Vombo vya habari viache kupotosha wapiga kura | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Vombo vya habari viache kupotosha wapiga kura

Discussion in 'Uchaguzi Tanzania' started by Dabomani, Sep 25, 2010.

 1. D

  Dabomani Member

  #1
  Sep 25, 2010
  Joined: Sep 25, 2010
  Messages: 18
  Likes Received: 0
  Trophy Points: 0
  Kiasi cha miaka kumi na tano iliyopita niliwahi kuona filamu moja inayoitwa 'THE PANAMA DECEPTION', yaani 'UDANGANYIFU WA PANAMA', kwa tafsiri isiyo rasmi. Filamu hii haikuwa ya kuigiza; ilikuwa ni muunganisho wa picha mbalimbali za televisheni zilizopigwa wakati wa operesheni ya uvamizi wa majeshi ya Marekani nchini Panama, mnamo tarehe 20 Desemba 1989. Uvamizi huo uliohusisha kiasi cha askari 27,000 wa Kimarekani waliosindikizwa na kundi kubwa la Helikopta za kivita aina ya Apache AH-64 ilipewa jina la ' OPERATION JUST CAUSE'.
  Jina hili lilimaanisha kuwa uvamizi huo ulikuwa ni 'KWA AJILI YA KUTETEA HAKI' ya wananchi wa Panama, ambao kwa mujibu wa maelezo ya rais wa Marekani wa wakati huo, George W. Bush Sr., 'waliokuwa chini ya ukandamizaji mbaya sana wa Dikteta Manuel Noriega'.
  Katika filamu hiyo yanaonekana matukio mengi ya kinyama na ya kutisha. Wanajeshi wa Kimarekani waliuwa raia wengi na kufanya uharibifu mkubwa, ikiwa ni pamoja na kuchoma moto kwa makusudi makazi ya watu wa kawaida kwenye vitongoji vingi vya jiji la Panama. Kitongoji cha El Chorillo hadi leo kinaitwa 'Hiroshima ndogo' kwa jina la utani kutokana na ukweli kwamba makazi yote ya wananchi katika uvamizi huo yalichomwa moto na wakaazi wengi wa eneo hilo kupoteza maisha.
  Ufukuaji wa maeneo mengi ya makaburi ya pamoja uliofanywa baada ya kukamilika kwa operesheni hiyo ulionesha kuwa watu wengi waliozikwa katika makaburi hayo walikuwa ni wahanga wa mauaji ya makusudi. Mabaki ya maiti nyingi yalionyesha kuwa waliozikwa humo hawakuwa wapiganaji.
  Maiti nyingi zikiwemo za watoto wengi wadogo wenye umri chini ya miaka mitano zilionyesha kuwa wahanga hao waliuwawa kwa kupigwa risasi kichogoni na huku wakiwa wamefungwa mikono kwa nyuma kwa kutumia nyaya za chuma!
  Jambo la kushangaza ni kwamba vyombo vya habari vya Marekani na Ulaya, ikiwa ni pamoja na TV na magazeti, vilichagua kwa makusudi kutotangaza kwa uhalisia kile kilichokuwa kinaendelea nchini Panama. Taarifa zilizoletwa na waandishi wa vyombo hivyo waliokuwa nchini Panama wakati wa tukio 'zilikaliwa' na mahala pake kukarushwa na kuandikwa habari zilizokuwa zinahalalisha uvamizi huo wa majeshi ya Marekani. Mfano wa habari hizo ni ile iliyotangazwa na televisheni za Marekani kwa mapana na marefu zikimnukuu rais Bush:
  '….and now freedom and democracy have been restored in Panama….', yaani '…na sasa uhuru na democrasia vimerejeshwa Panama….'.
  Bush alitoa kauli hii akilihutubia Taifa lake kufuatia mafanikio ya majeshi yake katika kulisambaratisha jeshi dogo la Panama lililokuwa na askari wasiozidi 3,000, kumkamata aliyekuwa rais wa nchi hiyo Manuel Noriega, na kumsimika kibaraka wao, Guillermo Endara, kama rais mpya.
  Filamu ya 'The Panama Deception' ilibuniwa na wale waandishi ambao taarifa zao halisi walizotuma kwenye vyombo vyao vya habari zilikaliwa, ikiwa ni jitihada zao za kujaribu kuufikisha ukweli kwa ulimwengu.
