Wabunge Waalikwa Kutembelea Mradi wa ECOP

Stephano Mgendanyi

JF-Expert Member
May 16, 2020
1,900
944
WABUNGE WAALIKWA KUTEMBELEA MRADI WA EACOP

Naibu Waziri wa Nishati, Wakili Stephen Byabato amewaalika Wabunge katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kutembelea Mradi wa Bomba la kusafirisha Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP) kutoka Hoima Uganda hadi Chongoleani Tanga ili kufahamu hatua mbalimbali za utekelezaji zinazoendelea.

Byabato alisema hayo wakati wa Semina iliyoandaliwa na mradi wa EACOP kwa ajili ya wabunge hao kwa lengo la kuwaeleza kile kinachofanyika katika mradi huo hasa maeneo yaliopitiwa na mradi huo iliyofanyika Bungeni Jijini Dodoma Mei 25, 2023.

Alisema kuwa ni muhimu kwa wabunge wakatembelea eneo la mradi huo ili kuona na kuthibitisha mazuri yanayofanyika na kuwaeleza watanzania kwa kuwa wao ndiyo wawakilishi wa wananchi.

“Nawashauri wabunge kila mmoja atembelee maeneo ya mradi, aone yaliyofanywa na mradi huo na kuwaeleza watanzania, kwa kuwa wabunge ndiyo wawakilishi wa wananchi hivyo mtatoa taarifa sahihi zitakazopuuza taarifa hasi zinazozungumzwa dhidi ya mradi huo na baadhi ya watu wasiopenda maendeleo ya nchi yetu,” alisisitiza Wakili Byabato

Alisisitiza kuwa Serikali itaendelea kusimamia mradi huo kikamilifu na kuendelea kutoa taarifa sahihi juu ya mradi huo.

Akizungumzia kuhusu uboreshaji wa miundombinu ya barabara katika eneo linalojengwa kiwanda cha kupasha moto mabomba yatakayosafirisha mafuta cha Sojo, Naibu Waziri amesema wa sasa Wizara ya Nishati na Wizara ya Ujenzi zinashirikiana kwa pamoja kuona namna bora ya kujenga barabara hiyo.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Dunstan Kitandula ameipongeza Wizara ya Nishati kwa kuandaa semina hiyo kwa wabunge wote kwa kuwa ni muhimu kwa wabunge hao kuufahamu kwa kina kile kinachofanyika katika mradi huo.

Kitandula aliielekeza Wizara ya Nishati, kuhakikisha kuwa kazi ya ulizi wa bomba hilo kwa upande wa Tanzania ifanywe na vyombo vya ulinzi na usamala vya ndani ya nchi.

Vilevile alieleza kuwa serikali iendelee kutoa elimu na mafunzo kwa vijana wa kitanzania ili kuwaanda katika kusimamia Sekta ya Mafuta na Gesi kwa kuzingatia miradi mikubwa ya sekta hiyo itakayotekelezwa hivi karibuni ukiwemo ule wa kusindika Gesi Asilia wa LNG.

“Serikali na Wizara andaeni mapema Vijana wa Kitanzania ili waje kusimamia miradi yetu ya Mafuta na Gesi nchini kwa weledi na uzalendo, hii itasaidia kuondokana na ombwe la kukosa vijana wa kitanzania kusimamia miradi yetu, pia EACOP iendelea kutoka elimu sahihi kwa wananchi ili kuulinda mradi huo mkubwa na muhimu kwa nchi yetu”, alisisitiza Kitandula.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa EACOP, Matrin Tiffen alisema kuwa mradi huo unaendelea vyema katika hatua za awali za utekelezaji na kwamba tayari kazi ya ujenzi wa kituo cha kupasha moto mabomba ya kusafirisha mafuta kilichopo Sojo mkoani Shinyanga zinaendelea.

Alisema kuwa, mradi huo utatekelezwa kwa kuzingatia utunzaji wa mazingira, viumbe hai na mazingira asili ya maeneo husika zikiwemo Mbuga za Wanyama, Misitu na vyanzo vya maji.
 

Attachments

  • uzHfySPEerw.jpg
    uzHfySPEerw.jpg
    50.3 KB · Views: 9
  • Fw_ByZAaEAAsOtx.jpg
    Fw_ByZAaEAAsOtx.jpg
    164.8 KB · Views: 8
  • PICHA2_copy_720x480-537x360.jpg
    PICHA2_copy_720x480-537x360.jpg
    33.3 KB · Views: 8
  • PICHA33_copy_720x480-537x360.jpg
    PICHA33_copy_720x480-537x360.jpg
    32.6 KB · Views: 8
  • PICHA42_copy_720x480-537x360.jpg
    PICHA42_copy_720x480-537x360.jpg
    35.2 KB · Views: 8
Back
Top Bottom