Uzinduzi wa Ndege za ATCL: Kutoka Uwanja wa JNIA eneo la Tanzania Government Flight Agency

barafu

JF-Expert Member
Apr 28, 2013
6,726
32,818
1.jpeg
2.jpeg


Rais Magufuli amesema kuwa Serikali iko kwenye mpango wa kununua ndege nyingine mbili kubwa zenye uwezo wa kubeba watu 170 na nyingine watu 240

Hatimaye ile siku imewadia,leo ndio uzinduzi rasmi wa ndege mbili za TGFA zitakazokodiwa na ATCL kwa ajili ya matumizi ya usafiri wa ndani na nje ya nchi.Zaidi ya ndani ya mipaka ya Tanzania,ndege mpya za ATCL zinatazamiwa kuwa na "route" ya kuelekea Hahaya-Commor ambapo imekuwa na soko la uhakika hata wakati ikiwa na ndege moja tu.

Uzinduzi huo unategemewa kufanywa na Rais wa JMT Mh.John P. Magufuli.Eneo la ufunguzi litakuwa ni eneo la maegesho ya Wakala wa Ndege za Serikali(Tanzania Gvt Flight Agency)maandalizi ya uzinduzi huo yanaendelea na tayari ndege hizo zimetolewa eneo la "Apron" ya JWTZ-Air Wing na kuletwa TGFA.

Waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali vya habari,wafanyakazi wa taasisi mbalimbali zinazofanya kazi uwanja wa ndege kama TAA,TGFA,TCAA,Swissport,Precision,ATCL,Police,State Security,JWTZ-Airwing na TMA watawakilisha raia wengine.

Kwa sbb za kiusalama na unyeti wa eneo,itakuwa ngumu kwa raia wengi kutoka nje bila kibali na vitambulisho kuingia moja kwa moja.Mpaka sasa utepe na eneo la kufanyia uzinduzi lipo tayari....Tutaendelea!!!

Hatimaye agizo limetoka na Raia wameruhusiwa kuingia na tayari kwa kumsubiri Rais anayetarajiwa kufika saa nne na nusu

======

UPDATES;



=> Waziri Prof. Mbarawa: Tangu ATCL ilipoundwa, haijawahi kununua ndege mpya, imekuwa ikikodi ndege kwa gharama kubwa-

=> Waziri Prof. Mbarawa: Tumekaa wizarani tukapendekeza ndege hizi ziitwe 'Hapa Kazi Tu' kwa sababu zimenunuliwa kipindi hiki.

=> Ndege hizi zitatua katika viwanja vifuatavyo;

- Dar es Salaam

- Z'bar

- Dodoma

- Arusha

- Bukoba

- Kigoma

- Tabora

- Kilimanjaro

- Mbeya

- Mtwara na

- Comoros

=> Rais Magufuli: Lakini unaweza ukajiuliza, ndege hii imetoka Canada imefika hapa, watu wanasema hazina spidi, ni bajaji.

=> Rais Magufuli: Ndege hizi hazitumiki tu Tanzania, Marekani wana ndege zaidi ya 40 za aina hii, Misri wanazo-

=> Rais Magufuli: Ukitaka kujenga uchumi, kuinua utalii, huwezi kufanya kama taifa halina ndege- Rais

=> Rais Magufuli: Ndege ya Jeti, kutoka Dar hadi Mbeya mafuta ni milioni 28, lakini hizi ni milioni moja

=> Rais Magufuli: Kama mtu anaona ana haraka sana ya kuwahi anapokwenda, akapande ndege za jeshi awahi

=> Rais Magufuli: Kutoka Dar hadi Mbeya, tofauti ya muda wa kufika kati ya ndege hii na Jet ni dakika 20 tu-

=> Rais Magufuli: Niwaombe watanzania tusipende kubeza, kama kitu hukitaki, basi ukae kimya

=> Rais Magufuli: Tungenunua ndege hizi kwa kulipa polepole, tungekuja kulipa gharama kubwa, ndio maana tumelipa zote

=> Rais Magufuli: Tuna mpango wa kununua ndege mbili kubwa, moja itabeba watu 160, nyingine itabeba watu 240

=> Rais Magufuli: Tuliamua kununua ndege, tutazikodisha kwa ATCL, mwendo wa kucheza sasa umekwisha

