Uzoefu wangu na Sharp Financial Limited (Flexi cash)- Naombeni ushauri

Uzoefu wangu na Sharp Financial Limited (Flexi cash)- Naombeni ushauri

Chicho_

Member
Joined
May 15, 2024
Posts
8
Reaction score
4
Ndugu wanajamii,
Napenda kushiriki uzoefu wangu na Sharp Financial Limited, inayofanya biashara kwa jina la Flexi Cash, pamoja na changamoto ninazokutana nazo katika kutafuta ufumbuzi kupitia mamlaka husika.

Nilinunua simu kutoka kampuni hii tarehe 19 Januari mwaka huu, nikiambiwa ni mpya. Siku ya pili ya matumizi, niligundua taarifa zilizobaki ndani ya simu — ikiwemo anwani za email na namba za simu ambazo si zangu — zikionyesha dalili kuwa kifaa hicho kilishatumiwa na mtu mwingine kabla. Niliwasiliana na huduma kwa wateja kwa simu na barua pepe, lakini majibu niliyopata hayakulenga kutatua tatizo wala kuridhisha.

Niliwasilisha malalamiko rasmi Benki Kuu ya Tanzania (BOT) kupitia Kitengo cha Malalamiko ya Watumiaji (FCRS), yenye namba ya kumbukumbu FCRS/BOT/2026/00021. BOT waliagiza Sharp Financial kunipatia nakala ya mkataba ndani ya siku 7 — agizo ambalo halikutekelezwa kwa wakati, kwani nilipokea mkataba huo baada ya siku 14.

Tarehe 9 Aprili niliwasilisha ombi la mapitio (review), na tarehe 28 Aprili tulifanya kikao cha mtandaoni pamoja na Mawakili wa BOT na Sharp Financial. Toka wakati huo, sijapata uamuzi wala taarifa ya maendeleo, licha ya kuandika barua pepe zaidi ya tatu kufuatilia. Sheria za BOT zinaeleza kuwa maamuzi yanapaswa kutolewa ndani ya siku 45 — lakini mpaka sasa muda huo umeshapita.

Kutokana na kuchelewa kwa mchakato wa kiutawala, nimepanga kuwasilisha shauri hili mahakamani.
Pia nimeandikia Tume ya Taifa ya Ushindani (Fair Competition Commission) kwa msaada wa ziada.

Lengo langu ni kuwaonya wateja wengine wawe waangalifu wanaponunua vifaa kwa mikopo.

Je?, kuna aliyepitia hali kama hii na Flexi Cash? Na je, kuna mwenye ushauri wa jinsi ya kuharakisha majibu kutoka BOT?

Ahsanteni kwa muda wenu, na nakaribisha maoni na uzoefu wenu.
 
Back
Top Bottom