Uzimwe usizimwe Zanzibar i gizani

aleesha

JF-Expert Member
Oct 17, 2016
792
1,144
Tangu Rais John Magufuli wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (SMT) atowe kauli yake ya kulitaka Shirika la Ugavi wa Umeme la Tanzania Bara (TANESCO) kuwakatia wadaiwa wake sugu, ikiwemo Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), khofu iliyochanganyika na dhihaka za mitandaoni (meme) imeenea ndani na nje ya mipaka ya Jamhuri hiyo kupitia watumiaji wa mitandao ya kijamii.

Kisha akaja Dk. Ali Mohamed Shein kutilia kasi zaidi dhihaka kwa kauli yake kwamba serikali anayoiongoza haitishiki na kitisho hicho cha kuzimiwa umeme kwa sababu ya deni la shilingi bilioni 121 (baadaye TANESCO ilirekebisha ikisema ni shilingi bilioni 127.8), haamini kuwa kitatekelezwa na kwamba hata kama kitatekelezwa, basi Zanzibar itakachofanya ni kurudi tu kwenye matumizi ya kibatari.

Miongoni mwa dhihaka hizo ni picha za vibatari vikiwaka kwenye giza totoro, katuni zikionesha matayarisho ya Zanzibar kuingia gizani, na tungo kadhaa za ushairi pamoja na nyaraka. Mojawapo ni utungo huu wa kukinasihi kibatari kimsamehe mtumiaji wake, ambaye alikuwa amekitupa siku nyingi kwa kuutegemea umeme ambao si wake:

“Ewe wangu kibatari
Utulize moyo wako
Wewe bado u mzuri
Liondowe sononeko
Umeme ulinighuri
Kukusahau mwenzako
Lakini sasa tayari
Takutafuta uliko!”

Mwangwi wa yanayoandikwa kwenye mitandao ya kijamii, na ambayo ni hoja yangu kwamba yanaakisi yanayosemwa mitaani miongoni mwa watu wa kawaida, unafanana na yale anayoyasema Dk. Shein. Wote hawaamini kuwa Tanzania Bara itatekeleza kitisho hiki cha kuizimia umeme Zanzibar ifikapo tarehe 30 Machi 2017, hata kama itakuwa haijalipwa hata nusu shilingi!

Lakini sababu za kutoamini hivyo zinatafautiana kati yao na katika tafauti hizo ndipo palipo na giza kubwa zaidi kuliko giza la kuzimiwa umeme. Giza la kwanza liko upande wa Dk. Shein na wenziwe waliowekwa madarakani visiwani Zanzibar, hapana shaka, kwa msaada mkubwa wa hao wenye kutishia kuwazimia umeme.

Kwao, kauli za Rais Magufuli na baadaye TANESCO ni vibao vya uso vinavyowatia vimurivimuri na kuwaletea giza. Hawakutazamia hata siku moja kwamba kuna siku kaka mkubwa atawashambulia hadharani kwamba wanadaiwa na hawalipi madeni yao, tena sauti hiyo ikitoka kwa kiongozi mkuu wa chama chao aliye pia amiri jeshi mkuu wa nchi, tena kwa tuni ya jazba, kiburi na jeuri. Walitarajia kwamba watasitiriwa aibu zao kama watendewavyo siku zote kwenye mengine yote, zikiwemo njia zinazowaweka madarakani kila baada ya uchaguzi.

Lakini giza jengine kwao wao ni upande wa waliokaa kifikra – ni upande wa gizani. Kwa vipi? Kwa kuwa hauakisi uhalisia wa mambo. Kwa nini? Kwanza, Shirika la Umeme la Zanzibar (ZECO) halina upungufu wa wateja ambao wanawalipisha kwa gharama kubwa umeme wanaowauzia. Mtumiaji wa kawaida wa umeme visiwani Zanzibar ni mlipaji mzuri kwa huduma anayopokea kutoka kwa shirika hilo la serikali. Kwa nini mkusanyajiwa fedha hizo asizifikishe zitakiwako? Kuna giza gani lililoziba pasionekane fedha ziendapo.

Upande huu wa kifikra uko gizani pia kwa kuwa unashindwa kuiona Zanzibar kama Zanzibar. Wanashindwa kuviona vyanzo vingi vya nishati mbadala vilivyonavyo visiwa hivi, wanashindwa kuwaona watu kibao wenye dhamira na uwezo wa kuwekeza kwenye nishati hiyo na hawawezi kuziona nguvu za kutosha kuweza kusimama wenyewe kwenye eneo la nishati, kwa kuwa wako upande wa kifikra ulio gizani.

Giza lililosababishwa na mfumo wa kutawaliwa ndilo lililoigubika nchi hii kiasi cha kwamba haiwezi kujishika zaidi ya kujishikiza. Ni giza hili la mfumo wa kutawaliwa, kwa hakika, ndilo linalompa Dk. Shein imani ya kwamba hakuna siku mtawala mwenyewe atathubutu kuchukuwa hatua ya kuuzima umeme kwenye sehemu yake anayoitawala, maana kufanya hivyo hakutakuwa na maslahi kwa mtawala huyo. Bali pia ni mfumo huu wa kutawaliwa ndio ulioweka giza kwenye kichwa cha mtawaliwa asiweze kuona chengine chochote zaidi ya kile kinachowashiwa taa na mtawala.

