo,” (Mwalimu J.K Nyerere, Chuo Kikuu chaToronto, Canada, 1969)
Hakika, hatuna budi kudumisha umoja na mshikamano kama alivyotuasa baba wa Taifa na katu tusiruhusu ukabila na udini ukaingia Tanzania.


 

Songambele

JF-Expert Member
Nov 20, 2007
4,486
2,171
Sifa zisizidi waungwana, hata alipokuwa hai hakupata sifa hizi jamani. Kama ilivyoada heading haiendani na content, manake wasomi kenya hawawakilishwi na watu wawili na wakenya wanampinga nyerere dhahiri na ujamaa huko hauna nafasi kitambo.
 

punainen-red

JF-Expert Member
Nov 18, 2010
1,732
446
Kushindwa kwa ujamaa siyo kosa la Nyerere, kama ambavyo kushindwa kwa ubepari siyo kosa la Kenyatta! Pamoja na shida zote, watu walioishi miaka ya 60 na 70 wanaweza kujivuna zaidi kuwa watanganyika kuliko kizazi chetu leo. Wakenya wa kawaida hawana unafuu mkubwa kihivyo kuliko watu wengine wa EA. Kwanza hata wao ubepari haujawapa maendeleo ktk sekta muhimu, wakati wa Moi walifanya kitu kizuri sana kutumia 'harambee' kujenga mashule, kugharimia matibabu, na hata kusomesha vijana wao nje. Sijui kama 'moyo' wa harambee ilikuwa ubepari au kionjo cha ujamaa wa kiafrika. Huwa najiuliza kama Nyerere angeuacha ujamaa wake akaufuata ubepari tungekuwa na maendeleo gani leo?.... Watanzania tumekuwa na tabia chafu ya kumlaumu Nyerere na sera ambazo tumeziacha kama miaka 20 iliyopita! Ukiuliza sera tunazofuata sasa hivi na faida zake kwa wananchi ziko wapi... watu wanabaki kung'aa macho tu!! Kama tuna akili zaidi ya kizazi cha wakati wa Nyerere hebu tuonyeshe matunda ya hizo akili zetu.
 
  • Thanks
Reactions: BAK

mwacheni77

JF-Expert Member
Apr 11, 2011
763
209
Tulimpenda,tunampenda,tulimuheshimu tuna muheshimu,na tunaheshimu kwa alichotuachia na tutaendelea kumuenzi but binadamu anabaki binadamu na malaika wanabaki kuwa malaika,kuna alipotukosea tumemsamehe cos yeye binadamu kama binadamu mwingine,hawezi kupewa sifa za malaika mungu amsamehe ana atusamehe na ss pia kwa sifa tunazompa sio zake
 

Toa taarifa ya maudhui yasiyofaa!

Kuna taarifa umeiona humu JamiiForums na haifai kubaki mtandaoni?
Fanya hivi...

Umesahau Password au akaunti yako?

Unapata ugumu kuikumbuka akaunti yako? Unakwama kuanzisha akaunti?
Contact us

1 Reactions
Reply
Top Bottom