fangfangjt
JF-Expert Member
- Apr 25, 2008
- 571
- 139
Wabunge wajadili mitambo ya Dowans gizani
Monday, 14 March 2011 21:29
Leon Bahati
SIKU ya kwanza ya wabunge kujadili mpango wa kubadilisha sheria ya manunuzi ili serikali iruhusiwe kununua mitambo iliyotumika ilikumbwa na kioja cha aina yake baada ya umeme kukatika ghafla na giza kutanda ukumbini hali iliyowafanya baadhi ya wabunge kupiga kelele; Dowans! Richmond! Dowans! Richmond! Dowans na baadaye CCM! CCM! CCM!
Ikipitishwa, sheria hiyo itaiwezesha Serikali kununua mitambo ya Dowans ili kutatua tatizo la umeme linalolikabili Taifa.Kelele hizo zilizoandamana na kejeli za kuwasha kurunzi za simu za mikononi na kumtaka mtoa mada kuendelea kwa kutumia mwanga huo hafifu zilisikika katika eneo walilokuwepo wabunge wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).
Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti Manunuzi ya Umma (PPRA), Dk Ramadhani Mlinga ndiye aliyekuwa akitoa mada juu ya taratibu za Usimamizi wa Mifumo ya Manunuzi Serikalini.
"Endelea! Endelea! Endelea!" Walisikika wabunge hao wakisema huku wakiwa wamewasha kurunzi za simu zao ambazo mwanga wake haukuhimili giza lililokuwepo kwenye ukumbi wa Hoteli ya Blue Pearl, Ubungo, Dar es Salaam." Wabunge walibakia gizani kwa takriban dakika 10 kabla ya umeme kurejea.
Waandishi wa habari nao walitumia fursa hiyo kuwahoji baadhi ya wabunge na wakati wa mahojiano hayo, wabunge hao waliwasaidia wapigapicha za televisheni kwa kuwasha kurunzi za simu zao na kuwamulika usoni wale waliokuwa wakihojiwa ili waonekane vizuri.
Mbunge wa Iringa Mjini (Chadema), Mchungaji Peter Msigwa alisema hayo ni matokeo ya Serikali ya CCM kukumbatia mikataba mibovu kama walioingia na kampuni ya Richmond Development LLC... "Mkataba huo ndiyo uliorithiwa na Dowans ambayo hukumu imetaka Tanzania iilipe kampuni hiyo Sh 94 bilioni."
Mbunge wa Viti maalumu (Chadema), Naomi Kihula alilibebesha mzigo wa lawama Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) akisema kuzima kwa umeme huo ni ishara kwamba shirika hilo la umma haliheshimu hata Bunge.
Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tindu Lissu alisema kitendo ni adhabu kutoka kwa Mungu kwa mjadala huo akidai kwamba Mkuu wa PPRA, Dk Milinga alipinga vikali utoaji wa zabuni kwa Richmond lakini vigogo serikalini wakashikilia msimamo wa kumpinga.
Alisema hakubaliani na mpango huo wa kubadili sheria hiyo ya manunuzi ili kuwezesha serikali kununua mitambo ya Dowans kama njia ya kutatua tatizo la umeme nchini.
Baada ya jenereta la hoteli hiyo kuwashwa, Dk Mlinga aliendelea na mada yake na kueleza kwamba kutatua tatizo la umeme nchini kwa kununua mitambo mipya itachukua muda mrefu. Lakini akasema sheria ya PPRA inayotumika sasa hairuhusu kununua mitambo iliyotumika jambo ambalo linaibana serikali kutafuta suluhu ya tatizo la umeme nchini kwa haraka.
Kwa mujibu wa Mlinga, siyo lazima sheria hiyo iruhusu moja kwa moja ununuzi wa mitambo iliyotumika, bali iwe ni mazingira magumu kama yalivyo nchini sasa na kwamba kutakuwa na vigezo.
"Taratibu (kwa sheria mpya) zitaandaliwa ili kukabiliana na mazingira ya kusaidia mitambo ikinunuliwa iwe na vigezo vya kitaalamu vinavyoonyesha uwezo wake wa kazi," alisema.
Lakini hakuna mbunge aliyechangia kwenye mkutano huo unaongozwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Uchumi na Fedha, Dk Abdallah Kigoda aliyeonyesha wazi kwamba anaunga mkono mpango wa kubadili sheria hiyo ya manunuzi.
Hali hiyo ilimfanya Dk Kigoda kuwataka wawe makini kwa sababu kamati yake ilijadili kwa undani suala hilo na kubaini kwamba sheria hiyo ina upungufu... "Suala la manunuzi tulifikirie kwa umakini," alisema akieleza kuwa wabunge ndiyo wanaotarajiwa kuokoa jahazi la tatizo la umeme nchini.
Aliwataka wajaribu kufikiria njia fupi ya kulitatua ili kuokoa uchumi, maana hali inaweza kuwa mbaya zaidi kwa taifa iwapo litadumu kwa siku 100.
Awali, akifungua mkutano huo, Naibu Spika wa Bunge, Job Ndugai aliwataka wabunge hao kutumia fursa hiyo kuishauri serikali kuhusu utaratibu mzima wa usimamizi na mifumo ya ununuzi wa umma kwani hali ya nchi ni mbaya.
"Eneo la manunuzi ni changamoto kubwa kwa serikali. Bado kuna udhaifu katika udhibiti na uwajibikaji katika eneo zima la manunuzi," alisema Ndugai na kuwataka wabunge kuwa makini na kutumia mjadala huo kuishauri serikali kwa sababu asilimia 70 ya bajeti yake inatumika kwa manunuzi na asilimia 90 ya bajeti ya maendeleo nayo hutumika katika suala hilo hilo.
"Fedha nyingi za Serikali zinapotea katika manunuzi. Ni changamoto kwetu sisi wabunge kuishauri ipasavyo Serikali katika eneo hili. Muswada wa Sheria ya Manunuzi ya Umma ya mwaka 2010 unategemewa kujadiliwa na kupitishwa na Bunge lijalo," alisema Ndugai.
Hata hivyo, alisema kabla ya kupelekwa bungeni, Kamati ya Bunge ya Fedha na Uchumi itawashirikisha wadau mbalimbali kuuboresha.