Vuvuzela ma simba wa ajabu

Vuvuzela ma simba wa ajabu

DUMIZI

Member
Joined
Apr 23, 2019
Posts
16
Reaction score
13
Mzee Vuvuzela alikuwa maarufu sana kwa tabiri zake. Alikuwa kama kenge aliyebarikiwa uwezo wa kunusa hatari kabla haijamfikia.

Aliwahi kutabiri kwa usahihi kuhusu uvamizi wa nzige, na akatoa mbinu madhubuti za kuwadhibiti. Watu walifuata ushauri wake, wakapuliza unga wa majivu, wakapanda mazao mbadala—na kweli, mashamba yao yaliokolewa.

Miezi michache baadaye, alitabiri mlipuko wa ugonjwa wa mapafu. Na kweli, watu wakaanza kukohoa kana kwamba mapafu yao yalikuwa yakiliwa na bacteria wa kigaidi. Kijiji kikamtegemea, kikamheshimu na kumwona kama shujaa wao.

Lakini alipotabiri kuhusu ujio wa mafuriko makubwa, na kuwaasa watu waache kulima mpunga kwenye makonde yao, utabiri haukutimia. Watu wakaanza kumpuuza na kumdharau. “Ni mzushi tu huyu.”

Usiku mmoja, Vuvuzela aliamka kwa mshituko. Alikuwa na maono ya moto wa ajabu unaoteketeza kijiji kizima. Akapiga mayowe ya tahadhari, watu wakaamka na kujiandaa.
"Jamani! Kuna moto mkubwa unakuja kuangamiza kijiji chetu!"

Moto haukutokea. Zilikuwa ndoto zake tu. Kuanzia hapo, heshima yake ikayeyuka kama barafu kwenye kikaango cha moto. Watu wakaanza kumchukia. Simulizi zake zikawa mzaha. Aligeuzwa kichekesho kwenye vikao vya jioni.

Lakini siku zilivyopita, zikaibuka tetesi nzito kuhusu Simba wala watu. Simba hawa walishambulia wachungaji na wakulima mchana kweupe. Taarifa zilienea, lakini watu wakaendelea na maisha yao.

Siku moja, kijiji kikiwa kwenye tamasha la ngoma kama kawaida yao, ghafla Vuvuzela alijitokeza kwa haraka, akitokwa jasho na kutweta kwa nguvu.

"Simba jamani! Simba wanakuja kutuangamiza. Andaeni kamba zenye ulimbo tuwadhibiti!"

Badala ya kumuunga mkono, wanakijiji walianza kucheka.

"Ana wazimu huyu! Nani asiyejua kuhusu simba? Unataka kutuambia habari tulizonazo tayari? Ili uonekane shujaa? Mbona hukuwahi kuonesha ushujaa wako zamani? Kwanini leo?"

Walimshambulia kwa maneno makali. Wengine walimtuhumu kwa kutaka sifa za bure, eti anatafuta huruma ya jamii. Alionekana kama mtu anayetamani kurudisha heshima yake iliyopotea kupitia ujio wa simba wala watu.

Dakika chache baadaye, Vuvuzela alipokea simu ya mama Ngedere. Mama huyo alikuwa akilia kwa uchungu.

“Wamenishambulia! Wamemrarua na kumla mtoto wangu mbele ya macho yangu… simba… simba jamani!”

Mzee Vuvuzela akaiwasilisha taarifa hiyo kwa wanakijiji. Lakini badala ya kuchukua hatua, walizidi kumzomea.

“Mbona hukusema mapema? Simba hawa si wageni. Hata sisi tumewahi kupoteza watoto wetu walioliwa na simba hawa hawa. Unaigiza tu, ili tukupe uenyekiti wa kijiji.”

Ghafla, ngurumo za simba zikasikika. Simba wenye njaa na kisirani walikuwa wakiwasogelea kwa kasi. Vuvuzela alichukua kamba zake zenye ulimbo, akawahimiza wanakijiji:

“Jamani wakati ndo huu! Tuwazingire na kuwaingiza mtegoni! Tuwe kitu kimoja!”

Lakini walimpuuza. Wakamzomea kwa nguvu zaidi, wakisema:

“Unajitafutia sifa tu! Unawajua Simba vizuri wewe? Wewe ni mwenezi wa hofu tu, una ajenda zako!”

Wakati huo, simba walikuwa tayari wamewazunguka wanakijiji. Mzee Vuvuzela akasogea mbele peke yake, akikabiliana nao. Alijaribu kupambana kwa mbinu zile zile ambazo zingesaidia wote, kama wangemsikiliza.

Wanakijiji walimkodolea macho kwa mbali, wakiwa wamejificha. Wengine walicheka kimyakimya, huku wakisubiri kwa shauku aangamizwe, ili waseme:

“Kiko wapi?!”

Je, Vuvuzela atanusurika dhidi ya Simba wenye nguvu?

Baada ya kuliwa na Simba, wanakijiji watabaki salama?

Usikose kufuatilia toleo lijalo....
 

Attachments

  • Screenshot_20250603-015810.jpg
    Screenshot_20250603-015810.jpg
    873 KB · Views: 14
Back
Top Bottom