GE2025 Wao wamepeleka baiskeli, sisi ADC tunapeleka Ng'ombe ili tutoke ngoma droo

GE2025 Wao wamepeleka baiskeli, sisi ADC tunapeleka Ng'ombe ili tutoke ngoma droo

Matukio, Taarifa, Habari na Mijadala ya Wananchi WAKATI wa Mchakato wa Uchaguzi Mkuu 2025

Just Pray

JF-Expert Member
Joined
Nov 7, 2023
Posts
2,142
Reaction score
4,777
Mwenyekiti wa Chama cha Alliance for Democratic Change (ADC), Shaban Itutu, amehoji uwiano wa mamlaka kati ya Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa na Tume Huru ya Uchaguzi, akisema kuna mgongano unaoweza kuathiri haki na uwazi wa uchaguzi.

Akizungumza Jumatatu, Agosti 18, 2025, katika Mafunzo kuhusu Sheria ya Gharama za Uchaguzi kwa Viongozi wa Kitaifa wa Vyama vya Siasa kwenye Ukumbi wa Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC), Itutu amesema kuwa mgongano huo wa kisheria unajitokeza pale ambapo Msajili ana mamlaka ya kupokea pingamizi dhidi ya wagombea huku Tume nayo ikiwa na nguvu ya kuwaondoa wagombea.

“Suala la rushwa na misukosuko ya kisheria limekuwa likiwatoa wanasiasa kwenye mtiririko mzuri wa ushindani wa haki. Kwa sasa Msajili ndiye mwenye mamlaka ya pingamizi, wakati Tume nayo inaweza kuwaondoa wagombea. Hali hii inaleta mkanganyiko mkubwa,” amesema Itutu.

Aidha, Itutu amelalamikia kile alichodai ni unyanyasaji wa Polisi dhidi ya wagombea wa upinzani wakati wa kampeni, akisema baadhi yao hukamatwa bila sababu za msingi.

“Polisi wamekuwa wakitusumbua kwenye kampeni. Wakiona mgombea ambaye hatokani na dola, mara moja anakamatwa. Tulishaomba hata kwenye mikutano kama hii na wao wawepo ili wajifunze kuwa kazi yao si kuwatisha wanasiasa,” ameongeza.

Akizungumzia Sheria ya Gharama za Uchaguzi, Itutu amesema haipaswi kuibana ADC, kwa kuwa chama hicho kimejipanga kwa kampeni za kipekee zenye muonekano wa kitamaduni na kisherehe.

“Sisi ADC tumepanga kila tutakapotembea, kila kituo tutachinja ng’ombe. Mimi nikienda kuchukua fomu Jimbo la Ilemela, tutaanzia Dar es Salaam hadi Mwanza tukifanya ngoma na droo. Wengine wamepeleka baiskeli, sisi lazima twendane na droo yetu,” amesema Itutu.

Mafunzo hayo yamekusudiwa kuongeza uelewa wa viongozi wa vyama juu ya utekelezaji wa Sheria ya Gharama za Uchaguzi, sambamba na maandalizi ya kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2025.


 
Back
Top Bottom