Wagweno: Kabila lenye asili ya Kenya lililohamia Tanzania kwa mbinu za kiintelijensia

Hussein Massanza

JF-Expert Member
Dec 26, 2012
1,015
2,191
Wagweno ni kabila la watu wenye asili ya Kenya wanaoishi Tanzania katika Mkoa wa Kilimanjaro, upande wa Kaskazini wa Milima ya Ugweno.

Lugha yao ni Kigweno.

ASILI

Kiasili Wagweno ni katika jamii zilizotoka Uhabeshi ya kale na ndiyo maana ukiangalia kwa makini utamaduni wao utaona kwamba hazifanani sana na Wabantu, bali na Wahamitiki. Tazama hata katika ngoma ya Kigweno ambayo wanaiita mrangi [mwanzi] hawatumii ngoma kama Wabantu.

SABABU YA KUKIMBIA KENYA NA KUHAMIA TANZANIA

Inasemekana asili yao wametoka maeneo ya Taita na Voi nchini Kenya. Kilichowakimbiza Kenya ya kale na kuhamia eneo linalojulikana kama milima ya Ugweno kwa sasa ni vita vya wenyewe kwa wenyewe huko Taita na Voi.

Lakini kuna nadharia moja inayosema kwamba kabla Wagweno hawajahamia rasmi katika milima hiyo ya Upare walituma wapelelezi kwanza; walifika eneo husika na kisha wakarudisha taarifa yao wakasema, "Mringa ua khona" (yaani mito ya huko inatoa sauti katika kutiririka kwake) na hapo jina Ugweno likazaliwa, yaani kughona ni muungurumo.

Kwa hiyo tunaweza kuhitimisha kwamba Mgweno ni yeyote aliyekuja na kufanya makazi yake katika milima hiyo mizuri ya ugweno. Ndiyo kusema kwamba wahenga walitoka Taita, Voi, Uchaga na hata Upare: ndiyo maana unaweza kukuta hata koo za Wasangi, Wanzava, nk.

Mfano mzuri ni mzee Modongo na wenzake ambao waliitwa na Wasuya kutoka Usangi ili kuja kuzuia vita visiingie Ugweno. Ukoo huu mpaka leo unapatikana maeneo ya Chanjale kwa Mkuti njia ya kwenda Mangio na Vuchama, tena kuna mzee maarufu wa ukoo huo aitwaye Kiogwe Msangi ambaye alifariki dunia mwaka 1995.

MILA NA DESTURI

Kwa asili, Wagweno hapo kale walikuwa Wapagani wanaoabudu mungu jua [RUBHA], pamwe na mwandani wake MWIRI [MWEZI], mkewe jua, sanjari na watoto wao nyota.

Ibada hii ya kuelekea jua iliambatana na kuabudu mizimu na ndiyo maana kuhani wa Kigweno alipochinja mnyama na kumchuna ngozi yake aliweza kutazama maini kupiga ramli kwa kutumia viungo kwenye tumbo la mnyama.

Tena wanyama hao walichinjwa kwenye eneo maalumu liitwalo kwa Kigweno Ngondinyi. Mara nyingi eneo hili walihusika wanaume bighairi wanawake kwa sababu kwa mila ya Kigweno wanaume ndio makuhani. Mara nyingi katika eneo la kuzunguka Ngondinyi kulipandwa mimea maalum iitwayo Mathale, ambayo kwa mujibu wa mapokeo ya Wagweno ni mimea mitakatifu.

Mnyama anapochinjwa kuhani hukata vipande vidogovidogo na kuviweka eneo husika, kisha huchukua pombe ama mbege au dengelua kisha atatazama mbinguni huku ameshika mkononi pombe kama ishara ya tambiko na kusema RUBHA KAGHU NGOMA MBAI; yaani, naamini mungu yuko juu, lakini chini kuna mizimu. Kisha humwaga pombe na kusema anachokusudia, kama anataka mvua inyeshe au anakusudia kuondosha MSINYANYO [mkosi].

Kwa maana kwa mujibu wa mapokeo ya Wagweno mkosi kwao ulikuwa jambo kubwa sana na ndiyo maana hata mtoto aliyezaliwa na ulemavu wa aina yoyote alitolewa kafara kwenye jiwe la watoto, kwa Kigweno IGHWE YA BHANA.

Mhanga alikuwa anachukuliwa kwenye jiwe husika, mamaye humbembeleza, akiisha kulala hulazwa kwenye kilele cha jiwe na anapoamka ghafla huporomoka na kufa na watakuwa wameondoa mkosi katika jamii na kumfurahisha mahoka.

Kuna kisa kimoja cha kale juu ya bwana mkubwa mmoja aliyeitwa Kindobhai wakati anafukuzwa na maadui kunako eneo ambalo kwa sasa kuna hifadhi ya wanyama ya Tsavo karibia na ziwa Jipe. Inasemekana alipiga fimbo yake kwenye maji na yeye, mifugo na wafuasi wake wakavuka salama!

