Wakonta Kapunda ni nani? Fuatana nami

Wakonta Kapunda ni nani? Fuatana nami

amu

JF-Expert Member
Joined
Aug 8, 2012
Posts
16,171
Reaction score
31,357
SEHEMU YA KWANZA

Mwaka 2012, siku ya mahafali yetu ya kidato cha sita, nilipatwa na tukio lililobadili mwelekeo wa maisha yangu.
Ilikuwa ni siku ya shamrashamra zisizo na kifani, tulipendeza sana ndani ya majoho yetu ya mahafali.

Ilipotimu saa nne, wanafunzi walijipanga kwenye mistari kwa ajili ya kumpokea mgeni rasmi. Pindi wengine wakiwa kwenye mistari, mimi na rafiki zangu wachache, tulikuwa tukizunguka kutafuta wapiga picha ili kupiga picha. Kufumba na kufumbua sikujua kitu gani kilitokea hadi nilipozinduka nikiwa hospitali.

Kwa jina naitwa Wakonta Kapunda, naomba umakini wako ili upate kujua nilipatwa na nini?

Kwa kuwa sikujua kilichotokea; wenzangu walinihaditha tukio lilivyokuwa…

Mmoja wa wanafunzi wenzetu alienda kwenye gari la ndugu yake aliyekuja kwenye mahafali na kuingia. Wakati huo gari lilikuwa halijazimwa, hakuna ajuaye nini kilitokea kwenye gari baada ya yeye kuingia, lakini baada ya muda mfupi wakashangaa kuona gari likianza kurudi nyuma kwa kasi sana.

Waliobahatika kuliona walikimbia lakini mimi sikumbuki kuona gari wala kusikia ngurumo yake. Wanasema lile gari lilipokuwa likirudi nyuma lilikuwa likigonga watu kwani walikuwa wamezagaa huku na kule. Gari lilipoteza mwelekeo na aliyekuwa akiendesha alipoambiwa asimame, ndipo aliongeza kasi zaidi hadi lilipogonga mti na kusimama.

Haieleweki kama niligongwa na gari au nilianguka, lakini baada ya gari kupita watu walinikuta chini, wakanichukua na majeruhi wengine kupelekwa hospitali. Tulipelekwa hospitali ya Magunga, Korogwe mkoani Tanga.

Niliposhtuka baada ya kuzirai kwa muda mrefu, nilishangazwa na kelele nilizokutana nazo. Nilikuwa nikisikia huyu analalamika mguu wake umefanya hivi, mara mwingine mkono wake umefanya vile ikawa tafrani. Nilikuwa kama nina maruweruwe, nikajiuliza kwanini watu wanalalamika vitu nisivyovielewa, lakini kabla ya kujua zaidi nilirudi tena usingizini.

Saa moja nilizinduka na kutambua kwamba nipo wodini. Nilikuwa nikikihisi kichwa tu na ndicho nilijua kilipo, lakini sikuhisi uwepo wa mikono wala miguu. Sikujua kama nimelala, nimesimama au nimekatwa kichwa. Kuona hivyo nikapiga kelele, “miguu na mikono yangu imefanya nini mbona siioni?” Wanafunzi wenzangu waliokuwa kando yangu walienda kumuita daktari haraka kwani alitoa amri nisishikwe!

Daktari alipofika, aliniambia kuwa nimepata ajali hivyo mwili wangu una ganzi, baada ya muda utarudi katika hali yake ya kawaida. Na hali ya kutohisi miguu na mikono ilisababishwa na hiyo ganzi. Kikubwa akanishauri ninywe maji.

Nilimwamini daktari na nikaacha kupiga kelele. Pia akaniambia familia yangu ipo njiani kuja kuniona. Hakika nilipata amani na kuamini kila kitu kingekuwa sawa punde.

Nilikuwa na majeraha madogo kichogoni na mguuni. Kutokana na uchache na udogo wa majeraha; niliamini siku itakayofuata ganzi ingenitoka na kuruhusiwa hospitali lakini wahenga walisema, "jambo usilolijua ni sawa na usiku wa kiza." Wakati huo sikuwa nafahamu sana kuhusu uti wa mgongo… nilisoma darasani lakini sikujua kama ungekuwa na madhara makubwa hivi kwenye mwili.

