Wanafunzi wote wa bweni kupimwa Kifua Kikuu

Display Name

JF-Expert Member
Feb 11, 2014
423
451
WANAFUNZI wote katika shule za bweni nchini, wametakiwa kupimwa kujiridhisha na afya zao, ikiwemo ugonjwa wa kifua kikuu (TB) na kuondokana na ujazaji wa fomu za afya bila kupimwa.

Agizo hilo limetolewa na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu ambaye ameagiza shule zote za bweni, kutekeleza kazi hiyo na wakati huo huo waganga wakuu wa kila mkoa, wametakiwa kufanya ukaguzi kama utekelezaji umefanyika.

Ummy alisema hayo jana jijini Dar e s Salaam wakati akikabidhi magari 10 na pikipiki 35 kwa uongozi wa mikoa, kwa ajili ya kusimamia na kuhakikisha wananchi wanapatiwa huduma ya kifua kikuu na ukoma ipasavyo.

“Waganga wakuu wote, pitieni mkague shule zilizoko katika mikoa yenu, hakikisheni wanafunzi wamepimwa na siyo kujaziwa fomu za afya kiholela huku afya zao zikiwa hazieleweki,” alisema Ummy.

Alisema, “Wazazi wamekuwa wakishiriki kutoa fedha hata elfu kumi ili watoto wao wajaziwe fomu za afya mashuleni, bila kupimwa, jambo ambalo linaonesha kuwa hakuna umakini katika kuzingatia afya.” Aliwataka madaktari kuzingatia miiko ya kazi zao kwa weledi kama inavyostahili. Alisema ni muhimu kwa waganga wakuu wa mikoa na wilaya, kutembelea shule za bweni kujua kama wanafunzi wamepimwa.

Aliwaelekeza kukagua fomu za afya, kwa kuwa wapo wanafunzi wanaokwenda shuleni wakiwa wanaumwa, jambo ambalo wanaweza kuambukiza wengine. Kuhusu magari na pikipiki, alisema yamenunuliwa na serikali kupitia wizara wakishirikiana na Shirika la Kijerumani la Mapambano dhidi ya Kifua Kikuu na Ukoma (GLRA).

Yamegharimu Sh milioni 778 lengo likiwa ni kuhakikisha huduma zinawafikia wananchi kwa wakati. Alisema yatasaidia katika usimamizi wa shughuli za mpango, kuhakikisha wagonjwa wa kifua kikuu na ukoma wanapatiwa elimu, wanagunduliwa na kupatiwa matibabu.

Alitaja mikoa iliyokabidhiwa magari hayo ni Lindi, Tabora, Songwe, Kilimanjaro, Ilala, Mtwara, Kagera, Rukwa, Ruvuma na Pwani. Pikipiki zimegawiwa katika halmashauri 35. Kwa mujibu wa waziri, kila mwaka Tanzania inakadiriwa kuwa na wagonjwa wapya wa kifua kikuu wapatao 154,000.

Kati yao, asilimia 44 ndiyo waliogunduliwa. Mwakilishi Mkazi wa GLRA, Burchard Rwamtoga alisema kuanzia mwaka 2016 shirika limekuwa likisaidia wizara kununua magari kwa bei nafuu hususani fedha zinazotolewa na Global Fund.

Alisema ununuzi wa magari kwa njia hiyo, una nafuu na wamenunua magari matatu zaidi na pikipiki 35 badala ya 28.

Sent using Jamii Forums mobile app
 
Haya ni maamuzi ya busara lakini tatizo ni utekelezaji. Wanashindwaje kuwapa utaratibu kuwapima wakiwa mashuleni ili kuhakikisha kila mwanafunzi anapimwa?
 
Hii liko sawa lakini naona hapo ni hela kubwa kumpa mtoto ambaye haoni thamani .
 
Ni kweli kabisa... watu wanatabia hizo za kutaka kujaziwa medical forms...

Hili tatizo linachangiwa sana na gharama za kufanya vipimo vyote...


Cc: mahondaw
 
Back
Top Bottom