Kakke
JF-Expert Member
- Dec 4, 2010
- 1,883
- 1,483
Jaji Joseph Warioba
Katiba ikitungwa kwa mbinu, hila haitadumu miaka 50
Toleo lililopita tulichapisha sehemu ya kwanza ya mahojiano yaliyofanyika kati ya gazeti la RAIA MWEMA na aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Katiba, Jaji Joseph Warioba. Ifuatayo ni sehemu ya pili na ya mwisho ya mahojiano hayo.
RAIA MWEMA: Hiyo adjust inafanywaje?
JAJI WARIOBA: Kwa kifupi, kila nchi iliachia madaraka katika mambo fulani fulani yaje kwenye Muungano. Nchi moja ikianza kuondoa mambo yake, inadhoofisha Muungano.
Wanaosema tubaki na serikali mbili ni lazima wayapatie ufumbuzi matatizo tuliyonayo. Huwezi kusema Zanzibar iendeshe mambo yake na ukabaki na Muungano wa serikali mbili. Kama Zanzibar ikirudishiwa mambo yake Tanganyika ndiyo itabaki kuwa Muungano.
Hivyo mambo yote 22 lazima yabaki kwenye orodha ya Mambo ya Muungano. Ni lazima turudi kwenye nchi moja badala ya kuwa na nchi mbili. Kama tukiwa na nchi mbili basi Tanganyika na Zanzibar zitakuwa na hadhi sawa.
Ni lazima pia kama Zanzibar itarudisha mambo yaliyoondolewa kwenye orodha na kubadili Katiba yake ili Zanzibar isiwe nchi bali iwe sehemu ya nchi, basi ifanye hivyo kwa hiyari. Ikilazimishwa kutakuwa na mgawanyiko mkubwa sana ndani ya Zanzibar. Tayari viongozi wa Zanzibar, Makamu wa Kwanza na Makamu wa Pili wameanza kulumbana.
Ukililazimisha suala hili utapata matatizo yaleyale tuliyokuwa nayo kabla ya Maridhiano. Na hiyo haitasaidia Muungano. Kwa hiyo bado sisi msimamo ni huo. Wasiseme tu kwamba serikali tatu zinavunja Muungano. Tumeonyesha nchi kwa nchi ambazo ni shirikisho na zimeendelea kuendesha mambo yao vizuri.
Kuna wengine wamezungumzia Sura ya Pili ya Rasimu yenye malengo. Hii ni dira. Wengine wanasema kwamba dira hii haiwezi kutekelezwa na Serikali ya Muungano kwa sababu Serikali ya Muungano haina madaraka ya kusimamia yale ambayo yametajwa kwenye Sura ya Pili.
Hilo nalo ni la kushangaza kidogo, kwa sababu bado tuna malengo hayohayo kwa Katiba ya sasa. Katika Katiba ya sasa yamo, sisi tumefafanua zaidi. Ukiangalia katika Katiba ya sasa, Serikali ya Muungano haina madaraka ya kusimamia malengo hayo kwa upande wa Zanzibar.
Lakini tunaona ni sawa kuwa na Serikali ya Muungano ambayo haina madaraka ya kusimamia Zanzibar. Ukigeukia Tanganyika nayo iwe kama Zanzibar wanasema hiyo si sawa. Sasa tunajiuliza kwa nini Serikali ya Muungano haina madaraka upande wa Zanzibar kwa malengo ambayo tumeyatia kwenye Katiba? Ukisema Tanganyika nayo iwe kama Zanzibar wanasema hiyo haiwezi kutekelezeka.
Sisi imani yetu ni kwamba Katiba ndiyo makubalino ya nchi hizi mbili na kila nchi lazima ikubali kuyatekeleza. Kwa hiyo, ukienda kutengeneza Katiba zao ni lazima zifuate haya yaliyomo katika Katiba hii kwa sababu usipoheshimu Katiba hii hakuna Muungano.
Mimi naona kwamba wanaona hayawezi kutekelezwa Tanganyika kwa sababu mpaka sasa hivi hayatekelezwi Zanzibar. Sisi bado tunaona kwamba hii si sawa.
Kuna mambo mengine yaliyotokana na wananchi kwa maana ya mawazo ya wananchi. Tunaona mwelekeo ni kuyakataa. Hayo ni kama haya ya malengo kwa sababu wananchi wanataka tuwe na haki za wakulima, haki za wafugaji, haki za wavuvi.