=> Rais Magufuli: ATCL ilikuwa haijiendeshi kibishara, walikuwa wapo tu, wanategemea serikali kila kitu

=> Rais Magufuli: ATCL haikuwa ikijenga uchumi wa nchi na utalii kama ilivyokuwa inatakiwa

=> Rais Magufuli: Maofisa wa ATCL walikuwa wakijilipa posho za TZS 50,000 kila wakitembelea uwanja wa ndege Dar-

=> Rais Magufuli: Vituo vya ATCL vya Comoro, Mwanza, Mtwara na Dar es Salaam, vilikithiri kwa ubadhirifu

=> Rais Magufuli: ATCL walikuwa hawafuati ratiba, unaweza kuambiwa ndege inaondoka leo, lakini isiondoke hadi wiki moja

=> Rais Magufuli: ATCL walikuwa wakijilipa overtime za uongo

=> Rais Magufuli: ATCL walikuwa wakinunua mafuta hewa, unaambiwa ndege imeenda Mwanza kumbe iko Dar es Salaam uwanjani

=> Rais Magufuli: Katika kituo cha Comoro, ilipotea TZS milioni 700, aliyepoteza akaongezewa muda ili apoteze nyingine

=> Rais Magufuli: Bodi ya ATCL naomba mchambuwe wafanyakazi, chambueni kama Saida Karoli anavyosema, chambua kama karanga

=> Rais Magufuli: Bodi ya ATCL msiogope kupunguza wafanyakazi, tulipunguza 500 wa NIDA, hawa hawatatushinda

=> Rais Magufuli: Mfanyakazi kama unataka kuendelea kufanya kazi ATCL, utubu, uwe tayari kuwatumikia watanzania

=> Rais Magufuli: Ndani ya ATCL kuna wake wa Mawaziri, Shirika halizalishi lakini wake wa Mawaziri wameng'ang'ani tu

=> Rais Magufuli: Wale ambao hawawezi kwenda na mwendo wetu, waje tuwalipe fedha zao watuache tufanyekazi

=> Rais Magufuli: Haiwezekani wageni wakitaka kuja Tanzania, lazima watue nchi nyingine, hii ni aibu kubwa

=> Rais Magufuli: Lakini mjue mnaenda kwenye ushindani, washindani wenu hawatawafurahia, mjipange vizuri kuwakabili-

=> Rais Magufuli: Niwaombe Bodi ya ATCL, msitumie mawakala kukatisha tiketi zenu

=> Rais Magufuli: Kuna wafanyakazi wa ATCL naona wapo wanafanya kazi tangu mimi nipo shule ya msingi

=> Rais Magufuli: ATCL ya sasa ukiona hata sare za wafanyakazi zinatia kichefuchefu, hazitamaniki

=> Rais Magufuli: Lakini niwaombe Watanzania tuwe wazalendo, tutumie usafiri wa ATCL ili tuweze kununua ndege nyingine

=> Rais Magufuli: Niwaombe Bodi na Menejimenti, msimruhusu kiongozi asafiri bure, hata kama ni mimi, mnitoze nauli

=> Rais Magufuli: Najua kunawakati ATCL mnajipendekeza kwa viongozi, lakini mjue mwishoni tutawapima kwa utendaji wenu

=> Rais Magufuli: Hata kama ni kiongozi wa ATCL, ukisafiri hakikisha unalipa nauli, vitu vya bure ndivyo vinatumaliza-

=> Rais Magufuli: Sasa tuna kazi ya kukarabati viwanja, shughuli hii tutaianza mapema sababu fedha tunazo

=> Rais Magufuli: Sisi hatutaki kufukuza wafanyakazi, lakini watajifukuzisha wenyewe kutokana na utendaji wao

=> Rais Magufuli: Ujenzi wa reli ya kisasa kutoka Dar- Mwanza- Kigali- Bujumbura tayari tenda zimetangazwa

=> Rais Magufuli: Tunataka kuanza ujenzi wa treni za umeme Dar es Salaam, haya si Ulaya tu, hata hapa yatafanyika

=> Rais Magufuli: Ujenzi wa daraja la Coco Beach hadi Agha Khan umeanza, Interchange ya Ubungo itaanza karibuni

