kbm
JF-Expert Member
- Oct 5, 2012
- 5,224
- 1,676
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Utumishi na Utawala Bora, Angela Kairuki.Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Utumishi na Utawala Bora, Angela Kairuki, amesema watumishi watakaobainika wamehujumu Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF), wachukuliwe hatua.
Aidha, ameagiza kuwa waliopewa ruzuku ya TASAF bila kuwa na sifa, wairudishe na kama watashindwa hatua kali dhidi yao zichukuliwe.
Waziri Kairuki aliyasema hayo wakati wa ziara ya Kamati ya Bunge Utawala Bora na Serikali za Mitaa iliyotembelea ofisi za TASAF Makao Makuu jijini Dar es Salaam.
Alisema lengo la kuanzishwa kwa mfuko huo ni kuzikomboa kaya ambazo zinaishi katika maisha maskini kwa kuziwezesha ili ziondokane na umaskini, lakini kuna baadhi ya watumishi badala ya kuwasaidia walengwa wamekuwa wakiuhujumu mfuko huo.
Aliongeza kuwa ukaguzi utafanyika kwa kila halmashauri ili kuona kama haki ilitendeka kwa walengwa au la na kama haki haikutendeka, wahusika wote watachukuliwa hatua.
Pia Waziri Kairuki alisema kutokana na mfuko huo kufanya kazi na kuzisaidia kaya maskini, atahakikisha katika Bunge lijalo unaombewa mswaada ili utambulike kutokana na kutoa msaada kwa jamii.
Mkurugenzi Mtendaji wa mfuko huo, Ladslaus Mwamanga, alisema kuwa lengo la kuanzishwa kwa mfuko huo ni kuzisaidia kaya maskini katika kuwaboreheshea maisha yao.
Mwamanga alisema kumekuwapo na changamoto mbalimbali katika kuendesha shughuli za mfuko huo kutokana na baadhi ya watu kuwatolea taarifa zisizo sahihi walengwa wanapotakiwa kupewa fedha.
Alisema pia masuala ya kisiasa nayo yamekuwa yakitumika katika mpango wa kuzinusuru kaya hizo, lakini wamefanikiwa kukabiliana nazo na kufikia yale waliyokusudia kuyafanya kwa kaya maskini.
Alisema mfuko toka kuanzishwa kwake kwa awamu ya kwanza, pili na tatu, kaya maskini zaidi ya milioni moja zimenufaika na mpango huo kwa kula milo mitatu, kwenda shule, kuboresha makazi yao, ajira kwa vijana na kuwapeleka watoto kliniki.
Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge Utawala Bora na Serikali za Mitaa, Jonson Rweikiza, ambaye pia ni Mbunge wa Bukoba Vijijini, aliupongeza mfuko huo kwa kazi ambazo umezifanya ya kuzisaidia kaya maskini.
Mbunge wa Jimbo la Ubungo, Said Kubenea, alisema halmashauri zinatakiwa kuisimamia miradi yote ambayo haikutekelezwa kwa wakati ambayo imefadhiliwa na TASAF.
Chanzo: NIPASHE