Masimulizi juu ya Wagweno ni mengi sana, kiasi kwamba unaweza ukastaajabu. Mpaka leo kuna mawe ya ajabu ambayo yako mithili ya watu; inasemekana maadui hapo kale walikuwa wanakuja kuiba mifugo huko, lakini kulingana na ujuzi wa wazee wakageuzwa mawe kwa njia ya miujiza.

 
Mkuu soma vizuri hapo juu uhusiano kati ya Wasuya na Wagweno umeelezwa pia.
Nimesoma, swali langu lilikuwa Msuya ni Mgweno maana anaongea Kigweno (kama sijakosea) au ni Wasuya kama lilivyo jina lake?...
 
Mkuu wakati wanahamia hakukuwa na tanganyika ilikuwa ni survival,story nzuri ya kiafrika vitu kama hivi hua adimu sana humu,shukran.
 
Nimepita huko kote kuna mito mingi na waterfalls. Kuna story nyingi tu kama hizo
 
hongera....
ntafurahi kwa sasa ukatuambia iyo milima ya ugweno iliitwaje kabla ya kuja kwa wagweno
pia uhusiano wao na koo nyingine kwa maelezo yako wasangi na wasuya si wagweno japo mzeee wa ukoo wa wagweno aliefariki ni msangi.
walipokuja walikuta jamii ipi?unaweza kadiria miaka ipi?jamii zingine zilizokuwepo maeneo ya ugweno ya sasa zilienda wapi?km kuna vita zilitokea je hali ilikuaje?unaweza tupa miaka ya safari toka asili yao hadi ugweno ya sasa?
je wagweno ni kabila au ukoo tu?
 
Wagweno na Wachaga wanahusiana? Maana lugha zao zinafanana sana hasa Wachaga wa Vunjo(Kirua, Kilema,Marangu,Mamba na Mwika)
 
kwa maelezo ya watu wengi,wagweno ni machotara wa wapare na wasambaa na wachaga,si walikuja toka nje,sehem nyingi wanapenda waonekane km wazawa na superior than the rest,kwa lugha nyingine tunaweza kuwaita ni koo ndani ya wapare (semi outonomous clan)
NadhaniWagweno ni mchanganyiko wa Wachaga na Wapare na kidogo Wasambaa.
 
hongera....
ntafurahi kwa sasa ukatuambia iyo milima ya ugweno iliitwaje kabla ya kuja kwa wagweno
pia uhusiano wao na koo nyingine kwa maelezo yako wasangi na wasuya si wagweno japo mzeee wa ukoo wa wagweno aliefariki ni msangi.
walipokuja walikuta jamii ipi?unaweza kadiria miaka ipi?jamii zingine zilizokuwepo maeneo ya ugweno ya sasa zilienda wapi?km kuna vita zilitokea je hali ilikuaje?unaweza tupa miaka ya safari toka asili yao hadi ugweno ya sasa?
je wagweno ni kabila au ukoo tu?
Nadhani utakuwa umemuonea mleta mada.

Milima inaweza kuwa ipo na haikuwa na wakazi, au walikuwepo lakini ni koo ndogo sana

Ukitaka kujua vema mahusiano ya makabila ni muhimu ukaangalia jiografia.
Maeneo ya zamani yalikuwa na watawala ambao maeneo yao yalikuwa madogo.

Ukisema milima ya Ugweno ni pamoja na safu ya milima yenye eneo la Usangi.

Kwa sasa inaitwa pare escapement kwasababu inaanzia Ugweno na kwenda hadi maeneo ya Mbaga halafu bonde linalotenganisha ni milima ya Lushoto(Usambara escapement)

Wagweno ni kabila linalojitegemea limetokea kuwa katika eneo linalojulikana kama Upare

Kama alivyosema mwenzetu mmoja, Wagweno ni ' sub clan' ndani ya kabila la Wapare
Muhimu kujua Wagweno wanazungumza kipare lakini Wapare hawazungumzi Kigweno

Kuna mwingiliano wa koo kutokana na tawala kwasababu ya vita

Koo ziliishi kwa kutegemeana na hivyo koo moja inaweza kuwa eneo lisilotarajiwa
Ni kwa mtazamo huo kuna mwingiliano unaotoa kitu kinachoitwa 'Wapare'

Wapare unaweza kuwakuta katika maeneo ya Wagweno na wanapohamia huko huzungumza lugha ya wenyeji wao.