=> Rais Magufuli: Mkoa wa Dar es Salaam, una jumla ya wanafunzi hewa 7000, Wafanyakazi hewa wapo 17,000

=> Rais Magufuli: Hii nchi ilikuwa imefika pabaya, kila kona ukigeuka ni hewa, hewa, hewa

=> Rais Magufuli: RAS, DED tuliowafukuza jana, leo wamefikishwa mahakamani, hii imesaidia Uingereza kutuchangia bilioni 6

=> Rais Magufuli: Uingereza imetuchangia bilioni 6 sababu wameona wakitupa fedha zao zitafika kwa walengwa kule Kagera

=> Rais Magufuli: Tunakagua vyeti ili kujua viwango vya elimu na sehemu watu waliposoma, lengo si kuwafukuza wafanyakazi

=> Rais Magufuli: Ndugu zangu kazi hii ni ngumu, Mawaziri msiwaone, hawana raha hawa

=> Rais Magufuli: Waandishi wa habari, ninyi ni muhimili kama ilivyo Bunge, tusaidiane tunapochukua hatua-

=> Rais Magufuli: Waandishi wakati mwingine mnaandika habari za uongo kama nyie mna mahali pengine pakuishi ila si hapa

=> Rais Magufuli: Watanzania mjue, tukishindwa sisi, tumeshindwa sote, tukiweza tumeweza wote

=> Rais Magufuli: No research, no right to speak, lakini hapa ni kinyume, watu hawajui lakini wanaongoza kuongea

=> Rais Magufuli: Kama kungewezekana mtu ukiwa Rais baada ya miaka miwili na nusu unamuachia mwingine, mimi ningefurahi-

=> Rais Magufuli: Natamani huyo aliyesema hazina spidi nimjue nimlipie nauli akae mbele aone zinavyokata mawingu-

=> Rais Magufuli: Ninaishukuru CCM kwa kuandika ilani inayotekelezeka, naamini tutafanya zaidi

=> Rais Magufuli: Mungu ibariki ATCL, Mungu bariki Bodi ya ATCL, Mungu bariki wafanyakazi wazuri, Mungu ibariki Tanzania

Rais anaelekea kwenye zoezi la uzinduzi wa ndege mbili mpya za Serikali, Bombardier Q-400.

Rais Dkt Magufuli amezindua rasmi ndege mbili za serikali, hafla inayoendelea katika uwanja wa JNIA, Dar es Salaam.

Ndege hizi zinachukua abiria 76, ambapo 6 ni daraja la juu (Business class) na 70 ni daraja la chini (Economy class).

======

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 28 Septemba, 2016 amezindua ndege mpya mbili aina ya Bombardier Dash 8 Q400 zilizonunuliwa na Serikali kwa ajili ya kutumiwa na Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL).

Uzinduzi wa ndege hizo za kisasa zilizotengenezwa nchini Canada, umefanyika katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na Viongozi mbalimbali wakiwemo Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Job Ndugai, Balozi wa Canada hapa nchini Mhe. Ian Myles, Mawaziri, Wabunge, Viongozi wa Wafanyabiashara, Taasisi mbalimbali na wadau wa usafiri wa anga.

Kabla ya kuzindua ndege hizo zenye uwezo wa kubeba abiria 76 kila moja, Rais Magufuli ameshuhudia makabidhiano ya mkataba wa ukodishaji wa ndege hizo kutoka kwa Katibu Mkuu Kiongozi Balozi John Kijazi kwa niaba ya Wakala wa Ndege za Serikali (TGFA) kwenda kwa Katibu Mkuu Uchukuzi Dkt. Leonard Chamriho kwa niaba ya Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL).

Taarifa ya ununuzi wa ndege hizo iliyotolewa na Katibu Mkuu Kiongozi Balozi John Kijazi imeeleza kuwa ndege hizo ni mali ya Serikali na zitakodishwa kwa Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL) kwa lengo kutoa huduma za usafiri wa anga ndani na nje ya nchi.

Imeongeza kuwa ndege hizo zimenunuliwa kwa kuzingatia kuwa zinafaa kufanya kazi katika mazingira ya Tanzania ikilinganishwa na ndege nyingine za jamii yake, na imetaja manufaa hayo kuwa ni pamoja na uwezo wa kuruka na kutua katika viwanja vya lami na visivyo vya lami, matumizi madogo ya mafuta, kuwa na injini zenye nguvu zaidi na kubeba mzigo mkubwa.