  Kazi kibwa ya vyombo vya habari ni kuhabarisha. Katika kufanya kazi hii chombo cha habari kinatakiwa kifanye kila jitihada kuhakikisha kuwa habari kinazotangaza ni kama zilivyotokea. Wadau wa vyombo vya habari, hususan watendaji wake na wamiliki wa vyombo hivyo wanapaswa kufanya kila linalowezekana kuhakikisha kuwa imani na hisia zao binafsi haziwi ni sehemu ya habari inayotakiwa kufikishwa.
  Kwa bahati mbaya sana hali halisi haiko hivyo. Wamiliki wengi wa vyombo vya habari duniani kote wameanzisha vyombo hivyo kama zana za kufinyangia akili za watu kwa nia ya kupelekea mbele agenda zao binafsi ambazo zimejificha katika nyoyo zao. Kwa bahati mbaya zaidi ni kwamba hata pale ambapo wamiliki wa vyombo husika wamenusurika na kusudio hilo, ni mara chache sana kwa wale waliokabidhiwa kuviendesha, yaani wahariri na waandishi, kunusurika.
  Mfano tulioutanguliza hapo juu wa filamu ya 'The Panama Deception' ni moja tu ya vielelezo vya hali hii. Ulaya na Marekani ni maeneo ya dunia ambayo watawala wake tangu karne na karne wanaamini kuwa wazungu wametukuka kuliko watu wengine wote na kwa maana hiyo wana haki ya kuwatawala, kuwaibia na kuwafanyia ubaya wowote kwa ajili ya maslahi yao na nchi zao; na iwapo hili litashindikana kwa njia ya udanganyifu, basi litawezeshwa kwa matumizi ya nguvu za kijeshi. Hii pia ndiyo falsafa inayofuatwa na vyombo vya habari vya mataifa hayo. Anayetaka kubisha kwamba hivi sivyo na tumuulize: Hivi ni kwa nini Waafrika kila mara wanalalamika kwamba vyombo vya habari vya nchi za Ulaya na Marekani vinaandika, kutangaza na kuonesha habari mbaya tu kuhusu Afrika?
  Kwa bahati mbaya sana Waafrika wengi, wakiwemo na Watanzania pia, tunaingia katika mkumbo wa kuvipa sifa mbaya vyombo vya habari vya nchi za Ulaya na Marekani, bila kufanya uchunguzi wa kina wa mwenendo wa vyombo vyetu wenyewe vya habari. Mwenendo wa vyombo vya habari vya hapa nchini Tanzania, bila kujali kama ni vya umma au ni vya binafsi, ni mfano halisi wa vyombo vinavyotumiwa vibaya kwa ajili ya kuendeleza agenda binafsi za wamiliki au watendaji wake.
  Kwa Tanzania, agenda hizi zimejikita zaidi katika maslahi ya kidini na kisiasa. Kwa mfano, wakati rais mstaafu wa Malawi, Bakili Muluzi, akiwa madarakani kila alipotajwa na vyombo hivi, bila kujali kwamba habari hiyo ilikuwa inahusu nini ilikuwa ni aghalabu kusikia:
  '….ambaye ni Muislamu…'.
  Ni kweli Bakili Muluzi alikuwa ni Muislamu, lakini uislamu wake ulikuwa unahusikaje na suala lililokuwa linaelezewa na habari hiyo?
  Mbona vyombo hivyo hivyo vilipokuwa vikimtaja, kwa mfano Fredrick Chiluba, rais mstaafu wa Zambia, hatukuwa tukisikia kiambatisho:
  '….ambaye ni mkristo mlokole….'?
  Wala hatukuwahi kusikia wakina Chisano, Dos Santos, nakadhalika wakitajwa na huku wakiambatanishiwa na imani zao za dini?!
  Kuna mifano mingi mno inayodhihirisha ni kiasi gani vyombo vyetu vya habari vinahangaika kutumika kama chombo cha kubebea maslahi ya ukristo dhidi ya yale ya uislamu na imani nyingine zilizopo kwenye Taifa hili. Hili lisingekuwa ni tatizo kubwa sana, kama jitihada hizi zingekuwa hazigusi ulingo wa siasa. Kwa bahati mbaya sana siasa inatumika kama ndiyo mbeleko ya kuyabebea hayo maslahi.
