UZALENDO WETU NA MAPENZI YETU KWA VYAMA VYA SIASA.
Dunia imeagana na nyonga, inakwenda mbio sana. Kuna mambo unatamani yasimame kama yalivyo, yasibadilike. Lakini katu haiwezekani. Kuna watu unatamani waishi milele, lakini bahati mbaya au nzuri tuliumbwa kwa udongo na tutarudi kuwa udongo. Leo nimewakumbuka sana watu wanne maarufu ambao dunia ina rekodi zao.
Che Guevara, mwanamapinduzi kutoka Argentina anabaki kuwa mtu wa pekee sana katika ulimwengu huu. Huyu hakuwa tu mzalendo kwa taifa lake, bali uzalendo wake ulivuka mipaka. Che alikuwa mzalendo wa dunia. Mapenzi gani haya! Che aliiacha nchi yake na familia yake, na kuungana na Fidel Castrol kwa ajili ya ukombozi wa mwanadamu. Kwa Che ,kauli ya binadamu wote ni sawa, ilikaa moyoni mwake. Nakumbuka maneno mazito aliyoyazungumza wakati anaagana na pacha wake, Fideral Castrol. Nimekumbuka maneno yenye hisia kali, yaliyo kwenye barua ambazo alikuwa anamwandikia mke wake.Mwisho wa safari wake iliishia Bolivia.
Kuna huyu W.P.Botha, Rais wa Kwanza wa serikali ya kibaguzi ya Afrika Kusini. Wakati anahutubia baraza lake la mawaziri tarehe 18/08/1985, alisema kuwa binadamu wote, haimaanishi kwamba Waafrika (watu weusi) wako sawa na wazungu. Hii inabaki kuwa hotuba mbaya zaidi katika ulimwengu wa ubaguzi. Pamoja na maneno hayo kuwa makali sana, kuna ukweli kwa baadhi ya mambo. Kwa Wazungu (Afrika Kusini), Botha alikuwa mzalendo. Alikuwa tayari kulinda masilahi ya watu wake kwa namna yoyote.
Mwana Halisi wa Afrika, Patrice Emery Lumumba, kabla hajafariki (akiwa anashikiliwa na watesi wake) alimwandikia barua mke wake. Ile barua ilikuwa na hisia kali sana. Ulikuwa ujumbe mzito sana kwa nchi yake, kuliko hata familia yake. Baadaye Lumumba alitolewa roho kwa namna isiyosimulika. Patrice Lumumba anabaki kuwa mzalendo halisi katika harakati za kuikomboa Zaire (sasa DRC) na Afrika kwa ujumla. Hata upande wa pili, wanaamini kwamba waliomuua Lumumba walikuwa wazalendo.
Angalia usaliti alioufanya Compaure kwa nchi yake na kwa comrade Thomas Sankara. Sankara alionyesha mwanga kwa nchi yake na kwa Afrika. Kasi yake iliwatisha sana wazungu na vibaraka wake. Ndipo wazungu wakaunda mpango wa kumuua Sankara kwa kushirikiana na vibaraka kama Blaise Compaore.
Hapa ndipo nachanganyikiwa kuelewa maana halisi ya neno Uzalendo. Neno hili linatamkwa sana kwenye majukwaa ya siasa na wanasiasa. Pamoja na kwamba, neno hili linatumika sana, lakini ukweli ni kwamba linatumika kulingana na masilahi ya anayelizungumza. Nini maana halisi ya uzalendo kwa vitendo? Mipaka ya uzalendo iko wapi? Mtu kuipenda sana nchi yake, ndio uzalendo? Tunapimaje kwamba mtu anaipenda sana nchi yake? Tuchukue mfano wa Che, Sankara na Lumumba kuwa ndio maana halisi ya uzalendo?
Katikati ya hii tafakuri, nikakumbuka tukio moja. Mwaka 2007, kulikuwa na fukuto la Mkataba wa Buzwagi. Zitto Kabwe aliadhibiwa vikali, kwa kusema waziri wa nishati wakati huo, alisaini mkataba wa Buswagi Hotelini Londoni. Zitto kabwe aliitwa majina yote mabaya. Msaliti na mtu aliyekosa uzalendo. Kesi kama hizo zimejitokeza sana katika nchi yetu. Lakini mwisho wa siku inathibitika kwamba yaliyokuwa yanasemwa ni kweli. Katika hali kama hiyo, nani anakuwa mzalendo, aliyesaini mkataba ambao hauna masilahi kwa nchi au aliyefichua siri hiyo?.
