Waalimu wetu na majina ya kejeli

vukani

JF-Expert Member
Dec 30, 2009
245
165



Katika kusoma kwangu nimebahatika kusoma katika shule mbalimbali zikiwamo za hapa Jijini Dar na za mikoani.


Nimegundua kuwa sekta ya ualimu ndiyo inayoongioza kwa waalimu kupewa majina ya utani na wanafunzi, na majina hayo yanaweza kuwa ni kutokana na tabia ya mwalimu, aina ya mavazi anayopenda kuvaa, kauli zake za mara kwa mara, matamshi na hata vituko anavyofanya, maana unaweza kukuta mwalimu ana vituko kama The Comedy.

Binafsi nakumbuka kuna mwalimu tulikuwa tunamwita darubini, huyu alikuwa ana macho makali, kwa mfano unaweza kuwa kwenye chimbo (Chimbo ni eneo la kujificha) na kama akipita eneo hilo ukawahi kukimbia, utashangaa siku ya pili mkiwa kwenye gwaride akikuita kwa jina kuwa upite mbele, na hapo ni lazima upate bakora.

Kingine ni pale ambao umejificha mahali, halafu ukawa unachungulia kwenye kona ya ukuta, akiona jicho tu utashangaa akikuita kwa jina na hapo pia utachezea bakora, alikuwa na kipaji cha kukariri majina na sura za wanafunzi wake, huyu alikuwa ni mwalimu wa nidhamu na mara nyingi waalimu wa nidhamu ndio wanaokutana na adha hii ya kupewa majina ya ajabu.

Mwalimu mwingine tulikuwa tunamuita Pindipo. Huyu alipenda sana kutumia neno la ‘Pindipo utakapobainika’ pale ambapo anatahadharisha juu ya jambo fulani. Kama kawaida wanafunzi wakampachika jina la Pindipo.

Mwalimu mwingine ninayemkumbuka tulikuwa tunamwita ‘Kala nini’ huyu naye kama umefanya makosa na amekasirika sana, alikuwa akipenda kusema ‘binti reo utaniereza nimekura nini usiku wa jana’ huyu alikuwa anatokea kule kwa akina Chacha Wambura. Na ndipo wanafunzi wakamwita Mwalimu Kala nini.

Huko Sekondari napo nikakutana na vituko hivyo, kuna mwalimu wetu wa Biology tulikuwa tunamwita mwalimu Mandible, Mandible ni zile antenna za Panzi, sasa yeye alikuwa akipenda kulitamka hilo neno mpaka tukamwita hilo jina la mwalimu Mandible.

Mwalimu mwingine alikuwa ni mwalimu wa Kiswahili huyu tulimwita jina la Ngoswe, kama mnakumbuka kile kitabu cha Ngoswe, Penzi kitovu cha uzembe.

Mwalimu mwingine alikuwa akiitwa ‘However,’ huyu, hawezi kusema maneno matatu ya kiingereza bila kutamka hili neno la However, na hapo wanafunzi wakampa jina la However.

Kwa kweli ni majina mengi mno na kama nikisema niyataje hapa, basi nitawachosha, ngoja niwaachie na wasomaji wengine watoe kumbukumbu zao.

 
Back
Top Bottom