Wapinzani wa Tanzania wanataka nini tena?

Nov 13, 2019
16
19
WAPINZANI WA TANZANIA WANATAKA NINI TENA?

Miaka ya 2010 kuelekea 2015 vyama vya upinzani vilipata nguvu kubwa sana ya kuungwa mkono mno na wananchi hasa kwa ajenda zao kubwa zilizowavutia sana Watanzania zilizobeba adhima ya kukemea vitendo vya ufisadi, rushwa, uzembe serikalini, matumizi mabaya ya rasilimali za nchi, miundombinu mibovu ya kiuchumi, kiafya na kijamii ndani ya nchi na mengine mengi ambayo vyama vya upinzani viliyapambania usiku na mchana.

Nakumbuka kipindi hicho vyama vya CUF na CHADEMA vilipata wafuasi wengi sana kila walipokuwa wanaenda. Wananchi wa Tanzania walichoka kusikia stori na habari za vitendo hivyo ambavyo vilishamiri serikalini kila mara na miaka hiyo wanasiasa wa vyama vya upinzani akina Wilbroad Slaa, Freeman Mbowe, Prof Ibrahim Lipumba na wengine wengi walikubarika na kupata uungwaji mkono mkubwa sana na wananchi kutokana na sera zao hizo za kupinga rushwa na ufisadi ambao ulikuwa mwiba mkali kwa wananchi na kuathiri sana maendeleo ya Taifa.

Nakumbuka ajenda kuu ya Mbowe na Dkt Slaa wakati wanagombea Urais mwaka 2005 na 2010 ilikuwa kupambana na rushwa na ufisadi serikalini na walizunguka nchi nzima kuwaambia ukweli wananchi na kupata uungwaji mkono mkubwa sana wa wananchi. Kipindi fulani Dkt Slaa alifikia mpaka kutaja majina ya mafisadi aliyoiita List of Shame, ambamo humo ndani alitaja majina ya manguli na vigogo wakuu aliowaita vinara wa ufisadi Tanzania. Upinzani ulipata nguvu kubwa kwa wananchi kwa sera hizo na walikubarika sana.

Kipindi hicho viongozi wa vyama vya upinzani akina Mnyika, Msigwa, Mbowe, Lissu, Lema, Heche, Halima Mdee na wengine wengi wa upinzani walipaza sana sauti kutaka Rais mkali, asiyeangalia sura, ambaye hatacheka na wezi na wala rushwa, wazembe, Rais atakayerudisha nidhamu Serikalini, Rais atakayekomesha misamaha holela ya kodi ambayo ilikuwa ikiigharimu sana Taifa, Rais atakayeweka mkazo mkubwa kwenye kukusanya kodi, Rais atakayelinda rasilimali za nchi kwa nguvu zake zote na mengine mengi. Hizo zilikuwa ndiyo ajenda kuu za upinzani na kwakweli kipindi hicho walipata uungwaji mkono mkubwa sana na Watanzania hasa kutokana na kushamiri kwa vitendo hivyo Serikalini.

Baada ya kuingia madarakani kwa Rais Dkt John Pombe Magufuli mwaka 2015 ni kama alikuwa akiishi kwenye ndoto za viongozi hao wa upinzani, alichukua ajenda na hoja zao zote walizokuwa wanazihubiri na zilizowapa nguvu kubwa sana wapinzani na kuzitekeleza kwa nguvu kubwa huku akinena kwa maneno na kutenda kwa vitendo.

Rais Magufuli akazichukua hoja za upinzani na kuzifanyia kazi kwa vitendo. Hapo ndipo pakaanza vuguvugu la tumbua tumbua ambayo ilisomba msululu mkubwa wa watumishi hewa na wenye vyeti feki zaidi ya elfu 40, akaanzisha mahakama ya mafisadi wala rushwa na wahujumu uchumi, akalala na wazembe na Rais akaweka msimamo mkali kulinda madini na rasilimali zetu zote ikiwemo kujenga ukuta wa zaidi ya Km 25 kule kwenye migodi ya Tanzanite pamoja na kuanzisha sheria kali za kulinda rasilimali zetu za madini kama ile ya permanent act ya 2017, ajenda ya mapato ikawa ndio ya kwanza ambapo suala la kulipa kodi likawa la kwanza, jambo lililopandisha mapato kutoka milioni 850 kwa mwezi mpaka zaidi ya trilioni 1 na nusu.

Hoja zote walizozilalamikia na kuwapa nguvu wapinzani na kupata uungwaji mkono mkubwa kwa wananchi, Rais Magufuli akazifanya za kwanza na kuzitekeleza kwa nguvu na vitendo vyote.

Leo upinzani umekosa nguvu kabisa kwa sababu kila wanalotaka na lililowapa nguvu kubwa huko nyuma, Rais Magufuli amelifanya na kulitekeleza kwa spidi ya ajabu kwa miaka mitano tu. Hii ilithibitika pia na mafuriko ya kihistoria ambayo haikuwahi kutokea toka Tanzania ipate uhuru kwa kushuhudia msululu wa hamahama ya viongozi na wanachama wa vyama vya upinzani kwenda CCM kuunga mkono juhudi kubwa ya utekelezaji wa yale waliyoyataka huko nyuma.

Sasa hata hao wapinzani kidogo waliobaki wametepeta hatari. Hawana hoja tena wanayoweza kusimama jukwaani kuieleza wakakubarika tena kwa wananchi na ndio maana wengi wao wameishia kudanganya watu, kupotosha, kulalamika na kutia huruma. Wataongea nini Magufuli hajafanya, watanadi nini wakati hoja zao zote zimetekelezwa. Wao wenyewe wameona, Watanzania wameona na dunia imeona na ndio maana palikuwa na mfululizo wa takwimu ambazo ziliiweka Tanzania uchumi wa kati na kuwa moja ya nchi 10 zenye maendeleo makubwa Afrika kwa kipindi kifupi tu cha Rais John Magufuli. Wapinzani wanapinga nini? Wanataka nini tena?

Maendeleo hayaletwi kwa kupinga maendeleo yanayofanyika.
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom