Tarehe 25 Machi 2013, baada ya Rais Xi Jinping kuchukua wadhifa wa Urais wa China, alitembelea Afrika kwa mara ya kwanza. Alipohutubia katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Mwl. Nyerere nchini Tanzania, alitoa mara ya kwanza wazo la sera ya China kwa Afrika ya “Ukweli, Matokeo Halisi, Ukaribu na Udhati” pamoja na dhana ya “Maadili Sahihi na Faida Sahihi”. Kwa miaka kumi na mitatu iliyopita, wazo hili limeendelea kutekelezeka hatua kwa hatua katika ushirikiano wa China na Afrika, na pia limeacha alama halisi katika bara la Afrika.
Nchini Ethiopia, wafanyakazi wanatumia kwa ufasaha mashine kwenye viwanda vilivyowekezwa na makampuni ya China; nchini Kenya, wafanyabiashara wadogo kando ya reli ya Mombasa-Nairobi wamepanua biashara zao kutokana na ufanisi wa usafirishaji; nchini Nigeria, miradi ya nishati haileti umeme tu bali pia inawawezesha wataalamu wa huko kupata uzoefu. Kwa makampuni na watu wa Afrika, ushirikiano wa China na Afrika haujatoa pesa tu, bali pia unaleta teknolojia na maarifa.
Kuanzia Mei Mosi mwaka huu, China itatekeleza sera ya ushuru sifuri kwa bidhaa zote za Afrika. Hii inafanya biashara ya Afrika kuelekea China kuwa rahisi zaidi na yenye gharama ndogo, na sera hii tayari inaanza kubadilika kuwa fursa halisi za biashara. Katika mkutano ulioandaliwa hivi karibuni na Studio ya Utengenezaji Vipindi ya Shirika Kuu la Utangazaji la China CMG mjini Nairobi, mtaalamu wa uchumi wa Kenya, James Shikwati, alisema wazi kwamba sera ya ushuru sifuri sio tu inarahisisha biashara, bali pia inaweza kuwa fursa ya mabadiliko ya muundo wa uchumi wa Afrika — kuruhusu nchi nyingi kuhama kutoka kuuza malighafi kwenda katika utengenezaji na maendeleo ya viwanda. Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Nairobi, Lemmy Mulaku, alibainisha kuwa kwa kuzingatia kuongezeka kwa vitendo vya kujilinda kibiashara duniani na kupanda kwa utaifa wa kiuchumi, sera hii ni ya thamani kubwa. Pia alikumbusha kuwa nchi za Afrika zinapaswa kuimarisha ushirikiano wa mnyororo wa thamani wa kikanda na ushirikiano wa mnyororo wa usambazaji wa mipaka, ili faida ya sera isambae kwa wingi ndani ya Afrika.
Kwa kupitia miaka kumi na mitatu iliyopita, tangu kanuni ya “Ukweli, Matokeo Halisi, Ukaribu na Udhati” ilipotolewa, ushirikiano wa China na Afrika umeendelea kuunda hali ambapo dhana inaongoza na utekelezaji unaibua dhana. China katika ushirikiano wake na Afrika imeweka msisitizo zaidi kwenye usawa na manufaa ya pamoja, jambo linalozipa nchi za Afrika nafasi kubwa ya kujitegemea. Mwaka huu, viongozi wa nchi kadhaa za Afrika wanatarajiwa kutembelea China, na mawasiliano ya ngazi ya juu yanasukuma uhusiano wa kimkakati wa siku zote kwenda kwenye hatua ya kina na thabiti.
Kuna methali ya China inayosema: “Wale wanaopendana na kuwa na lengo moja, milima na bahari si vikwazo.” Kwa kuangalia mbele, ushirikiano wa China na Afrika utakuwa na mkazo zaidi katika viwanda, biashara, uwekezaji na mawasiliano kati ya watu. Kwa watu wa kawaida wa Afrika, maana ya ushirikiano huu inaweza kuwemo katika reli inayotumika, ajira thabiti, au mlango mpana zaidi wa soko la China unaofunguka.