Tumeeleza kwamba huwezi ukaingiza kwenye Haki za Binadamu vitu kama mkulima ana haki ya kupata ardhi, ana haki ya kupata pembejeo, ana haki ya kupata bei nzuri. Hiyo haiwezekani. Lakini ni vizuri mambo haya yakaingia kwenye Katiba, kwa maana ya dira ili serikali inapoandaa sera izingatie mambo haya.
Ijue mkulima anahitaji ardhi, pembejeo, anahitaji bei nzuri ya mazao yake. Mfugaji anahitaji ardhi, anahitaji malisho, anahitaji bei nzuri na maji. Wavuvi ndiyo kwanza wanalalamika, hata maeneo waliyokuwa wakivua, wamepewa wawekezaji wakubwa, hawa nao wanataka wapate sehemu ya kuvua, wapate na zana.
Tukasema tuyatie kwenye rasimu ya Katiba. Haya yakikataliwa, wananchi ambao tulitaka watoe maoni yao, watoe mawazo yao, watakuwa wameachwa kabisa. Katiba hii kama hayo yataachwa, haitawahusu sana wakulima, wafugaji na wavuvi.
Lakini pia kuna wasiwasi juu ya maadili. Inaonekana kuna mwelekeo wa kutokubali hili. Wananchi wameonyesha kufadhaishwa sana na kuporomoka kwa maadili. Wanasema eneo moja la kuchochea rushwa ni zawadi. Kwao hicho ndicho chanzo cha rushwa. Wanataka jambo hili liingie kwenye Katiba, lakini naona uwezekano wa kulikataa umetanda.
Wananchi walizungumzia kwa uzito sana kwamba wabunge wao wasiwe mawaziri; kwamba ubunge uwe na ukomo kwa sababu sasa inaonekana kama ubunge umebinafsishwa. Wanataka kuwe na ukomo, na wakiona mbunge hawafai, wamuondoe. Sasa naona kama halikubaliki hivi. Lakini haya ni maoni ya wananchi.
Wamezungumzia kuhusu madaraka ya rais. Hili ni suala ambalo lilizungumzwa sana, na tulitaja mifano. Tukasema hata wakati wa kutunga Sheria ya Mabadiliko ya Katiba lilikuwa linazungumzwa sana. Kutokana na mawazo yale, tumeona ni kweli, pengine ingefaa tumuondoe rais asiwe sehemu ya bunge na kwa maana hiyo, mawaziri wake hawatakuwa katika bunge. Tunaona hata hili halikubaliki.
Watu wanasema hata uchaguzi wa rais unaweza kuwa na hitilafu kwa hiyo nafasi itolewe ya kuhoji kwenye Mahakama. Tunaona hili nalo kama linakataliwakataliwa hivi. Wananchi wamesema punguzeni madaraka ya rais. Tumejitahidi, tumesema madaraka ya rais yaanzie hapa, huko chini tuiachie tume. Huku juu anaowateua tumwekee utaratibu. Tunaona nalo hili halikubaliki .
Tume za Kitaifa tumeziangalia sana. Tukataka ziwe na nguvu zaidi. Tume ya Uchaguzi; Tume ya Haki za Binadamu na Tume ya Maadili. Sasa sote haya tumeyapata kwa wananchi. Maana sasa kila kitu wanasema ni maoni ya Tume. Tumetoa kitabu kizima cha maoni ya wananchi.
Wameyazungumzia mambo haya yote lakini sasa ninavyoona, kila nikiwasikiliza wabunge, kila mbunge anadai anazungumzia kwa niaba ya wananchi. Lakini ukiona mawazo ya wabunge ni tofauti na yale tuliyoyapata kutoka kwa wananchi.
Ndiyo maana nasema tuwe makini sana, kwa sababu Katiba hii kama haitazingatia maoni ambayo wametoa wananchi, bado tutakuwa na matatizo.
Ninafuatilia wanavyoendesha mambo bungeni. Wamechukua muda mrefu sana kuzungumzia aina ya kura. Sheria inataka wapige kura, kwa hiyo kura watapiga ili kukubaliana na kitu chochote bungeni. Lazima wapige kura na wamewekewa kiwango kwamba theluthi mbili kutoka kila upande, kwa hiyo lazima wapige kura.
Mimi kwangu iwe ya wazi, iwe ya siri si la muhimu. Kwangu muhimu ni namna watakavyojadili haya mambo kwa lengo la kufikia muafaka. Nataka tuwe na Katiba ambayo itakubaliana na wananchi wote.
