Vyama kuwa na kukosa sera

Jatropha

JF-Expert Member
Apr 9, 2009
1,151
199
WIZARA YA ARDHI INAWAFANYA WANYONGE KUWA MASKINI ZAIDI.

Mwaka 2009 umewadia, na hivi karibuni tutaanza kusikia tambo za wanansiasa mbali mbali wakijinadi kwa wananchi ili waweze kupigiwa kura katika chaguzi zijazo za serikali za Mitaa na hatimaye uchaguzi mkuu mwakani.

Moja ya silaha za wanasiasa katika kipindi hiki ni Sera za vyama vyao ambazo wamezibuni ili kuwaletea wananchi maendeleo; na ndizo ambazo watakuwa wakizinadi ili kupata ridhaa ya wananchi katika maeneo husika kuongoza ili watekeleza sera walizozinadi na hatimaye wananchi wapate maendeleo. Kama wananchi watapata maendeleo au la, hilo hubaki kitendawili.

Ni katika kipindi hiki ambacho utasikia wanasiasa wa kambi moja wakiwaambia wenzao wa kambi ingine kuwa hawana Sera. Ni kauli hizi ndio zimenifanya nijiulize kunatofauti gani kati ya wanansiasa wasiokuwa na sera na wale wenye sera laikini wakishachaguliwa na kushika hatamu za uongozi hawatekelezi sera walizozinadi kwa wananchi?

Sera ya Uwezeshaji wa Wananchi Kiuchumi ilitolewa na Ofisi ya waziri Mkuu mwaka 2004. katika suala la Ardhi Sera hiyo inatamka bayana kuwa “Serikali itatumia ardhi kama njia ya kuwawezesha wananchi wake kushiriki kikamilifu kiuchumi. Lengo ni kusaidia wananchi watumie ardhi waliyo nayo ama kwa kujipatia hisa katika shughuli za uwekezaji huo au pato lenye kuwanufaisha kushiriki kikamilifu jkatika shughuli zingine za kiuchumi”. Mkakati wa utekelezaji wa tamko hilo ibara ya 4.9.3.(ii), “Kutoa ardhi kwa wawekezaji wakubwa kwa shughuli mbali mbali za kiuchumi.Pale ambapo itabidi Wananchi wahamishwe ili kuwapisha wawekezaji wakubwa. Serikali itawasidia utaalamu wa kuingia katika makubaliano muafaka na wawekezaji kwa nia ya kuwanufaisha”.

Sera ya Uwezeshaji wa Wananchi Kiuchumi ilitolewa na Ofisi ya Waziri Mkuu mwaka 2004 ni moja mihimili iliyotumika kutunga Ilani ya uchaguzi ya CCM ya mwaka 2005; mathalani katika Ibara ya 48 ya Ilani ya CCM ya 2005 inatamka kuwa “utekelezaji wa dhati wa Sera ya Uwezeshaji wa Wananchi Kiuchumi itatuepusha na balaa la kuwa na jamii ambayo ina matajiri wachache walionacho na wananchi wengi wasio nacho”.

Katika miaka ya hivi karibuni limekuwepo ongezeko kubwa la migogoro ya ardhi kati ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi na wananchi. Wananchi wakipinga viwango vidogo vya fidia wanayolipwa ili kupisha miradi mbali mbali ya maendeleo inayopendekezwa na Wizara ya Ardhi. Kibaya zaidi Wizara ya Ardhi inatumia kutokuelewa kwa wananchi kuhusu thamani halisi ya ardhi na nyumba zao kukiuka kwa makusudi Sheria za Ardhi namba 4 & 5 za mwaka 1999 zinazotamka bayana kuwa “fidia itakuwa ni kwa bei ya soko”; na pia zinaelekeza utaratibu wa kufikia bei ya soko “kuwa itakuwa ni kwa kulinganisha na mauzo ya hivi karibuni ya ardhi au nyumba katika eneo husika”.

Madhumuni ya Wizara ya Ardhi kukiuka Sheria za Ardhi ni kujipatia faida kubwa ya zaidi ya 1000% (asilimia 1000) kwa kuuza ardhi ilizozipoka kutoka mikononi mwa wananchi wanyonge, ilihali wananchi wanaohamishwa kwa malipo ya fidia hafifu wakishindwa kujirejeshea viwango vya makazi na maisha waliyokuwa nayo awali kabla ya kuhamishwa kwao. Wengi wao hushindwa kujijengea nyumba bora kama walizokuwa nazo, kujirejeshea huduma za umeme, maji, barabara, ajira n.k na hivyo kurudisha nyuma jitihada za kufikia malengo ya milenia.

