VIPEPEO WEUSI: MKAKATI NAMBA 0034
EPISODE 18
Tayari ilikuwa inakaribia majira ya saa tisa alasiri, tulikuwa tumeshamaliza kula chakula na muda huu nilikuwa natoka katika ofisi ambapo niliitwa na yule askari wanayemuita Obama.
Asubuhi ya siku hii nilipo maliza kuongea na wageni wangu, Cheupe na Hasnat nilirejea yard kumcheki Godi nikoongea naye mawili matatu na kumpa mrejesho juu juu pasipo kuingia kwa undani sana kuhusu nilichoongea na Isack na Cheupe kisha baada ya hapo tukaanza kusubiri kuona kama Hasnat na Isack watafanikisha kuleta document ambayo Kaburu alikuwa anaitaka ziletwe kwake kabla ya siku hii kuisha.
Cheupe na Issac hawakuniangusha, kwani majira ya kama saa nane na nusu mara tu baada ya kumaliza kula chakula, nikaitwa ofisini na Obama, kisha akanikabidhi hizo document zikiwa kwenye bahasha ya kaki, nikazisweka ndani ya suruali na ndio sasa nilikuwa natoka ofisini kwake kuelekea yard.
Baada ya kufika yard nikamtaarifu Godi kuwa niliitwa kwenda kuchukua documents na ndio sasa natakiwa nifanye mpango kumkabidhi Kaburu.
Kwahiyo Godi akaenda moja kwa moja mpaka yard namba moja ambako Kaburu alikuwa amepumzika na kumtaarifu kuwa nataka nionane nae.
Mimi nikatangulia mpaka pale uchochoroni panapo unganisha yard ya kwanza na ya pili.
Dakika kama tatu baadae Kaburu akafika akiwa anatembea kwa kuchechemea. Inaonyesha bado alikuwa na maumivu ya virungu vya juzi.
"Umefanikisha?" Akaniuliza kwa sauti ya chini mara baada kufika kwenye uchochoro.
Sikusema chochote. Nikaingiza mkono ndani ya suruali na kuibuka na bahasha ya kaki.
"Hizi hapa" nikaongea huku nimezigandamiza document kifuani kwake. "Nadhani sasa tumebakisha suala moja tu"
"Umeshapata wazo unanitoaje humu" akaongea huku anazisweka ndani ya suruali yake haraka haraka zile documents.
"Nina wazo, ila ni wazo nusu tu! Nadhani mpaka kesho asubuhi naweza kuwa nimepata wazo kamili.!" Nikaongea huku nageuka kuondoka kwenye uchochoro.
"You better come up with something fast, la sivyo wote sidhani kama tutamaliza wiki tukiwa hai" akongea huku naye akigeuka kutoka uchochoroni.
Nikoaondoka kutoka pale uchochoroni na kurejea yard huku kichwani napiga mahesabu makali sana. Ni namna gani naweza kumtorosha mfungwa kutoka gerezani?? Hivi vitu nimekuwa naviona kwenye sinema tu lakini sasa natakiwa nivifanye mimi kwenye maisha halisi.
Katika sinema mara zote watu wanaotoroka ufanya hivyo kwa urahisi sana au tuseme kwa ujanja ambao unahusisha matukio machache tu kisha anafanikiwa kutoroka.
Lakini kila nikiangalia ulinzi wa hii jela, ambapo hapa yard kwenyewe , kila yard ina maaskari wanne wa doria.. Wawili wanakaa nyuma mwishoni kabisa kwenye yard na wawili wanakaa mbele ya yard.
Pia nikiangalia jinsi zile kuta zilizozunguka gereza jinsi zilivyokuwa ndefu, pia nyuma ya hizi kuta huko nje kila upande una askari wawili wenye silaha wanaofanya doria.
Pasina shaka, suala hili lilikuwa haliwezekani.
Lakini siku zote katika maisha hakuishi kuwa na vitendawili vinavyotutaka tufanye yasiyowezekana ii tuendelee kuishi au kupata tunavyovihitaji.
Mara zote katika maisha unatakiwa utende miujiza ili ufike pale unapopataka.
Watu wamekariri katika akili zao kuwa, miujiza ni labda kupaa juu angani, labda kutembea juu ya maji, au labda kumfanya mfu afufuke au kubadilisha karatasi kuwa hela.