Wakati mkasa huo ukitokea, zilikuwa zimebaki siku tano tufanye mtihani wa taifa wa kidato cha sita.

***

Nilipoamka nikaanza kuhisi maumivu makali ya kichwa. Kichwa kilikuwa kikiuma kama kinawaka moto. Nikawa siwezi kula wala kunywa na sauti ikapotea. Pia nikawa siwezi kuhema vizuri, nilijihisi mzito kupumua. Jinsi muda ulivyokuwa ukienda, ndivyo nikawa nachoka sana. Nikawa sielewi vitu vinavyoendelea.

Siku iliyofuata, gari la wagonjwa lilifuatwa Tanga kuja kunichukua ili kunipeleka hospitali ya taifa Muhimbili. Hiyo ilikuwa tarehe 2 mwezi wa pili.

Bahati mbaya sana tulipofika Muhimbili, tukaambiwa kuna mgomo wa madaktari, hivyo nikapokewa na madaktari wa jeshi na kupelekwa ICU. Huko nikawekewa mashine lakini hakuna kilichoendelea zaidi ya huduma ya kwanza licha ya kuwa wakati huo nilihitaji sana kufanyiwa upasuaji. Pingili moja ya uti wangu wa mgongo ilikua imesogea na ingine ilikuwa imesagika na kuukandamiza uti mgongo hivyo nilihitaji nitolewe ‘pressure’ haraka iwezekanavyo lakini hapakuwa na daktari.

Waliokuwepo wakanifunga kichwani jiwe la kilo nne na kutaka nipelekwe wodini kusubiri hadi madaktari waliogoma watakaporudi kazini.

Wauguzi walionipokea wodini waliuliza ninachoumwa, walipojibiwa wakasema sitoweza kutoka siku za karibuni hivyo nipelekwe kitanda cha mwisho kabisa. Baada ya hapo mama alitolewa nje kwani wodini hapakuruhusiwa mtu yeyote kukaa. Wakati huo nilikuwa na maumivu makali sana ya kichwa, koo likawa linakauka sana na muda wote nikawa nahitaji maji lakini mazingira ya wodi hayakuwa rafiki sana.

Sikuwa na sauti, nilipotaka msaada wa maji watu hawakunisikia na mimi sikuwa naweza kufanya chochote hata kutikisa miguu. Hakika usiku wa kwanza pale wodini ulikuwa mgumu sana. Asubuhi mama alipokuja nikaanza kumlaumu sana kwanini aliniacha peke yangu, akanieleza sababu lakini sikumuelewa kabisa.

Ukaanza mchakato wa kuwatafuta madaktari, ndugu walikuwa wapo radhi kutafuta hata madaktari binafsi ili nifanyiwe upasuaji lakini wakaambiwa hakuna daktari atakayenitibu inabidi tusubiri mgomo uishe tu. Waliambiwa wasihangaike, watapoteza hela bure kwani hakuna mtu mwenye majeraha kama yangu ambaye huwa anapona. Maneno hayo yaliingilia sikio la kushoto na kutokea la kulia, waliendelea kuhangaika japokuwa hawakufanikiwa kumpata.

Nilikaa siku 18 kitandani bila huduma zaidi ya lile jiwe la kilo nne kichwani ambalo waliamini litanisaidia. Nilipata vidonda na nilikuwa nikishindwa kupumua kabisa na pale nilipokuwepo hapakuwa na mtungi wa gesi. Watu walipokuwa wakija kunisalimia waliposimama karibu yang tu, nikawa nashindwa kupumua hivyo natafutiwa mtungi. Hali ilikuwa mbaya mno ni Mungu tu alisaidia kuweza kuishi zile siku 18.

Mauguzi waliposema watu wenye matatizo kama yangu huwa hawaishi sana, ni kweli kabisa. Nikiwa pale nilishuhudia wagonjwa wakija na kuondoka, nilibaki mimi tu peke yangu ambaye nimeumia. Siku 18 ni nyingi sana kwa hali niliyokuwa nayo.

