Wanafunzi TAMOSE watelekezwa kwa muda wa mwaka mzima

Boa vida

New Member
Dec 25, 2019
1
0
KWAKO WAZIRI MKUU WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA.
Part I.
TULICHOJIONEA MAPUTO KWENYE PROGRAM YA TAMOSE (Tanzania and Mozambique Students Exchange program):

 WANAFUNZI WATELEKEZWA TOKA FEBRUARY 2019,
 WENGINE WATUMIWA NAULI KIMAKOSA KABLA YA KUMALIZA MASOMO.
• Wakata Rufaa, waonekana kuwa na haki lakini waambiwa (Hatuwapangii Mkopo kwa sababu tulishawatumia nauli ya kurudi)
• Baadhi wajilipia ili kumalizia masomo yao, wengine washindwa kumaliza, baadhi warudi nyumbani.
 BAADHI YAO WATELEKEZWA MWAKA MZIMA BILA MKOPO WALA NAULI
• Wakaa mwaka mzima bila msaada wowote
• Walinyimwa mkopo na wakasahaulika nauli.
• Wamo wasichana ambao huishi bila matumaini ya kuiona kesho yao.

 PESA ZA BAADHI YA WALIOSIMAMA KUSOMA MWAKA MZIMA KWA KUUMWA/KUACHA MASOMO ZALIWA,
• Walazimishwa kwamba pesa ya muda wote walishatumiwa, bank statements zaonesha kutokufanyika malipo yoyote toka HESLB kwa mwaka husika
• HESLB yashikilia msimamo kwamba ilishatuma hizo pesa, yatuma mwakilishi wake kuja kujichunguza ili kufunika kombe.
 HESLB YASHINDWA KULIPA ADA ZA WANAFUNZI KWA MUDA.
• Wanafunzi wafukuzwa kwenye vyumba vya mitihani

 WAZIRI APEWA TAARIFA ZA UONGO NA KUFANYA MAAMUZI BILA UCHUNGUZI.

Na Mwandishi Wetu.
Katika hali ya kusikitisha, wanafunzi waliopo masomoni kwa program ya kubadilishana wanafunzi iliyoanza wakati wa rais Jakaya Kikwete wametelekezwa na wizara ya elimu pamoja na bodi ya mikopo wakiwa mwishoni mwa masomo yao.
Sokombingo la wanafunzi hawa lilianza mwanzoni mwa mwaka huu baada ya baadhi yao kuonekana wako nje ya muda wa masomo (Overstay). Katika hali ya kuonesha kutokuwa makini na kutokuwa na taarifa sahihi, bodi ya mikopo ilituma majina ya watu 78 walioonekana kuwa nje ya muda wa masomo ambapo uongozi wa wanafunzi ulizipinga taarifa hizo na kuiomba bodi ya mikopo ipitie upya taarifa zake. Bodi ya mikopo baada ya kupitia upya taarifa,ilipunguza majina na kubakiza majina 41 ya wanafunzi ambao ilituma taarifa kwenda ubalozini kuwa wapo nje ya muda. Uongozi wa wanafunzi baada ya kuona kuwa wanafunzi hawatendewi haki na wanazidi kucheleweshwa kwenye masomo yao, mwezi wa tatu wanafunzi waliuomba ubalozi uingilie kati kwa kuwaita wizara ya elimu watume wachunguzi na kutuma taarifa sahihi juu ya wanafunzi 41 ambao walisemekana kuwa nje ya muda kwani ndani ya wanafunzi hao 41, ni wanafunzi wachache tu ambao ndio hasa walikuwa nje ya muda. ubalozi uliahidi kufanya hivyo na baada ya muda wa kama mwezi mmoja hivi mbele wa mawasiliano kati ya ubalozi na bodi ya mikopo, majina yalipungua tena hadi kufikia 32 yaani wanafunzi tisa walitumiwa pesa ya kujikimu na wengine wakaendelea kuambiwa wapo nje ya muda. Ikumbukwe wakati haya yakiendelea, masomo ya wanafunzi yalikuwa yalishaanza toka mwezi wa pili kwa maana hiyo wanafunzi hawa waliendelea kusoma bila pesa.

