'Walanguzi' mchele walivyoacha vilio mimba za wanafunzi

Donatila

JF-Expert Member
Oct 23, 2014
7,557
21,513

Ni mji ambao kuanzia Juni mpaka Septemba unakuwa na hekaheka kuliko wakati mwingine wowote.

Wafanyabiashara kutoka maeneo mbalimbali wanaingia katika mji huo kununua mchele kwa ajili ya kwenda kusambaza katika kila pembe ya nchi kwa ajili ya kuuza. Wenyeji wa Ifakara wamezoea kuwaita wafanyabiashara hao wa mchele'Walanguzi'.

Hata hivyo, furaha ya wakulima kufaidi jasho lao wakati wa mavuno, hali huwa tofauti kwa watoto wa kike, wakiwamo wanafunzi wa shule za msingi na sekondari. Kwa baadhi yao huwa mwanzo wa maumivu na vilio maishani mwao.

Kutokana na uwapo mkubwa wa wafanyabiashara katika mji huo, wasichana, hasa walio shuleni hujikuta wamerubuniwa na baadhi ya wafanyabiashara wanaoingia kila siku katika mji huo. Matokeo yake ni kwamba wengi hukatishwa masomo kwa kupata ujauzito.

Miongoni mwa waathirika wa matukio hayo ni Pili Juma (14) ambaye mwaka huu alipaswa kuwa kidato cha pili katika Shule ya Sekondari ya Mofu. Hivi sasa Pili ambaye sasa ana ujauzito wa miezi saba, yuko nyumbani anakoishi na mama yake pamoja na wadogo zake wawili akisubiri kujifungua.

Pili pamoja na wadogo zake hawana baba, kwani alifariki dunia miaka minne iliyopita kwa ajali ya gari.

Binti huyo aligundulika kuwa mjamzito mapema mwezi huu baada ya kuugua kiasi cha kushindwa kwenda shule. Alipelekwa zahanati kupimwa na Kaimu Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Mofu, Aderick Mpuiki.

Mpuiki anasema baada ya kubaini Pili ni mjamzito, waliripoti shuleni ambako kiliitishwa kikao cha kamati ya shule ambacho kiliazimia mambo mawili; kwanza ni kumsaka muhusika wa ujauzito huo na pili ni kumpima upya binti huyo katika Hospitali ya St. Francis iliyopo Ifakara.

Alisema baada ya kupimwa ilithibitika kwamba ni kweli alikuwa na ujauzito wa miezi karibu saba na kwamba jitihada za kumpata mwanaume anayehusika na ujauzito wa mwanafunzi huyo bado hazijazaa matunda.

Katika kijiji hichohicho cha Mofu, Nipashe lilikutana na binti mwingine, Zainabu Dalata (16), ambaye alipata ujauzito wakati akisoma kidato cha kwanza katika Shule ya Sekondari Mofu mwaka 2014.

Zainabu ambaye hivi sasa analea mtoto wake anasema alirubuniwa na mwanaume mfanyabiashara wa mchele ambaye alikuwa akimsaidia fedha kwa ajili ya gharama za shule.

Sheria ya Elimu ya mwaka 1978 inatoa adhabu ya kifungo cha miaka 30 jela kwa mtu ambaye atabainika kukatisha masomo mwanafunzi wa shule ya sekondari au shule ya msingi awe wa kike au wa kiume kwa kuingia naye uhusiano wa ndoa.

Kifungu cha 60(3) cha sheria hiyo iliyorekebishwa mwaka jana kupitia muswada wa marekebisho ya sheria mbalimbali wa mwaka 2016 pia kinatoa adhabu kama hiyo kwa mtu ambaye atatiwa hatiani kwa kosa la kumpa mimba mwanafunzi wa sekondari au wa shule ya msingi.

Mabadiliko hayo yanaifanya sheria ya elimu isomeke sawa na adhabu zinazotolewa katika Kanuni za Adhabu (Penal Code) pamoja na Sheria ya Mtoto ya mwaka 2009 na ile ya Makosa ya Kujamiiana ya mwaka 1998 ambazo kwa pamoja zinakataza kujamiiana na mtoto. Sheria hizo zinatambua mtoto kuwa ni mtu yeyote mwenye umri chini ya miaka 18.

Hata hivyo, changamoto ipo kwenye Sheria ya Ndoa ya mwaka 1971 ambayo mpaka sasa inaruhusu ndoa kwa mabinti wenye umri wa miaka 16 ikiwa wazazi wataridhia na miaka 14 kwa idhini ya mahakama.

