Wabunge wa CCM waondolewa woga | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Wabunge wa CCM waondolewa woga

Discussion in 'Habari na Hoja mchanganyiko' started by Rutashubanyuma, Jan 23, 2011.

 1. Rutashubanyuma

  Rutashubanyuma JF-Expert Member

  #1
  Jan 23, 2011
  Joined: Sep 24, 2010
  Messages: 158,305
  Likes Received: 417,643
  Trophy Points: 280
  Wabunge wa CCM waondolewa woga

  Imeandikwa na Mwandishi Wetu; Tarehe: 22nd January 2011 @ 23:59

  WAKATI Mkutano wa Pili wa Bunge la Jamhuri ukikaribia kuanza mapema mwezi ujao, wabunge wa CCM wamepewa ujasiri.

  Wameambiwa safari hii wajadili masuala yenye maslahi ya Taifa kwa ujasiri mkubwa na bila kumwogopa wala kumpendelea mtu.

  Ujasiri huo walipewa jana na Kiongozi wa Shughuli za Serikali Bungeni, Waziri Mkuu Mizengo Pinda, ambaye aliwataka watimize wajibu wao ili ukweli ujitenge na uongo na wasaidie kulinda
  uadilifu wa chama na wa wabunge binafsi.

  “Wabunge wana wajibu wa kushauri na kuhoji utendaji wa Serikali bila kumpendelea mtu.

  Kwa kujituma kila mmoja na kwa pamoja, malengo ya kitaifa yatafanikiwa na kuwanufaisha wananchi,” alisema Pinda alipokuwa akihutubia kwenye semina ya siku tatu itakayofungwa kesho na Rais Jakaya Kikwete ambaye ni Mwenyekiti wa CCM.

  Aliwataka wabunge hao, kufanya juhudi za ziada kama wanataka kujijengea heshima na kuwa na mafanikio.

  “Kufanya utafiti ili utoe mchango uliochambuliwa vizuri bungeni, ni jambo muhimu.

  “Hoja nzuri zinapatikana baada ya kufanya utafiti na uzito wa mchango wa mtu, unaonesha uwezo wake katika kuibua mijadala makini yenye lengo la kunufaisha nchi,” alishauri Pinda.

  Alisema haitoshi tu kuchangia hoja bungeni, lakini pia wanapaswa kufanya kazi katika majimbo yao na kuwa karibu na wananchi.

  Akichangia hali iliyozoeleka ya kuwa na viti visivyo na wabunge wakati vikao vya Bunge vikiendelea, Pinda alisema mawaziri wanaiwakilisha Serikali, hivyo wana wajibu wa kuhudhuria vikao vyote na kuwa tayari kujibu hoja zote zitakazoibuliwa na wabunge.

  “Wabunge wa CCM pia wanapaswa kutumia vizuri fursa ya maswali na majibu kwa Waziri Mkuu badala ya kukaa kimya na kuwapa nafasi wapinzani,” alisema.

  Awali, Katibu wa Halmashauri Kuu (NEC) ya Chama anayeshughulikia itikadi na uongozi, John Chiligati, alisema warsha hiyo imefanyika wakati muafaka kwa kuwa vikao vya Bunge lijalo vitaanza wiki mbili zijazo.

  “Kuna wabunge 260 wa CCM, lakini kati yao, asilimia 60 ndio wanaingia bungeni kwa mara ya kwanza. Ni muhimu kuzifahamu kanuni za Bunge na taratibu zake ili mtoe mchango wenu vizuri,” alisema Chiligati.

  Mbunge wa Viti Maalumu, Riziki Lulida (Lindi), alikiri kuwapo changamoto katika vikao vijavyo vya Bunge, kwa kuwa upinzani umepata nguvu baada ya kuongeza viti vyao.

  “Warsha hii ni muhimu sana. Itatupa muda wa kukusanya nguvu na ufahamu kuhusu njia sahihi ya kutoa hoja.

  Kuwa mbunge wa chama tawala, haimaanishi kuwa mkimya katika mambo yenye maslahi ya nchi. CCM itaendelea kusimama kwenye ukweli,” alisema.

  Changamoto hii kwa wabunge inatolewa huku mkutano ujao ukionekana huenda ukawa na hoja nyingi binafsi hasa kutoka kwa wabunge wa upinzani.

  Masuala makubwa ambayo yanatarajiwa kujitokeza kupitia hoja binafsi ni la Katiba mpya ambapo Mbunge wa Ubungo John Mnyika (Chadema) anatazamiwa kuiwasilisha.

  Lakini pia Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila (NCCR-Mageuzi), anatazamiwa kuibuka na hoja kuhusu kampuni inayojadiliwa sana hivi sasa ya Dowans ambayo inatakiwa kulipwa fidia ya Sh bilioni 94 na Tanesco kutokana na kuvunjiwa mkataba wake.

  Mnyika katika hoja yake, anataka Bunge lipitishe maazimio ya kuweka utaratibu wa kiusimamizi na wa kisheria wa kuratibu mchakato mzima wa kuandikwa kwa Katiba hiyo mpya.

  Naye Kafulila kwa upande wake, hoja yake ni ya kuitaka Serikali itoe maelezo juu ya mgawo wa umeme na matokeo ya hukumu ya Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhisho ya Migogoro ya Kibiashara (ICC) kuhusu kesi ya Dowans dhidi ya Tanesco.

