Wabunge wakosa imani na Kenya, Uganda | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Wabunge wakosa imani na Kenya, Uganda

Discussion in 'Habari na Hoja mchanganyiko' started by kilimasera, Apr 20, 2010.

 1. kilimasera

  kilimasera JF-Expert Member

  #1
  Apr 20, 2010
  Joined: Dec 2, 2009
  Messages: 3,073
  Likes Received: 17
  Trophy Points: 135
  WABUNGE wametaka raia wa Kenya na Uganda walioajiriwa katika sekta mbalimbali nchini, kabla ya kuanza kwa Itifaki ya Soko la Pamoja la Jumuiya ya Afrika Mashariki, warudishwe makwao.

  Pia wameitaka serikali kuhakikisha inawanyang’anya ardhi raia wa nchi nyingine za Jumuiya ya Afrika Mashariki walionunua ardhi nchini na irudishwe mikononi mwa Watanzania.

  Wakijadili azimio la Itifaki ya Soko la Pamoja la Jumuiya ya Afrika Mashariki iliyowasilishwa na Waziri Dk. Diodorus Kamala, wabunge hao walisema haiwezekani raia hao wa nchi nyingine wajazane kwenye ajira za nchini wakati kuna Watanzania wengi hawana ajira.

  Mbunge wa Same Mashariki, Anne Kilango Malecela (CCM) ametaka kufanyike kwa sensa katika hoteli na sekta nyingine kubaini raia wa Kenya na Uganda wanaofanya kazi nchini na warudishwe makwao kusubiri kuanza utekelezaji wa Itifaki hiyo.

  “Tunao vijana wengi tu hapa nchini wamesoma vizuri na wanaongea Kiingereza vizuri, lakini ukienda kwenye mahoteli waliojazana ni Wakenya, hawa naomba warudishwe makwao wasubiri mpira uanze tucheze sawa,” alisema mbunge huyo.

  Kwa upande wa ardhi, alisema serikali ifanye utafiti kubaini raia wa kigeni hasa wanaotoka kwenye nchi za Rwanda, Burundi, Kenya na Uganda walionunua ardhi katika mikoa ya mipakani wanyang’anywe ardhi hiyo.

  “Ardhi ya nchi ndio mali yetu, wenzetu hawa wana matatizo ya ardhi, serikali itambue ardhi hii ni kwa ajili ya Watanzania, hivyo serikali ikafanye tafiti mipakani na kama kuna ardhi imeshanunuliwa kinyemela na wenzetu hawa irudishwe,” alisema.

  Mbunge wa Masasi, Raynald Mrope (CCM), aliishambulia Kenya kuwa ndio chanzo cha kuvunjika kwa jumuiya ya awali ya Afrika Mashariki mwaka 1977 na akaonya kuwa vitendo vya Wakenya vinatishia uhai wa jumuiya ya sasa hasa vya kuibia rasilimali Tanzania kama madini ya tanzanite.

  Alisema Serikali ya Kenya inawatia kiburi raia wao kuendelea kuibia Tanzania hivyo akaitaka serikali iwakemee haraka likiwemo hili suala la kupinga Tanzania kuuza meno ya tembo katika mkutano wa Cites huko Doha nchini Qatar.

  Mbunge wa Makete, Dk. Binilith Mahenge alisema Tanzania sasa hivi inazalisha wasomi wengi kila mwaka na isipokuwa makini katika utekelezaji wa Itifaki ya Soko la Pamoja, vijana wengi wanaweza kujikuta hawana ajira.

  Alitaka vyuo vikuu vinavyotoa elimu kuhakikisha vinawapa mafunzo na ujuzi vijana hao ili wamudu ushindani katika soko hilo. Pia aliwataka wajasiriamali kuzalisha bidhaa bora ambazo zitakubalika katika nchi zingine za jumuiya ya Afrika Mashariki.

  Mbunge wa Kahama, James Lembeli (CCM), alisema kama ajira wataachiwa wageni hao kuingia holela, vijana wa Kitanzania wataenda wapi. Alitaka serikali ihakikishe kwenye sekta ya utalii inawapunguza raia hao wa Kenya ili Watanzania nao wapate ajira hizo.