Serikali imekuwa ikilaumiwa na taasisi za utetezi wa masuala ya jinsia na watoto kwamba inakumbatia sheria hiyo ambayo ni kikwazo cha haki kwa mtoto wa kike, elimu ikiwa mojawapo.

Kikwazo kingine kinaweza kuwa ni kutoripotiwa kwa matukio husika. Mary Raymond ambaye ni msimamizi wa Dawati la Jinsia,

Wilaya ya Kilombero, anasema wamekuwa wakipata malalamiko mengi ya watoto wadogo wanaopata ujauzito lakini taarifa hizo haziripotiwi polisi kwa sababu ya watuhumiwa kutojulikana.

Alisema hata zile zinazoripotiwa zimekuwa zikikosa ushahidi.

YALIYOMKUTA PILI
Pili anasimulia kuwa Agosti mwaka jana, mama yake naye alisafiri kwenda mkoani Mbeya kwa ajili ya kuuguza ndugu yake na hivyo nyumbani alibaki yeye na wadogo zake wawili.

Anasema katika kipindi hicho chote, yeye ndiye aliyekuwa msimamizi na mwangalizi mkuu wa wadogo zake, akipangilia maisha ya kila siku nyumbani hapo.

Anasema pamoja na kwamba mama yake alimuachia fedha kwa ajili ya matumizi ya kila siku ya nyumbani pamoja na wadogo zake kabla ya kusafiri, kiasi hicho hakikutosheleza mahitaji kama ilivyokusudiwa.

Binti huyo anasema ilikuwa Februari mwaka huu alipokutana na mwanaume ambaye alijitambulisha kwake kuwa ni mfanyabiashara kisha kumshawishi awe mpenzi wake lakini yeye alikataa.

"Nilikuwa naenda dukani, nikiwa njiani nilikutana na kaka mmoja... nilikuwa simjui," Pili alisema. “(kaka huyo) alisema yeye amekuja kwa ajili ya kununua mchele, akasema anaomba niwe mpenzi wake.

"Nilikataa kwa sababu naogopa wanaume na huwa sina mazoea nao. Alinishawishi kwamba angenisaidia kunipatia fedha za kunisaidia.

"Kwa siku ile nilimkatalia kabisa na akakubali kuniacha akanisindikiza dukani, akanisubiri mpaka nikarudi nyumbani, akapafahamu nyumbani, kisha akaondoka."

Anasema siku ya tatu wakati anarudi nyumbani kutoka shuleni, alikutana tena na mwanaume huyo karibu na nyumbani kwao akiwa kwenye baiskeli. Anasema aliumuita na alipokataa kwenda, alimfuata hadi nyumbani.

Anasema baada ya kufika nyumbani aliwakuta wadogo zake wamerudi kutoka shuleni na hakukuwa na mboga ndani na pesa aliyokuwa nayo haikutosha kununulia mboga.

"Nilikuwa na Sh. 500 mfukoni," anasimulia. "Kulikuwa na mchele kidogo ambao ningeweza kuuza nikapata fedha, lakini wakati huo nimefika nyumbani wadogo zangu walikuwa wanalalamika njaa, na sehemu ya kwenda kuuza mchele ni mbali.

"Kwa sababu huyo kaka alikuwa bado yuko hapo nyumbani na kwa sababu alikuwa ameniambia kwamba ananunua mchele, nilimuuliza kama anaweza kununua mchele wangu ili ninunue mboga haraka niwapikie wadogo zangu.

"Alisema kama nina haraka anipatie Sh. 2,000 nikanunue kwanza mboga halafu atanunua mchele wangu baadaye watoto wakiwa wamekula.

"Nilikubali kuchukua hiyo pesa, nikanunulia mboga, nikapika na wadogo zangu wakala. Lakini kabla sijamaliza kupika yeye aliniaga anaondoka akaniambia baadaye atakuja nikishamaliza kupika na ilipofika jioni akaja nikaanza kuzungumza naye.

"Nikaona kama ni mtu mwema, nikamzoea, nikakubali kufanya naye mapenzi na baada ya hapo hakuja tena nyumbani.”

Pili anasema wakati anakubali kuingia kwenye uhusiano, hakuwahi kuelekezwa kijana huyo anakoishi kwa hiyo hata mchele aliotaka kumuuzia aliuuza sehemu nyingine ili kupata fedha kwa ajili ya matumizi ya nyumbani.