Nakusudia kuwa andasa ya kuwa chini ya himaya ya mtawala, kunawafanya hata walio madarakani visiwani Zanzibar kushindwa kuwaza nje ya mduara huu wa kutawaliwa. Ni kinyume cha kinyume kwamba aliye madarakani naye ana mtawala wake, lakini ndio uhalisia hasa wa hili giza lenyewe ninalolizungumzia hapa.

Giza hili lina upande mwengine pia. Nalo ni upande wa wananchi wa kawaida, ambao maoni na mawazo yao yameakisika kwenye kile wanachokizungumza mitandaoni hivi sasa, tangu Rais Magufuli na Dk. Shein watowe kauli zao. Kitu kimoja unachokumbana nacho moja kwa moja unapoyasoma baina ya mistari yale yanayosemwa na wachangiaji hawa, ni ukweli kwamba wanataka hasa Zanzibar ikatiwe umeme na kweli irudi kwenye matumizi ya kibatari, kama alivyojiapiza Dk. Shein.

Mmojawapo, aliyejiita Al Habshy, ‘amemuandikia’ barua refu Rais Magufuli akimtaka asije akachelewa hata nusu siku kuchukuwa hatua ya kuuzima umeme. Mahala pamoja kwenye barua hiyo, anaandika hivi:

“Mheshimiwa Rais, ikumbukwe hawa washazowea ubwanyenye, hivyo hata uwape karne, basi deni hawalipi. Ni nyingi sana. Mtu anakwambia huwezi kukata umeme, kwani kashajiandaa na kibatali? Kwa maana halipi kwa makusudi kwa kuwa ameshajiandaa na yatakayojiri. Kwa kweli wanakutania. Kwani tangu lini umeanza utani na wao?”

Na huyu si pekee. Wengi wengine wamechangia kwenye mitandao ya kijamii kwa dhihaka na mizaha kama hii, ambayo inaashiria kuichongea SMZ ya Dk. Shein kwa SMT ya Rais Magufuli. Inashangaza na kushitusha sana kuona kwamba Wazanzibari wanaoishi ndani ya Zanzibar yenyewe wanafikia mahala pa kutamani kuiona Zanzibar yao inatumbukia gizani.

Lakini unapojiuliza swali la kwamba je, ni kweli wanataka TANESCO iwakatie umeme? Jibu nii kwamba hawataki ukatwe umeme kwa maslahi tu ya kukatwa kwake, bali wanataka ukatwe kwa minajili ya kuwathibitishia wanaounga mkono utawala (mfumo wa Muungano uliopo) kuwa wako upande usio sahihi.

Wanataka ukatwe ili kuthibitisha kuwa serikali zinazoongozwa na Chama cha Mapinduzi (CCM) kwenye pande zote mbili za Muungano, zimeshindwa kumuhudumia mwananchi wa kawaida. Wanataka umeme uzimwe ili sehemu fulani ya watu ikomolewe, tabaka fulani liaibike na jambo fulani lidhihirike hata kama nchi nzima itaumia kwa ujumla wake.

Kwamba imefika mahala ambapo mwananchi wa kawaida yuko tayari abebe machungu mazito na ateseke kwa machungu hayo, ili tu amthibitishie mtawala wake kuwa hayuko sahihi, hafai na, au, hana uwezo wa kumuongoza inavyostahiki, hakika ni kipimo cha mahala pabaya sana ambapo sasa nchi yetu imefikia. Mahala hapo ndipo ninapopaita gizani. Gizo zito. Giza totoro. Giza limetanda pande zote.

Giza hili kwa upande wa wananchi linamaanisha ukosefu wa Imani wa kiwango cha juu walichonacho kwa serikali iliyopo madarakani, ambayo wanaamini haipo kwa ajili yao, haikutokana na wao na si sehemu yao. Giza la kujitenga na mfumo na kujiweka mbali na chochote ambacho kina mkono wa mfumo huo.

Watu hawa hawana nguvu wala hila za kukabiliana na mfumo huu, lakini katikati ya giza walilomo wanatumia silaha ndogo ya puuzo na dhihaka. Mwanaadamu anapoamua kuyadharau mashaka yaliyopo mbele yake, anapoamua kumpuuzia anayemuona ni dhalimu wake, akaamua kuwa njia pekee ya kushughulika naye ni kumdhihaki, basi ujuwe amechaguwa silaha ndogo kabisa lakini yenye nguvu kubwa mno sizisoweza kushindwa kwa bunduki wala mzinga. Na hicho ndicho kinachosomeka kwenye kadhia hii.