Baada ya hapo, nimegundua kwamba tunatumia neno UZALENDO vibaya. Tunatumia neno hili, kwa masilahi binafsi (mara nyingi). UZALENDO au UTAIFA hauwezi kumilikiwa na mtu mmoja. Kila mtu anaweza kuwa mzalendo au vinginevyo kwa nafsi yake. Kila mwananchi anawajibika kuhakikisha nchi inakwenda mbele kimaendeleo. Maendeleo ya nchi hayawezi kuletwa na mtu mmoja.
Sambamba na hilo, UZALENDO lazima uambatane na ukweli. Kwa bahati mbaya sana, nchi za ulimwengu wa tatu, mambo ya ubeuzi ndio hupewa kipaumbele. Wakati mwingine unashindwa kuelewa nani mzalendo hasa, kati ya serikali na vyama vya upinzani. Kuna wakati inachanganya sana. Kama usipokuwa makini unaweza kujikuta unaegemea upande mmoja. Ni mambo gani wapinzani wanatakiwa kuyasema, na ni yepi hawatakiwi kusema? Je, kama kumetokea ubadhirifu wa mali za umma, vyama vya upinzani vinatakiwa kusemea wapi? Nini nafasi ya wananchi katika hilo? Kunyamaza kimya ndio uzalendo? Au kusema ndio usaliti au kinyume chake? Tatizo liko kwenye nini? Namna ya kusema au jambo lenyewe?.
Kuna hili, suala la vyama vya siasa. Neno vyama vya siasa nalo linachanganya. Kama utaita chama tawala, hapo ni sawa. Ni neno linaloeleweka. Lakini ukiita “chama cha upinzani” kuna ukakasi. Sijui kama tulikuwa tayari kuwa na neno “vyama vya upinzani”. Watu wengi wanaelewa kwamba vyama vya upinzani ni uhaini. Ili kutenda haki, pande zote mbili hazielewi maana ya siasa za vyama vingi. Upinzani wanaelewa kwamba kila wakati ni kupinga tu, hata kama kuna jambo jema linafanywa na serikali. Serikali yenyewe haivielewi kabisa vyama vya upinzani. Kila linalosemwa na upinzani inaonekana ni uchochezi na usaliti. Hapa neno uzalendo ndipo linajitokeza sana.
Kibaya zaidi watu wako tayari kupigana kwa ajili ya vyama vyao kuliko hata Taifa lao. Jamii imegawanyika katika makundi mawili. Kijani au magwanda!Hata jambo linalohusu Taifa/Nchi linajadiliwa katika mlengo wa vyama. Neno uzalendo hutumika kulinda masilahi ya chama badala ya Taifa. Tanzania hatuna tatizo la ukabila. Badala yake tuna tatizo la kupenda sana vyama vya siasa kuliko nchi/Taifa. Nikitazama mbele naogopa sana. Kizazi kijacho kitakuwa hatari sana, kama hili tatizo halitatuliwa.
Tuweke masilahi ya nchi/taifa mbele kuliko vyama vyetu. Sisi sote tuna wajibu wa kuona nchi yetu inasonga mbele. Uzalendo wetu uwe kuipenda nchi yetu. Kuipenda nchi yetu, ni pamoja na kutimiza wajibu wetu, ikiwa ni pamoja na kusema ukweli. Unafiki na uzalendo havifungamani. Kusema ukweli ni pamoja na kuipongeza serikali inapofanya vizuri, na kuikosoa inapofanya vibaya. Hata upande wa pili, tuwapongeze wanapofanya vizuri na tuwakosoe wanapofanya vibaya. Huu ndio uzalendo wa kweli.
“Mwanadamu aliyezaliwa na mwanamke siku zake za kuishi si nyingi, naye hujaa taabu. Yeye huchanua kama vile ua, kisha hukatwa, hukimbia kama kivuli, wala hakai kamwe. Hapa hatuna mji udumuo, bali twautafuta ule ujao. Kwa maana hatukuja na kitu duniani, tena hatuwezi kutoka na kitu. Uliumbwa kwa udongo, unarudi tena kuwa udongo kwa udongo, mavumbi kwa mavumbi”.Walazwe mahala pema peponi wote waliokufa wakitetea nchi zao (Che, Lumumba, Amical Cabral, Samora Machel, John Garang, Kwame Nkurumah, n.k).