Viongozi wa dini

Viongozi wa dini

Kiwalani finest

Senior Member
Joined
Jul 6, 2024
Posts
116
Reaction score
85
Ninatambua mchango wenu mkubwa katika kudumisha amani na haki nchini. Hata hivyo, nawaomba muache kabisa kutoa kauli zinazobeba viashiria vya uchochezi wa kuamsha hisia za kidini. Kumbukeni ninyi ni Watanzania mnaowajibika kujisomea maandiko ya kimfumo ya nchi yetu. Jifunzeni vitabu vya mfumo, jengeni hoja kwa kurejea moja kwa moja maandiko hayo. Jiepusheni na matamko yenye ubaguzi na upendeleo, yanayokwenda kinyume na matakwa ya Katiba ya Nchi.

Nilisikika nikikoroma ndotoni, baada ya mijitu ijitamkishayo jina la Mwenyezi Mungu kunivutia bangi aina ya Skanka. Huko ndotoni nikaanza kuropoka. Nakumbuka tarehe 28/03/2025, Prof. Abubakar Bin Zuber Bin Ally Bin Mbwana, Mufti na Sheikh Mkuu wa Tanzania, aliposema katika Usiku wa Lailatul Qadr:

"Mtu mwenye akili, akiiona ishara kidogo tu, tayari ameishaelewa."

Naye Padre Dkt. Faustine Kamugisha, Paroko wa Parokia ya Minziro, tarehe 06/04/2025 alisema:

"Ukweli kama hautashinda leo, basi kesho utashinda. Ukiuzika ukweli, ukweli utafufuka. Yesu ni ukweli wenyewe. Alisema: ‘Mimi ndimi njia, ukweli na uzima’."

Kwa hivyo, wanaomfuata Yesu ni wasema kweli, hawamung’unyi maneno.

Tarehe 08/04/2025, Wakili Boniface Anyisile Kajunjumele Mwabukusi, Rais wa TLS alisema:

"Lazima kila Mtanzania apate nafasi ya kuzungumza."

Tusome Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, toleo la 2005: Ibara ya 8(d), 18(a), 19(1), 26(1)(2), 9(a)(b)(f)(h), pamoja na Ilani ya CCM ya mwaka 2020–2025.

Sisi kama nchi bado tunakabiliwa na tatizo la adui ujinga. Tusiposema, adui huyo ataendelea kutugawa. Askofu Almachius Rweyongeza wa Jimbo Katoliki la Kayanga alisema tarehe 20/03/2025, akiwa na Waziri Mkuu katika Jubilei ya Askofu Kilaini:

"Tulipopata uhuru mwaka 1961, Baba wa Taifa Mwl. Nyerere alisisitiza vita dhidi ya maadui watatu: Ujinga, Umaskini na Maradhi. Je, tumefanikiwa kwa kiwango gani kupambana nao?"

Katika nyakati hizi, adui ujinga anatuzidi nguvu. Anatutawanya kwa mipira ya burudani na kutufanya tusome maandiko ya kihisia badala ya maandiko ya kimfumo yanayotufundisha namna ya kuondoa ujinga huu.

Viongozi wa dini wana haki ya kushiriki siasa, lakini ni lazima wajipe muda wa kujisomea maandiko ya kimfumo. Viongozi wa Kikristo wasome Biblia kwa tafakari kubwa na vitabu vingine vya historia ya Ukristo. Viongozi wa Kiislamu wasome Qur’an (juzuu zote 30), Sunnah za Mtume Muhammad (S.A.W), na vitabu vya maimamu maarufu.

Nchi ya Tanzania ina maandiko ya kimfumo kama Katiba, kanuni, miongozo, na taratibu. Viongozi wa dini na wa kimfumo lazima wayasome na kuyaishi. Viongozi wa kisiasa lazima wasome katiba na sheria za vyama vyao, na wazingatie viapo vyao vya kulinda Katiba ya nchi.

Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan alisema tarehe 25/04/2025:

"Dola ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inasimamiwa na mihimili mitatu: Serikali, Bunge na Mahakama. Pia, taasisi nyingine zinashirikishwa katika uendeshaji wa nchi, zikiwemo taasisi za kidini. Kazi zao ziongozwe kwa mujibu wa Katiba, sheria na miongozo ya kitaifa na kimataifa."

Prof. Eginald Pius A.M. Mihanjo, Mkuu wa Idara ya Historia SAUT, tarehe 25/04/2025 alisema:

"Kukanyaga Katiba kunatokea mara nyingi."

Watu wanakanyaga Katiba, huku viongozi wa kidini wakiwa hawasemi. Hili ni tatizo. Padre Dkt. Charles Kitima alisema:

"Tusiongelee amani kama hatutaki kuongelea haki."

Askofu Dkt. Benson Bagonza naye aliongeza:

"Tuna tatizo kubwa la kutokuwa na usawa mbele ya sheria."

Sheikh Othman Khamis Juma, Imam wa Msikiti Mtoro, alisema:

"Ukimuona mtu asiyemuogopa Mungu, muogope yeye."

Viongozi wa dini wanapokemea ukiukwaji wa Katiba, wafanye hivyo wakiwa na uelewa wa maandiko ya kimfumo. Wasikimbilie kutetea mtu kwa misingi ya hisia bila uhakika kama huyo mtu anafuata kiapo chake.

Mheshimiwa Dkt. Dotto Biteko tarehe 27/04/2025 alisema:

"Tuzingatie sheria wakati wote tunapotekeleza majukumu yetu. Bila sheria, hatuwezi kupeleka taifa letu mbele."

Mheshimiwa Godbless Lema alisema:

"Kazi kuu ya Maaskofu na Mashekhe ni kuusema ukweli, hata kama ukweli huo unawaua."

Tusome tena Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ibara ya 12(1)(2), 13(1)(4)(5), na 26(1)(2).

Viongozi wa dini, kabla ya kumtetea mwanasiasa yeyote, wachunguze kama anafuata misingi ya kiapo chake kwa mujibu wa Katiba.

Historia ya nchi yetu inaonyesha kuwa hata wakati wa wakoloni, wamisionari walihubiri Ukristo na kujenga shule. Mifumo mingi ya kiutawala ina mizizi ya kimisionari. Hivyo basi, kuelewa mfumo wa utawala kunahitaji kujisomea.

Kiongozi wa dini ni lazima awe na maarifa ya maandiko ya dini yake, na pia maandiko ya kimfumo ya nchi. Hoja za Kiislamu zijibiwe Kiislamu kwa maandiko sahihi; hoja za Kikristo zijibiwe Kikristo; na hoja za kimfumo zijibiwe kwa kutumia Katiba, kanuni, na taratibu rasmi.

Profesa Mussa Assad, Makamu wa Chuo Kikuu cha Kiislamu Morogoro, tarehe 29/04/2025 alikumbuka mazungumzo ya Hayati Benjamin Mkapa:

"Waislamu walirudi nyuma sana katika elimu ya kisekula. Lengo la Mkapa kutoa chuo kilikuwa kuchangia elimu kwa Waislamu."

Muda tunao. Tujisomee. Tuelewe maandiko ya kimfumo. Tuyaishi. Tuseme ukweli kwa kutumia maandiko sahihi.

Nilishtuka kutoka usingizini ndani ya ulimwengu wa kiroho, huku nikiwa kimya...

Mathias Mugerwa Kahinga.
 
Back
Top Bottom