Ilipofika siku ya 19, madaktari walianza kufanya upasuaji nami nikawekwa kwenye foleni. Asubuhi ya siku ya upasuaji nilipopimwa nilibainika nina damu kiasi kidogo hivyo ukaahirishwa na ilikuwa Ijumaa. Nilijiona sina bahati kabisa kwani nilijua kwa sababu hiyo lazima wangesogeza mbele. Kweli ilisogezwa hadi Jumatatu, na mara moja wakaanza kutafutwa watu wa kuchangia damu. Nashukuru marafiki na ndugu zangu walijitolea na nikawekewa damu siku ile yote na jumamosi yake. Jumapili nilipumzika.

Usiku walipokuja kuniandaa kwa ajili ya upasuaji, nikakutwa na homa, na mtu mwenye homa hawezi kufanyiwa upasuaji hadi homa itakaposhuka. Mimi niliomba kufanyiwa hivyohivyo kwa kuamini asubuhi homa ingeshuka. Wakaanza jitihada za kuipunguza. Usiku mzima walitumia kuipunguza kwa kunikanda n.k lakini homa haikupungua. Nilikata tamaa kabisa!

Bahati nzuri kufika asubuhi homa ikawa imepungua, hivyo wakaliondoa jiwe na kunipeleka kwenye upasuaji. Kabla ya upasuaji nilikuwa nikilala miguu juu, kichwa chini huku kichwani nimefungwa jiwe hilo la kilo nne likivuta kichwa. Kwa hiyo, siku hiyo nilikuwa na furaha ya jiwe kuondolewa.

Upasuaji ulifanikiwa. Kipingili cha uti wa mgongo kilichokuwa kimesagika kiliondolewa na kile ambacho kilihama kilirudishwa mahali pake kisha nikawekewa vyuma. Baada kama ya siku tano hivi, nikawa nimepona kidogo. Afya ikaanza kuboreka na nikaanza kuhisi mwili ukipitisha hisia. Hapo kila mtu akawa na matumaini.

Madaktari husema ukweli kuhusu afya ya mgonjwa, nami waliniambia kama nimepooza lakini kutokana na hali ile ya kuhisi unafuu nikaanza kuhisi labda ni maneno yao tu walijiongelea lakini kila mtu hupona kwa namna yake. Baada ya wiki tatu mwili ukaanza kurudi kiasi, nikaanza kupumua vizuri na kuongea.

Nilifundishwa namna ya kupumua, kukohoa na kuongea mwenyewe. Baada ya mwezi nikaanza mazoezi; ‘physiotherapy’ lakini yalikuwa mepesimepesi kwani kutokana na kulala muda mrefu nilipata kidonda ‘bedsore’.

Baada ya mazoezi kama wiki tatu hivi, shingo iliimarika lakini bado nilikuwa nikitumia ‘neck collar’ na baadaye nikaruhusiwa. Yaani niliingia hospitali mwezi wa pili nikatoka wa mwezi tano, tarehe 10.

Wakati wa kutoka hospitali miye nilifurahi sana japo mikono wala miguu haikuwa imeanza kufanya kazi lakini mama yangu akawa analia hataki nitoke.

Uzuri wa hospitali nilipata usaidizi mzuri na mazingira yalikuwa rafiki kwa mgonjwa wa aina yangu, mama alihofia ataishije na mimi nyumbani. Baada ya kutoka hapo nikaanza maisha mengine magumu kuliko yale ya hospitali.

Habari hii naitokea moja kwa moja Facebook kwenye ukurasa wa Gemima mabula.

Nitakuwa ninaupdate kila mara.

FB_IMG_1592810682070.jpg
 
INAENDELEA...

Ukiwa hospitali kuna unafuu kidogo kwani kila mtu anaumwa, pia kuna wauguzi na madaktari kwa ajili ya usaidizi. Ukiwa unaendea vizuri unajiona kama ndiyo umepona kabisa!

Kwa mtu aliyepooza hospitali kuna nafuu kuliko kuwa nje. Ukitoka nje unakutana na walio wazima, kila mtu anakushangaa wewe na kukupa pole. Hiyo si nzuri.