"Ni dhairi kuwa ndege hizi zitaimarisha mtandao wa huduma za usafiri wa anga kwa soko la ndani, lakini pia zitaongeza ushindani na kuleta unafuu wa bei kwa watumiaji wa usafiri wa anga, vilevile zitaimarisha sekta za biashara na uwekezaji na kuwezesha watalii kutembelea vivutio vya ndani ya nchi" ameeleza Balozi Kijazi.

Kwa upande wake Rais Magufuli ameelezea kufurahishwa na kutimia kwa ahadi aliyoitoa ya kununua ndege mpya ili kufufua usafiri wa anga kupitia ATCL na ameahidi kuwa Serikali imeanza mazungumzo ya kununua ndege nyingine mbili zitakazofanya safari za ndani na nje ya bara la Afrika ambapo moja itakuwa na uwezo wa kubeba abiria 160, na nyingine itakuwa na uwezo wa kubeba abiria zaidi ya 240.

"Kwa sababu fedha za kununulia ndege hizo zote mbili kubwa zipo, tukinunua ndege ya kubeba watu 240 itakuwa inatoka hapa Dar es Salaam hadi Marekani bila kutua popote, itaondoka hapa Dar es Salaam mpaka China bila kutua popote ili watalii wanaotoka China, Marekani, Urusi, Ujerumani na nchi nyingine wasifikie nchi nyingine, watue hapa moja kwa moja na waangalie maliasili zetu tulizonazo, utalii wetu upande, na huo ndio mwelekeo wa nchi yetu tunaoutaka" amesema Rais Magufuli.

Rais Magufuli amewataka Watanzania kuunga mkono juhudi zinazofanywa na Serikali katika kuleta mabadiliko yenye manufaa kwa nchi na kuwapuuza watu wanaobeza juhudi hizo wakiwemo waliobeza ununuzi wa ndege hizo kwa kujenga hoja zisizo za msingi.

Aidha, Dkt. Magufuli ameitaka Bodi na Menejimenti ya ATCL kufanya kazi kwa weledi na ufanisi huku akiisisitiza kuondoa kasoro zote zilizosababisha kampuni hiyo kudorola ikiwemo kuchuja na kuwaondoa wafanyakazi watakaoshindwa kuendana na mwelekeo unaostahili, wasio waadilifu na waaminifu, wasaliti na wahujumu.

Rais Magufuli pia amewataka Watanzania wote wafanyabiashara, wakulima na wafanyakazi kusafiri kwa kutumia ndege hizo ili Kampuni ya ATCL ijiimarishe na iweze kujiendesha badala ya kutegemea ndege za Serikali.

Gerson Msigwa

Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU

Dar es Salaam

28 Septemba, 2016
a52.jpg
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli akiwa na maafisa na viongozi wengine mbalimbali akikata utepe kuzindua rasmi ndege mbili mpya aina ya Bombadier Q400 zilizonunuliwa na serikali kwa ajili ya Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Dar es salaam leo Jumatano Septemba 28, 2016
a56.jpg

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli na mkewe Mama Janeth Magufuli pamoja na maafisa wengine waandamizi wakiwa kwenye ndege mojawapo baada kuzindua rasmi ndege mbili mpya aina ya Bombadier Q400 zilizonunuliwa na serikali kwa ajili ya Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Dar es salaam leo Jumatano Septemba 28, 2016
a75.jpg
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli, Mama Janeth Magufuli pamoja na viongozi wengine waandamizi katika picha ya kumbukumbu na Brass band ya Polisi mara baada ya Rais Magufuli kuzindua rasmi ndege mbili mpya aina ya Bombadier Q400 zilizonunuliwa na serikali kwa ajili ya Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Dar es salaam leo Jumatano Septemba 28, 2016
 
Kwa sbb za kiusalama na unyeti wa eneo,itakuwa ngumu kwa raia wengi kutoka nje bila kibali na vitambulisho kuingia moja kwa moja


Kwanini vyombo vya habari vimehamasisha wananchi kujitokeza kwa wingi wakati hawataruhusiwa kwenda kuona uzinduzi
 
Back
Top Bottom