Wadau watoa kauli upatikanaji wa mafuta Tanzania

Kikwajuni One

JF-Expert Member
Mar 18, 2013
13,142
6,947
Dar es Salaam. Wamiliki wa maghala ya mafuta nchini wameihakikishia Serikali kuhusu upatikanaji wa mafuta wakisema wana petroli na dizeli za kutosha na wapo tayari kutoa ushirikiano wa kuyasambaza kwenye maeneo mbalimbali yenye uhitaji.

Wadau wameiambia Serikali kuwa hivi sasa wanafanya kazi saa 24 hadi siku za mapumziko ili kuhakikisha magari yanaingia na kutoka katika maghala kwa lengo la kuchukua mafuta na kuyasafirisha katika maeneo mbalimbali.

Wametoa hakikisho hilo jana Jumapili Julai 23, 2023 mbele ya Waziri wa Nishati, January Makamba aliyeambatana Kamishna wa Mafuta na Gesi Asilia, Michael Mjinja na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura), Dk James Andilile. Viongozi hao wamefanya ziara ya kukagua maghala hayo.

Hii mara ya pili kwa Ewura kukagua na maghala hayo na kuzungumza na wamiliki kuhusu hali ya upatikanaji wa mafuta katika maeneo mbalimbali baada ya hivi karibuni kuzuka sintofahamu kwa baadhi ya maeneo kutopata nishati hiyo kwa uhakika.

Meneja Mkuu wa Meru Petroleum, Charles Maingu amesema ndani ya siku 10 zilizopita wametoa mzigo wa mafuta wa lita milioni 28 yaliyosafirisha ndani ya nchi na nje ya nchi, akisema Agosti pia watapokea mzigo mwingine dizeli milioni 27 na petroli lita milioni 40.

"Pia mzigo wa Septemba mafuta ya petroli ni lita milioni 19.5 na dizeli lita milioni 18. Waziri (Makamba), hapa shughuli zinaendelea huu mzigo unaotoka unakwenda nje ya nchi ndani ya tumeshawapelekea hasa maeneo ya pembezoni.

"Kuna maeneo yoyote yenye changamoto ya upatikanaji wa nishati hii, tupewe taarifa tutaifikisha, nisema tu hakuna changamoto ya mafuta yapo ya kutosha," amesema Maingu.

Wakati Maingu akieleza hayo, Mkurugenzi Mtendaji Puma Energy, Fatma Abdallah amesema Julai mwaka huu kumekuwa na mahitaji makubwa ya mafuta akisema hadi jana wameuza petroli na dizeli lita zaidi ya milioni 36. Amesema hali hiyo ni tofauti na mwaka 2022 waliuza milioni 30.

"Tunatarajia kuuza zaidi ya lita milioni 50 za mafuta hadi mwezi huu unaisha. Tunauza mafuta yetu kwa wateja wakubwa wadogo, meli zinazokuja pia zina mzigo wetu na kabla ya Julai haijaisha tunatarajia kupata lita milioni 16.

"Lakini Agosti tutapata mafuta ya dizeli na petroli lita zaidi ya milioni 60, niwatoe hofu wauzaji wakubwa na wadogo mafuta yapo ya kutosha na tunashirikiana kwa ukaribu na Serikali.Nawahakikishia Watanzania mafuta yapo ya kutosha waondoe hofu," amesema Fatma.

Mbali na hilo, Fatma amesema wanakabiliana na changamoto ya dola za Marekani akiomba Serikali kuangalia namna ya kuwasaidia ili wafanyabiashara wakubwa waagize mzigo kwa ufanisi.

Akijibu ombi hilo, Waziri Makamba amemuhakikishia Fatma kwamba Serikali inatambua changamoto hiyo, na inalifanyia kazi kwa ukaribu.

Meneja Uendeshahi wa Total Energies, John Bernard amesema bado wanaendelea na kuuza mafuta ili kuhakikisha wananchi wanapata nishati hiyo kwa wakati, akisema hadi jana Jumapili wamefungua maghala yao ili kutoa huduma kwa magari yanayochukua nishati hiyo.

"Ni muhimu Watanzania kufahamu kwamba mafuta yapo ya kutosha na meli zinaendelea kuingiza nishati hii na tunashirikiana na Serikali kwa ukaribu kwa changamoto itakayojitokeza," amesema Bernard.

Mkuu wa Kitengo cha Usimamizi wa Meli wa Wakala wa Uagizaji Mafuta Pamoja (PBPA), Bruno Tarimo amesema meli zote zilizopangwa kuleta mzigo wa mafuta kwa mwezi Julai zimefika kwa wakati, akisema hivi sasa meli ya pili inamalizia kupakua mzigo.

"Niwahakikishie Watanzania hakuna tishio la upungufu wa mafuta tunakwenda vizuri hata katika mpangilio wa meli hadi zitakazoleta mzigo mwezi ujao," amesema Tarimo.

Mkurugenzi wa Bandari ya Dar es Salaam, Mrisho Mrisho amesema shughuli ya kushusha mafuta inafanyika kila siku akisema hivi kuna meli inayopakua petroli na dizeli huku akiwatoa hofu wa Watanzania kuhusu upatikanaji wa nishati hiyo.

"Katika mipango ya baadaye tunajipanga zaidi kuboresha maeneo mbalimbali ya bandari likiwemo la kupokelea mafuta.Leo ni siku ya tatu meli inashusha kesho inamaliza na kuingia nyingine," amesema Mrisho.

Kwa upande wake, Makamba amesema lengo ziara hiyo ni kujua hali ya mafuta yaliyopo katika maghala ya wafanyabiashara hao, sambamba kusikia na kuzibeba changamoto zinazowakabili wadau hao wa sekta hiyo.

Naye, Dk Andilile amesema wamepita takribani maghala sita yanayohifadhi mafuta, akisema wamehakikishiwa kuwa nishati hiyo ipo na Watanzania wasiwe na hofu. Akisema kwa sasa wanaendelea na utaratibu wa kuyasafirisha kupelekwa katika maeneo mbalimbali hasa pembezoni.

"Nchi ina mafuta ya kutosha, kinachofanyika hivi sasa ni kuyapeleka maeneo mbalimbali hasa pembezoni ambayo yalikuwa na changamoto ya upatikanaji wa mafuta.Wamiliki wa maghala wametuhakikishia kuwa yatafika kwa wakati wananchi wasiwe na hofu," amesema Dk Andilile.
 
Back
Top Bottom