Mwezi wa nne wanafunzi waliuomba ubalozi tena uiandikie barua wizara itume wakaguzi ili kuja kujionea hali halisi ya mfumo wa elimu ya Mozambique na ili watende haki kwa wanafunzi ambao wako ndani ya muda na wanastahili kupewa mkopo na ubalozi ukaahidi kufanya hivyo na hawakuishia hapo kwani walimpigia simu Katibu Mkuu wizara ya elimu na kumweleza juu ya suala hili. Katibu Mkuu aliahidi ndani ya wiki moja, yeye mwenyewe na timu yake wangeenda kushughulikia suala hili na kupata taarifa sahihi kutoka vyuo vya wanafunzi na hatimaye wanafunzi waliokuwa wanastahili kupewa pesa wapewe na wale waliostahili kurudishwa nyumbani wapewe nauli. Wanafunzi walisubiri ujio wa Katibu mkuu hadi tarehe 03 June 2019 walipoitwa na ubalozi na kupewa taarifa iliyotolewa maamuzi tarehe 29 May 2019 ya kusitishwa mkopo wao na kutakiwa kurudi nyumbani na kama kuna mwanafunzi anaona hakutendewa haki, aende akakate rufaa wizarani. Baada ya muda wa kama wiki mbili mbele, bank iliwapigia simu kuwataarifu kuwa kuna pesa imetumwa na waende na barua za kuthibisha ili wawekewe kwenye account zao. Pesa iliyokuwa imetumwa ni pesa ya nauli na ilitumwa bila wanafunzi kufanya maombi. Ikumbukwe kwa mujibu wa barua ya Katibu Mkuu kwenda kwa wanafunzi wa kitanzania nje ya nchi yenye Kumb. Na. FA.348/502/01A/80 ya tarehe 24 April 2018 inaeleza; “Wanafunzi wanaosoma nje ya nchi chini ya utaratibu wa mikopo inayotolewa na HESLB hupewa mkopo wa nauli (ticket) ya ndege wakati wa kuanza masomo na hutumiwa nauli wakati ANAPOMALIZA MASOMO.

Pamoja na maelezo ya katibu mkuu, baadhi ya wanafunzi hao waliokuwa ndani ya muda wa masomo, kwa uzembe wa wizara na HESLB, walitumiwa nauli kabla hawajamaliza masomo, wakiwa ndani ya muda wa masomo na bila kufanya maombi ya nauli hiyo. kwa maana hiyo, kwa mujibu wa barua ya Katibu Mkuu, kama kigezo cha mwanafunzi kutumiwa nauli ya kurudi ni kumaliza masomo, kwa nini wanafunzi hawa watumiwe nauli kabla hawajamaliza?? Tena kabla uchunguzi haujafanyika juu ya malalamiko yao?

WANAFUNZI WAKATA RUFAA KAMA BARUA YA KUSITISHA MASOMO YAO ILIVYOTAKA
 Wizara yaamua kutuma wakaguzi
 Wakaguzi wahakiki kwamba kuna wanafunzi hawakutendewa haki, wapo ndani ya muda
 HESLB yagoma kuwapatia pesa za kujikimu, yatoa sababu kuwa ilishawapa nauli ya kurudi.
Mnamo mwezi wa saba, baada ya wanafunzi wenyewe kuamua kuomba taarifa sahihi za kila kozi kutoka kwenye vyuo vyao, walituma mwakilishi wao ambaye alienda wizarani na kukutana na Katibu Mkuu pamoja na mkurugenzi wa Elimu ya Juu ambapo wizara iliamua kutuma wakaguzi wake ili kushughulikia madai ya wanafunzi na mwezi wa tisa wakaguzi walienda Mozambique. Wanafunzi ilibidi wafuatilie wenyewe taarifa za kila kozi kwa sababu kwanza wizara na HESLB haikuwasikiliza toka mwanzo na haikuwa tayari kutuma watu wake ili kuja kujionea kama wanafunzi bado wapo masomoni, pili ubalozi baada ya kuona wizara ya elimu haijishughulishi na wanafunzi wake toka february uliamua kujiweka pembeni na suala hilo kwa hiyo wanafunzi wakawa wamekosa msaada.