MAJERAHA YA UTI WA MGONGO
Majeraha ya uti wa mgongo yamegawanyika kwenye makundi mawili; ‘complete’ na ‘incomplete spinal cord injury’. Jeraha likiwa ‘complete’ maana yake uti wa mgongo unakuwa umeumizwa kabisa na mwili unapooza. Mwili unakuwa hauna hisia wala hauwezi kujongea hata kidogo. Katika 'incomplete' mwili unaweza kuhisi na kujongea kidogo, lakini hii hutofautiana kati ya mtu na mtu.

HALI YANGU KIUJUMLA
Mimi, baada ya ajali, mwili wangu ulikufa ganzi kabisa, sikuwa nikihisi chochote. Baada ya upasuaji hisia zilianza kurudi na baadhi ya sehemu za mwili zilianza kujongea kidogo. Nilijianza kujongea mabega kisha kidole cha kati. Kwa maana hiyo mimi nina ‘incomplete’ ambayo kitaalam inaitwa ‘c3-c4 incomplete spinal cord injury’.

Majeraha ya uti wa mgongo yamegawanyika katika vipengele mbalimbali lakini hakuna watu wawili wenye jeraha la aina moja ambao wanafanana kwa kila kitu. Mfano mimi nina ‘c3-c4 incomplete injury' lakini akija mwingine mwenye aina hiihii hawezi kuwa kama mimi. Yaani kila mtu yupo tofauti. Suala hili ni linachanganya hata daktari hawezi kulielezea vizuri.

Zaidi ya kupoteza uwezo wa kushika na kunyanyua miguu, pia uwezo wangu wa kupumua na mmeng’enyo wa chakula vilibadilika baada ya ajali. Mmeng’enyo unaenda taratibu kidogo. Vilevile haja ndogo na kubwa, kupiga chafya, kutapika, kukohoa na kucheka vilibadilika baada ya ajali.

Ni miaka nane tangu nimepata ajali, hivyo vitu vingi vimebadilika. Vitendo kama kucheka na kupumua ambavyo mwanzo vilikuwa vimepotea, vilianza kurudi taratibu kadri siku zilivyokuwa zinasonga mbele. Hivi sasa naweza kukohoa kidogo. Haja ndogo ambayo mwanzo niliipoteza kabisa, nikawa siwezi kuidhibiti kwa namna yoyote, kwa sasa naweza kuidhibiti kwa kiasi kidogo, pia naweza kuhisi kibofu kikiwa kimejaa. Vivyo hivyo kwa haja kubwa.

Pia natumia kiwambo (diaphragm) kupumua kwani nimepoteza uwezo wa kifua kujongea (chest movement), maana yake napumua kwa kutumia tumbo. Nikiwa napumua utaona tumbo likicheza lakini kifua hakichezi.

***
Wengi wananiuliza mbona miguu yangu ni minene na sijapungua sana. Kusema kweli hata mimi sijui ni kwa nini, kwani hakuna kitu maalum ambacho nakifanya au nakitumika kinachonifanya niwe hivi. Mwanzo nilipoteza misuli lakini baadaye ilianza kujirudi yenyewe.

Jeraha langu bado lipo palepale lakini naweza kujongeza mabega na mikono. Napumulia tumbo lakini napumua vizuri.
Nina hisia mwili mzima; nikishikwa nahisi, japo upande wa kushoto unahisi vizuri zaidi ya upande wa kulia.

Majeraha ya uti wa mgongo huwa tofauti kwa kila mtu, kikubwa ni kufanya mazoezi na kula vizuri, haijalishi jeraha ni la namna gani.

USHAURI

Pale ulipopatia jeraha ndipo mawasiliano yatakapokatikia. Mfano mimi nilijeruhiwa shingoni maana yake mawasiliano yatatoka kichwani na kuishia shingoni, na yale yanayotoka chini yataishia shingoni hayatopanda kichwani. Ikitokea umepata jeraha mgongoni basi mawasiliano yataishia hapo, maana yake ukipata shingoni, huku chini kote kutakuwa hakuna mawasiliano. Wengine wanajongea mikono sababu jeraha linakuwa chini ya mikono, mimi langu lipo juu ya mikono ndiyo maana mikono yangu haijongei.