Na ndio maana wamejaa wahubiri wenye kujigamba kutenda miujiza, kufanya viwete watembee, viziwi wasikie na mabubu kuongea. Na ajabu zaidi sasa wameanza kuibuka "mashehe" wenye kujigamba kuwa nao wanafanya dua ili kutoa watu "majini" yaliomo ndani yao, kuleta bahati, kupata Mali na kuponya magonjwa.
Binafsi, kama Rweyemamu ni mkristo safi kabisa na mwenye kuamini katika Mungu na kuijua imani yangu.
Lakini mara zote haijalishi niko mahali gani nimekuwa nikijizuia kuchangia mijadala kuhusu dini na imani kwa sababu imani maoni yangu ni tofauti kabisa na watu wengi.
Maisha yangu yote nimekuwa na mtazamo tofauti kabisa na hivi vitu watu wanavyoviona kuwa ni miujiza. Binafsi sivioni kama miujiza bali naviona kama mazingaombwe. Yes, ni mazingaombwe sio miujiza.
Miujiza ni mfano wa mama mjane anayekaa uswahilini kabisa. Anaishi kwa kupika maandazi au chapati.. Lakini anamudu kuwalisha watoto wake watatu au wanne milo yote mitatu kila siku.. Anamudu kuwanunulia sare za shule na mahitaji mengine na bado anamudu kuwalipia watoto wake ada ya shule na anafanya jukumu hilo kwa miaka kibao mpaka watoto wake wanafika Chuo kikuu.
Hiyo ndio mijuiza.
Miujiza ni pale ambapo kijana Charles Odhiambo, mtoto yatima wa mitaani nchini Kenya anaanzisha biashara yake ya kuuza maji ya kufunga ambayo tunaita jina la utani "dripu", na anaifanya biashara hiyo kwa mwaka mzima akitunza faida yake kiduchu kidogo kidogo. Kisha anajifunza namna ya kufanya purification ya maji ya mvua na kuyasindika kwenye chupa.
Anachukua faida yake kiduchu akiyoitunza mwaka mzima na kununua chupa kadhaa za kusindikia kutoka "SIDO" na kimashine kidogo cha kusafisha maji.
Miaka mitatu baadae kijana huyu biashara yake hii ya kuuza maji imekuwa kubwa na kuwa kampuni inayoitwa "Sky Drop" ambayo hatimaye inapata uwekezaji wa dola laki tatu kutoka kampuni nyingine ya usindikaji maji kutoka Ulaya na kumfanya kijana Charles Odhiambo mwenye miaka 23 tu kutoka kuwa mtoto wa mitaani na kuwa moja ya vijana waliofanikiwa zaidi barani Afrika.
Hiyo ndiyo miujiza.
Miujiza ni mfano wa rafiki yangu mwanadada maarufu mjini Morogoro kwa jina la "Mama Halima", baada ya kufanya kazi za ndani kwa miaka mingi, hatimaye anapata "bahati" ya kuolewa. Licha ya kuolewa na mwanaume mwenye kipato cha chini kabisa lakini mme wake huyo anampa mtaji wa shilingi elfu hamsini ili afanyie biashara aipendayo. Anachukua elfu hamsini hiyo na kuunganisha na akiba yake ya elfu ishirini na kuwa elfu sabini na kisha ananunua cherehani na kuanza kujifunza kushona.
Leo hii miaka takribani saba baadae, dada huyu ndiye "Top Designer" kwenye mji wa Morogoro akimiliki 'brand' kubwa na maarufu inayojilukana kama "Mama Halima Collections"
Hiyo ndiyo miujiza. Sio mazingaombwe tunayoaminishwa kwenye vipindi vya televisheni na watu wenye kujigamba kuwa wao pekee ndio wamejaliwa "vipawa" vya kufanya miujiza.
Mungu alipotuumba sote, aliweka uwezo wa ajabu wa kutenda makubwa ambayo hayaelezeki kwa akili ya kawaida.
Nikageuka huku na huko kuangalia pale yard. Nikawaangalia wale maaskari wa doria walioko mbele ya yard na nyuma. Nikaangalia zile kuta ndefu za kutisha zilizo zunguka yard. Hakika nilichokuwa nataka kukofanya kilikuwa hakiwezekani.
Nikavuka pumzi ndefu ndani na kuitoa nje. "Natakiwa kufanya muujiza", nikaiambia nafsi yangu. Hakuna namna nyingine kama nataka kilichonileta humu gerezani kikamilike, basi sina budi kuchekecha akili na kufanya kile kisichowezekana.
Na natakiwa nifanye hivyo sio kwasababu yangu na cheupe tu, au baba yake cheupe tu, hapana! Natakiwa nifanikishe kisichowezekana kwa sababu ya mwanangu.
"Kaba seloooooooooooooo"
Nilishtushwa kutoka katika dimbwi la haya mawazo na mipango kichwani mwangu, na sauti ya nyapala akitangaza muda wa kulala.
"Oiii" kuna mtu akiniita nyuma yangu.
Alikuwa ni Godi anakuja pale nilipokuwa nimesimama.
"Siamini kama unapanga kile ukichinieleza Jana" akaongea huku tunaongozana kuondoka hapo yard kuelekea selo.
"Kitu gani?" Nikamuuliza.
"Nimekuona muda mrefu tu umesimama anaangalia kila kona ya yard na kila upande wa ukuta unazunguka 'ngome'. Nina hakika ulikuwa kichwani unapanga kuhusu kumtorosha Kaburu" akaongea kwa sauti ya chini.
"Yeah! Sina jinsi.. Inabidj nifanye hivyo" nikamjibu.
"Haahaha! Sijawahi kusikia mtu ametoroka hii ngome.. Dah nasubiri nione hiyo miujiza aisee" akaongea kwa mzaha huku anacheka.
"Yeah! Uko sahihi kabisa.. Utakuwa ni muujiza" nikajibu kwa kutabasamu nikikumbuka kuwa na muda mchache tu nilikuwa nawaza kuhusu miujiza.
"Alafu unakumbuka kuwa tunadaiwa shilingi elfu kumi na deadline ilikuwa leo na hatujalipa!! Sijui tutambebea mbeleko gani yule nyapara kesho.." Godi akaongea huku anashusha pumzi kwa kuogopa hicho kitakachotukuta kesho.
"Usijali! Hiyo pia ni fursa kwenye mpango wangu" nikamueleze huku natabasamu lakini nikimaanisha ninachomueleza.
"Nini?" Akaniuliza kwa mshangao.
"Subiri utaona" nikamjibu kwa kifupi tu.
Tulikuwa tumeshafika nje ya selo. Tukavua mashati na kuchuchumaa kusubiri kuhesbabiwa na kuingia kwenda kulala. Siku ilikuwa imeisha.
****************************
SIKU YA SITA
Licha ya siku hii kuwa naitegemea kugubikwa na sinto fahamu nyingi, lakini ilikuwa imeanza kwa uchangamfu mkubwa. Labda ni kutokana na haya mazoezi ya asubuhi, na hapa ndipo naemdelea kusema na kuamini huyu aliyebuni utaratibu wa mazoezi kila asubuhi gerezani alifikiria kwa ufahamu wa sita.
Yule afande mwingine alikuwa amemaliza kutuimbisha nyimbo za halaiki.. Sasa ulikuwa umewadia muda pendwa wa Msauzi kuimbisha nyimbo za "kihuni".
Ile kupanda tu pale juu kwenye kibaraza, wafungwa kama kawaidawakaanza kushangilia na kupiga miluzi.
"Wiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiii"
"Waaaaaaaaaaaaaaaa" wafungwa wakaitikia.
"Wiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiii" akasalimia tena.
"Waaaaaaaaaaaaaaa"
Akarudia hivyo karibu mara tano, kisha akaanza kuimbisha.
"Nenda kalitoeeeeee nenda kalitoeeeeee"
"Kama ulitaki hill busha nenda kalitoeeeeeeeeeee" wafungwa wakaitikia kwa makelele na furaha.
"Nenda kalito, nenda kalito, nenda kalitoeeeeeee"
"Kama hutaki hilo busha nenda kaliyoeeeeeeee"
Wafungwa walichangamka kweli kweli. Wanajinwaya mwaya utadhani wako kwenye klabu ya usiku.
Msauzi sijui alikuwa amekula nini leo, maana akatubadilishia "gia angani" akaanza kutuimbisha nyimbo za 'Kiluguru'. Lakini hii haikufanya wafungwa waacje kujimwaya mwaya na kuimba kwa furaha.
"Lidomo fulemu mijino biasharaaaa" akaanzisha nyimbo.
"Oooooohh tumalize kesi mamaaaaaaa" wafungwa wakaitikia kwa furaha na kwa sauti ya juu.
"Nunu nunu nunu nunu nunuuuuuu"
"Oyaaaaaaaaaaaa"
"Unamnunia nani?"