Kwa mujibu wa ukaguzi uliofanyika kutoka kila kozi,
 kuna kozi zilionekana wanafunzi wake hawakupewa mwaka wa nyongeza huku baadhi ya kozi wakiwa wamepewa. Hali hiyo imefanya wanafunzi hao kushindwa ku-concentrate vizuri kwenye masomo yao ama kushindwa kuhudhuria kabisa vipindi.
 kuna wanafunzi wengine ambao bado walikuwa ndani ya muda wa masomo na hawakupewa pesa kimakosa na kwa maana hiyo walistahili kupata haki yao. Mfano, mwanafunzi ‘C’ ambaye kozi yake ni miaka minne na yupo ndani ya mwaka wa nne, akiwa amekamilisha kutuma kila kitu HESLB walichokihitaji toka kwake, mpaka leo hajapata hela ya kujikimu na ni moja ya wanafunzi ambao hata nauli walisahaulika kutumiwa.
 Ada haijalipwa kwa muda mrefu na vyuo vimewasiliana na ubalozi mpaka baadhi ya kozi wakafikia hatua ya kuwafukuza wanafunzi/kuwanyima mitihani na hivyo wanafunzi hawa kujikuta wakiongeza muda wa masomo kwa uzembe wa wizara.
 Baadhi ya kozi ambazo zina miaka minne na kuendelea, hakuna mwanafunzi hata mmoja anayefanikiwa kumaliza mwaka wa nne na badala yake wanafunzi bora humaliza mwaka unaofuatia (mwaka wa tano). Tatizo hili si la wageni tu bali hata wenyeji wazawa. Hali hii ilisababisha mabishano kati ya wizara na wanafunzi juu ya muda sahihi wa kuongezwa kwa mwanafunzi aliyepatwa na tatizo la kitaaluma. Wanafunzi walitaka muda wa kuongezwa uwe ni mwaka wa sita badala ya mwaka wa tano kwani kozi iliyoandikiwa miaka minne, hakuna mwanafunzi hata mmoja anayemaliza mwaka wa nne na mwaka wa tano ni kama 10% - 20% tu ya wanafunzi wote ndio wanafanikiwa kumaliza na 80% (include wazawa) wote wanaangukia mwaka wa sita. Suala hili hadi vyuo husika vililithibisha kwa njia ya barua na kutoa sababu ya kwamba mwanafunzi akishamaliza masomo ya kawaida, kama hakufeli somo lolote, huwa anaanza kufanya Final Project ambayo ndiyo humpeleka mpaka mwaka wa tano. Kwa hiyo mwanafunzi yoyote mwenye tatizo la kitaaluma ni lazima aende mpaka mwaka wa sita. Pamoja na hayo, vyuo vilisema, miaka hii miwili haipo kwenye mitaala ya vyuo lakini kitabu cha sheria za chuo (School Regulations) kinaitambua kama muda sahihi wa mwanafunzi kuwepo chuoni na hata vitambulisho vyao vya mwanafunzi vinajumuisha miaka miwili. Yaani kama mwanafunzi alianza masomo 2015 kitambulisho huonesha kuanza 2015 kumaliza 2020. Pamoja na maelezo ya vyuo, bado wizara ilishikilia msimamo wa kuongezwa mwaka unaofuta baada ya miaka ya kwenye mtaala hali inayowaacha na kuwakomoa wanafunzi wa kitanzania kwani, kama wanafunzi wazawa wanaweza kufaulu 10% mwaka wa tano na mwaka wa nne uliopo kwenye mtaala hakuna hata mmoja anayefaulu, ni vipi mwanafunzi mgeni wa lugha anaweza kuingia ndani ya 10% na kumaliza ndani ya muda(mwaka wa tano) bila kupatwa tatizo lolote?

Wakaguzi waliporudi wizarani, mwezi wa kumi walisoma ripoti yao wizarani na walipendekeza watu kadhaa walipwe, ambapo baada ya wizara kujiridhisha na madai hayo ya wanafunzi, mwezi wa 11 ilituma majina ya wanafunzi bodi ya mikopo ili yashughulikiwe na waweze kulipwa. Bodi ya mikopo baada ya kukaa mwezi mzima, mwezi wa 12 ilituma list ya majina ya wanafunzi kwenda ubalozini ambapo wanafunzi wote wenye madai ya mkopo walinyimwa pesa kwa kigezo cha kwamba walishatumiwa nauli na ni mwanafunzi mmoja tu ambaye wakati wa kutumwa nauli, yeye alisahaulika ndiye aliandikiwa atapangiwa ambapo hadi sasa naye bado hajapangiwa. Kwa maana hiyo, wizara ilithibitisha pasipo na shaka kuwa wanafunzi kadhaa wanastahili kulipwa pesa ili wamalizie masomo yao lakini bodi ya mikopo ikaona haiwezi kuwalipa kwa sababu walishatumiwa nauli ambayo hata wao hawakuiomba.
Katika kundi la wanafunzi 32
 Lipo kundi lililostahili kupewa nauli maana lilikuwa nje ya muda
 Lipo kundi lilistahili mwaka wa kuongezwa maana taarifa za kozi zao hazikuwa sahihi wizarani na HESLB
 Lipo kundi ambalo wanafunzi bado wapo ndani ya muda wa kawaida wa masomo na kila taarifa iliyohitajika walituma lakini wakaendelea kusahaulika
 Lipo kundi ambalo liliahirisha masomo kwa mwaka mmoja na kutoa taarifa wizarani pamoja na heslb na pesa zao kusitishwa kwa muda wa mwaka huo kwa maana hiyo mwaka huu wakaomba mwaka wa kuongezwa wakitolea taarifa ya mwaka walioahirisha masomo.