  Hoja hizi kama zitawasilishwa na kujadiliwa, bila shaka zitaibua mjadala mzito na huenda hata wabunge wa CCM wakiwamo baadhi ya mawaziri wakakosa uzalendo na kuigeuka Serikali.

  Hali hiyo inatokana na jinsi hivi karibuni kulivyoanza kujitokeza malumbano ya nje ya vikao, kwa mawaziri wawili kulijadili suala la Dowans hadharani na kuonesha wazi kuwa hawakubaliani na msimamo wa Serikali kulipa fidia hiyo.

  Kama hali hiyo itajitokeza kama ambavyo ilishaoneshwa na Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki Samuel Sitta na Naibu Waziri wa Ujenzi, Dk. Harrison Mwakyembe, ni wazi kuwa msimamo uliotolewa na Pinda kwa wabunge wa CCM unaweza ukatibuka.

  Lakini pia wapinzani bungeni watapata nguvu na kuichachafya Serikali na hata kuiweka pabaya kama ilivyowahi kutokea huko nyuma katika mjadala uliohusu kampuni ya kufua umeme ya Richmond ambayo ilisababisha mawaziri watatu kujiuzulu akiwamo aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa.

  Wengine waliojizulu kutokana na kashfa hiyo Februari 2008, alikuwa ni Waziri wa Nishati na Madini wa zamani Nazir Karamagi na aliyekuwa Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk. Ibrahim Msabaha.
   
 2. Rutashubanyuma

  Rutashubanyuma JF-Expert Member

  #2
  Jan 23, 2011
  Joined: Sep 24, 2010
  Messages: 158,305
  Likes Received: 417,643
  Trophy Points: 280
  Wabunge wakemee maovu, wasizibwe midomo

  [​IMG]

  [​IMG] CHAMA Cha Mpinduzi (CCM), jana kilifanya uzinduzi wa semina kwa wabunge wake yenye lengo la kuwakumbusha majukumu yao, hasa wanapokuwa bungeni na wajibu wao kwa taifa na chama.
  Semina hiyo ya wabunge wa CCM iliyofanyika katika ukumbi wa Ubungo Plaza, jijini Dar es Salaam, ilifunguliwa na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, ambaye alikemea kauli za wabunge katika ukosoaji wa serikali na chama.
  Kwa mujibu wa Pinda, ni kwamba kauli wanazotoa wabunge wa CCM zimekuwa zikijenga taswira mbaya kwa chama na kukipa wakati mgumu kwa wananchi.
  Tunaamini kuwa mafunzo kwa taasisi, chama au idara yoyote ni jambo muhimu sana kwa mustakabali wa taifa na sekta husika, lakini mafunzo hayo yasiwe ya kuwaziba midomo.
  Kwa hali ilivyo hivi sasa, si jambo la busara kwa chama kuandaa mazingira ya kuwaziba midomo wabunge wao wasiweze kukemea kile wanachokiona hakiendi sawa.
  Tukiendeleza utaratibu wa namna hiyo tutajenga taifa la watendaji na wanasiasa waoga ambao watakosa kujiamini na matokeo yake taifa halitapiga hatua kwenye maendeleo.
  Hakuna asiyejua kuwa mbunge anapokuwa huru mijadala bungeni huwa moto na watendaji wa serikali huwa makini katika shughuli zao za kila siku.
  Katika Bunge la tisa tuliweza kujua ubadhirifu mkubwa uliofanywa na wabunge, watendaji wa serikali na raia ambao wengine walifikishwa mahakamani na kesi zao zinaendelea.
  Kilichofanya maovu mengi ya serikali, wabunge yajulikane ni kwa sababu ya wabunge kutominywa katika utoaji wa maoni.
  Tungependa uhuru uendelee bila vyama kuwafunga makufuli wabunge kuzungumzia masuala yanayowakera hata kama yanagusa masilahi ya chama chao.
  Tabia ya kulindana kwa kivuli cha chama ni mbaya na ndicho kilichochangia ubadhirifu katika wizara, idara na mashirika ya umma.
  Hatuoni sababu ya wabunge kupigwa msasa wa kulinda masilahi ya chama badala ya kuambiwa masilahi ya taifa ndiyo yawe ya kwanza.
  Umaskini unazidi kushamiri siku hadi siku hapa nchini kutokana na rasilimali za taifa kutotumika ipasavyo, ambapo wajanja wachache kwa kushirikiana na watendaji wa serikali ndio wananufaika.
  Limekuwa jambo la kawaida hivi sasa kwa wanasiasa (wabunge) kushiriki katika vitendo vya utafunaji wa rasilimali za taifa huku wananchi wakiendelea kudhoofu kwa sababu ya ugumu wa maisha.
  Tunawaomba wabunge wasikubali kuzibwa midomo na vyama vyao katika kufichua maovu, kwani kwa kufanya hivyo watakuwa wanawasaliti wananchi waliowachagua, pia ni kuendelea kulea uovu,
   
 3. Rutashubanyuma

  Rutashubanyuma JF-Expert Member

  #3
  Jan 23, 2011
  Joined: Sep 24, 2010
  Messages: 158,305
  Likes Received: 417,643
  Trophy Points: 280
  Safari hii tunataka kufahamu hawa wabunge wa CCM waajiri wao ni akina nani? CCM au wapigakura kwenye majimbo wanayotoka...........
   
Loading...