MABADILIKO YA MWILI
Anasema kadri siku zilivyokuwa zinaendelea, alianza kuona mabadiliko katika mwili wake na wakati mwingine alikuwa anaugua hata kushindwa kwenda shule.

Anasema aliendelea na maisha hayo akiwa hajui kama alikuwa na ujauzito, lakini siku moja mwezi Agosti mwaka huu akiwa amelala nje nyumbani kwao; akiwa anajisikia vibaya, alipita Kaimu Ofisa Mtendaji wa Kijiji (Mpuiki) aliyemshauri aende hospitali kupatiwa matibabu.

Pili anasema alimjibu mtendaji kwamba asingeweza kwenda kwa sababu hakuwa na pesa ya kutosha. Anasema siku iliyofuata,

Kaimu Ofisa Mtendaji huyo alimpeleka hospitali ambako daktari alishauri apimwe vipimo vya ujauzito. Ndipo akagundulika kuwa na ujauzito, tukio ambalo liliripotiwa shuleni Mofu.

Ofisa Mtendaji, Mpuiki anasema: "Mimi niko kwenye kamati ya shule… huyu binti sijawahi kusikia kwamba alikuwa na matatizo ya kulegalega shuleni. Nafikiri tatizo kubwa lililochangia ni kushawishika tu na hiyo pesa ya yule kijana.”

"Hata kama mama yake alimuachia (fedha ya) matumizi nyumbani, si unajua bado ni mdogo? Sidhani kwamba angeweza kupangilia vizuri. Huenda alitumia (fedha) vibaya, akaishiwa mapema na kwa sababu ya kuogopa kuulizwa kama angeomba tena pesa kwa mama yake, akaamua kuingia kwenye vishawishi."

MAMA ALALAMA
Mama mzazi wa Pili, Hadija Saidi, anasema dada yake alivunjika mguu Januari mwaka huu, hivyo ilimbidi aende kusaidia kumhudumia.

"Mimi niliondoka kwenda kumuuguza dada yangu tangu mwezi wa kwanza mwaka huu, alivunjika mguu, na kabla ya kuondoka niliacha matumizi ya kutosha nyumbani," anasema Hadija.

"Mwanzoni mwa mwezi huu, kwa sababu mimi sina simu, ndugu yangu akapigiwa simu kwamba mtoto wangu amepata ujauzito kwa hiyo haendi shuleni na aliyempatia hajulikani.

"Ndiyo ikabidi nije haraka. Na kama unavyoona, tumekuja tena hospitalini kumpima. Mtoto wangu bado ni mdogo, inaniuma sana na nilikuwa namtegemea kwamba angalau akimaliza shule aje anisaidie mimi mjane, lakini nimepata mkosi."

Hadija anasema tangu mume wake afariki dunia, amekuwa akiishi maisha ya taabu na wakati mwingine kukosa kabisa chakula cha watoto.

Alisema hufikia kuombaomba kwa majirani na marafiki wake wa karibu na kwamba kabla Rais John Magufuli hajaondoa ada ya shule, watoto wake walikuwa wanasoma kwa taabu.

"Nilishukukuru sana baada ya Rais wetu kuondoa ada shuleni," anasimulia Hadija. "Niliaanza kuona kwamba sasa ndoto ya watoto wangu inaenda kutimia kwa sababu niliona sitakuwa tena na mawazo ya kukatishwa masomo kwa sababu wamepata ukombozi.

"Inaniuma sana mtoto wangu ambaye ndiye wa kwanza niliyekuwa namtegemea kwamba ataanza kunilea, ameharibiwa. Inaniuma sana na sijui la kufanya. Naona kama dunia imenielemea."

MAJANGA YA ZAINABU
Kwa upande wake Zainabu (16), anasema yeye ni yatima kwani wazazi wake walifariki dunia akiwa darasa la nne, hivyo kulelewa na bibi yake.

Anasema bibi yake ndiye alimgharamia ada wakati akianza kidato cha kwanza, kabla ya serikali kufuta ada.

Anasema wakati anasoma alirudishwa nyumbani kwa kukosa ada na alipomweleza bibi yake huyo, alimwambia kwamba hana fedha kwa kipindi hicho hivyo asubiri mpaka itakapopatikana.

Anasema alikaa nyumbani mwezi mzima bila ya bibi yake kupata ada na kwamba hakuwa na raha, hasa pale alipoona wenzake wanaenda shule.