PESA ZA BAADHI YA WALIOSIMAMA MASOMO NA KUFUATA TARATIBU ZOTE KWA KUTOA RIPOTI HESLB ZAPOTEA.
 Waambiwa wakitaka uchunguzi ufanyike, warudi ili wakafungue kesi
Katika hali nyingine, ndani ya kundi la watu 32, kuna mwanafunzi ‘A’ ambaye aliahirisha mwaka mmoja kutokana na kuugua na akapitia taratibu zote za kusimama kusoma kwa mwaka mmoja ikiwemo kutoa taarifa HESLB. Mwanafunzi huyo ambaye kozi yake ni ya miaka minne, alipofika mwaka wa sita aliomba mwaka wa kuongezwa(ambao ungekuwa mwaka wa tano kwake maana kuna mwaka hakupewa pesa) kwa sababu bado alikuwa anamalizia masomo yake lakini akaambiwa kumbukumbu za HESLB zinaonesha kwamba pesa yote alishalipwa hadi ule mwaka wa kuongezwa. Uchunguzi ulipofanyika ili kubaini kama ni kweli mwanafunzi huyu alilipwa na kama bank ilipokea pesa zake, bank ilitoa bank statements ambao zilionesha kuwa mwaka fulani mwanafunzi huyo hakutumiwa pesa.

Baada ya taarifa hiyo toka bank, na HESLB kushikilia msimamo kwamba pesa ilishatoka, mwanafunzi aliomba tena mwaka wake wa nyongeza lakini majibu yalitoka kwamba “Hawezi kupangiwa pesa kwa sababu alishatumiwa nauli” na afisa mmoja ambaye jina tunalihifadhi alimwambia “ sisi uchunguzi hatuwezi kufanya kwa sababu si kazi yetu” na kwamba akitaka kujua pesa yake ilienda wapi, achukue taarifa zake zote za kutoka bank halafu arudi Tanzania ili akafanye uchunguzi kwa kushirikiana na HESLB. Ikumbukwe aliyeambiwa hivi ni mwanafunzi, anatakiwa kuwa darasani na awe na pesa kwa ajili ya kuishi.

Pia kuna mwanafunzi ‘B’ aliacha chuo ila pesa yake ikatumwa. Wanafunzi wenzake wakampigia simu kwamba pesa yake imeingia na akarudi kuthibitisha, alipoenda bank hakukuta chochote na haifahamiki ni nani aliichukua. Taarifa za kuacha chuo kwa mwanafunzi huyo zilitolewa kabla ya kutumwa pesa.

PESA ZA KUJIKIMU ZA KILA MWAKA ZAPUNGUA BILA MAELEZO YOYOTE, RATE CHANGE YAWA KISINGIZIO
Katika hali nyingine ya kushangaza, kuanzia mwaka 2016 pesa za wanafunzi zilianza kupungua. Walipouliza ni kwa nini zinapungua, bodi ilisema (kwa mdomo) ni kwa sababu ya rate change
Ikumbukwe malipo yamegawanyika katika vipengele vifuatavyo
 Pesa za kujikimu ambazo ni kiwango “Y” kwa kila mwanafunzi
 Stationary fees ambazo ni dola 200 kwa mwanafunzi wa science na dola 100 kwa Arts.

Kwa maana hiyo, mwanafunzi wa sayansi alipewa kiwango “Y+200” na Arts “Y+100” lakini imefikia kipindi kwanza kiwango chote kikapungua kwa kama hadi dola 500 kwa kila mwanafunzi na pesa ya stationary fees ikapotea ghafla kwani wanafunzi wote walianza kupokea kiwango sawa kilicho pungufu ila wakiuliza ni kwa nini, jibu ni hilo hilo la rate change. Yaani rate change ikawa na effect mpaka kiwango kikawa sawa kwa wanafunzi wa Arts na Science na wote wakapokea kiwango “X”.