"Oyaaaaaaaaaaaaa.!"
"Kamnunie mkeo!"
"Oyaaaaaaaaaaaaa"
"Aliyekuleta jelaaaaaaaa"
"Oyaaaaaaaaaaaaaa"
Alafu anaanza tena kuanzia mwanzo wa wimbo.
"Lidomo fulemu mijino biasharaaaaaa"
"Oooooooo tumalize kesi mamaaaaaa" wafungwa kama kawaida wakashangilia na kuimba.
Nyimbo zikaimbwa na watu wakafurahi.
Leo hii ndio siku ambayo Dr. Shirima alinieleza kuwa italetwa hati ya dharura ya kunihitajo mahakamani, ambako alidai kuwa kesi itafutwa na alitaka niende moja kwa moja kwenye makazi ya askofu kuonana naye.
Utaratibu wa hapa magereza nimba, mkimaliza kunywa uji kila siku.. Anapita askari magereza kwenye yard zote mbili ambapo, anasoma majina ya mahabusu ambao wanatakiwa kwenda mahakamani siku hiyo kusikiliza kesi zao.
Baada ya kunywa uji, askari alipita na kuita majina ya wanaotakiwa mahakamani siku hiyo.. Ni kweli jina language lilikuwepo pamoja na wemzangu wengine wanne.
"Daaaahh kwahiyo kuna uwezekano usirudi humu mwanangu!" Godi akaniluza huku ananiangalia kijicho cha wivu.
"Yeah! Nadhani sitarudi humu" nikamjibu.
"Naamini hautasahau ishu yangu" akaongea huku amenikata kijicho cha wasiwasi.
"Siwezi kusahahu aisee! Uzuri ishu yako ni simple.. Unahitaji wadhamini tu.. Nitakutafutia wadhamini"
"Ma ukumbuke nataka wadhamini wa….."
Nikamkatisha kabla hajamaliza sentesi.
"Yeah yeah nakumbuka yote hayo.. Unataka wadhamini wa kijiwe cha stendi cha chamwino.. Nikawalipe hela wao wana vitambulisho bandia na hizi ndio Mishe zao zinawaweka mjini, wanajua wafanyaje kuweka picha za uongo kwenye hati za dhamana na blah blah nyingine.. So unataka hivyo ili ukitoka ukimbie kesi usionekane tena..! Nakumbuka vyote hivyo don't worry"
Nikamjibu kwa kirefu kumuelezea ili abaki na amani kuwa nakumbuka tulichokubaliana.
"And nakukumbushwa kuwa tunadaiwa elfu kumi na Nyapara.. Sijui inanichaje humu.. Sitaki kuoleqa kwa lazima"
"Nimekwambia toka jana kuwa hiyo ni fursa nataka kuitumia ili kufanikisha ishu ya Kaburu"
"Mwanangu umeanza kuvuta bangi humi jela au?? Tangu lini deni likawa fursa ya kumtorosha mtu jela" akang'aka huku akoongea kipande cha mwisho cha sentesi kwa sauti ya chini.
"Tuliza mshono Dogo, utaona na utaelewa" nikamjibu huku naanza kuinuka. "Naenda kumcheki Kaburu kuna maagizo nataka kumpa kabla sijaondoka"
"Kilala heri jini mipango hahahahah" akaongea kwa mzaha na kuanza kunicheka.
Sikumjibu chochote, nikageuka nikamuonyesha kidole cha kati na kuondoka. Hakina jela ilishaanza kunikaa kwenye damu. Sikumbuki ni lini mara ya mwisho nilimnyooshea mtu kidole cha kati.
Nilipofika kwenye uchochoro wa kuelekea yard namba moja nikakutana na Kaburu anatembea haraka haraka kuja yard namba mbili.
"Unajifanya mjanja sana sio" kaburu alifoka baada ya kuniona. Mkononi alikuwa ameshika ile bahaasha ya kaki niliyompa jana.
"Ujanja wa nini?" Nikauliza huku nimeduwaa.
"Hiki nini?" akaongea kwa mkato huku ananionyesha bahasha aliyoishika mkononi.
"Hiyo imefanyaje" nikauliza nikiwa bado nimeduwaa.
"Hizi documents sio zenyewe" akaongea huku akitoa kwa hasira karatasi kutoka kwenye bahasha na kuniwekea mkononi mwangu kwa hasira.
