Waliosamehewa na Rais wawe mfano kwa jamii

Herbalist Dr MziziMkavu

JF-Expert Member
Feb 3, 2009
42,316
33,125
11th December 2013





Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete alitoa msamaha kwa watu 1,475 waliokuwa wakitumikia vifungo katika magereza mbalimbali nchini ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 52 ya uhuru iliyoadhimishwa nchini juzi.

Taarifa iliyotolewa na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi ilieleza kuwa mbali na kutoa msamaha kwa wafungwa hao, rais pia amewapunguzia asilimia moja chini ya sita ya adhabu wanazotumikia wafungwa wengine wote nchini.

Baadhi ya wafungwa walionufaika na msamaha wa moja kwa moja wa rais na hivyo kuwa na uhakika wa kutolewa gerezeni ni pamoja na wafungwa wenye magonjwa ya Ukimwi, Kifua Kikuu (TB), saratani na wazee wenye umri wa kuanzia miaka 70.

Wengine ni wafungwa wanawake wajawazito, walioingia gerezani na watoto pamoja na wenye ulemavu wa mwili na akili.

Hata hivyo, msamaha huo hauwahusu baadhi ya wafungwa wakiwamo wale waliohukumiwa kunyongwa, wenye adhabu ya kifo na kubadilishwa kuwa kifungo cha maisha, wanaotumikia kifungo cha makosa ya kujihusisha na biashara ya dawa za kulevya, wanaotumikia kifungo cha makosa ya kupokea au kutoa rushwa, makosa ya unyang`anyi wa kutumia silaha, makosa ya kutumia silaha na pia wenye kosa la kuwapa mimba wanafunzi wa shule za msingi na sekondari.

Sisi tunawapongeza wafungwa wote waliopata bahati ya kuwa miongoni mwa waliosamehewa. Tunampongeza pia Rais Kikwete kwa huruma yake dhidi ya wafungwa hao ambao sasa watapata nafasi ya kuungana tena na familia zao na kufurahia maadhimisho ya siku ya uhuru.

Hata hivyo, NIPASHE tunaona kuwa kuna kila sababu ya kuwakumbusha wale wote waliosamehewa kuwa wanapaswa kuonyesha shukrani zao baada ya kupata msamaha huu kwa kujitahidi kufuata sheria za nchi ili wasirudi tena gerezani.

Tunaona kuwa kamwe, haitapendeza hata kidogo kusikia kuwa kati ya wale walionufaika na msamaha wa rais wakiwa ni miongoni mwa watuhumiwa wa uhalifu wanaofikishwa mahakamani kwa makosa mbalimbali ya jinai na mwishowe kutiwa hatiani kabla ya kurudishwa gerezani wakatumikie vifungo virefu.

Tunakumbushia jambo hili kwa kuwa siyo geni kutokea.Tunafahamu kuwa wapo wafungwa kadhaa ambao wameshawahi kuripotiwa kuwa ni miongoni mwa waliobahatika kupata msamaha wa rais na kuachiwa huru lakini haikuchukua muda mrefu kabla ya kurejea tena gerezani, ikiwa ni baada ya kukutwa na hatia ya kujihusisha makosa mengine ya kihalifu. Hilo halipaswi kujitokeza.

Ni imani yetu kuwa katika hawa waliosamehewa mwaka huu, hakuna atakayekutwa na mkasa mwingine wa kukiuka sheria za nchi na kujikuta akirudishwa tena gerezani ili kutumikia vifungo virefu vya kuanzia miezi sita na kuendelea.

Bali, ni matarajio yetu kuona kuwa watu wote walionufaika na msamaha wa Rais wakijitahidi kadri wawezavyo katika kuheshimu sheria za nchi, kuzitekeleza kivitendo na mwishowe kuonyesha mfano mzuri kwa jamii.

Baada ya misukosuko waliyopata kufuatia kile tunachoamini kuwa ni kuteleza kwao awali na kujikuta wakiingia katika matatizo yaliyowapeleka gerezani, ni wazi kwamba wafungwa hawa walionufaika na msamaha wa rais watakuwa ni kama watu waliozaliwa upya.

Kwamba, kuanzia sasa, badala ya kutenda uhalifu, ni wao ndiyo watakaokuwa mstari wa mbele katika kutekeleza kila lililo jema kwa jamii. Hakika, ni wao ndiyo wanaopaswa kuwa kiigizo chema.

Bila shaka, hata rais amejawa na matumaini makubwa dhidi yao na ndiyo maana akatumia mamlaka yake kuamuru wafungwa hao waachiwe huru ili wakalitumikie taifa kwa namna nyingine, mbali kabisa na maisha ya ndani mwa kuta za gereza.

Tunaamini vilevile kuwa wafungwa wote wanaokabiliwa na maradhi watapata nafuu na mwishowe kuungana na Watanzania wengine katika kuendeleza gurudumu la maendeleo ya taifa.

Wahenga hunena kuwa kutenda kosa si kosa bali kurudia kosa.

Ni imani yetu kuwa wafungwa hawa waliopata msamaha wa rais hawatarudia kosa kwa kutenda dazeni ya makosa mengine wawapo uraiani bali kudhihirisha uadilifu wao kwa kuheshimu sheria za nchi kivitendo.
Abadan, hatutarajii wafungwa waliosamehewa kurudi tena gerezani.




CHANZO: NIPASHE


 
Back
Top Bottom