HESLB YASHINDWA KULIPA ADA, WANAFUNZI WAFUKUZWA KWENYE VYUMBA VYA MITIHANI.
Wakati ukaguzi wa wanafunzi vyuoni ukiendelea chini ya wakaguzi wa wizara, kulijitokeza suala jingine la wanafunzi kutokulipiwa ada kwa muda mrefu na baadhi ya vyuo wanavyosoma wanafunzi hao vimekuwa vikiwafukuza kwenye vyumba vya mitihani na taarifa zimewahi kupelekwa ubalozini ili zifanyiwe kazi na hakuna utekelezaji ambao umekuwa ukifanyika. Hali hiyo imesababisha baadhi ya wanafunzi washindwe kumaliza masomo yao na wengine kuongeza muda pasipo matarajio yao.


NINI KILISABABISHA WANAFUNZI KUAMBIWA WAPO NJE YA MUDA NA WARUDI NYUMBANI?
Wakati suala hili linaanza, waziri wa elimu hakupewa taarifa na wasaidizi wake (kwa mujibu wa taarifa tulizozipata kutoka kwenye vyanzo vyetu ) hadi mwanzoni mwa mwezi May baada ya balozi wa Tanzania Msumbiji kuishinikiza wizara ilifanyie kazi suala la wanafunzi hao na malalamiko yao. Kwa mujibu wa balozi mwenyewe ni kwamba, “waziri hakuwa na taarifa juu ya uwepo wa TAMOSE hadi muda huo kwani aliamini wanafunzi walishamaliza wote na TAMOSE ilishaisha” na kwamba balozi alipompigia simu waziri alikuwa Kigali Rwanda kwa ajili ya masuala ya kiofisi na baada ya kupewa taarifa hizo, waziri aliahidi akifika tu Dar es salaam angelishughulikia na kulimaza. Baada ya waziri kurudi toka Kigali, aliomba mafaili ya wanafunzi wote (ambayo kwa mujibu wa wanafunzi, ndiyo mafaili ambayo hayakuwa na taarifa sahihi juu ya muda sahihi wa kozi zao) na akafikia hitimisho la kufanya maamuzi ya kurudisha wanafunzi wote 32 na bodi ya mikopo ikaagizwa itume nauli kwa wanafunzi hao.

Kwa maana hiyo, kwa mujibu wa uchunguzi ulioitishwa na kufanywa na wizara yenyewe mnamo mwezi wa tisa, waziri hakupewa taarifa sahihi na wasaidizi wake kwani ndani ya kundi alilolifanyia maamuzi ya kurudi nyumbani, kuna wanafunzi walikuja kuonekana walikuwa bado na masomo na wapo ndani ya muda sahihi wa masomo.

Sababu nyingine kuu iliyosababisha wanafunzi kuingia kwenye mgogoro huu ni wizara ya elimu baada ya kuingia mkataba na wizara ya elimu ya Mozambique, program kwa upande wa Tanzania ilitelekezwa. Wasimamizi wa program kwa upande wa Mozambique wamewahi kuilalamikia wizara mara nyingi wakiitaka ije ishughulikie matatizo ya wanafunzi wao lakini wizara iliishia kutoa ahadi na haikutekeleza hata suala moja.

Pia wizara ya elimu Tanzania haikujishughulisha na wala kuwasiliana na vyuo husika ambavyo wanafunzi wake walikuwa wanapelekwa kusoma. Hii ilipelekea kwanza wizara kutokuwa na taarifa sahihi juu ya program zinazofanyika vyuoni, pili kutokea kwa malalamiko kutoka wakuu wa vyuo husika kwa kupelekewa wanafunzi tu pasipo kupewa taarifa ya nini kinaendelea

Madhara ya maamuzi ya wizara ni kwamba,
 Ndani ya kundi la watu 32, kuna wanafunzi ambao bado walikuwa wapo ndani ya muda wa kozi zao(yaani kozi ya miaka minne na mwanafunzi yupo mwaka wa nne) na wakanyimwa pesa ya kujikimu na wanafunzi hao mpaka sasa hawajapata hela licha ya wizara kutuma wakaguzi na kujiridhisha kwamba wanafunzi hao wapo ndani ya muda.
 Kuna wanafunzi pia ambao walikuwa wawanastahili kuongezwa mwaka mmoja wa nyongeza ambao wizara inautambua kwa mwanafunzi ambaye amepatwa na matatizo ya kitaaluma na kushindwa kumaliza ndani ya muda wa kawaida wa kozi ambapo, kwa sababu wanafunzi waliopo Msumbiji wanasoma kwa lugha ya kireno, ni karibia asilimia 99 huwa wanaomba huo mwaka wa kuongezwa na hata mwaka huu huu kuna kundi la wanafunzi walikuwa wameshapewa mwaka wa kuongezwa na kundi jingine lenye case kama hiyo likaingia ndani ya wanafunzi 32 na kutumiwa nauli.
 Wizara iliachisha masomo wanafunzi walio ndani ya muda sahihi wa masomo bila kufanya ukaguzi na uchunguzi uliokuwa umeombwa na wanafunzi wenyewe
 Wanafunzi waliishi kwenye nchi ya watu bila msaada wowote hadi mwezi wa sita na wengine tayari walikuwa walishaingia kwenye madeni