Tuchukue mfano wa mradi wa mji wa mfano wa Luguruni ulioanza kutekelezwa na Wizara ya Ardhi Januari mwaka 2007. Tokea mwaka 2005 viwanja katika eneo la Kata ya Kibamba vilikuwa vikiuzwa kwa bei ya Shs Milioni 6 (6,000,000/=) kwa kiwanja cha Mita 20 X 20. Kiwanja cha Mita 20 X 20 kina Mita mraba 20 X 20= 400. Ukikokotoa utagundua kuwa ardhi katika Kata ya Kibamba inauzwa kwa bei ya Shs 15,000/= kwa Mita 1 Mraba tokea mwaka 2005. Cha kushangaza Wizara ya Ardhi na pasipo utu wala ubinadamu Mwezi Desemba 2007 iliwalipa fidia wakazi 259 wa eneo la Luguruni walitakiwa kuhama kupisha mradi huo Shs 300 tu kwa Mita 1 Mraba; sawa na Shs 120,000/= kwa kiwanja cha Mita 20 X 20. Iliwabidi wananchi walioathriwa na mradi huo kuikaba koo Wizara ya Ardhi ndipo wakalazimika ikapandisha kiwango hicho kufikia Shs 1977/= tu kwa Mita 1 Mraba, sawa na fidia ya Shs 790,800/= kwa kiwanja cha Mita 20 X 20.

Kwa upande wa fidia za nyumba, awali fidia zilipwa kwa kiwango cha kati ya Shs 100,000/= na 150.000/= na baadye kupandishwa kufikia 250,000/= kwa Mita 1 Mraba ya nyumba. Kwa mujibu wa wakandarasi wa majengo bei halisi ili nyumba iweze kukamilika kikamilifu ikiwa na huduma zote muhimu ikiwemo umeme, maji, barabara n.k. ni katia ya Shs 500,000/= hadi 650,000/= kwa Mita 1 Mraba ya jengo kulingana na hadhi ya jengo husika. Ndugu msomaji utabaini kuwa kutokana na mchakato wa fidia kutokuwa shirikishi wafidiwa wa Luguruni walipunjwa kati ya Shs 250.000/= hadi 400,000/= kwa Mita 1 Mraba ya jengo. Tukikumbuka kuwa pia waathrika hawa walilazimika kuchota fidia za nyumba ili kumudu kununue viwanja mbadala kwa ajili ya ujenzi wa nyumba mpya kwa bei ya Shs Milioni 6 hadi 8, ni wazi kuwa wengi walishindwa kujirejeshea viwango vya makazi kama waliyo kuwa nayo hapo awali.

Mara tu baada ya kukamilisha kuwahamisha wananchi kutoka eneo hilo, Wizara ya Ardhi ilitangaza tenda kuuza mapori hayo (pasipo uendelezaji wowote). Nyaraka za tenda zinagharimu Shs 300,000/= na bei ya Mita 1 Mraba ni Shs 30,000/=. Mnunuzi yoyote anayetuma ombi chini ya kiwango hicho hukataliwa kwa kutofikia bei iliyopangwa. Kutokana na bei hiyo, Wizara ya Ardhi inauza kiwanja 20 X 20 chenye Mita Mraba 400 kwa Shs Milioni 12, ilihali yenyewe ilimfidia mwananchi Shs 790,800/= tu; na hivyo kujipatia faida ya asilimia 1500 (1500%).