  Kwa mfano: Japokuwa kuna ushahidi mwingi sana na wa wazi unaoonyesha kuwa serikali ya CCM, na kabla ya hapo ile ya TANU, imekuwa ikitumika sana kusimamia na kuendeleza maslahi ya ukristo dhidi ya yale ya dini nyingine, vyombo vyetu vya habari vimechagua kukaa kimya. Hata hivyo vyombo hivi ni hodari sana wa kupiga kelele zinazohusu 'udini' pale kunapokuwa na tukio au jambo lolote linaloashiria kuwa uislamu au Waislamu watanufaika. Hakuna hata haja ya kutoa mifano kwa sababu ni mingi mno, na iko wazi kabisa.
  Wakati tukiwa kwenye mchakato wa kampeni za uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba ya mwaka huu 2010, hali hii ya mwenendo mbovu wa vyombo vyetu vya habari imeendelea kujitokeza na safari hii, kwa wale tunaojua 'kusoma katikati ya mistari', bila hata kificho.
  Kwa kuzingatia matokeo ya chaguzi za nyuma, matokeo ya uchaguzi wa serikali za mitaa uliofanyika mwaka 2009, na kuenea kwa mtandao wa chama kitaifa, kampeni hizi zinaonekana kutawaliwa na vyama vitatu vya CCM, CUF na CHADEMA. Tayari vyombo vingi vya habari kupitia maudhui ya taarifa wanazotoa, picha na hata mpangilio wa taarifa hizo, wameshawaamulia wapiga kura kuwa ni mgombea gani wa nafasi ya urais na kutoka chama gani anatakiwa ashinde!
  Kati ya wagombea watatu wa nafasi ya urais waliosimamishwa na vyama hivi uchambuzi wa taarifa za vyombo vya habari unaonesha wazi kuwa kuna hekaheka nyingi na za kila siku za kumtukuza na kumpamba mgombea wa CHADEMA, Dr. Wilbroad Slaa; huku pia kukiwa na juhudi kubwa za kufukia madhaifu yake na ya chama chake. Jitihada hizo pia zimejikita katika kutilia mkazo udhaifu wa wagombea wenzake na kufukia sifa zao.
  Ni vigumu kusema kwa uhakika Dr. Slaa ana sifa gani zinazompelekea apigiwe debe kiasi hicho na vyombo vya habari. Yote anayoyazungumza hivi sasa kuhusu KATIBA, ELIMU, AFYA, MAKAAZI, KUDHIBITI MATUMIZI YA UMMA, KUWA NA SERIKALI NDOGO nakadhalika, na kuonekana kuwa ndiyo yaliyobeba kampeni yake na ya chama chake wala siyo 'original'. Sehemu kubwa ya hayo ameigiza kutoka katika ilani za CUF za mwaka 2000 na mwaka 2005.
  Kwa bahati nzuri CUF mwaka 2005 waliichapisha ilani yao yote katika mfumo wa gazeti na kuisambaza nchi nzima. Wale wote waliobahatika kuhifadhi nakala za ilani ile wanaweza wakaipitia tena kujiridhisha kuwa haya ninayoyasema siizushii CHADEMA. Naamini kuwa vyombo vya habari jambo hili wanalitambua japokuwa hawataki kusema ukweli. Aidha, huwezi ukahalalisha 'promosheni' hii ya vyombo vya habari kwa kisingizio kuwa CHADEMA ni chama makini!
  Hivi unawezeje kukiita makini chama ambacho kinaweka mgombea mwenza mwenye elimu ya darasa la saba? Hivi ikitokea bahati mbaya rais akafariki kabla ya kumaliza muda wake, kweli sisi kama Taifa tuko tayari kumkabidhi uongozi mtu wa elimu ya darasa la saba ili atufikishe tunakotaka kwenda? Ni chama gani makini ambacho leo kinataja majina ya mafisadi kwa kinywa kipana lakini siku chache baadaye viongozi wake waandamizi wanapigana vikumbo mahakamani kutaka kuwawekea dhamana baadhi ya 'hao mafisadi' kwa kisingizio kuwa ni ndugu zao? Ni chama gani makini ambacho katika uzinduzi wa kampeni zake kinamruhusu mmoja wa makada wake waandamizi asimame hadharani na kushutumu jinsi kulivyokosekana dhamira ya kisiasa ya kuwatia hatiani waliofikishwa mahakamani kwa tuhuma za ufisadi lakini wakati huohuo baadhi ya watuhumiwa hao ni wateja wake anaowatetea huko mahakani?! Ni chama gani makini ambacho kinaanza kuomba kura kabla ya kampeni kuzinduliwa rasmi huku kikijua wazi kuwa kufanya hivyo ni kinyume na sheria ya uchaguzi na inaweza kupelekea wagombea wake wazuiliwe kushiriki uchaguzi?
