Wanne Singida wasombwa na mto, Serikali mnataka wafe wangapi?

Suphian Juma

Senior Member
Apr 2, 2019
133
546
WATU WANNE WASOMBWA NA MTO SINGIDA, SERIKALI MNATAKA WAFE WANGAPI MZINDUKE?


Na: Suphian Juma


Januari 8, 2020 niliandika katika Mitandaoni, na andiko hilo kuchapishwa pia na Gazeti la Tanzania Daima kwamba Katika Wilaya ya Ikungi, Singida kuna madaraja mawili "tegemewa sana" katika mito miwili tofauti yanayoiunganisha Kata ya Minyughe na Kata zingine, YAMEVUNJIKA zaidi ya mwezi.


Katika andiko langu nilimsihi Mkuu wa Wilaya ya Ikungi aachane na kuwasweka mahabusu vijana waendesha Noah, waliogoma darajani kwa lengo la kutaka madaraja ya Mto Saiwa na Ntika yajengwe, na hivyo DC na Mamlaka husika wadili na Tatizo la Daraja, walitatue waokoe maisha ya watu.


Aidha nilitoa tahadhari na kuhoji, kwamba katika Daraja la Mto Saiwa, kuna mtoto wa miaka mitano amefariki dunia baada ya gari aliyobebwa kushindwa kupita hapo kuelekea Hospitali ya Mkoa wa Singida, na hivyo nikahitaji kama mwananchi, daraja lijengwe haraka, tusisubiri watu wengine zaidi wapoteze maisha.


Sikuishia hapo katika ushauri wangu kwa Serikali ni kwamba, vema wachukue hatua za haraka kujenga madaraja hayo mawili, ama wakiwa kwenye 'process' ya kuyajenga, waangalie namna/njia mbadala ya wananchi kupita wakisubiria madaraja ya kudumu, kwakuwa si tu kutokwepo madaraja haya panatishia uhai wa wananchi bali pia shughuli za uchumi zimesimama, ukizingatia sasa ni majira ya mvua, mito inajaa karibia kila siku.


HADI SASA SIKUSIKILIZWA, WALA WANANCHI WANAOLALAMIKA KILA SIKU HAWAKUSIKILIZWA NA HAKUNA HATUA YOYOTE YA DHARURA ILIYOCHUKULIWA.



Sasa ukaidi huu wa Serikali ya Magufuli umesababisha watu wanne (wanaume wawili na mama na mtoto) wamesombwa na maji ya Mto Ntika Januari 18, 2020 walipojaribu kupita baada ya kukosa daraja la kupitia, kuanzia Jana Januari 19 hadi Leo Januari, 20, 2020 wameokotwa wakiwa wamekufa. INAUMA SANA! TENA SANA!



Naulizia tena, Serikali upo kwa ajili ya nani? Kama wananchi hawa ndio wanalipa kodi kuwalipa mishahara, halafu hamuwalindi wao na uhai wao, mna maana gani kuwepo hapo maofisini? Au kwakuwa hawa wananchi sio ndugu zenu wa damu? Au mnataka wafe hadi wangapi ndio msikilize vilio vyao?



Tafadhali, nendeni mkajenge vivuko vya dharura wananchi waweze kupita katika mito hii. Kuweni na UBINADAMU, wajibikeni kwa wananchi.



Suphian Juma,

Afisa Habari, ACT wazalendo na Mzaliwa wa Singida.

Januari 20, 2020.



Andiko lililoliandika Januari 08, 2020


DC WA IKUNGI, SINGIDA JENGENI DARAJA LA MINYUGHE, WATU WANAKUFA, UCHUMI UMESIMAMA, ACHENI UBABE NA JANJA JANJA.


Na: Suphian Juma


Kama Mtanzania niliyezaliwa Mkoa wa Singida na hata kama nisingezaliwa huko, nimefadhaishwa na taarifa kwamba DARAJA LA MTO SAWIA ambalo linaiunganisha Kata ya Minyughe na Kata Kata zingine kama Makilawa na Iyumbu, limevunjika (limekaribia kuzama kabisa) takribani mwezi sasa na kuleta tafrani kwa wananchi isiyo kifani.


Wananchi wa maeneo haya wamelalamika sana kwa viongozi wao wa ngazi ya Kijiji, Kata hadi Wilayani bila mafanikio. Ikumbukwe sasa ni majira ya mvua, ambapo karibia kila siku mto Sawia huwa umejaa, na hivyo kusababisha maelfu ya wananchi kushindwa kusafiri katika pande hizo mbili ambazo kimsingi zina mahusiano makubwa ya kibiashara, kiuchumi na kijamii.


Sio hivyo tu; wananchi pia wanapata wakati mgumu mno hata kwenda Ofisi za Wilaya yao ya Ikungi ama kwenda Ofisi za Mkoa wao wa Singida kupata huduma za kiutawala pale, inapobidi, maana mfano mwananchi wa Mtavira ili afike Halmashauri ya Ikungi au Singida Mjini lazima akatishe Mto huo.


Imagine; majuzi nataarifiwa kuna mtoto wa miaka ipatayo mitano amefariki hapo darajani baada ya wazazi wake waliotokea upande wa Mtavira kukesha hapo na gari bila kupata namna mbadala ya kukatisha ng'ambo ya pili ili wawahi kwenda kwenye matibabu katika Hospitali tegemewa ya Mkoa wa Singida.


Cha pili kinachokera zaidi; Jana baada ya malalamiko ya wananchi ya muda mrefu bila kusikilizwa, vijana waliojiajiri na wengine kuajiriwa katika usafiri wa gari ya aina ya 'Noah' unaotumiwa kuwasafirisha wananchi wa pande hizo mbili; kwa kutaka kupaza sauti zao, walipogoma hapo darajani, Mkuu wa Wilaya ameenda na Polisi badala ya kukisikiliza kilio chao, yeye AKAAGIZA WAKAMATWE na hatimaye kusekwa ndani kwenye kituo cha Polisi cha Wilaya ya Ikungi.


Yaani Mkuu wa Wilaya unaenda kwa wananchi wako badala utoe mpango mbadala kuwasaidia wananchi wako, unawakamata hao vijana wanne na kuwaweka mahabusu bila dhamana tangu Jana Jan 7, 2020 hadi leo Jan 8, 2020 ndio unawaachia na kuwaagiza wakaripoti Ijumaa ya kesho kutwa, huku ndio kulijenga daraja??


DC tunakuuliza kuwakamata hao vijana ndio njia mbadala ya kulijenga daraja? Kama mmeambiwa mwezi sasa daraja limevunjika, mpo kimya, hakuna suluhu ya dharura, mlitaka wananchi watembee kwa magoti hadi mlipo? Watumie njia gani kuwaeleza maumivu yao?


Yes tunajua mnawatisha hivi ili wao na wananchi wengine wakae kimya, na wakikaa kimya, hamuoni wagonjwa watazidi kukata roho hapo bila msaada? Au wakifa wengi zaidi ndio furaha yenu? Na mnafurahia kazi za kiuchumi zisimame? Maendeleo gani mnayoyataka nyie wawakilishi wa Serikali ya Rais Magufuli?


Halafu mnawachukua vijana mnawasekwa ndani bila dhamana, hivi kugoma hapo kwa jambo nyeti la maisha ya wananchi ndio tuseme imegeuka Uhujumu uchumi ama Ukatatishaji fedha ambao hauna dhamana? Mmetumia Sheria gani? Mtasema ile ya DC ya masaa 24? Kwa kosa hili? Sheria gani tuambieni au ubabe tu dhidi ya wanyonge? Ooops!!


Hold on; hivi Mbunge wangu wa Singida Magharibi, Elibariki Kingu, uko wapi wananchi wako wanateseka bila daraja? Vijana wako wanasekwa rumande 'kiholela holela'? Wewe unamwakilisha nani Bungeni? Rais Magufuli au? Au unasubiri kampeni zifike ukaendeleze stori zako za ahadi hewa kama za mwaka 2015? Come on show your presence, ni wajibu wako, wananchi hawa wanakulipa mshahara, watendee haki.


RAI YANGU;


Mkuu wa Wilaya achana na hao vijana, umeenda Minyughe, umeliona tatizo, tunajua unajua namna ya kufanya na Kiongozi/Viongozi/Mamlaka gani ya kukusaidia utufanyie yafuatayo;


1. Kwa haraka sana, kwa udharura, kwa ajili ya uhai wa wananchi, watengenezeeni njia mbadala ya kukatisha huo mto wakati;


2. Mnafanya utaratibu wa kulijenga upya au kuboresha hilo daraja kwa kiwango vinavyostahili na si vile dhoofu vilivyosababisha dhahama hii.


3. Jengeni daraja la Mto Ntika pia kimesemwa na maji zaidi ya miezi sasa, watu wa Minyughe wanashindwa kwenda Minyughe, msisubiri hadi wananchi wasombwe pia na maji.


4. Chunguzeni zile tuhuma za baadhi ya viongozi wa Kata hizo za Minyughe na Makilawa wanaopokea rushwa na kuruhusu magari makubwa kupita usiku. Ni hatari kwa uhai wa madereva hao na si maadili ya Kiuongozi.


Suphian Juma,


Afisa Habari ACTwazalendo,


Kijiji cha Minyughe,


Januari 08, 2019.



20200115_193604.jpeg
20200108_205203.jpeg


Sent using Jamii Forums mobile app
 
Back
Top Bottom