Nikapepesa macho kwenye zile karatasi, kisha nikamuangalia tena Kaburu.
"Sielewi unanichanganya ujue" nikaongea kwa mshangao mkubwa.
"Dogo usinifanye mimi mpumbavu, hizi documents umenibadilishia, hiki sicho kilichopo kwenye email nilichokwambia watu wako wakaprint na kuniletea" Kaburu akaongea kwa hasira nusura aanze kunikunja shati.
"Hey, wait.. hebu kuwa mtulivu kidogo! Mimi nikubadilishie hizo documents alafu nizifanyie nini?"
"Basi ni hao wenzako wamezibadilisha"
"No way! Hawawezi kufanya hivyo"
"Kama wewe haujabadilisha na wenzako hawajabadilisha, ni nani aliyezibadilisha na ziko wapi?" kaburu akaongea kqa hasira huku anahema.
Taa ikawaka kichwa. Shiiiiit!!
Hizi documents zimepita kwenye mikono mitatu kabla ya kumfikia Kaburu. Zimepita kwangu, kwa kina Cheupe na kwa Obama ambaye alikabidhiwa anipe mimi kwa siri.
Mimi sikubadilisha hizi documents, na nina hakika Cheupe na issack hawakuwa na sababu ya kubadilisha, kwahiyo dhahiri aliyebadilisha atakuwa ni Obama.
"Oooohh shiiiiitt.! No no no noooo." Nikalalamika na kufumba macho, mwili ukakosa nguvu nilitamani nikae chini.
"Whaaaatt!" Kabutu akauliza kwa kukereka na hasira.
"Obama ndiye amebadilisha!" Nikamwambia kwa kifupi.
"What?? Obama anahusikaje kwenye hili?" Akauliza tena kwa hasira.
"Yeye ndiye alipewa bahasha na watu wangu ili aniletee" nikamfafanulia.
"Na kwanini abadilishe??" Kaburu akauliza.
Ilinibidi nikae chini ili nisidondoke kutokana na mshtuko nilioupata. Hapa ndipo nikang'amua kosa kubwa nililolifanya, na kosa hili nilianza kulifanya tangu siku nne zilizopita.
SIKU NNE ZILIZOPOTA (ALHAMISI)
Nilikuwa nimeondoka yard namba mbili na kumuacha Godi kwa kumpa maagizo kuwa ahakikishe sinyorita yuko karibu nikitoka hukj kwenye ofisi ya magereza ili niweze kuongea naye.
Mpango niliokuwa nao kichwani kuhusu namna nitakavyo fanikisha kumuondoa Kaburu kutoka kushinda ofisini kwa mkuu wa gereza na aanze kushinda yard, mpango huu ulokuwa unahitaji wahusika kadhaa na mmoja wao nilimlenga Sinyorita. Lakini pia nilikuwa nahitaji msaada wa askari yule mstaarabu wanayemuita Obama.
Nilikuwa nimefika upande huu wa gereza wenye jiko ambao unaungana na maofisi. Kwenye mlango wa kutoka hapa kuelekea kwenye maofisi kulikuwa na askari wa doria.
"We mseng* unafanya nini huku?" Yule askari akaniuliza baadabya kuniona.
"Nimekuja kumuona Obama ameniita" nikamdanganya.
"Subiri hapo hapo" akaongea huku anaingia ndani kule kwenye maofisi.
Dakika mbili baadae akarejea.
"Ingia… Si unajua ofisi yake ilipo?" Akaniuliza akiniruhusu kuingia kule kwenye maofisi.
"Yeah najua"
Kama dakika moja baadae nikawa mbele ya ofisi ya Obama. Nikagonga mlango na akaniruhusu niingie.
"Wow! Hahah, nilijua lazima iko Siku utaniomba msaada kuhusu jambo lolote humu gerezani lakini sikudhani kama itakuwa haraka hivi.. Karibu uketi" akaongea huku ana tabasamu kama kawaida yake.
Nikaketi. Sikusema chochote mpaka mda huu. Kichwani nilikuwa natafakari ni namna gani niongee kile nilichokuja kuomba msaada hapa.
"Sijui nikusaidie nini Ray" akaongea kwa utulivu akinitazama.
Nikajisemea rohoni liwalo na liwe. Kama nitakuwa 'wrong' katika hisia zangu jinsi nilivyohisi basi na iwe hivyo. Ni bora kujaribu kuliko kutojaribu kabisa.
Itaendelea Kesho Jumamosi..