Angalia majadiliano yale. Si ya kutaka wapate Katiba ya muafaka. Ni mbinu. Kila mmoja anatoa hoja lakini ukiwaangalia unajua malengo yao ni nini. Wale ambao wanataka mambo wayaamue kwa kura, wanataka kura ya wazi. Wale ambao wanataka kuwazuia hawa walio wengi wanataka kura ya siri.
Sasa hiyo haitoi matumaini kwamba kutakuwa na jitihada za kweli kweli kufikia muafaka. Watakuwa wanazungumza lakini mwisho tutakwenda kupiga kura.
Kwa mambo mazito kama la Muungano, kama tusipokuwa na muafaka, muundo wowote ule utakaouleta utaanza kupingwa tangu siku ya kwanza ya kupata Katiba. Hamtakuwa mmemaliza hayo matatizo. Wajue kwamba unaweza kufanya mbinu ukapitisha, lakini ujue Katiba itaanza kupingwa siku hiyo hiyo ya kwanza.
Kusema kwamba tuwe na Katiba itakayokuwa ya miaka 20 au 50, hilo halitakuwapo. Watakuwa wanangojeana tu kwamba kundi hili limepitisha katiba yake, likija kundi jingine litapitisha katiba yake pia.
Huo ndio wasiwasi wangu.
Sioni kama kuna nia ya dhati kwenye Bunge hili ya kwenda kuzungumza wakapata maridhiano. Wakatoa Katiba ambayo wengi wao watakwenda kuiunga mkono. Naona itatoka pale Katiba ambayo tunanza kampeni ya kuanza kuipinga kwenye kura ya maoni, na hata ikipita kwenye kura ya maoni, itaanza kupingwa kwenye uchaguzi wa mwaka kesho. Na itaendelea hivyo, na tutaendelea kuwa na matatizo yaleyale tuliyokuwanayo awali.
RAIA MWEMA: Rasimu inavyopingwa kwa nguvu na baadhi ya makundi utadhani mlikwenda nje ya hadidu za rejea. Kuna uwezekano, labda, mlichepuka?
JAJI WARIOBA: Wakati wowote tulipokuwa tunafanya ile kazi kila kitu kilikuwa wazi. Kila awamu ilikuwa tunakuja kutoa maelezo kwenye vyombo vya habari.
Tulifuata hadidu za rejea kama zilivyokuwa. Tulikuwa tumetumwa tukusanye na turatibu maoni ya wananchi. Tulifanya hivyo. Tukatumia miezi mitano tunazunguuka nchi hii tukiwa kwenye timu nane. Tumefanya mikutano mingi. Tumepata maoni ya watu wengi.
Maoni yale tumeyachambua. Tukatengeneza rasimu ya kwanza, na kufuatana na hadidu za rejea, kila rasimu tukaipeleka kwenye mabaraza yapitie ibara kwa ibara yajiridhishe kama yaliyomo yanazingatia maoni waliyotoa.
Tulipeleka hata kwenye mabaraza yale ya wazi yalikuwa 614. Wakaangalia kifungu kwa kifungu wakarudisha na mapendekezo. Tukayangalia yale mapendekezo. Baadhi yakatufanya tubadili vifungu vya Rasimu. Vingine tukaviacha ili tupeleke kwenye Bunge la Katiba.
RAIA MWEMA: Kuna wanaosema mbona mmetoa takwimu za maoni ya wananchi mlipokwenda awamu ya kwanza, lakini hamkutoa takwimu za maoni ya wananchi kwenye mabaraza?
JAJI WARIOBA: Hao ni wanaotaka waone ni wangapi wamependekeza muundo wa serikali moja, mbili na tatu. Kwa hadidu zile za rejea haya ni mazoezi tofauti kabisa.
La kwanza tulikuwa tunapata maoni ili itengenezwe Rasimu. La pili, hili ilikuwa kuangalia ibara kwa ibara. Tusingekwenda kuwauliza wananchi wangapi wanataka ibara hii, wangapi hawataki.
Ilikuwa kwa ujumla waangalie ibara kwa ibara. Hatukuwapelekea waangalie jambo la Muungano peke yake.
Na kwa kweli kwenye mabaraza yale, kama wangefuatilia, wananchi wenyewe hoja yao ilikuwa ni mambo yanayowahusu.
Mambo ya uchumi; mambo ya kijamii; elimu, afya, maji ndiyo yalikuwa muhimu kwao. Sasa huku juu wenye suala ni Muungano. Nafikiri huko juu jambo la muhimu kwao lilikuwa ni Muungano. Tunasahau kwamba hata wa chini nao wana mambo yao ya msingi wanayotaka yawemo kwenye Katiba.
