Wapinga Muungano Washtakiwa kwa 'Uhuni'

abdulahsaf

JF-Expert Member
Aug 31, 2010
858
130
polisi-564x272.jpg


Salma Said,

KESI ya watu 12 wanaopinga Muungano jana imesomwa katika Mahakama ya Wilaya ya Mwanakwerekwe Mjini Zanzibar huku baadhi ya watu kadhaa wakiwa wamefurika katika Mahakama hiyo kusikiliza. Kesi hiyo imesikilizwa chini ya hakimu Omar Mcha Hamza na kusomewa mashitaka matatu tofauti ambayo hata hivyo wote kwa pamoja waliyakana makosa hayo.

Waliofikishwa mahakamani hapo ni pamoja na kiongozi wao Rashid Salum Ali (48) mkaazi wa Kikwajuni, Khamis Hassan Hamad (51) wa Jang'ombe, Rashid Ali Rashid (21) anayeishi Mombasa, Hashim Juma Issa (54) mkaazi wa Mbweni.

Wengie ni pamoja na Suleiman Mustafa Suleiman (31) anayeishi Mombasa pamoja na Haji Sheha Hamadi (49) anayeishi Chumbuni, Rami Mbaraka Ahmed (48) wa Michenzani na Salum Masoud Juma (38) anayeishi Rahaleo.

Wengine walioyajwa katika kesi hiyo ni Mussa Omar Kombo (67) mkaazi wa Mpendae, Omar Kombo Is-hak (21) wa Magogoni, Ali Omar Omar (54) anayeishi Bububu na Masoud Faki Massoud (31) mkaazi wa Kilimahewa.

Wote hao kwa pamoja wameshitakiwa kwa makosa ya kufanya mkusanyiko usio halali, kuendelea kukusanyika baada ya kutangazwa kutawanyika na Ofisa wa Pilisi pamoja na shitaka la uhuni na uzururaji.

Mashitaka hayo yaliwasilishwa na Mwendesha Mashitaka wa mahakama hiyo Said Ahmed Mohammed, Mwanasheria wa serikali kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka Zanzibar (DPP).

Akiendesha kesi hiyo mahakamani hapo, Mwanasheria huyo wa serikali aliwasomea watuhumiwa hao shitaka la kufanya mkusanyiko usio halali kinyume na vifungu vya 55 (1) (2) (3) na 56 vya kanuni ya adhabu sheria namba 6/2004 sheria za Zanzibar.

Katika shitaka hilo aliifahamisha mahakama kwa kudai kuwa, April 20 mwaka huu, majira ya saa 2:30 za asubuhi, huko Mbweni wilaya ya Magharibi Unguja, kwa pamoja na bila ya halali watuhumiwa hao walijikusanya katika barabara ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar.

Alidai kuwa, mkusanyiko huo uliwafanya majirani na watu waliokuwa wanakwenda kwenye Baraza kupata khofu, kuwa wangeliweza kusababisha uvunjifu wa amani wakati hawakuwa na sababu za msingi za kukusanyika.

Akielezea shitaka la kuendelea kukusanyika baada ya kutangazwa kutawanyika na Ofisa wa Polisi, Mwanasheria huyo alidai kuwa baada ya mkusanyiko huo walitakiwa kutawanyika kwa amani na Ofisa wa Polisi, lakini waliendelea kukusanyika kinyume cha sheria.

Kwa mujibu wa Mwanasheria huyo, kitendo hicho cha kukataa amri hiyo halali ni kosa kwa mujibu wa kifungu cha 60 cha kanuni ya adhabu sheria namba 6/2004 sheria za Zanzibar.

Shitaka la mwisho linalowakabili watuhumiwa hao ni la uhuni na uzururaji, ambapo mahakama ilifahamishwa kuwa siku hiyo walipatikana wakiwa wamejikusanya kwenye barabara hiyo ya Baraza la Wawakilishi, wakiwa na mabango yenye maneno yanayopinga Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

Kitendo hicho ambacho ni kosa chini ya kifungu cha 182 (d) cha sheria namba 6/2004 sheria za Zanzibar, ambacho walidaiwa kukifanya katika wakati na mazingira yanayoonesha kuwa hawakuwa na madhumuni halali.

Mahakama ilipowapa nafasi watuhumiwa hao kujibu madai hayo ya upande wa mashitaka waliyakana, na Mwanasheria huyo wa serikali kudai kuwa upelelezi wake bado haujakamilika.

Mwanasheria huyo aliiomba mahakama hiyo kuiahirisha kesi hiyo na kuipangia tarehe nyengine kwa ajili ya kutajwa, ili kutoa nafasi ya kuweza kukamilisha upelelezi huo.

Baada ya hoja hizo, watuhumiwa hao waliomba mahakama hiyo iwapatie dhamana ombi ambalo hata hivyo upande huo wa mashitaka haukuwa na pingamizi nalo.

Wahutumiwa hao iwapo watakuwa na wadhamini madhubuti watakaoweza kutekeleza masharti ya dhamana yatakayotolewa na mahakama hiyo.

Kwa kuzingatia hoja za pande mbili hizo, hakimu Omar Mcha Hamza pamoja na kuwapatia watuhumiwa hao masharti ya dhamana lakini alifahamisha kuwa endapo watashindwa kuyatekeleza watalazimika kubakia rumande hadi kesi hiyo itakapotajwa tena.

Masharti hayo kila mtuhumiwa, awasilishe dhamana ya fedha taslimu shilingi 500,000 pamoja na wadhamini wawili wenye vitambulisho kikiwemo cha Mzanzibari Mkaazi, na mmoja kati ya wadhamini hao awe ni mfanyakazi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar. Kesi hiyo imeakhirishwa hadi Mei 7 mwaka huu kwa kutajwa tena.


Chanzo: Zanzibar yetu
 
Back
Top Bottom