  Dr. Slaa wakati wa kutafuta wadhamini wa kumdhamini kuwa mgombea alikuwa anaomba kura za wafanyakazi alizodai Kikwete kazikataa! Mpaka sasa bado nimepigwa na bumbuwazi kuwa ni vipi CCM haikujaribu kulitumia tukio hilo kumwekea pingamizi. Au kuna kamchezo? Sitashangaa sana iwapo CCM na CHADEMA lao ni moja katika kile kinachoendelea. Tusisahau pia kuwa mwanzoni mwa mwezi wa Julai, 2010, kada maarufu wa CCM mzee Mustapha Sabodo alitangaza kuwa anaichangia CHADEMA shilingi 100,000,000.00. Kwa wale wanaoijua vizuri CCM, kitendo cha kulikalia kimya tukio hilo ni cha kutia mashaka makubwa! Wengi wetu tunajua kuwa vyama vingi vya upinzanzani ni dhaifu sana kiraslimali kutokana na watu wenye uwezo kuogopa kuvisaidia ili wasije wakalipiziwa kisasi na CCM. Wengi wetu tunajua pia kuwa wachache wanaojaribu kufanya hivyo hufanya kwa siri kubwa!
  Lakini labda kubwa kuliko yote linalosababisha 'promosheni' ya vyombo vya habari kwa Dr. Slaa iwe ni yenye kutia sana shaka ni taarifa kwamba Dr. Slaa amekilazimisha chama chake kuingia naye mkataba kuwa ili agombee ni lazima kimlipe shilingi 12,000,000.00 kwa mwezi kwa muda wa miaka mitano iwapo hatafanikiwa kushinda nafasi ya urais. Kiasi hiki cha fedha ni wastani wa asilimia kumi na mbili (12%) ya ruzuku ya chama hicho ya kila mwezi kwa kiwango cha sasa! Kama taarifa hizi ni za kweli, na uwezekano mkubwa ni kuwa ni za kweli kwa sababu tangu zimechapishwa CHADEMA haijazikanusha, basi Dr. Slaa pamoja na viongozi wenzake waandamizi katika chama chao au hawajui wanachokifanya, au wana unafiki unaotisha! Hivi si huyu huyu Dr. Slaa na viongozi wenzake ambao wamekuwa wakiwaambia Watanzania kuwa mishahara ya wabunge ati ni mikubwa mno na wanataka ipunguzwe? Pamoja na ukweli huu bado wana-habari mnataka mtu wa aina hii awe kweli ndiye rais wetu?
  Katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2005 niligombea ubunge katika jimbo la Mwanga kwa tiketi ya CUF. Katika vitu vilivyonishangaza sana ni mgombea mwezangu wa ubunge kwa tiketi ya CHADEMA, kuacha kufanya kampeni za kujinadi na kukinadi chama chake; na badala yake akaunganisha nguvu na mgombea wa CCM, Profesa Jumanne Maghembe, kuhangaika kuipaka CUF matope. Mgombea huyo, Bwana Nathanael Mlaki, alipewa shehena kubwa ya vivuli (photocopies) vya habari iliyokuwa imeandikwa na gazeti la CCM la Mzalendo kuwa ati CUF ilikuwa imetia kinyesi kwenye visima vya maji huko Tabora! Kazi ya Mlaki ilikuwa ni kuzunguka kijiji hadi kijiji akigawa vivuli hivyo kwa Wananchi; na aliifanya kazi hiyo kwa juhudi kubwa hadi pale alipotaka kupigwa na Wananchi wenye hasira kali katika kata ya Kifula.
