Viroba Na Mihadarati Ni kama Mapacha

Ambiele Kiviele

JF-Expert Member
Dec 29, 2014
15,271
29,879
VIROBA na mihadarati ni kama mapacha.

Hupatikana kila mahali, ingawaje mihadarati
huapatikana kwa kificho. Lakini viroba, huhitaji
kwenda dukani au kwenye baa—vipo kila kona,
hata kwenye vituo vya daladala, stendi kuu zote
na kwenye vichochoro.

Jina kiroba limetokana na mfuko wa unga wa
kilo hamsini wenye ujazo wa kilogramu 50.
Viroba sasa ni vifungashio vya vitu mbali mbali
ikiwemo sukari, maharage, mahindi, karanga,
njegere na bidha nyingine za viwandani.

Lakini vifungashio vidogo ya plastiki vyenye mils
kati ya 100 na 50 za pombe kali kama vile
Konyagi na Kiroba Original, vimebadili matumizi
ya neno kiroba.

Labda imetokana na ukweli
kwamba wanywaji wa ‘viroba’ huchoka haraka
kana kwamba walikuwa wanabeba mizigo katika
viroba.

Hii ni kwa sababu wanavyonza pombe hizo kali
bila kuchanganya na kitu chochote. Wanywaji
wengine hupenda kunywa viroba vya konyagi,
kwa sababu bei yake ni nafuu ukilinganisha na
bia, na wengine ndio kinywa murua kwao.


Lakini
wanakunywa kwa ustaarabu.
Baadhi ya wanywaji wanasema ni vizuri kunywa
vinywaji vikali baada ya kula. Wengine
wanasema hawanywi konyagi kavu kavu.


Lazima
wachanganye na soda au maji ili kupooza
makali. Lakini vijana wengi wanakunywa viroba
bila kula na bila kuchanganya na kitu chochote
na wanaonekana kuathirika kiafya—wamedhoofu,
mabega yao yamepanda na nywele ambazo
rangi yake ni nyeusi, zinaonekana kupoteza
uasilia.

Pombe kwa ujumla wake zina madhara
kwa afya ya binadamu na si nia ya makala haya
kutaja zote, lakini kubwa ni kwamba hata
madaktari wanaonya wateja wao kwamba
wanywe kwa umakini ili kulinda afya zao.

Lakini inaeleweka kwamba kunywa pombe kali
bila kuipooza, mwili hupungukiwa maji unakuwa
‘dehydrated’—unapoteza maji.


Mbali na madhara hayo, viroba sasa limekuwa
janga la kitaifa—vinapatikana kila mahali na kwa
bei rahisi sana—kama ilivyo upatikanaji wa
sigara ambazo pia zinauzwa na vijana popote.

Zamani sigara na pombe viliuzwa grosari na
kwenye bar tu, kwa sababu wauzaji wanatakiwa
kukata leseni.

Lakini baada ya viwanda vinavyotengeneza vileo
kubuni vifungashio vya karatasi ya plastiki,
imekuwa rahisi kwa yeyote anayetaka kununua.

Vijana wananunua na kunywa viroba hapo hapo
wakiwa wima, au huweka mfukoni na kufyonza
taratibu, kimoja baada ya kimoja.


Viroba havijapangiwa muda maalumu wa
kunywa, iwe alfajiri, alasiri au usiku wa manane,
anayetaka kunywa atakunywa. Baadhi ya
madreva wanaoamsha daladala alfajiri, hununua
viroba na kuvipiga hapo hapo eti apate kile
wanachokiita kukata ‘stimu’—eti kuchangamsha
mwili.

Lakini hii haiko kwa madereva tu, hata vijana
wanaofanya vibarua, hasa wajenzi na
wanaofanya kazi za shruba, huwa wanaanza na
viroba.

Madereva wanaoendesha malori na
mabasi ya masafa marefu, hujaza pombe kali
kwenye chupa za maji na kubughia konyagi huku
wanaendesha.