Katika yote haya, mwelekeo wangu ni kwa waliopo madarakani visiwani Zanzibar. Njia munazotumia kujiweka madarakani zenyewe ni njia za giza na zinazolidumisha giza, na ndio msingi wa magiza mengine yote. Kwa hivyo, hata kama TANESCO haitazima umeme wake, bado mujuwe kuwa nchi imo gizani.

Hakuna giza kubwa zaidi ya giza la nafsi, ambalo sasa limeigubika Zanzibar. Liondosheni giza hili kubwa kwanza ndipo muondoshe viza vyengine viduchuduchu, kikiwemo kiza cha kukosa umeme wa TANESCO.

Mukiweza kuliondosha giza hili kuu, mutakuwa na Zanzibar inayojiamini kuzungumza kama Zanzibar mbele ya yeyote, akiwemo huyo mwenye TANESCO. Mutathubutu kumuambia kuwa muliingia naye makubaliano kwenye kuuziana umeme, ambayo yaliipa Zanzibar wajibu wa kugharamika kwenye usambazaji nyaya na nguzo na pia kuihudumia mitambo ya kukusanyia na njia za kusambazia umeme ndani ya ardhi ya Zanzibar. Hivyo nyinyi hamuwezi kuuziwa wala kuchukuliwa kama wateja wa kawaida.

Mukiweza kuliondosha giza hilo kuu, mutapata uthubutu pia wa kupigiana hisabu ya madeni kati yenu na huyo mwenye TANESCO, sio tu kwenye haya ya umeme, bali pia kwenye mengine mengi ambayo munadaiana kwa nusu karne sasa, na hadi leo hisabu haijakaa sawa. Hisabu ya mgawo wa hisa za Benki Kuu ya Tanzania (BoT), hisabu za 4.5% kutoka misaada ya nje, hisabu za hisa za mashirika ya Posta na Simu, Shirika la Ndege, mbali ya fedha za kigeni na mgawo wa kodi itokanayo na ajira za Muungano ndani ya ardhi ya Zanzibar.

Na mwisho, mukiweza kuliondosha giza hilo kuu, mutaweza kuvitambua, kuvigundua na kuvifanyia kazi vyanzo vyenu wenyewe vya nishati ndani ya ardhi ya Zanzibar, na kama taifa lenu lilivyokuwa la kwanza kwenye Afrika ya Mashariki na Kati kwa kuwa na umeme wake lenyewe, ndivyo litakavyokuwa la kwanza kutegemea umeme wa nishati mbadala kwa kujiendesha. Na hizi si ndoto za mchana. Ni ukweli unaowezekana.

Tanbihi: Makala hii ilichapishwa kwa mara ya kwanza kwenye gazeti la Mwelekeo la tarehe 14 Machi 2017

Zanzibar Daima
 
Ninaamini Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ikipeleka ombi la kurudisha kiti chake UN watakubaliwa siku hiyo hiyo. Sijui nini kinawafanya wasiamke kutoka usingizini mapema. Labda wana hofu ya kuanza. Ila mwanzo wa kila kitu ni changamoto. Wanasubiri hadi wafukuzwe kwenye huu Muungano ndio wajitambue?? Shame
 
Unaandika maneno mengi hadi habari inapoteza mvuto na maana !!!
 
Aleesha,
Shukrani kwa makala iliyochambua masuala ya sayansi ya siasa na utawala bora ktk taifa lolote linalotaka kuwa na uongozi bora na nchi imara kiuchumi.

Wasomajji wa Jamiiforums tunafaidika sana na makala-chambuzi kama hii.
 
"Muungano ni kama koti tu, ukiona linakunyima raha basi unalivua, wazanzibar hatutishwi na hizo kelele za TANESCO, Uhuru wetu ni muhimu kuliko umeme wa masimango, Deni sio la leo wala la jana, deni hilo halilipiki na kamwe hatutalilipa hata senti tano, tumeshajipanga, mkikata umeme tutateseka kwa muda mfupi sana kwa kutumia vibatari, tupo kwenye mipango ya kufunga mitambo yetu ya kuzalisha umeme wetu, kuliko kulipa hizo bilioni zaidi ya 120 ni bora tukanunua mitambo yetu ya kudumu kwa pesa hizo."

NUKUU KUTOKA ZANZIBAR.
 
Shein aache kujilegeza.

Hata bakhresa mzanzibari mwenzao,tajiri mkubwa wakimwambia alete mitambo ya kuzalisha umeme kwa kushare na serikali,ni biashara ya mwaka au miezi umeme umefika,kutegemea cha kuazima kila siku unaadhirika na kuwa mtumwa

Ikumbukwe Zanzibar ni nchi ya kwanza afrika mashariki kuwa na reli na treni,nchi ya kwanza kuwa na taa za umeme barabarani hapa afrika mashariki.

Leo mmekuwaje?

Hebu changamsheni akili wazanzibari
 
amekoma na amesatubu hatakuja kurudia tena kuropoka chochote kuhusu Zbar! Hutakuja kusikia lolote
 
Back
Top Bottom