Kwa upande wa walemavu, kwa sababu nao walikuwa ni sehemu ya Mabaraza, walikuwa wanakwenda kuangalia kama mambo yao yameingia mule. Haki za Walemavu. Sasa hii ninayosema ni kwamba tusichanganye haya mambo, tusikazanie takwimu, wakati wote tuangalie hoja.
Hoja yetu haikujengwa kwenye msingi wa takwimu. Wanaokosoa takwimu ni ujanja wa kukwepa hoja ya msingi ya Tanganyika kuvaa koti la Muungano na mambo ya Muungano kuondolewa kinyemela. Pia wanakwepa kuzungumzia kuvunjwa kwa Katiba na kuwa na nchi mbili badala ya moja. Hata watumie mbinu gani, mwisho lazima watoe majibu kwa matatizo ya Muungano.
RAIA MWEMA: Kuna ambao wanasema hili la Tanganyika ni lako. Kwamba mlikuwa nalo wakati ule wa G55. Tunajua kwamba wewe hukuwa mwanakundi hilo. Lakini kwa kuweka kumbukumbu sahihi unaweza kulizungumzia mwenyewe?
JAJI WARIOBA: Kama ulivyouliza, sisi tulifuata hadidu za rejea na tuliifanya kazi ile kama tulivyotakiwa. Siku moja nilimuona Jenerali Ulimwengu kwenye kipindi chake cha Jenerali On Monday akijaribu kumsahihisha mgeni wake, kijana mmoja, aliyejiita msomi hivi, aliyesema mimi nilikuwa G55.
Ulimwengu akamkumbusha kwamba yeye, alikuwa G55 namba 11. Mimi sikuwamo. Huko nyuma, mwaka 1994, mambo hasa yalipozuka, kuanzia hiyo G55, kuja taarifa ya awali ya Serikali ya Tume ya Shelukindo, niliandika makala kwenye gazeti la Rai.
Baada ya kuandika ikachukuliwa ikachapishwa kwenye kijitabu. Na wengi walikisoma kijitabu kile. Msimamo wangu wakati wote nilikuwa nikisema serikali mbili kwenda serikali moja.
Wakati ule ikaonekana mapendekezo ambayo serikali imeleta ilikuwa ni maamuzi ya Shelukindo, kuondoa mambo mengi kutoka kwenye Muungano. Nikasema mkifanya hivyo mnakwenda kwenye serikali tatu. Nikasema ningependa tuwe na serikali mbili kwenda moja.
Wengine wanataka moja lakini sasa inaonekana hakuna uwezekano wa serikali mbili. Nikasema basi kama tunataka kwenda kwenye serikali tatu lazima serikali hiyo iwe aina ya fulani. Hayo yote yalikuwa kwenye kijitabu kile, lakini sikuwa kwenye G55.
Lakini G55 haikuibuka mwaka 1994. Mizizi yake inaweza kukurejesha mwaka 1992 wakati tukienda kurejea kwenye mfumo wa vyama vingi vya siasa. Kulikuwa na mjadala kuhusu nafasi ya Rais wa Zanzibar.
Kwamba tunakwenda kwenye vyama vingi lakini tunataka Rais wa Zanzibar abaki kuwa makamu. Msimamo ulikuwa wakati ule kwamba hawezi kuendelea kuwa makamu kwa sababu mbili.
Kwanza, kikatiba ukisema lazima awe makamu, unaweza kupata rais kutoka Zanzibar, kisha makamu wa rais kutoka Zanzibar, nikasema kisiasa hiyo itakuwa na matatizo.
Pili, mnaweza kupata rais kutoka chama hiki, kisha Rais wa Zanzibar akatoka chama kingine. Ukiwaweka hawa pamoja utadhoofisha utendaji wa serikali. Hilo nilikuwa nakubaliana nao. Kwenye OIC nilikuwa nakubaliana nao lakini kwenye serikali tatu nilikuwa sikubaliani nao.
RAIA MWEMA: Hii ni Tume yako ya pili. Ile ya kwanza ya Rushwa kwenye Awamu ya Tatu nayo haikupokewa vizuri na wakubwa. Unajisikiaje ukisikiliza mashambulizi haya ya sasa na ukikumbuka ya wakati ule?
JAJI WARIOBA: Ninajisikia nimemaliza kazi.
