Viongozi na falsafa ya Afrika

Victor Mlaki

JF-Expert Member
May 1, 2016
3,659
3,572
FALSAFA YA AFRIKA NA VIONGOZI WA LEO.
Afrika ina namna yake ya pekee sana ya kuutafsiri ulimwengu wake kwa kuzingatia misingi yake.
Licha ya falsafa hiyo kupewa majina mengi ya lugha jamii bado misingi yake ni ileile.

Mathalani kwa Afrika ya kusini wao waliita UBUNTU na ukiangalia kwa ndani Ubuntu ndiyo ujamaa wa Kiafrika.
Iliaminika Mtu ni watu na kila mtu alipaswa kuliheshimu kila mtu kwa nafasi yake,thamani ya mtu ilikuwa ni watu na siyo yeye peke yake.

Mkubwa alipaswa kumsaidia Mdogo kujifunza kivitendo kwa kuangalia kinachofanywa na wakubwa na yeye kufanya.
Utii haukuwa utumwa ila ulikuwa ni sehemu ya kuthaminiana ambapo Mkubwa hakulazimisha kuonekana kuwa ni mkubwa na Mdogo hakulazimishwa kumheshimu mkubwa ila misingi ya utu na kuheshimiana ilikuwa kama imani.
Kuwa na mali au vitu vingine hakukufundisha Uafrika kuzalisha matabaka yaani mwenye nacho na asiye nacho kwa sababu misingi iliiimarishwa katika kushiriki ambapo kila mwanajamii alipaswa kushiriki katika kazi na vilevile kufaidi matunda ya kazi hiyo kwa pamoja.

Kiongozi aliheshimiwa kwa nafasi yake na siyo utisho wake kwa anaowaongoza,hakukuwa na haja ya kiongozi kujitambulisha kuwa yeye ni Kiongozi au ana uwezo gani kwa sababu jamii ilimtambua na kutambua nafasi yake halikadhalika wanajamii nao walijua wajibu wao kwa a anayewaongoza.

Mfumo wa maongezi jamii na upashanaji habari kwa njia ya mazungumzo hai "social constructive dialogue"ndiyo uliobeba dhima kubwa katika falsafa hii.

Leo viongozi mnatujengea mambo tofauti sana na falsafa hii ya Ujamaa wa Kiafrika kwa kutanguliza ubinafsi na kujikweza.

Nadharia za uongozi zinatukumbusha kuwa mamlaka ya Kiongozi inatokana na kitendo cha mwanajamii mmoja mmoja kukasimisha mamlaka yake kwa kiongozi.Kwa maana hiyo mamlaka ya viongozi inatokana na ukasimishwaji wa mamlaka kutoka kwa kila mwanajamii.

Tatizo viongozi wetu leo wanaamini mamlaka waliyonayo ni yao na siyo zao la mamlaka za wanajamii mmojammoja.
Mtu hawi kiongozi nje ya mfumo wa ukasimishwaji wa mamlaka iwe kinguvu au hiari ndiyo maana mamlaka ya kiongozi haitokani na kiongozi ila inatokana na zao la mamlaka ya mwanajamii mmojammoja iliyokasimishwa.

Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere aliwahi kusema..."kazi ya kiongozi ni kuunganisha watu na siyo kuwagawanya".

Msingi wa hoja hiyo ni nadharia ya ukasimishwaji wa mamlaka ambapo kiongozi hukasimishwa mamlaka ya mwanajamii mmojammoja (wote) na siyo kudi fulani tu la watu na hii ndiyo maana ya maana ya "..uongozi ni dhamana".Ni dhamana kwa sababu Wanajamii ndiyo waliomdhamini kiongozi wao kwa kumkasimisha mamlaka zao.

Kiongozi yeyote yule kwa namna moja au nyingine amedhaminiwa na wanajamii hata kama ni uongozi wa kuteuliwa kwa sababu anayeteua naye napata mamlaka kutokana na hukasimishwa mamlaka za wanajamii.

Viongozi wanapaswa kukumbuka mara zote kuwa lengo lao kuu ni kuweka utaratibu mahali pasipo na utaratibu "to bring order out of chaos".Hii inatokana na ondoleo la jamii ya asili ilivyokuwa ikiishi pasi na ukasimishaji wa mamlaka ambapo kila mmoja aliweza kufanya chochote dhidi ya yeyote "The state of war of all against all".

Uhuru huo usiokuwa na mipaka "Natural state"ulionekana kuwa sababu ya kutaka pawepo na utaratibu wa kusimamia mipaka ili kuondoa vita ya kila mtu dhidi ya kila mtu.

Natamani kuhitimisha andiko hili kwa kusema"thamani ya mtu ni watu na siyo vitu,jifunze toka kwa kila mtu bila kujali hali yake ilivyo,yeyote yule a aweza akawa Mwalimu kwako katika Dunia hii yenye mengi ambayo hayupo ayajuae yote hata kama akisoma kwa miaka yake yote,Dunia ni Darasa wazi na yeyote anaweza kujifunza au kufundisha".
 
Back
Top Bottom