Matokeo yake, pombe ikiingia nyingi kichwani,
madereva wanakosa umakini na kuendesha kwa
mwendo mkali hata sehemu wanazotakiwa
kupunguza mwendo.

Ajali nyingi zinatokana na
madereva kupoteza umakini na kutozingatia
alama za barabarani.


Upatikanaji wa viroba kwa urahisi, umeathiri
kundi kubwa la vijana wengi mitaani ikiwa ni
pamoja na wanafunzi, hasa wa shule za
sekondari zilizopo mijini.


Ukitafiti kidogo, utagundua kwamba, baadhi ya
wanafunzi wanapokwenda shule, au wakati wa
mapumziko, huchepuka pembeni na kufyonza
viroba—hii inawafanya kutokuwa makini
darasani, pombe huwapa jeuri ya kutowatii
walimu—wanatenda lolote wanalotaka na kama
hakuna udhibiti, nidhamu ya shule hushuka.


Matokeo yake, shule hizo hazifanyi vizuri katika
mitihani ya kitaifa kwa vile wanafunzi huwa
watoro, hata wanapohudhuria madarasani,
wanakuwa wapo wapo tu—badala ya kujazwa
elimu na maarifa, wanabeba ‘viroba’ vichwani!
Kwa vijana waliokatika mahusiano ya unyumba,
wanashindwa kuyamudu majukumu—kila siku
wanarudi nyumbani wakiwa wamelewa—hufikia
kitandani na kulala—hawataki usumbufu.

Katika
baadhi ya maeneo hapa nchini, inaripotiwa
kwamba hata uzalishaji—hasa mashambani,
umekuwa ukishuka—wanaume huamkia viroba
wakidhani vinawapa nguvu, kumbe ni kinyume
chake.

Akili ikichoshwa na kilevi, mwili hauwezi
kuwa na nguvu ya kufanya kazi ngumu.
Tatizo la viroba linaweza kudhibitiwa, lakini kuna
tatizo linguine sugu linalowasibu vijana hapa
Tanzania—dawa za kulevya. Dawa hizi zimeingia
hata shuleni na vyuoni.

Hili ni tatizo sio tu kwa
walimu, walezi na wazazi, ni tatizo la kitaifa.


Kuna mtaalamu moja anasema kwamba tofauti
na risasi ambazo zinaua mara moja, dawa za
kulevya na pombe kali vinaua taratibu, bila mtu
kujijua—ndio maana watengenezaji wa pombe
wameweka umri wa miaka 18 kwenda juu ndio
wanaoruhusiwa kuuziwa pombe.


Wanasema—drink responsibly, kunywa kwa
wangalifu na sheria ya mojawapo ya Usalama
Barabarani inakataza kuendesha chombo cha
moto ukiwa umelewa pombe.


Biashara ya dawa za kulevya ni vigumu
kuidhibiti kwa kuwa mtandao wake ni mpana na
wa kificho.

Ugumu wake umeongezeka zaidi
baada ya kuingia mfumo wa soko huria na
utandawazi. Na maendeleo ya teknojia
yameifanya dunia kuwa kama kijiji.


Taifa linapoteza nguvu kazi kwa kuwa vijana
wakibobea kwenye ulevi na dawa za kulevya,
wanakuwa legelege, hawana msaada kwa
familia zao na taifa kwa jumla.


Kwa kuwa mwisho wa siku, hata kama walikuwa
na kazi, huwa wanapoteza ufanisi. Jamii yetu
imeshuhudia kutoweka kwa haraka vijana
walioinukia kwenye sanaa, wamegeuka kuwa
mazombi.


Kijana huwa anabadilika tabia, na kama alikuwa
na uwezo wa kifedha, huziharibu na kugeuka
kuwa mdokozi, au akimzoea mtu fulani, anakuwa
tegemezi—ombaomba ili apate fedha kidogo za
kununua kete.