  Lakini tusisahau pia kuwa ni CHADEMA ndiyo ilihujumu juhudi za vyama vya upinzani kuwa na utaratibu wa kuachiana majimbo kutokana na nguvu ya chama katika jimbo linahusika. Katika uchaguzi mdogo wa jimbo la Kiteto, CUF iliiunga mkono CHADEMA kutokana na ukweli kuwa katika jimbo hilo CHADEMA ilikuwa inaonekana kuwa na nguvu kuliko CUF. Jambo la kushangaza ni kwamba katika uchaguzi mdogo wa jimbo la Tunduru ambako CUF ina nguvu zaidi kuliko CHADEMA kwa kila hali, chama hicho bila kuzingatia umoja uliokuwepo kiliamua kumweka Shaibu Akwilombe apambane na mgombea wa CUF, Rajab Mazee! Hali hiyo ilijitokeza pia Mbeya vijijini na Busanda, ambako kwa mujibu wa matokeo ya uchaguzi wa mwaka 2005, CUF ilikuwa na nguvu zaidi kuliko CHADEMA kwa kuwa ya pili nyuma ya CCM kwa wingi wa kura. Katika uchaguzi mdogo wa jimbo la Tarime, pamoja na kwamba tayari CHADEMA ilikwisha kuvunja makubaliano ya umoja, kwa kuzingatia kuwa jimbo hilo hapo awali lilikuwa mikononi mwa CHADEMA, CUF ilichagua kutoweka mgombea na kuwataka wanachama wake wampigie kura mgombea wa CHADEMA. Sasa hapa chama makini ni kipi? Siku zote hoja ya CHADEMA kujitoa katika umoja wa vyama vya upinzani ni kuwa ati hawawezi kufanya kazi na vyama ambavyo siyo makini! Ni umakini gani huo wanaouzungumzia?
  Kwa bahati nzuri au mbaya, hawa wenzetu historia inawatuhumu vibaya. Ni hawa hawa ndiyo walioisambaratisha Kamati ya Kuratibu Mabadiliko ya Katiba Tanzania (KAMAKA) mwishoni mwa miaka ya tisini iliyokuwa inajumuisha takriban vyama vyote vya upinzani, na hivyo kuua kabisa nguvu ya pamoja ya kudai katiba mpya. Ndugu zangu wana-habari, je, hiki kweli ndiyo chama ambacho kwa dhati kabisa mnaamini ni mbadala wa CCM?
  Kati ya wagombea waliofanywa wahanga wa mwenendo huu mbaya wa vyombo vya habari, walau Dr. Jakaya Kikwete ana bahati kuwa Chama chake kina nguvu kubwa ya kiuchumi ilinayokiwezesha kuwa na sauti katika baadhi ya vyombo vya habari vinavyomilikiwa na baadhi ya makada wake, au vile kinavyovimiliki chenyewe moja kwa moja. Walau basi kupitia vyombo hivi kampeni yake inapata fursa za hapa na pale kupamba kurasa za mbele za baadhi ya magazeti. Lakini ni kitu gani kimetokea hadi 'uswahiba' wake mkubwa na vyombo vya habari uliojidhihirisha katika uchaguzi wa mwaka 2005 ukatoweka kwa kasi? Mbeleko ile imekwenda wapi ukizingatia kuwa Kikwete ni yule yule tuliyeambiwa kuwa ni 'CHAGUO LA MUNGU'?
  Tatizo kubwa liko kwa Profesa Lipumba. Kwa kuwa Lipumba ni Muislamu, tena Muislamu anayetekeleza majukumu yake ya kiibada, na kwa kuwa sehemu kubwa sana ya Waislamu wa kawaida wa nchi hii wamelazimika kukiunga mkono chama chake kutokana na sera yake ya 'HAKI SAWA KWA WOTE', Lipumba amejikuta katika mazingira magumu ya kukosa 'marafiki' wenye nguvu katika medani ya vyombo vya habari. Aidha, kwa kuwa chama chake ni cha 'Wananchi' kwa kila hali – wengi wao hata uwezo wa kuwanunulia watoto wao madaftari ya shule kwa wakati ni tatizo – uwezekano wa kuwa na makada wenye uwezo wa kumiliki vyombo vya habari haupo.
  Uzuri ni kwamba, hata historia ingepindishwa vipi, ukweli utabaki pale pale kwamba Waislamu walikuwa ndiyo wenye mchango mkubwa katika kuasisiwa kwa chama cha TANU na katika mapambano ambayo hatimaye yalileta uhuru wa Tanganyika. CCM ni zao la TANU NA ASP, kwa maana hiyo siyo kosa kudhania pia kuwa Waislamu walikuwa na mchango mkubwa katika kuzaliwa kwa chama hicho. Badala ya kukimbilia kuituhumu CUF kuwa chama cha udini kwa kuwa tu kinaungwa mkono na Waislamu wengi, changamoto kwa wasomi, wana-habari na wachambuzi ni hii: HUKO CCM KUMETOKEA NINI HADI WAISLAMU WANAPAKIMBIA?