Ni kwa msingi huo koo za Wasangi zilikuwa 'warrior' na kuna nyakati zilitumika katika vita za koo. Kuwakuta Wasangi eneo la Wagweno ni kawaida

Wasuya kwa asili yao ni watawala na hivyo kuwakuta Usangi si jambo la kushangaza

kutokana na kuhama na udogo wa eneo la milima ya Ugweno.
Kutoka Ugweno na Usangi ni ''walking distance''

Lakini pia utakuta Wambaga ambao kwa asili walikuwa wataalam wa mvua.
Hawa walichukuliwa kutoka milima ya Mbaga kule Same ili kusaidia shughuli za mvua

Kuna Washana, walikuwa ni mahiri kwa uhunzi na ufuaji wa vyuma 'smith'

Nao walikarbishwa maeneo mengine ya Usangi na Ugweno ili kusaidia uhunzi na utengenezaji zana ziwe ni silaha au zana za kilimo

Wapo Wasemo, walijulikana kama 'wanasheria' laiti ingekuwa zama hizi tungewaita 'lawyer' . Walisifika sana katika mashauriano hasa pilikuwepo na mitafaruku

Kuna koo ndogo kama Wafinanga, Wachomvu n.k. ambao nao kila mmoja ilikuwa na specialty katika eneo fulani. Hivyo walikaribishwa

Kwa maneno mengine, ukienda Ugweno au Usangi utakuta kila koo inayotengeneza jamii ya Wapare

Kwasababu ya ukaribu wa milima ya usambara (usambara escapement') kuna mwingiliano wa Wasambaa na Wapare ambao kabila linalojulikana ni Wambugu

Wambugu wanazungumza lugha ya mchanganyiko kipare na kisambaa wakiiba maneno toka pande zote. Hawa Wambugu ni maarufu sana kwa ufugaji.

Kiuhalisia wasambaa walitakiwa wawe mkoa wa Kilimanjaro, au Wapare wawe mkoa wa Tanga

Hata hivyo kiutamaduni Wapare wapo karibu sana na Wachaga.

Hao Wagweno wanazungumza lugha inayoingiliana sana na Warombo na hata tamaduni alizosema mleta mada za matambiko zinaingiliana

Kutokana na mwingiliano ni rahisi sana kukuta majina ya Wachaga upareni hasa ugweno
Huko utakuta akina Minja, Kimaro n.k.

Kwa mtazamo huu, si lazima Msuya au Msangi atoke eneo fulani

Mshana wa Wilaya ya Same, yupo pia Ugweno au Usangi ingawa wana shina moja
Shina la Wasuya lipo Ugweno, Shina la Wasangi lipo Usangi. Watu wanahama hata hivyo

Nimalizie kwa kusema katika Mkoa wa Kilimanjaro Wapare wana identity kwasababu unaweza kuwakusanya katika hall la mikutano wakazungumza lugha ya Kipare na kuelewana

Tatizo lipo kwa Wachaga ambao mara nyingi tunafanya makosa kuita kabila.

Wachaga si kabila ni shirikisho la makabila ya kichaga.

Huwezi kuwaweka Wachame, Warombo, Wakirua, Wamasama, Wavunjo wakaongea lugha moja katika hall la mikutano. Ndio maana ni shirikisho na si kabila ha ha ha

Ngoja siku nitarudi nyumbani Kicheba, Mjasani na Magoroto nako nina jambo
 
Mkuu Naomba Tofauti kati Ya Wagweno Na Wapare??
Ndugu wataka tofauti ya Kabila au Lugha? Kwa mujibu wa Atlasi ya Lugha za Tanzania (Mradi wa Lugha za Tanzania Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, 2009), ingawa kuna uhusiano mkubwa kati ya Lugha na Jamii inayotumia Lugha (Kabila), kuna baadhi ya jamii ambazo jina la Lugha ni TOFAUTI na JINA la KABILA. Katika Ukurasa wa xii wa Atlasi hiyo upo mfano wa WAPARE (Kabila) ambao hujipambanua kwa LUGHA 2, yaani: KIGWENO na KIASU.
Kwa muktadha huu, jibu la swali lako ni kuwa: Wapare ni KABILA na WAGWENO ni wana Jamii (ambao ni WAPARE) wanaotumia LUGHA ya KIGWENO....
Karibu..
 
Tatizo lipo kwa Wachaga ambao mara nyingi tunafanya makosa kuita kabila. Wachaga si kabila ni shirikisho la makabila ya kichaga. Huwezi kuwaweka Wachame, Warombo, Wakirua, Wamasama, Wavunjo wakaongea lugha moja katika hall la mikutano. Ndio maana ni shirikisho na si kabila
Ndugu yangu, utafiti wa Lugha za Tanzania unaoripotiwa katika Atlasi ya Lugha za Tanzania (Mradi wa Lugha za Tanzania Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, 2009), una maelezo tofauti kidogo na uliyo yatoa hapa. KICHAGGA ni KABILA, ila kuna LUGHA tofauti ndani ya kabila hili, ndio sababu ya tofauti ulizotaja hapa. Lugha hizi ni: Kimochi, Kimashami, Kirombo, Kivunjo, Kiuru na Kiwoso.
 
Back
Top Bottom