Vitongoji 4,000 Pwani kupata umeme karibuni

elivina shambuni

JF-Expert Member
May 31, 2018
461
295
1574341507033.png


KUTOKANA na serikali kutenga Sh bilioni 179 kwa ajili ya kusambaza umeme nchini, zaidi ya vitongoji 4,000 mkoani Pwani ambavyo havijapata huduma hiyo vitanufaika kupitia mradi wa ujazilizi.

Hayo yalisemwa na Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu, alipokuwa akizungumza na wananchi wa kijiji cha Mwidu, kata ya Ubena, halmashauri ya Chalinze, wilayani Bagamoyo juzi. Alisema vitongoji hivyo vitaingia kwenye mradi huo unaotarajiwa kuanza Desemba mwaka huu ambavyo Pwani ni moja ya mikoa tisa iliyomo kwenye mradi huo.

“Awamu ya kwanza ya ujazilizi ilikamilika mwaka jana na sasa tunaingia awamu ya pili ambayo inaanza mwezi ujao na hii ni kwa ajili ya vitongoji, tunatarajia vijiji kukamilika kupata umeme na kwenda kwenye vitongoji,” alisema. Mgalu alisema uunganishaji umeme ni kazi endelevu ili kuhakikisha vijiji vyote vinapata huduma hiyo muhimu na kwa upande wa vitongoji waliolipia wanapaswa kuunganishiwa kuanzia sasa.

“Nawapongeza Tanesco kwa kutenga Sh milioni 39 kwa ajili ya kufidia vijiji ambavyo wigo wake ulikuwa mdogo hivyo kushindwa kufikiwa na huduma ya umeme, haijawahi kutokea, haya ndiyo tunayoyataka,” alisema. Aidha, Naibu Waziri huyo alisema hadi Oktoba 15, mwaka huu, vijiji zaidi ya 8,150 kote nchini vimewashiwa umeme kwa bei ya Sh 27,000 tu kwa nyumba huku nguzo zikitolewa bure na kuwataka wananchi wasiwe na wasiwasi kwani hakuna atakayekosa huduma hiyo.

Meneja wa Tanesco wilaya ya Chalinze, Patrick Mtukananje, alisema mradi wa Wakala wa Nishati Vijijini (Rea) awamu ya tatu mzunguko wa kwanza unaotekelezwa na mkandarasi Sengerema Engineering Group, una thamani ya Sh bilioni 17.2 na umewafikia wateja zaidi ya 536 kwa wilaya nzima, ambapo makadirio yalikuwa ni kuwafikia wateja 477.

Alisema kwa mradi wa kijiji cha Mwidu, lengo lilikuwa ni kuwafikia wateja 23, lakini mpaka sasa wamewafikiwa wateja 50 na kwamba zimetengwa Sh milioni 269.8 na Tanesco imetenga Sh milioni 39 kwa ajili ya kazi hiyo. Mbunge wa Chalinze, Ridhiwani Kikwete, aliishukuru serikali kwa kusambaza huduma hiyo, akisema tangu alipochaguliwa kuwa mbunge mwaka 2015, vijiji vilivyokuwa na umeme vilikuwa 35, lakini sasa vimeunganishwa 52 kati ya 78 vya halmashauri ya Chalinze.

Alisema vijiji hivyo kuunganishiwa umeme kutasaidia kuinua shughuli za kiuchumi za ujasiriamali, pamoja na kuanzishwa viwanda vidogo vidogo kupitia vikundi vinavyowezeshwa na halmashauri.

Chanzo: Habari Leo
 
Hivi hiyo program ya kudesign mchoro kwa nia yakuwekewa umeme n lazima iwe 10,000/=?
 
Back
Top Bottom