  Tatizo kubwa la Tanzania ni umasikini wa Wananchi. Nchi yenyewe kama pande la ardhi si sahihi kuiita maskini kwa kuwa imejaaliwa raslimali nyingi sana. Watanzania ni masikini sana kwa sababu nchi yao imeongozwa hovyo sana kwa muda wa miaka 49 mfulululizo. Raslimali za nchi zikitumika vizuri umasikini utaondoka na pamoja nao yataondoka matatizo ya ajira, uhalifu, elimu duni, miundo mbinu hafifu, afya mbovu, njaa, rushwa, nakadhalika. Japokuwa wana-habari wetu hili hawalikubali, lakini ukweli unabaki kuwa Profesa Lipumba akiwa kama mchumi aliyebobea wa kiwango cha kimataifa, ndiye pekee mwenye uwezo wa kutuvusha kati ya wagombea wote wanaogombea urais kwa sasa. Ukilinganisha na wagombea anaochuana nao, wasifu wa Lipumba katika nyanja za uchumi na uzalendo kwa nchi yake unang'ara kama mti wa Krisimasi, na hilo hakuna anayeweza kupingana nalo! Hebu tutazame haya machache:
  • Lipumba ni mjumbe wa kamati ya Umoja wa Mataifa ya kuangalia jinsi ya kuondoa umasikini katika nchi za dunia ya tatu. Angekuwa ni mtu asiye na uzalendo wa dhati kwa nchi yake, hivi sasa angekuwa huku na kule duniani akijikusanyia 'mapesa' na kuishi kitajiri na nyie 'wavimba macho' wa Tanzania mtajua wenyewe!
  • Japokuwa Lipumba ndiye aliyesimama na kujenga hoja katika Bunge la Marekani (Congress) akitaka nchi za dunia ya tatu ziondolewe mzigo wa madeni, jambo ambalo lilitekelezwa, hata siku moja sijamsikia akijipigia debe kwa mafanikio hayo. Kwake yeye suala muhimu ni kwamba madeni yameondolewa, sasa nani anapewa sifa kwa mafanikio hayo siyo jambo la msingi
  • Wakati wa mtikisiko wa kifedha wa nchi za mashariki ya mbali na kusini mwa bara la Asia, Lipumba ndiye aliyekabidhiwa jukumu na Umoja wa Mataifa la kuyashauri mataifa husika ni kitu gani wafanye. Sote ni mashahidi kuwa ndani ya miezi michache uchumi wa mataifa hayo ulikuwa umerejea kwenye hali yake ya kawaida.
  • Namibia ilipopata uhuru, Lipumba ndiye aliyeitwa kulisaidia Taifa hilo kuunda mfumo wake wa fedha.
  • Museveni wa Uganda, pamoja na uswahiba wake na CCM hakusika kumwomba Lipumba amshauri ni nini Uganda ifanye ili kuisadia nchi hiyo kukarabati uchumi wake.
  • Brazil, moja ya mataifa makubwa sana kiuchumi hivi sasa duniani haikusita kumtafuta Lipumba awashauri wafanye nini na ardhi yao ya ziada ili ichangie kikamilifu katika uchumi wa nchi hiyo.
  Naamini kuwa pamoja na jitihada za wana-habari wetu kujaribu kufinyanga akili zetu ili twende kupiga kura na 'KUJIUZIA MBUZI KWENYE GUNIA', Watanzania wanajua tatizo lao ni nini; na watapiga kura wakiwa na dhamira ya kujikomboa. Wito wangu kwa wana-habari ni kwamba, bado hatujachelewa, tuwape wagombea wote nafasi sawa na kisha tuwaachie Wananchi wafanye maamuzi yao.
   
 2. m

  mtemiwao JF-Expert Member

  #2
  Sep 25, 2010
  Joined: Sep 5, 2010
  Messages: 384
  Likes Received: 0
  Trophy Points: 0
  Kazi ya propaganda na uenezi inakufaa
   
Loading...