KIINI NA CHANZO CHA TATIZO LENYEWE
Pogram ya TAMOSE ilitelekezwa toka mwanzo na ilikuwa inajiendea tu bila usimamizi wowote wa msingi. Wizara ya elimu haikuwa na taarifa muhimu za muda sahihi wa kozi za wanafunzi. Wizara iliamini kuna kozi za miaka mitatu na kwa hiyo wanafunzi wanajifelisha tu. Pesa ilitumwa hata kwa watu ambao walishaacha chuo na haikufahamika iliishia wapi. Wanafunzi walijitahidi kuisihi wizara itume msimamizi wa program ama itume wakaguzi ambao wangekuja kupewa taarifa sahihi na vyuo ambamo wanafunzi wanasoma. Wizara iliishia kutoa ahadi hewa mpaka suala lenyewe lilivyoanza kuwa gumu, hawana taarifa sahihi ya nani anastahili na nani hastahili kulipwa pesa.

Ikumbukwe kwamba, ndani ya kundi la watu 32, wapo waliokuwa nje ya muda na wengine walikuwa ndani ya muda. Wizara ilipoona suala limekuwa halieleweki na wanafunzi wametelekezwa kwa muda wa miezi mitano bila chochote, iliamua kumfukuza aliyekuwa msimamizi wa program mwenye makao Dar es salaam.

Toka mwanzo mwa program, wanafunzi walikuja mpaka Mozambique na hawakupata mapokezi yoyote hali iliyosababisha baadhi ya intake kulala Airport. Program haikuwa na msimaizi wa moja kwa moja aliyekuwa Maputo licha ya wanafunzi kuomba mara kwa mara suala hilo lishughulikiwe

HITIMISHO
Pamoja na maelezo hayo, wanafunzi wanamuomba waziri mkuu aingilie kati ili kutatua changamoto hii, wanaomba waziri mkuu asiishie kuongea na katibu mkuu ama wafanyakazi wa wizara tu ama HESLB, bali aiombe ripoti ya wizara ili aipitie upya na hata ikibidi atume wakaguzi chini ya ofisi yake ili waende wakafanye uchunguzi mwingine wa masuala ya ,kupungua na kupotea kwa pesa za wanafunzi.

Pia wanafunzi wanaomba malipo yafanyike kulingana na taarifa ya ukaguzi ambayo wizara waliiridhia na kuituma HESLB. Sababu ya kuwanyima mkopo kisa walishatumiwa nauli, haiwezi kuwa ababu ya msingi ya kumnyima mwanafunzi stahiki zake ikizingatiwa kwamba aliyekosea toka mwanzo si mwanafunzi bali ni wizara na HESLB. Pia kosa moja haliwezi kuhalalisha kosa la pili. HESLB ikubali kwamba ilifanya kosa kwanza kutokuwasikiliza wanafunzi toka mwanzo na pia kutuma nauli bila kujiridhisha na taarifa sahihi toka vyuoni.

Part II
HESLB yatelekeza wanafunzi Algeria
To be continued
 
Hivi ukisoma Mozambique unakuwa unajisikiaje? This is one of the poorest of the poor former Portuguese colony! Mnaenda kufanya nini mnachotegemea kukipata? Si bora ukae bongo mara 10,00%
 
Kwanini msiombe credit transfer mje mmalizie masomo yenu nyumbani kuliko kuteseka huko ugenini.
Halafu kwa ninavyojua, hizo gharama zote za kusoma huko ni mkopo na mtazilipa zote. Bora ingekuwa scholaship. Sijui ni nani aliwadanganya mkaingia mkenge kwenda kujisomesha miaka mitano nje kwa pesa ya mkopo. Mtajuta siku mkiajiriwa na kukuta salary slip inasoma deni milioni 50
 
Back
Top Bottom