Anasema kabla ya kwenda sekondari, baada ya kuhitimu darasa la saba, kulikuwa na mwanaume ambaye alikuwa anaenda nyumbani kwa bibi yake kumwomba amuoe, lakini yeye alikataa kuolewa kwa sababu alikuwa anapenda kusoma.

"Nilitaka niendelee na sekondari kwa sababu nilikuwa napenda kusoma japokuwa maisha ya nyumbani ni magumu sana hata wakati mwingine uhakika wa chakula unakosekana."

"Sasa, wakati nimerudishwa ada, nilipata mwanaume mmoja hivi mfanyabiashara akanishawishi, nikaanza naye mahusiano ya kimapenzi.

"Alinipatia mahitaji yangu yote na nikawa nimerudi shuleni, aliniahidi atanisubiri mpaka nimalize shule ndio anioe.

"Lakini ilipofika mwezi wa nne (Aprili) 2015, nikiwa shuleni, tulipimwa nikagundulika nina ujauzito. Nikafukuzwa shule."

Anasema mpaka sasa analea mtoto akiwa na bibi yake tu kwa sababu mwanaume alimkimbia na hata matumizi ya mtoto hatumi.

Anasema hivi sasa anafanya vibarua vya kupepeta mchele kwenye mashine na katika mashamba ya mpunga ili kupata fedha ya kujikimu yeye, bibi yake na mtoto. Anasema ndoto yake ilikuwa awe askari wa Jeshi la Polisi.

Kwa mujibu utafiti wa sababu na athari za ndoa za utotoni nchini Tanzania uliofanywa na Taasisi ya Utafiti wa Kupambana Umaskini (REPOA) kwa kushirikiana na mashirika mengine ya ndani na nje ya nchi mwaka huu, umaskini umetajwa kuwa moja ya sababu kubwa ya ndoa za utotoni nchini.

Sehemu ya ripoti ya utafiti huo iliyopewa jina la Mtazamo wa Ndoa za Utotoni Tanzania ya Machi 2017 inasomeka: “Familia zenye uchumi mbaya zimekuwa zikipambana kuwapa watoto mahitaji kama nguo na chakula, achilia mbali ada na gharama nyingine za kuwezesha watoto kusoma”.

“Matokeo yake ni kwamba kwa familia hizi kuoa mabinti zao kuna maana ya ‘kuwalinda kiuchumi na kijamii’. Si kwamba familia hizi zinapunguza mzigo wa kuwalisha watoto hawa, bali mahari ikilipwa kwa ajili ya binti iwe mifugo au fedha inasadia kuongeza kipato cha familia husika”.

Bibi yake Zainabu, Hajra Darata, anasema tangu wazazi wa binti huyo wafariki dunia, amepata wakati mgumu kumlea mjukuu wake kwa sababu ya kukosa kipato cha kutosheleza. Anasema hana nguvu za kufanya kazi kama zamani kwa hiyo hazalishi.

SHAUKU YA KURUDI SHULE
Zainabu anasema kama angepata mtu wa kumlipia ada angeweza kurejea shule kusoma hadi kidato cha nne, lakini hajapata mfadhili.

Hata hivyo, tayari serikali imetoa msimamo wake ikisema haitaruhusu mtoto aliyepata ujauzito kurudi shuleni baada ya kujifungua.

Akiahirisha mkutano wa saba wa Bunge la Bajeti Julai 5, mwaka huu, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, alisema msimamo wa serikali wa kutoruhusu wanafunzi waliopata ujauzito kuendelea na masomo ni katika mfumo rasmi ya elimu ni kwa mujibu wa sheria na wala siyo utaratibu mpya.

Kanuni za Elimu za mwaka 2002 zinataja mwanafunzi kujihusisha na ngono kuwa moja ya makosa yanayoweza kusababisha mwanafunzi kufukuzwa shule. Mimba kwa wanafunzi zimekuwa zikitumika kama uthibitisho wa kutenda kosa hilo.

Ripoti ya Shirika la Ufuatiliaji wa Haki za Binadamu la Human Rights Watch ya Febaruari mwaka huu, inaweka wazi kuwa sheria hiyo ni ya kibaguzi kwa kuwa inamweka kando mwanafunzi wa kiume anayekuwa ametenda kosa kama hilo kwa sababu tu hana uthibitisho.

Majaliwa katika hotuba yake alisema tatizo la mimba kwa wanafunzi ni kubwa akisema mwaka 2015 wasichana 3,637 waliacha masomo kutokana na kupata mimba.