Na tulipokutana mara ya mwisho, kwa kweli, tulijaribu kufanya tathimini tukafikia hitimisho kwamba tukiangalia kazi tuliyopewa, tumeifanya kama tulivyoagizwa na sheria na tumeridhika na hicho ambacho tumependekeza. Tumefanya, tumemaliza, sasa tunakwenda kupumzika.
Kazi hii ilikuwa ngumu sana. Haikuwa kazi rahisi kimwili na kiakili. Haikuwa kazi rahisi kwa mtu wa umri wangu. Ndiyo ilinisaidia mambo mengine kwa sababu ya uzoefu wa utumishi wa umma. Nimejifunza mambo mengi.
Ilikuwa ni kazi ngumu kwa sababu tulipata maoni mengi sana ya wananchi. Kuchuja ni lipi tupendekeze na lipi tuache haikuwa kazi rahisi. Lakini tumefanya na tumewasilisha.
Mimi naridhika kwamba kazi imefanywa vizuri. Nilipata heshima kubwa kuongoza Tume ambayo imeweza kushughulikia jambo kubwa kama hili.
Hii ilikuwa Tume nzito kwa maana ya kazi iliyokuwa mbele yetu na aina ya wajumbe. Tulikuwa wajumbe 36; watu wenye misimamo mbalimbali. Kwamba kundi hili liliweza kutoa mapendekezo ambayo wote wanakubaliana, haikuwa kazi rahisi.
Nawashukuru sana wenzangu. Walijitahidi. Wote tumejitahidi. Na kama nilivyosema wakati nawasilisha Rasimu ile, tunakubaliana na yote ambayo yako kwenye Rasimu. Sasa nataka nipumzike. Rafiki yangu mmoja aliniuliza sasa utafanya nini baada ya hapa? Nikamwambia nilitumikia nchi hii nikiwa mtumishi wa umma kwa muda mrefu na wakati huo sikupata nafasi ya kulea watoto wangu. Sasa hao ni wakubwa. Naomba sasa niachwe nilee wajukuu.
RAIA MWEMA: Kuna ambao wanakushangaa. Wewe mfuasi mzuri wa Mwalimu Julius Nyerere, muumini wa serikali mbili, iweje leo unapendekeza serikali tatu? Mbona hamkupata kutaja hizo tatu mbele yake Mwalimu?
JAJI WARIOBA: Suala hili ni gumu. Ni vizuri tukazingatia hoja. Tusilifanye ni la Warioba.
Naona viongozi wengi, hasa wa ngazi za juu, wanalifanya ni la binafsi, hasa hasa kwa baadhi yetu tuliopata kufanya kazi na Mwalimu Nyerere.
Kiongozi mmoja aliniuliza akasema haya matatizo ya Muungano yalikuwapo hata wakati wa Mwalimu, na wewe ulikuwa mshauri wa Mwalimu mbona wakati ule hukumshauri juu ya serikali tatu?
Jibu langu ni kwamba Mwalimu alikuwa anajenga Muungano, hakuwa anabomoa. Mwalimu na Sheikh Karume walianza na mambo 11 ya Muungano. Mwalimu aliacha mambo 21 kwenye orodha na yote yaliingizwa kwa kufuata Katiba. Hakuwa anabomoa, alikuwa anajenga. Alikua anaimarisha Muungano.
Hao wanaosema nimemsaliti Mwalimu Nyerere wamepunguza mambo ya Muungano kinyume cha Katiba. Katika mambo yaliyoondolewa ni pamoja na bandari na biashara ya nje yaliyokuwa kati ya mambo 11 ya mwanzo kabisa.
Mwalimu alilenga kwenda kwenye serikali moja, kwa kuongeza mambo ya Muungano, si kuyapunguza.
Wanamtumia Mwalimu kama hirizi lakini wao wanabomoa kazi aliyofanya. Mwalimu alifuata Katiba kuongeza mambo ya Muungano, wao wanayaondoa bila kufuata Katiba.
Nawauliza wanaosema kwamba tumemsaliti Mwalimu, hivi Mwalimu angetokea leo akakuta yale mambo wameyaondoa angeshangilia? Asingeshangilia. Angetokea akakuta tunazungumzia nchi mbili angeshangilia? Asingeshangilia.
Msimamo wangu wakati wote ulikuwa serikali mbili kwenda serikali moja. Kutokana na hali halisi iliyopo sasa, mimi nasema twende kwenye serikali tatu.
Chanzo Raia Mwema