SoC02 Utoaji holela wa leseni za udereva ni chanzo kikubwa cha ajali za barabarani

Stories of Change - 2022 Competition

MKAKA WA CHUO

Member
Aug 13, 2022
11
6
Udereva ni kitendo cha mtu kuendesha chombo cha moto kwa ajili ya kusafiri au kusafirisha watu au mizigo mbalimbali ya watu kutoka sehemu moja hadi sehemu nyingine. Mtu ambaye huendesha chombo cha moto kama vile pikipiki, gari na bajaji huitwa dereva. Kwa kawaida dereva ni mtu ambaye anaongoza safari katika chombo cha moto kama vile gari na vyombo vingine vya moto vya usafisiri.

Ili mtu awe dereva anatakiwa apate kibali cha kuendesha chombo husika kama pikipiki au gari. Kwa kawaida kuna utaratibu maalumu ambao umewekwa ili mtu anayehitaji kuendesha chombo cha moto aruhusiwe kuendesha chombo hicho ni lazima apitie taratibu na vigezo husika. Kibali ambacho mtu ambaye amekidhi vigezo vya kuwa dereva anapewa huitwa leseni , hii hutumika kama kibali halila cha kuendesha chombo cha moto kama vile gari na pikipiki. Kuna vigezo mbalimbali ambavyo mamlaka husika imeviweka ili vifuatwe wakati wa utoaji wa leseni za udereva hapa nchini, miongoni mwa vigezo hivyo ni kwamba muombaji wa leseni anatakiwa apeleke cheti cha mafunzo ya udereva ili kuhakikisha kwamba kweli muombaji wa leseni amehitimu mafunzo ya udereva.

Jambo linalosikitisha, kutokana na sababu mbalimbali ambazo mamlaka husika huenda Inakumbana nazo ikiwemo rushwa na vitu vingine kama hivyo kwa baadhi ya wafanyakazi wa mamlaka husika, kumepelekea tabia ambayo inaendelea kukua katika nchi yetu ambayo ina madhara makubwa sana hapa nchini, tabia hii ni utoaji wa leseni za udereva bila ya muombaji kuwa na cheti cha kuhitimu mafunzo ya udereva, kasumba hii hufanyika sana kwa madereva wa magari, wengi katika madereva wa magari ni kweli wana miliki leseni sahihi lakini changamoto kubwa ni kutokuwa na mafunzo yakutosha kuendesha magari hayo, jambo hili linachangia kwa kiasi kikubwa ongezeko la ajali za BARABARANI hapa nchini.

Ni muhimu kuzingatia hizi sheria za utoaji wa leseni za udereva kwa sababu, suala la kumpatia mtu leseni ya kuendesha gari bila ya kujua ana uwezo kiasi gani wa kuendesha hilo gari lenyewe ni kosa kubwa ambalo linaweza kuwa chanzo cha vifo vya watanzania wengi kutokana na ongezeko la ajali katika jamii zetu. Hali hii ya utoaji holela wa leseni za udereva inasababisha nchi na serikali yetu kuingia hasara mbalimbali kama vile kupotea kwa arasilimali watu kama vile walimu, wanafunzi,wanavyuo, madaktari, viongozi na wengine wengi kutokana na uwepo wa madereva wasio kuwa na ustadi mzuri wa uendeshaji wa magari husika.

Katika nchi kubwakubwa kama vile marekani, unapohamia kule kutoka nchi kama Tanzania, hata kama uwe umeenda kwa ajili ya kazi ya udereva na leseni yako ya TANZANIA unayo, hauwezi kuruhusiwa kuendesha gari mpaka wahakikishe kivitendo kwamba wewe unaweza kuendasha gari katika nchi yao, na huwa hawazingatii kabisa leseni kutoka katika nchi zetu hizi kama Tanzania labda kama mtu atakua na leseni ya kuendesha gari kimataifa kama kutakuwa na leseni ya mfumo huo, lakini takribani mara zote marekani huwa hawakubali leseni kutoka nchi nyingine mpaka wa hakikishe kabisa kwamba huyo mtu ni dereva mzuri na anaweza kuendesha gari bila kuhatarisha usalama wa watumiaji wengine wa barabara.

Kanuni au sheria hii inasaidia kwa kiwango kikubwa kupunguza ajali za barabara kwa sababu wengi katika madereva wa vyombo vya moto huwa wana uzoefu na ujuzi mkubwa wa kuendesha vyombo hivyo, hali hii ni kinyume kabisa na utaratibu au usimamizi uliopo katika nchi yetu , kwasababu takribani idadi nusu ya madereva huwa hawana ujuzi au uzoefu wa kutosha wa kuendesha vyombo husika, kwa mfano madereva wa pikipiki maarufu kama bodaboda, hawa ndio wamekuwa miongoni mwa madereva wanao sababisha ajali na vifo vingi katika barabara zetu hapa nchini, hii ni kutokana na kasumba ya kuwa wengi wao wanamiliki leseni za udereva wa pikipiki lakini hawana mafunzo ya kutosha juu ya uendeshaji wa pikipiki hizo.

Ikumbukwe ni muhimu kuhakikisha muombaji wa leseni anazifahamu sheria za barabarani kikamilifu na ana uwezo mzuri wa kuendesha chombo husika bila huhatarisha usalama wa watu wengine huko barabarani, jambo hili litasaidia kuhakikisha kupungua kwa ajali za barabarani kwa sababu ajali nyingi za barabarani zinasababishwa na watumiaji wa vyombo vya moto kutokuzijua au kutokuzifuata sheria za barabarani kikamilifu. Vilevile polisi wa usalama barabarani pia inawapasa wawe chachu ya usalama katika barabara zetu kwa sababu licha ya kuwa madereva wengi wanamiliki leseni lakini pia madereva haohao huwa hawafati sheria nyingi za barabarani, kwa wasimamizi wa usalama barabarani ni muhimu kusimamia sheria hizi kikamilifu ili kama taifa tuweze kuepuka au kupunguza matatizo yatokanayo na ajali za barabarani.

Mamlaka zinazohusika na utoaji wa leseni za udereva hazina budi kuhakikisha zinawapatia leseni za udereva watu ambao wana uwezo na ustadi mzuri wa kuendesha vyombo husika bila ya kuhatarisha usalama kwa watumiaji wengine wa barabara zetu, hii ni kwasababu kama taifa tumeshapata madhara mengi kutokana na utoaji wa leseni kinyume na utaratibu uliowekwa, vilevile sheria za barabarani zisimamiwe kikamilifu ili kupunguza upotevu wa Maisha ya watanzania kutokana na utumiaji usio sahihi wa vyombo vya moto. Kuna baadhi ya madereva wana endesha vyombo vya moto wakiwa wamelewa na wengine wanaendesha mwendo mkubwa kupita kiasi, hawa wote wanahatarisha Maisha yao na Maisha ya watumiaji wengine wa barabara, hivyo basi madereva kama hawa ni muhimu sana kushughulikiwa kikamilifu kabla hawajaleta madhara katika jamii yetu.

BY : MKAKA WA CHUO.
 
Back
Top Bottom