Katika hotuba yake hiyo, Majaliwa alisema kila mtanzania ana wajibu wa kuhakikisha watoto wa kike wanapata elimu stahiki na masomo yake hayakatizwi kwa ujauzito na kwamba serikali yenyewe imewekeza kwa mtoto huyo.

HALI ILIVYO KILOMBERO
Matatizo yaliyowakumba Pili na Zainabu yanaakisi uhalisi wa changamoto zinazowakabili wanafunzi wa kike katika shule za msingi na sekondari katika wilaya ya Kilombero mkoani Morogoro.

Ofisa Elimu Sekondari wa Halmashauri ya hiyo, Ephraimu Simbeye, anasema katika shule za sekondari 12 zilizopo, tayari mabinti 39 wamepata ujauzito kati ya Januari na Agosti mwaka huu.

Simbeye anasema waliopata ujauzito ni sita wa kidato cha kwanza, kidato cha pili (11), kidato cha tatu (14) na kidato cha IV wanane (8).

Naye Ofisa Elimu Msingi wa Halmashauri hiyo, Zakia Fandey, anasema katika shule 131 zilizopo, wanafunzi watano wamepata ujauzito.

Anasema kwa mwaka 2014, wasichana ambao hawakufanya mtihani wa darasa la saba ni 94, huku sababu kubwa zikiwa mimba na utoro.

Pia anasema mwaka 2015 wanafunzi wa kike ambao hawakufanya mtihani wa darasa la saba walikuwa 64, mwaka 2016 (38) sababu kubwa ikiwa ni mimba na utoro pia.

Ofisa Maendeleo ya Jamii Halmashauri ya Mji wa Ifakara wilayani Kilombero, Brigita Mchene, anasema tatizo la mimba kwa wanafunzi wameliona na wamechukua hatua za kutoa elimu kwa umma vijijini ili kuwawezesha wazazi na wananchi kuchukua hatua za kuwalinda wanafunzi wasichana.

Mchene anasema watoto wengi wanaharibikiwa katika kipindi hicho cha msimu wa mavuno kutokana na mwingiliano wa watu na kwamba lipo tatizo la kuficha taarifa za watoto wanapopata ujauzito.

"Tunatembea sana huko majumbani kuzungumza na wazazi, tunakutana na idadi kubwa ya watoto wameacha shule kwa sababu wamepata mimba, lakini ukiwauliza wameripoti wapi, hawajaripoti popote," anasema Mchene.

"Hii ndiyo changamoto tunayokumbana nayo huku. Ukiwauliza kwanini hawajaripoti wanasema hawamjui muhusika, kwa hiyo na wewe nafikiri utakuwa umejionea huko mitaani."

Anasema katika miezi ya Julai na Agosti tu wanafunzi walioripotiwa kupata ujauzito sekondari na msingi katika halmashauri ya mji huo wa Ifakara ni 14.



Chanzo: Nipashe
 
Inasikitisha sana lakini haihalalishi kuendelea na Masomo baada ya kupata ujauzito
 
ninaingia moyo wa huruma kwa vile mwanamke mwenzangu, ila kiukweli wanawake wa upande huo mna tamaa ya kupitiliza na hamjui thaman ya ujanajike eti unampa mtu mapenz kisa hela ya mboga, khaa! mnachekesha sana halaf mnataka huruma cjui ya nani kulalamika eti maisha magumu yaliyosababisha. Pumbav zenu, mkiskia baadh ya maeneo yanaongoza kwa kua na bikra nying mnaanza maneno mabov mabov simwonei huruma wala nini coz wanawake tunatakiwa tujiheshim, kwan maisha magum yko huko tu?
 
Katika Mkoa wa Morogoro maeneo anayoathirika na mimba za wanunua mchele na mpunga ni haya hapa:
1. Ifakara
2. Lupiro
3. Mang'ula
4. Itete
5. Mtimbira
6. Malinyi
 
Dah!
Huyo mama yake Pili sidhani kama ana akili timamu ya kustahili kuwa mzazi. Unawezaje kumuacha mtoto mdogo wa miaka 14 aendeshe familia na kutunza watoto wenzake wawili!? Kama suala lilikuwa kwenda kumuuguza mgonjwa, mgonjwa angeweza kuja Ifakara na kupata uangalizi huku mama Pili akiendelea na majukumu ya kuiangalia familia pia. Inasikitisha mtoto Pili hatakuwa na nafasi tena ya kutimiza ndoto zake za elimu na maisha bora.
 
Back
Top Bottom