Wengine huanza kuuza mali na vitu vyake
kidogo kidogo, mwishowe anauza hata nguo
zake. Inakuwa vigumu kumgundua mlevi wa
dawa za kulevya kwa sababu anakuwa msiri.


Lakini jinsi siku zinavyokwenda, na asipopata
dozi, utamgundua. Anakuwa hana utulivu na
anakuwa na wasi wasi.


Hivi sasa vijana wengine wako katika vituo
maalumu vya kuwarekebisha—‘rehabilitation
centres’ ambako wanafundishwa njia mbadala
ya kuachana na dawa za kulevya.


Sisi kama taifa tunachukua hatua gani kuzuia
upatikanaji rahisi wa viroba na matumizi ya
dawa za kulevya miongoni mwa vijana? Njia
moja wapo ni Serkali kupiga marufuku
vifungashio vya plastiki vya Konyagi na Kiroba
Original, lakini pia Sheria ya Vileo (1968)
pamoja na maboresho yake, iweke mkazo kwa
kuziba mianya ya upatikanaji wa vileo .


Aidha, mtu akikamatwa anauza pombe mahali
ambapo si rasmi, na wala hana leseni,
akamatwe kama anavyofuatiliwa muuza
mihadarati na apelekwe mahakamani.


Hili la dawa za kulevya ni ‘pasua kichwa’ dunia
nzima. Tanzania imejaribu njia mbali mbali,
kupambana na uingizaji na uuzwaji wa dawa za
kulevya—ikiwa ni pamoja na kuunda kikosi
maalumu cha kupambana na ‘wazungu wa
unga’—bila mafanikio.


Rais aliyepita, Jakaya Kikwete, aliwahi kutamka
kwamba alikuwa na orodha ya watu
wanaojihusisha na biashara haramu ya dawa za
kulevya, lakini akaondoka madarakani kimya
kimya bila kuwataja na kuwachukulia hatua.
Kwa nini na orodha ya majina alimwachia nani?

Tunaweza kuhisi tu kwamba suala hili
linawagusa vigogo wengi na huenda baadhi yao
ni maswahiba wa viongozi, au ni watoto wao.

Labda viongozi wetu wachukue hatua kama
anazochukua Rais wa Ufilipino, Rodrigo Duterte,
ambaye ametoa amri kwa vigogo wote serkalini
na wafanyabiashara wanaojihusisha na biashara
ya dawa za kulevya wajisalimishe, vinginevyo
vigilante—sungusungu na polisi,
wawashughulikie.
Hadi mwishoni mwa mwezi uliopita, imeripotiwa
kwamba watu 1,900 ambao wanahusishwa na
biashara ya dawa za kulevya, wameuwawa
tangu rais huyo aingie madarakani mwezi Mei,
2016.

Kuna vijana wa Kitanzania zaidi ya 200, ambao
wanatumika kama punda wa kubeba mihadarati,
wanasota kwenye magereza ya Hong Kong
pekee.

Hadi Machi, 2015, vijana 185 walikuwa
wamefungwa nchini China adi na wengine
wamenyongwa huko ughaibuni kwa kosa hilo!

Wakati umefika sasa, Bunge litunge sheria kali
zaidi ili watu waogope.

Waziri wa Mambo ya
Ndani, Mwigulu Nchemba, alisema mara baada
ya kuapishwa Juni, 2016 kuwa ataipa
kipaumbele vita dhidi ya dawa za kulevya.

Waziri Nchemba apelike muswada bungeni
wenye vipengere vikali zaidi ikiwa ni pamoja na
kifungo cha maisha, na kuwafilisi vigogo
watakaopatikana na hatia, ikiwa ni pamoja na
wake na ndugu zao wa karibu na watoto wao—
maana hawa hufaidika kwa njia moja au
nyingine na

matunda ya biashara hii haramu.

@ Ambiere
 
Back
Top Bottom