SoC03 Utawala bora na maslahi binafsi

Stories of Change - 2023 Competition

Sittrah Nkhambi

New Member
Jun 5, 2023
3
1
Utawala bora ni mchakato wa kupima jinsi taasisi za umma zinavyoendesha shughuli zake, kusimamia rasilimali za umma na kuhakikisha utekelezwaji wa haki za binadamu kwa njia ambayo kimsingi haina dhuluma na ufisadi kwa kuzingatia sheria.

Kulingana na Umoja wa Mataifa, Utawala Bora hupimwa kwa vipengele vinane ambavyo ni Ushirikirikishwaji, Utawala wa Sheria, Uwazi, Uwajibikaji, Mwelekeo wa Makubaliano, Usawa , Ufanisi na Uwajibikaji.

Maslahi binafsi ni hali ya kutumia nafasi ya uongozi au kazi kwa manufaa binafsi au kikundi cha watu fulani. mgongano wa maslahi ambao hauonekani moja kwa moja kwa Viongozi, watumishi wa umma au wafanyakazi kutokana na kutumia mbinu tofauti tofauti. Wengi wao wamekuwa wakitumia vyeo vyao kama miamvuli ya kujipatia wanachohitaji Mfano mali pamoja na kutengeneza jina au kujulikana. Maslahi binafsi yamekuwa na athari hasi katika Utawala Bora.

Katika katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Sura ya Sita, sehemu ya kwanza, Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora Sheria ya 2000 Na.3 ibara.17 namba 129(1) "Kutakuwa na Tume itakayoitwa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, ambayo majukumu yake yatakuwa kama ilivyoelezwa katika ibara ya 130 ya Katiba hii"

Katiba inaendelea kufafanua zaidi kuhusu ibara ya 129(6)" Kwa madhumuni ya kuwakinga Makamishna kutokana na migongano ya kimasilahi, mtu yeyote akiteuliwa kuwa Kamishna wa Tume atalazimika kuacha mara moja madaraka yoyote katika chama chochote cha siasa au madaraka ya aina nyingine yoyote." Kifungu hiki kinalinda maslahi ya kikundi fulani. Maslahi ya mtu binafsi hayajawekwa wazi wala kutolewa ufafanuzi zaidi. Vifungu hivi vya katiba vinafafanua juu ya maslahi. Je ni zipi athari zake katika nchi?

ATHARI ZA MASLAHI BINAFSI KATIKA UTAWALA BORA.
Kupungua kwa Umoja na mshikamano miongoni mwa wananchi. Mgongano wa maslahi binafsi kwa Viongozi umesababisha kuwagawa wananchi na viongozi katika makundi hivyo kupungua kwa Umoja na mshikamano kwani Katika kuijenga nchi lazima wananchi wawe kitu kimoja.

Kupungua kwa uwazi;Uwazi ni moja ya sifa ya Utawala Bora. Maslahi binafsi kwa baadhi ya viongozi na wafanyakazi kufanya shughuli za umma kwa siri hivyo wananchi kukosa haki yao ya msingi ya kujua kinachoendelea katika nchi yao au shirika husika.

Kupungua kwa Ushirikishwaji katika shughuli za umma au nchi; Maslahi binafsi kwa baadhi ya viongozi yamesababisha wananchi wakose haki zao za msingi za kushiriki katika shughuli za kiserikali, hasa katika kutoa michango juu ya bajeti au mikataba inayolenga maendeleo ya nchi.

Kuwepo kwa nidhamu ya Woga;Baadhi ya viongozi wamekuwa ni watu wa kufuata mkumbo kwa kuhofia kupoteza nafasi zao hasa za uteuzi. Hivyo kuogopa kukosoa makosa yanayojitokeza katika utendaji kazi ili kulinda nafasi zao.

Kufanya maamuzi mabovu. Kwa mfano Kushindwa kuweka viongozi sahihi wenye maono na mikakati kwa maslahi ya taifa; Hii ni kutokana kutokukubali kukosolewa kwa baadhi ya viongozi hivyo kutafuta watu ambao wapo upande wao ilimradi mambo yao yaweze kwenda. Sababu kubwa ni kuwepo kwa mifumo ambayo si rafiki kwa maslahi yao binafsi.

Kupungua kwa Ufanisi katika Uwajibikaji. Kwa mfano kukosekana kwa uhalisia wa bajeti na shughuli zinazofanyika.

Ikiwa hakuna mgongano wa maslahi binafsi kwa baadhi ya viongozi na wafanyakazi wa mashirika ya umma basi haina haja ya kuwepo kwa usiri wa jambo ambalo Lina manufaa kwa wananchi wote hasa kupitia rasilimali zilizopo nchini. Ipo haja ya kufanya maboresho katika baadhi ya vifungu vya katiba na Kuvifanyia kazi kwa Ufanisi vile vilivyopo, kuongeza vifungu vipya kama italazimu kufanya hivyo hasa katika Sura ya Sita ambayo inaeleza na kufafanua juu ya Utawala Bora na Haki za binadamu. Hii itasaidia kuijenga nchi katika msingi mmoja wa Uwajibikaji na utawala bora ambao hauna matabaka miongoni mwa wananchi, rangi, Kabila, dini, chama au ukanda.
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom