TUME ya Kudhibiti Ukimwi Tanzania (TACAIDS) imewataka wananchi kuchukua tahadhari ya maambukizi mapya ya Virusi vya Ukimwi (VVU) kutokana na watu 10 kwa saa kila siku kupata maambukizi hayo.
Akizungumza jana katika semina ya Kamati ya kudumu ya Bunge inayoshughulikia Ukimwi, dawa za kulevya na kifua kikuu na kamati ya bunge inayoshughulikia sheria ndogo, Mkurugenzi Mtendaji wa TACAIDS, Dk. Leonard Maboko, alisema katika utafiti uliofanywa mwaka 2016/17 kwa kushirikiana na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) ilionyesha kiwango hicho cha maambukizi kwa saa.
Alisema kuanzia Januari hadi Desemba walikadiria maambukizi mapya kila mwaka ni watu 72,000, hivyo ni vyema wakachukua tahadhari kujiepusha na hali hiyo na pia kujitokeza kupima ili kujua afya zao. Kwa mujibu wa Mkurugenzi huyo, kwa mwezi ni watu 6,000, kwa siku ni watu zaidi ya 200 na kwa saa ni watu 10 kila siku wanapata maambukizi mapya ya virusi.
Takwimu hizi zinabainisha kuwa hali ya maambukizi ya VVU inatisha, hivyo kinachotakiwa ni kwa jamii kushtuka na kuchukua hatua zaidi za kuepusha tishio hilo kuwa janga zaidi kwa jamii yetu. Ikumbukwe kwamba mwarobaini dhidi ya maambukizi mapya ya virusi ni kuchukua tahadhari wakati wote, na tahadhari dhidi ya VVU ambavyo husababisha ugonjwa hatari wa Ukimwi inajulikana. Tunasema hivyo kwa kuwa kila uchao serikali, wadau na wataalamu wa afya wamekuwa wakitoa elimu kwa umma kupitia njia mbalimbali kama semina, mikutano, warsha, makongamano, mijadala pamoja na vyombo vya habari. Tahadhari ni kuacha vitendo vya zinaa, kutumia mipira wakati wa kufanya tendo la ndoa, kupina afya mara kwa mara ili kuepuka kuambukizana, kwa kutaja baadhi
Hata hivyo, tunachokiona sisi kuwa kichocheo cha maambukizi mapya ya virusi ni jamii kukaidi ushauri huo utolewao kila uchao wa kuchukua tahadhari wakati wote. Hili linathibitishwa na kutolewa takwimu zinazoonyesha kupungua kwa maambukizi, lakini baada ya muda fulani maambukizi kuongezeka.
Ushauri wetu kwa jamii ni kuwa ifike mahali ibadilike kwa kuacha uzembe na ukaidi pale inapopewa ushauri na wataalamu wa afya kuhusiana na hatua za kuchukua kuepusha maambukizi mapya ya VVU. Ukweli huo inatokana na kila mmoja kuwa ameshaguswa na janga la Ukimwi kwa kupoteza ndugu, jamaa, rafiki au jirani. Tunapaswa kukumbuka kila wakati kuwa hadi sasa Ukimwi hauna tiba wala kinga, hivyo njia pekee ni kijiepusha na maambukizi mapya.
Kujiepisha na maambukizi mapya ni kitu kinachowezekana ikiwa kila mmoja katika nafasi yake atatambua kuwa Ukimwi ni janga la taifa, hivyo kuchukua tahadhari kwa ajili ya kuzuia maambukizi. Ndiyo maana serikali imekuwa ikitumia rasilimali na kuda kuhakikisha maambukizi ya VVU yanapungua kwa kiwango kikubwa kama si kuisha kabisa, kwa lengo la kuhakikisha kuwa taifa linabaki na rasilimali watu kwa ajili ya kukuza uchumi na maendeleo yake. Ni matumaini yetu kuwa kila mmoja atatafakari takwimu hizi mpya za TACAIDS ambazo zinatisha, hivyo kuchukua hatua za kujiepusha dhidi ya maambukizi mapya ya VVU. Kimsingi, kuelezwa kuwa watu 10 kwa saa kila siku wanapata maambukizi hayo, ni jambo ambalo kwa mtu mwenye akili timamu hushtuka na kujitafakari kuhusu hatima ya maisha yake.