Tuko tofauti, utakuta huyu mikono yake inafanya kazi, yule haifanyi, mwingine anahisi lakini hawezi kunyanyua mikono, mwingine ananyanyua mikono lakini ukimgusa hahisi chochote.

Licha ya kuwa tofauti lakini kuna vitu ambavyo sote wenye majeraha ya uti wa mgongo tupo sawa.

●Sote tupo kwenye hatari ya kupata ‘pressure sores’ ikiwa tumekaa muda mrefu pasi na kujongea.

●Sote tupo kwenye hatari ya kupata magonjwa ya moyo kwani tunatumia muda mwingi tukiwa tumekaa.

●Sote tunapata ‘frozen joints’. Hii ni hali ya mikono kukakamaa na kuhisi mifupa ikisagika kutokana na kutojongea kwa muda mrefu.

●Sote tupo kwenye hatari ya kupata ‘autonomic dysreflexia’. Hii ni hali ambayo mwili unakuwa kama umechanganyikiwa hivi.
Kwa mfano, mtu asiye mgonjwa akiungua mguu, fahamu huenda haraka kichwani kisha hurudi tena mguuni sasa kwetu majeruhi, ikifika kwenye jeraha haivuki. Hapo mwili unashindwa kufanya chochote, hii inaweza husababisha ‘pressure’ kupanda sana, jasho kutoka sana na maumivu makali ya kichwa, pia mtu anaweza kupata shambulio la moyo kwani mwili unakuwa umetatizika haujui uamue vipi.
Spasming. Hii ni hali ambayo mikono hujisukuma mbele na miguu kujivuta nyuma bila sababu yoyote.

SAFARI YA MAFANIKIO

Baada ya ajali kila kitu kilibadilika kwenye maisha yangu, lakini sikuwa na namna zaidi ya kuikubali hali yangu na kusonga mbele.

Kwa kuwa muda mwingi niliutumia kutazama filamu; nilianza kujifunza taratibu namna ya kuandika miswada ya filamu (scripts). Nilijifunza na kuimarika, mwaka 2016 nilishiriki shindano la miswada ya filamu, lililokuwa limedhaminiwa na kampuni ya Maisha ya nchini Uganda. Nilishiriki na kufanikiwa kufuzu hatua ya kwanza japo sikuibuka mshindi.

Siku moja mdogo wangu aliniachia simu. Kwa bahati nzuri simu ile iliita, wakati nikihangaika kuipokea, nikagundua kumbe nikiigusa hata kwa mwili inakubali siyo kidole tu. Mdogo wangu alipoamka nikamwambia tufanye namna hiyo ili simu iweze kunifikia. Aliishirikisha familia na wakakubali kuniwekea mito, nikaweza kuitumia.

Nilianza kwa kudonoa taratibu. Awali kichwa kilikuwa kikiniuma, nilihisi kizunguzungu na ulimi uliniuma lakini nilifanya kila siku hadi nikazoea. Kwa sasa ninafanya kazi kubwa kupitia ulimi wangu, naandika siku nzima.

Pia nafanya ujasiriamali mtandaoni tangu mwaka 2016. Kulikuwa na changamoto kadhaa hapo mwanzoni lakini sikukata tamaa kwani niliamua kwa dhati ya moyo wangu, nilijitahidi kujifunza zaidi. Nilijifunza vingi pia nimesaidia watu wengi na hadi sasa nafundisha watu.

Tangu mwaka umeanza nimejikita kwenye ‘network marketing’, nafanya mimi mwenyewe pia nafundisha watu wengine kufanya.

Najivunia kugusa watu wengi na mpango wangu mkubwa ni kuwafanya wanawake wajisikie vizuri kihisia na kiuchumi.

Asante!

Mrembo mwenyewe.
FB_IMG_1592811278173.jpg
FB_IMG_1592811073120.jpg
 
Pole sana sana tu Maisha haya basi tu tunapitia changamoto nyingin hujui kila baada ya saa mbele kitatokea kitu gani? Au usiku ukilala asubuhi utaamkaje?
 
Back
Top Bottom