  Lakini alionya kuwa katika utekelezaji wa Itifaki ya Soko la Pamoja, Wakenya wamejiandaa kujenga hoteli za nyota nne hadi tano katika sehemu mbalimbali nchini, hali itakayowezesha kumiliki uchumi katika maeneo hayo.

  Alisema serikali ya nchi yao imeahidi kuwasaidia kwa kuwapa mkopo hivyo akataka Serikali ya Tanzania nayo kuwawezesha wafanyabiashara nchini waweze kuwa na uwezo wa kwenda kujenga hoteli katika nchi zingine za Afrika Mashariki.

  Mbunge wa Kuteuliwa, Jussa Ismail Ladhu (CUF), alitaka Watanzania wajihami kulinda ajira zao na akasema kufanya hivyo sio jambo baya na wala sio kuogopa ushirikiano wa Afrika Mashariki.

  Mbunge wa Shinyanga, Dk. Charles Mlingwa (CCM) alisema ni vigumu kukaa meza na Kenya wakati nchi hiyo inaongoza kupinga mipango ya Tanzania yenye lengo la kujikwamua kiuchumi.

  Alisema kama juhudi za makusudi hazitafanywa za kuionya Kenya, anaamini ni vigumu kuijenga Jumuiya ya Afrika Mashariki wakati hulka ya nchi nyingine ni kutaka wenzao waporomoke kiuchumi.

  Maoni ya kambi ya upinzani yalitaka Bunge likemee kwa nguvu zote vitendo vya ujangili vinavyofanywa na Kenya ambavyo lengo lake ni kudhoofisha uchumi wa Tanzania.

  Kambi hiyo katika hotuba yake iliyosomwa na Abubakary Khamis Bakary, ilieleza kuwa ni jambo la kushangaza kuona kwenye hoteli, maduka waliojazana huko ni wafanyakazi kutoka Kenya.

  “Mbona maeneo haya yamejaa wakenya wakati sisi Watanzania bado hatujapata nafasi hizo, hii inatokana na kutojali uzalendo na ushirikiano wapamoja ndio uliotufikisha hapa,” alisema Bakary.

  Wabunge walitoa maoni hayo wakati Wakenya wengi wanafanya kazi kwenye hoteli huku raia wengi wa Uganda wao wamejikita kufundisha kwenye shule za msingi zinazofundisha kwa Kiingereza.
   
 2. Lekanjobe Kubinika

  Lekanjobe Kubinika JF-Expert Member

  #2
  Apr 20, 2010
  Joined: Dec 6, 2006
  Messages: 3,067
  Likes Received: 18
  Trophy Points: 135
  Ni kawaida ya wabongo kushabikia nchi za kigeni.
   
 3. Drifter

  Drifter JF-Expert Member

  #3
  Apr 20, 2010
  Joined: Jan 4, 2010
  Messages: 1,968
  Likes Received: 668
  Trophy Points: 280
  Kwa upande mwingine nafikiri soko la pamoja linaweza kuwa jawabu la kumaliza "uswahili" uliojikita katika uongozi na jamii yetu kwa ujumla. Ujio wa Wakenya, Waganda, Wanyarwanda na Warundi kwenye soko letu (kwanza ulishaanza taratiib) kutatoa changamoto ya kutosha kwetu Watanzania kuachana na ubabaishaji na kuanza kuendesha nchi na uchumi wetu kwa umakini zaidi. Huu mchezo wa kuchangamkia hongo (peanuts) za wageni na kuruhusu ufujaji uliokithiri wa rasilimali ya taifa hautibiki kwa siasa uchwara tunazoendekeza hivi sasa. Hayo mawazo ya wabunge wetu labda ni kutafuta jawabu la muda mfupi tu. Tunaogopa kuliwa na wana-Afrika mashariki wenzetu? Mbona tumejiachia kikamilifu kwa makaburu, wadosi, wachina, wazungu, waburushi, n.k.? Ni rasilimali zipi na ajira gani tunazozilinda hadi sasa? Tunaangalia nje? Mbona tatizo ni sisi wenyewe? Mgeni gani atayetuogopesha endapo tutakuwa na utashi, nia halisi, sera sahihi, uongozi imara na mikakati thabiti ya kuendeleza nchi yetu? Kuongea kwa jazba dhidi ya soko la pamoja na kunywea kwenye hoja za ufisadi uliokithiri nchini ni cheap politics.
   
Loading...