Waislamu, Maaskofu waungana

Averos

JF-Expert Member
Aug 6, 2010
993
695
headline_bullet.jpg
Waitaka serikali kuingilia haraka kurejesha amani
headline_bullet.jpg
Mbeya, Iringa wachangia fedha majeruhi waliolazwa
headline_bullet.jpg
Maandamano mengine ya Chadema yazuiwa Songea





Waziri Mkuu, Mizengo Pinda



Viongozi wa dini ya Kiislamu wameungana na wenzao wa Kikristo kulaani mauaji yaliyofanywa na Jeshi la Polisi jijini Arusha wiki iliyopita na kuwajeruhi wengine kadhaa.
Wakizungumza na waandishi wa habari jijini Arusha jana, viongozi hao wa Kiislamu wa Mkoa wa Arusha walisema wanalaani mauaji hayo na kuitaka serikali kuhakikisha inawachukulia hatua haraka waliosababisha mauaji hayo.
Imamu wa Msikiti Mkuu wa Arusha, Mohamed Said, alisema hatua hiyo itasaidia kuepusha baadhi ya watu wasio na nia nzuri kuitumia nafasi hiyo kuendelea kupandikiza chuki.
Imamu Said aliwaambia wanahabari katika mkutano huo uliofanyika kwenye ofisi za msikiti huo kuwa viongozi wa kisiasa wanatakiwa kuelewa kuwa migogoro yao inayaathiri makundi mengine ya watu wasio wanasiasa.
Alisema wanasiasa wanapaswa kutambua kuwa amani iliyopo ikitoweka na wao hawatasalimika.

MAASKOFU WAMVAA PINDA
Nao maaskofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) wa Dayosisi za Kaskazini, Pare na Kaskazini Kati, wamemtaka Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, kuingilia kati haraka mgogoro wa kisiasa jijini Arusha ili kurejesha hali ya amani.
Mgogoro huo wa kisiasa umesababisha vifo vya watu watatu na kujeruhi wengine zaidi ya 30 na kusababiasha uharibifu mali na kuendelea kuongeza hali ya wasiwasi jijini humo.
Tamko hilo lilitolewa na Askofu wa Dayosisi ya Kaskazini, Askofu Martin Shao, katika ibada ya kumsimika Askofu Msaidizi wa Dayosisi ya Kaskazini Kati, Mchungaji Solomon Masangwa, iliyofanyika jana katika Kanisa la Kimandolu, jijini Arusha na kuhudhuriwa na Askofu Thomas Laizer wa Dayosisi ya Kaskazini Kati na Askofu Charles Mjema wa Dayosisi ya Pare.
Alisema kuwa hali ya usalama bado haijatengamaa jijini Arusha ambapo polisi wenye silaha wanaendelea kushika doria kwa saa 24 katika mitaa mbalimbali.
“Ofisi ya Waziri Mkuu inaweza kumaliza tatizo hili, busara na hekima ni nyenzo muhimu za kutatua mgogoro huu ili uishe kwa amani,” alisema.
Shao alisema kuwa kauli ambazo zimekuwa zikitolewa na vyama vya siasa na watendaji wake zinazidi kukuza mgogoro huo na kwamba pande zote kupitia ofisi ya Waziri Mkuu ambaye ndiye msimamizi mkuu wa kazi za serikali inapaswa kuingilia haraka sana.
“Yaliyotokea ni mambo ya aibu na dhambi kubwa mbele za Mungu, wahusika wote wakutane kuzungumza na kumaliza kabisa mgogoro huu ili kuepusha shari nyingine katika siku za usoni,” alisema Askofu Shao.
Maaskofu hao wakiongozwa na Askofu wa Dayosisi ya Kaskazini Kati, Thomas Lazier, walikwenda katika Hospitali ya Mkoa wa Arusha Mount Meru na kuwatembelea majeruhi walioathirika katika tukio hilo.
Hadi kufikia jana, polisi walikuwa wakiendelea kuweka ulinzi mkali katika mitaa mbalimbali ikiwa ni pamoja na taasisi za benki, ofisi za umma na maeneo mengine nyeti.
Tamko hilo linafuatia tamko lingine lililotolewa na maaskofu wa madhehebu ya dini za kikristo mkoani Arusha kulaani mauaji ya raia yaliyofanywa na polisi na kuitaka serikali kuchukua hatua dhidi ya wahusika wa mauaji hayo yaliyotokea Jumatano ya wiki iliyopita, wakati polisi walipokuwa wakisambaratisha maandamano ya Chama Cha demokrasia na maendeleo (Chadema).
Katika tamko hilo, Askofu Josephat Lebulu wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Arusha, alililaumu Jeshi la Polisi kwa madai ya kutumia nguvu kubwa kushambulia watu katika maeneo ya hospitali na makazi ya watu kwa mabomu na risasi za moto.
 
Back
Top Bottom