Katika hali inayothibitisha kuwa maadili ya kitaifa yameporomoka kwa kiwango cha kutisha sana. Taasisi ya Serikali inabuni mpango wa kujipatia faida kubwa sana kiasi hicho kwa kuwanyonya wananchi kwa kukiuka sheria zilizopo kwa makusudi. Katika lengo hili hilo la kujipatia faida kubwa zaidi Wizara ya Ardhi imewavamia wananchi wa eneo la Kwembe walioko jirani na kituo cha mji wa wa Luguruni na kupima viwanja vidogo vidogo ndani ya ua wa makazi yao. Makaro ya maji machafu, matanki ya maji, nyumba za watumishi, mabanda n.k vimemegwa na kuingizwa katika viwanja vipya vilivyotengenezwa kwa ajili ya kuuzwa pasipo kujali hawa binadamu wataishi vipi kuanzia sasa. Wakazi waliokuwa wakipakana na barabara ardhi zao zimemegwa kwa mbele kutengeneza viwanja vya kibiashara kwa ajili ya kuuzwa kwa faida kubwa. Haki za kibanadamu wala utu havijaliwi kabisa, kinachozingatiwa ni idadi ya viwanja vinavyoweza kuzalishwa ili Wizara ya Ardhi iweze kutengeneza fedha zaidi kutokana na mauzo ya viwanja hivyo.

Wakati haya yakitendwa na taasisi ya kiserikali, Sera za uwezeshaji wananchi kiuchumi kwa kutumia ardhi zilizonadiwa kwa wananchi mwaka 2005 ziko wapi? Je wanaopaswa kutekeleza sera hizi wako wapi? Hawaoni yanayotendeka; tena wengine ni viongozi waandamizi katika chama tawala. Ni nini kinwafanya wakae kimya kuhusu hali hii ya kinyonyaji? Wanaopaswa kusimamia utekelezaji wa sera hizi wako wapi? Ina maana hawasikii malalamiko ya wananchi katika maeneo yao na katika vyombo vya habari? Kama huu ndio mwendo wenyewe ni afadhali ya kukosa sera kuliko kuwa na sera za kuwadanganyia wananchi na kisha kushindwa kuzitekeleza.
 
Jatropha

Nakubaliana kwa sehemu ya maelezo yako. Ni kweli kuna tatizo na kisera kwa maana ya sera za CCM za ardhi na mipango miji lakini pia kuna tatizo la kiuongozi/kiutendaji ambalo linachangiwa kwa kiasi kikubwa linachangiwa na ufisadi. Yote haya yanashindwa kushughulikiwa kikamilifu pale wananchi wanapokuwa hawafahamu haki zao. Nimezungumzia hayo katika hii makala yangu hapa: https://www.jamiiforums.com/jukwaa-...-maendeleo-ya-mgeni-njoo-mwenyeji-akonde.html

Hata hivyo, kichwa cha habari ambacho umechagua cha 'vyama vya siasa kukosa sera' ni kipata mno. Walau ungechagua kichwa kama hicho ulichoanzia uchambuzi wako cha Wizara ya ardhi dhidi ya wanyonge ama ungeweka kichwa cha kutufanya tulijadili suala la kwembe moja kwa moja. Nashukuru pia umetuletea picha zinazoonyesha hali ilivyo.


JJ
 
Ni kweli kuwa kicha cha habari ni kipana sana na huwezi kupinga ukweli kwamba watanzania tulio wengi, suala la sera ni geni sana kwetu na hata unapoangalia wakati wa uchaguzi, watu 'wapiga kura' hawachagui sera.

Tunapiga kura tu kwa mazoea na kwa kuwa wengi tuna ugonjwa wa dominant party basi tunadhani vyama vingine havina sera.

ukiangalia kwa umakini utagundua kuwa sera nyingi zilizotangazwa na ccm wakati wa uchaguzi, hazitekelezeki na kwa vile uchaguzi unakaribia basi tunaona jinsi wizara zinaavyokimbizana magazetini kuelezea kufanikiwa kwa sera.

Chukulia kwa mfano, ahadi ya kutoa ajira, hii ipo kwenye ilani na sera ya ccm, leo hii tunaambiwa ajira ambazo hazina 'usalama' eti nazo ni mafanikio ya ccm. Bado ardhi imekuwa si kitu sana cha kumsaidia mwananchi wa hali ya chini.

Wananchi wanaporwa ardhi kadri 'wakubwa' wanavyopenda.

Nadhani ni wakati wa vyama vya siasa na hasa vya upinzani kuwa na lengo, la muda mfupi, kuhakikisha kuwa umma wa watz unaelewa unawajibu gani kwa taifa

MABUBUBU TUMESEMESHWA, TUJIBU KWA VITENDO
 
0 Reactions
Reply
Back
Top Bottom